Sura 8 · dakika 9 za kusoma
Mzigo Usiohitajika
“Basi na sisi, kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na dhambi ile ituzingayo kwa upesi; nasi na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu” (Waebrania 12:1).
Wengi huzuiwa katika vita, si kwa sababu ya simba angurumaye au mishale ya uongo, bali kwa sababu wamejitwika mzigo ambao hawapaswi kuubeba; wamechukizwa na mtu fulani nao wameichukua chuki moyoni.
Nilikuwa mahali pa kutazamia, nikitazama chini kuelekea Gibraltar. Palikuwa na alama nyingi zikiwaonya watazamaji wasiwalishe tumbili wadogo walioishi katika miti iliyozunguka eneo hilo. Bila shaka, watu wengine waliamua kuzipuuza alama hizo, na matokeo yake, punde si punde, tumbili angeruka na kutua mabegani mwa mtu. Wakati kamera zilipokuwa zikifanya kazi, tumbili huyo angeanza kufumba vidole vyake katika nywele hata ilipokuwa maumivu, mhusika alipata ugumu wa kumwondoa.
Shetani ana jeshi la ‘tumbili’ waliozoezwa, tayari kuruka begani mwa mtu ili kufumba vidole vyao katika nywele za mwathiriwa wao.
Tunahitaji kumtambua tumbili wa chuki na kumwondoa haraka kabla hajatunyang’anya amani yetu.
Wengi huzuiwa katika vita, si kwa sababu wamejeruhiwa na wengine, bali kwa sababu wamejitwika mzigo ambao hawapaswi kuubeba. Wamechukizwa na mtu fulani nao ‘wameichukua chuki moyoni.’
Ni lazima tutambue kwamba chuki na dhambi ni vitu tofauti kabisa.
Ingawa chuki yaweza kuwa ‘tunda’ la maisha ya dhambi, si tendo la dhambi la makusudi la yule anayechukiza. Naam, twaambiwa kwamba Yesu alikuwa ‘kikwazo’ kwa viongozi wa dini wa wakati wake, naye alikuwa hana dhambi. Ni imani yangu kwamba alisababisha chuki kwa makusudi zaidi ya mara moja, kama nitakavyowaonyesha punde.
Zaweza kuwako sababu nyingi za chuki, lakini zifuatazo ndizo za kawaida zaidi: ● Migongano ya tabia : Watu mara nyingi hutumia maneno haya kama ‘kisingizio’ cha kutoelewana wao kwa wao!
● Matarajio yasiyo ya kweli : Yamkini, sababu namba moja inayowatenganisha wachungaji na makanisa. Sisi si hodari sana wa kuyaweka wazi matarajio yetu kabla chuki haijatokea.
● Kutoelewana : Mawasiliano hafifu.
● Karama na vipawa : Mara nyingi huwaona watu wakiwaonea wivu wengine kwa umaarufu wao, badala ya kujihisi salama katika huduma au ‘wito’ wao wenyewe.
● Kiburi : Jeuri dhidi ya ‘nafsi’ ya mtu. (kwa mfano: baba anayekasirishwa (kuchukizwa) na alama za wastani za mwanawe shuleni, akiamini kwamba zinamvunjia heshima yeye mwenyewe).
● Uasi : ‘Utu wa kale’ unakataa kufa!
Mfano mzuri wa chuki hizi zikiwa kazini ulikuwa wakati kanisa moja lilipokuwa likikarabatiwa - walikuwa wakijenga upya patakatifu pao. Ulikuwa umepita muda wa miaka miwili mirefu ya kazi ngumu kwa kutaniko lililokuwa likijenga kanisa hili, lakini Mungu alikuwa amejithibitisha kuwa mwaminifu.
Kulikuwa na hadithi nyingi za ‘miujiza’ ya maruzuku kutoka kwa Yehova Yire. Sasa ilikuwa wakati wa kuamua mpangilio wa rangi kwa ndani ya patakatifu, hivyo kamati ndogo iliundwa ya waumini wa kanisa, naye John, mwalimu wa sanaa katika shule ya eneo hilo, aliombwa kuongoza kikundi hicho. Katika mkutano wao wa kwanza, John aliwasili na jalada lililoainisha mapendekezo yake (wengine husema ‘maamuzi’) kuhusu mpangilio wa rangi. Haukupita muda kabla wengine waliokuwako kuonyesha kutokubaliana na mapendekezo yake, wakiwa na maoni yao wenyewe.
Hatimaye, kura ilipigwa na uamuzi wa pamoja ukafanywa - ambao haukuakisi maoni ya mwalimu wa sanaa. John alichukizwa, na mrindimo wa chuki yake ulihisiwa katika kanisa hilo kwa muda baada ya hapo. Naam, wengine hata walisema kwamba hapo ndipo ‘miujiza’ iliposimama.
John si tofauti na sisi sote! Ni rahisi mno kuchukizwa bila kutambua athari mbaya ya kutisha ambayo jambo hili laweza kuwa nayo juu yetu wenyewe na juu ya kazi ya Kristo. Ni silaha kuu itumiwayo na Shetani katika kutushinda vitani. Uwe na hakika ya jambo hili - machukizo yataja (Luka 17:1). Yesu alituambia juu ya hakika yao, naye alituonya jinsi tuwezavyo kuhifadhiwa tusijikwae kwa chukizo: kwa kuitikia matakwa yake ya uanafunzi, aliyoyatoa katika chumba cha juu. Na tuangalie mifano kadhaa ya Kibiblia ya watu waliochukizwa. Tutatafuta sababu na kuchunguza matokeo ya chuki yao. Kwa matumaini, tutatambua pia makusudi ya Bwana katika kuruhusu machukizo yaje. Ameahidi kutuokoa kutoka kwa ‘yule mwovu,’ lakini hajaahidi kamwe kutuokoa kutoka katika machukizo! Hata hivyo, angetufundisha kukitambua chukizo na kuipokea neema yake katika nyakati kama hizo za majaribu.
Tafsiri mbalimbali za Agano Jipya zaweza kutuchanganya juu ya somo hili, hivyo na tuelewe kwamba neno la Kiyunani, “skandalon” hutafsiriwa kwa namna mbalimbali kama “kikwazo.” Kwa maneno mengine, “chukizo,” au “kuanguka.”
Mpanzi na Mbegu → Mathayo 13:18-21 Katika mistari iliyo hapo juu, Yesu anaufundisha umati mfano huu maarufu na pia anawafasiria mfano huo, akifananisha aina nne za udongo na aina nne za wasikiaji wa Neno la Mungu.
‘Penye miamba’ humwelezea mtu yule “alisikiaye lile neno, na mara akalipokea kwa furaha; lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; na dhiki au udhia vikitokea kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa” (Mathayo 13:20-21).
Huyu ni mwamini asiyependa yale ambayo Biblia inamfundisha. Alikuwa ametazamia kwamba kuwa Mkristo kungekuwa rahisi!
Alitaka furaha na amani, lakini hakuwa tayari kuuchukua msalaba wake (Mathayo 16:24), kulipa gharama ya utumishi. Baada ya muda, anachukizwa na kuanguka, matokeo yake ni kukosa tunda !
Nabii Asiyekuwa na Heshima → Mathayo 13:54-57 Yesu alikuja mji wake mwenyewe wa Nazareti ambako alifundisha katika sinagogi. Majirani zake walishangazwa na mafundisho yake, wakiuliza alipoipata hekima kama hiyo. “Huyu si mwana wa yule seremala?” wakasema. “Tumemjua tangu utotoni! Anajidhania kuwa nani?” Kuna msemo wa kawaida, ‘kuzoeana mara nyingi huzaa dharau,’ na kama tusomavyo katika mstari wa 57, wale wa mji wa Yesu “walichukizwa naye.”
Ni vijana wangapi wa kiume na wa kike, wakiitikia wito wa Mungu juu ya maisha yao, wamejaribu kuujibu wito huo, lakini wamezuiwa na ‘hekima’ kubwa zaidi ya majirani zao: jamaa, marafiki, na viongozi wa kanisa! Nakumbushwa juu ya yule nabii mzee katika 1 Wafalme 13 aliyechukizwa kwa sababu Mungu alikuwa akimtumia kijana mwingine kulitangaza neno lake. Kwa sababu ya chuki yake, nabii mzee alimdanganya kijana, matokeo yake yakawa kunyamazishwa kwa ushuhuda wake, kupitia kifo!
Kutokana na chuki yao huko Nazareti, “hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutokuamini kwao” (Mathayo 13:58). Njia ya hakika ya kumzuia Bwana asitende kwa njia za kimiujiza katika maisha yako, ni kuchukizwa. Matokeo ya kuchukizwa kwao yalikuwa kukosa miujiza !
Msaliti → Mathayo 26:6-14 Yesu alikuwa nyumbani kwa Simoni, mkoma, hapo mwanamke mmoja alipoingia na chupa ya thamani ya marhamu yenye harufu nzuri. Aliivunja juu ya miguu ya Bwana na kuanza kuipangusa kwa nywele zake, hata harufu ile nzuri ikaijaza nyumba. Mathayo atuambia kwamba wanafunzi walichukizwa walipoona ‘upotevu’ huu, wakisema kwamba manukato yale yangaliweza kuuzwa kwa bei ghali na fedha zikapewa maskini (Mathayo 26:8).
Mara baada ya haya, Yuda Iskariote alikwenda kwa wakuu wa makuhani ili amsaliti bwana wake (Mathayo 26:14-16). Katika masimulizi ya Yohana juu ya tukio hili, twaambiwa kwamba ni Yuda mwenyewe aliyeleta lalamiko hilo, akiwa amechukizwa, “si kwa kuwahangaikia maskini, bali kwa kuwa alikuwa mwivi, naye ndiye aliyeshika mfuko, akiiba yaliyotiwa humo” (Yohana 12:6).
Nakumbuka wakati shirika moja maarufu la kimataifa la hisani lilipotumia zaidi ya dola milioni moja kutengeneza filamu ya hali halisi kuhusu kazi yao. Wafuasi wao wengi walionyesha hasira kwa ‘upotevu’ kama huo na wakazuia michango yao ya kila mwezi. Walijihisi kuwa na hasira ya haki; hata hivyo, ndani ya mwaka mmoja, mapato yatokanayo na kuonyeshwa kwa filamu hiyo, yalizidi mara tano gharama ya kuitengeneza! Naamini heri tuwe upande wa tahadhari tunapokuja kutumia fedha za Bwana, lakini kuchukizwa kwaweza kuwa chanzo kikubwa zaidi cha aibu!
Yuda alichukizwa, hivyo akatoka nje kumsaliti bwana wake. Uwezekano wa usaliti ulikuwako tayari, lakini chuki iliuchochea uwezekano huo hata ukawa tendo. Matokeo ya chuki yake yalikuwa kwamba hakumtumaini tena Bwana kufanya yale aliyosema angeyafanya. Yuda angemsukuma atende. Ikiwa yeye ndiye Masihi aliyeahidiwa ambaye angeusimamisha ufalme wake mahali pa milki ya Kirumi, sasa ulikuwa wakati wa kulithibitisha jambo hilo! Lakini jambo moja tu lilithibitika - kwamba yeye, Yuda, alikuwa mwanasiasa duni na rafiki duni hata zaidi!
Yuda alikuwa amepoteza tumaini katika Bwana! Tumaini lako limewekwa wapi? Unaweka wapi imani yako na tumaini lako? ‘Tumaini’ la Kikristo ni kutarajia kwa shauku kwamba yale aliyoahidi, atayakamilisha! Mtunga nyimbo asema “Tumaini langu limejengwa juu ya kitu kisichopungua damu na haki ya Yesu!” (My Hope is Built On Nothing Less, Robert Critchley).
Mwandishi wa Waebrania anatutia moyo “tusiutupe ujasiri wetu, ambao una thawabu kubwa” (Waebrania 10:35).
Tunapochukizwa, matokeo yake yatakuwa kukosa tumaini, na kwa hiyo, hatutakuwa na ujasiri !
Kukana kwa Petro → Mathayo 26:31-35, 69-75 Yesu alikuwa ndipo tu amefika Mlima wa Mizeituni, akiwa amesimamisha agano la ushirika pamoja na wanafunzi wake. Sasa anawafundisha kwamba yu karibu kuondolewa kwao.
Yesu anawaambia wanafunzi wake, “Ninyi nyote mtachukizwa kwa ajili yangu usiku huu wa leo.” Lakini Petro, akiwa jasiri na mpumbavu, asema, “Mimi sitachukizwa nawe kamwe, hata kama wengine wote watachukizwa!” (Mathayo 26:31-33). Jinsi gani lazima aliyajutia maneno hayo saa chache tu baadaye! Namwonea huruma Petro kwa sababu anafanana nami sana! Jinsi gani tunaye Mwokozi wa ajabu ambaye, akiihisi maumivu yake, angemtokea Petro kwanza baada ya kufufuka kwake, na kabla wengine hawajamwona (Luka 24:34). Naweza tu kuiwaza taswira ile walipopatanishwa wao wawili kupitia upendo wa Mwokozi.
Yohana na Petro waliingia nyumbani mwa Kuhani Mkuu ambako Yesu alikuwa akihukumiwa. Petro alipopita mlangoni, kijakazi mmoja alimwambia, “Wewe si mmoja wa wanafunzi wake?” Akajibu, “Mimi siyo!” Kisha kwa mara mbili zaidi anamkana Bwana wake, akiongeza viapo vikali kabla jogoo hawajawika.
Napenda kumwazia yule kijakazi mchanga na swali lake. Je, ingaliwezekana kwamba alikuwa akimpenda Bwana na alitaka kujua zaidi juu yake? Kama Petro angalikubali uanafunzi wake, je, angalimwomba amwambie juu ya rafiki yake kwa kuwa naye alitaka kumpenda? Hata hivyo, Petro alichukizwa , na matokeo ya chuki yake yalikuwa kukosa ushuhuda !
Wengi Wageuka Kumwacha → Yohana 6:53-61 Katika kifungu hiki, Yesu anawaambia wafuasi wake mambo magumu kadhaa. Anawaita “kuula mwili wangu na kuinywa damu yangu” (Yohana 6:53). Leo, tukitazama nyuma, twalielewa jambo hili kwa maana ya kikombe cha ushirika na agano jipya alilotuita ndani yake, lakini kwao lilikuwa neno gumu lililokuwa vigumu kulielewa.
Yesu aliwauliza, “Je, mnachukizwa?”
Je, wewe unachukizwa na wito wake wa uanafunzi unaotakiwa katika agano la ushirika? Uanafunzi ambao ndio changamoto kuu ya kitabu hiki? Matokeo ya chuki yao yalikuwa kwamba wengi katika wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena (Yohana 6:66). Matokeo ya chuki yao yalikuwa kukosa ushirika.
Hivyo tunayo mifano mitano ya Kibiblia ya wale waliochukizwa, matokeo yake wakapoteza tunda , ujasiri , na ushuhuda wao. Ndani yao mlikuwa na mfarakano, na Mungu hakufanya miujiza yoyote kati yao! Kwa hiyo twaweza kuwa na hakika kwamba Shetani lazima alishangilia kwa dharau.