Sura 19 · dakika 3 za kusoma
Roho Mtakatifu Na Mwili Wa Mwaminio
Ubatizo kwa Roho Mtakatifu ni uzoefu dhahiri, wenye nguvu ulio tofauti na wokovu, uwawezeshao waaminio kwa ajili ya utumishi na ushuhuda. Unaonyesha mifano ya kibiblia inayodhihirisha kwamba ubatizo huu ni dhahiri na wa kutambulikana, mara nyingi ukiambatana na ishara kama kunena kwa lugha. Ingawa Wakristo wote wanao uwezo wa kuipata karama hii, ni lazima kila mmoja aipokee binafsi ili kuupata kikamilifu nguvu zake.
Roho Mtakatifu hufanya kazi kwa ajili ya miili yetu vile vile kama kwa ajili ya nia na mioyo yetu. Twasoma katika Warumi 8:11, 'Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu.' Roho Mtakatifu huihuisha mwili wa mwaminio ulio katika hali ya kufa. Ni dhahiri sana kutokana na muktadha kwamba hili lahusu ufufuo ujao wa mwili (mistari 21-23). Ufufuo wa mwili ni kazi ya Roho Mtakatifu. Mwili uliotukuzwa watoka kwake; ni 'mwili wa roho.' Kwa sasa, tunazo malimbuko ya Roho tu na twangoja mavuno kamili, yaani ukombozi wa mwili wetu (mstari 23).
Lakini, kuna namna ambayo Roho Mtakatifu hata sasa huihuisha miili yetu. Yesu atuambia katika Mathayo 12:28 kwamba aliwatoa pepo kwa Roho wa Mungu. Nasi twasoma katika Matendo 10:38, 'Jinsi Mungu alivyomtia mafuta Yesu wa Nazareti kwa Roho Mtakatifu na nguvu; naye akazunguka huku akitenda kazi njema, na kuwaponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.' Katika Yakobo 5:14, Mtume aandika, 'Mtu wa kwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa; nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana.' Mafuta katika fungu hili ni mfano wa Roho Mtakatifu, na kweli ni kwamba kuponya ni kazi ya Roho Mtakatifu. Mungu, kwa Roho wake Mtakatifu, hutia afya mpya na nguvu katika miili hii iliyo katika hali ya kufa katika maisha ya sasa.
Kwenda kwenye mipaka ya kupita kiasi kama wafanyavyo wengi na kushikilia msimamo kwamba mwaminio anayekwenda katika ushirika na Kristo kamwe hana budi kuugua ni kwenda mbali kuliko Biblia inavyoturuhusu kwenda. Ukombozi wa miili yetu kwa kweli umehakikishwa na kazi ya upatanisho ya Kristo, lakini mpaka Bwana atakapokuja, twafurahia malimbuko tu ya ukombozi huo. Twangoja na wakati mwingine twaugua kwa ajili ya nafasi yetu kamili kama wana idhihirishwayo katika ukombozi wa mwili wetu (Warumi 8:23). Lakini ingawa hili ni kweli, ni fundisho dhahiri la Maandiko na jambo la uzoefu binafsi kwa upande wa maelfu kwamba uzima wa Roho Mtakatifu kwa kweli hupita katika miili hii yetu katika nyakati za udhaifu na za maumivu na ugonjwa, ukitia afya mpya ndani yake, ukiokoa kutoka maumivu na kuijaza uzima utele.
Ni pendeleo letu kuujua mguso wa kuhuisha wa Roho Mtakatifu katika miili hii vile vile kama katika nia zetu na hisia, na utashi. Ingekuwa siku kuu kwa Kanisa na kwa utukufu wa Yesu Kristo, kama Wakristo wangeacha milele udanganyifu wote wa shetani wa kazi ya Roho Mtakatifu Christian Science, Uponyaji wa Kiakili, uwepo wa uongo wa Kiungu, Hipnotizimu na namna nyingine mbalimbali za uchawi na kumtegemea Mungu kwa nguvu ya Roho wake Mtakatifu afanye ndani ya miili hii yetu kile ambacho yeye katika hekima yake kamili aonacho kwamba twakihitaji zaidi.