Sura 7 · dakika 7 za kusoma
Hila za Shetani
Yesu alipokufa msalabani kisha akafufuka, aliwashinda Shetani na majeshi yake ya kipepo, akiwaondolea nguvu zao zote, “akiisha kuzivua enzi na mamlaka, aliwafanya kuwa mkogo waziwazi” (Wakolosai 2:15). Sasa wanapigana vita kwa uongo, udanganyifu, na hofu, ambavyo huvipandikiza katika kila eneo la maisha yetu: mitazamo yetu, hisia zetu, mawazo yetu, hata na hali ya mwili.
Lakini wana nguvu katika maeneo haya tu kadiri sisi tunavyowapa! Mtume Paulo alitangaza kwamba hatughafiliki na hila zake (2 Wakorintho 2:11), lakini kwa masikitiko jambo hilo si kweli kwa waumini wengi leo!
Nafasi ya Ibilisi Je, umewahi kukasirika? Bila shaka umewahi. Mimi pia. Na hivyo ndivyo alivyokuwa Yesu alipowaona wabadili fedha hekaluni.
Nina hakika pia alikasirika alipoona makutano wakiwa katika umaskini mkubwa na maradhi mengi. Moyo wake ulihuzunika alipoona matokeo ya kutotii kwa Adamu yakiwaangukia wanadamu wote. Hisia ya hasira si dhambi. Hisia si za maadili wala kinyume cha maadili - hazina uhusiano na maadili. Lakini tunachofanya na hisia zetu ndicho chenye maana kubwa. Paulo anatuhimiza kwamba tunapokasirika hatupaswi kutenda dhambi. Kisha anaendelea kuongeza, “jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka” (Waefeso 4:26).
Ni lazima tushughulikie hali hiyo mara moja. Tukiiacha hasira iliyo ndani yetu itote, itazaa uchungu utakaotunyang’anya yaliyo mema zaidi ya Mungu. Muda wote tuwapo katika ulimwengu huu, watu watatutenda mabaya, na machukizo yatakuja. Yesu alituonya juu ya hilo (Luka 17:1). Huenda kukawa na sababu ‘nzuri’ nyuma ya hasira iliyo ndani yetu, lakini ametupa Roho wake Mtakatifu ili kutuwezesha kuijua neema katika nyakati hizo.
“Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao. Mkiangalia sana mtu asiipungukiwe na neema ya Mungu; ‘shina la uchungu’ lisije likachipuka na kuwasumbua, na kwa hilo watu wengi wakatiwa unajisi” (Waebrania 12:15).
Tusiposhughulikia hasira kwa njia ifaayo (ambayo tutaijadili baadaye), tunacheza sawasawa mikononi mwa adui! Paulo anaendelea kwa kusema “wala msimpe Ibilisi nafasi” (Waefeso 4:27). Baadaye, katika sehemu iyo hiyo ya Maandiko inayohusu mazungumzo yetu sisi kwa sisi, anatuonya kwamba huenda tunamhuzunisha Roho Mtakatifu (Waefeso 4:30).
Tunapochukua hasira (au mitazamo mingine mibaya), adui hupata mahali pa kuingia katika mawazo yetu, akieneza uongo na udanganyifu wake ili kuzidisha mfarakano. Punde inaonekana kwamba upatanisho hauwezekani, naye ameshinda vita hiyo.
Yesu alituonya tuwe macho (Luka 17:3) na Paulo alituagiza tuhakikishe kwamba Shetani asitufaidie ubaya wowote (2 Wakorintho 2:11). Vyote viwili vipo katika muktadha wa kuwasamehe wale tunaowaona kuwa wametukosea. Mtazamo wa kutokusamehe (kama hasira) humpa adui faida - nafasi - mahali pa kukanyagia katika maisha yetu. Mitazamo iliyo kinyume ya msamaha na amani humshinda.
Simba Angurumaye Je, umewahi kumwona simba akinyemelea mawindo yake? Mimi sijawahi, lakini nadhani ni kama paka wangu anaponyemelea ndege au panya bustanini mwetu. Hujikunyata chini sana na kusonga polepole ili asimtahadharishe windo lake kuhusu nia yake. Kwa hakika hawajulishi kwamba anakuja kwa kulia ‘miao’ kwa sauti kubwa!
Basi, mtume Petro ana maana gani anapotuambia, “Mwe na kiasi na kukesha; adui yenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka akitafuta mtu ammeze” (1 Petro 5:8)?
Katika kitabu “Pilgrim’s Progress” cha John Bunyan, tunasoma kwamba Pilgrim alikuwa akikaribia Palace Beautiful, jengo lililojengwa kwa ajili ya faraja na usalama wa waumini. Sasa alielewa kwa nini Timorous na Mistrust, wengine waliokuwa wakiutafuta Mji wa Mbinguni (Celestial City), walikuwa wamempita wakikimbia kwa hofu kuu, kwa maana lango la kuingilia lilikuwa likilindwa na simba wawili.
Mara moja, moyo wa Pilgrim ukazama, naye pia akaingiwa na hofu.
Kama simba angeliingia kwa kurukaruka chumbani mwako na kukugurumia, nadhani ungeitikia kama wao - umejaa hofu! Mimi ningefanya hivyo!
Simba wangurumao wana matokeo hayo kwetu - wanatisha sana.
Punde, Pilgrim akatambua kwamba simba wote wawili walikuwa wamefungwa minyororo, na kwamba maadamu angetembea katika njia nyembamba iliyo kati yao, hakuna hata mmoja aliyeweza kumfikia ili kumdhuru. Tunahitaji kuelewa kwamba yule simba, Shetani, amengolewa meno yake naye amefungwa minyororo.
Hawezi kuwadhuru watu wa Mungu maadamu tunashikamana na njia nyembamba. Hata tunapokengeuka kutoka njia nyembamba, upendo wa Baba hutunyoshea mkono kutururudisha kabla adui hajaweza kutuangamiza. Lakini atanguruma, na wengi hushindwa kwa sababu hisia zao huitikia mngurumo huo.
Mngurumo wake mara nyingi ni ule wa mshitaki, ukileta hukumu ya adhabu.
Ilikuwa mara ya kwanza kwa Mary kuimba sehemu za pekee katika kwaya ya vijana. Ilikwenda vizuri isipokuwa katika ile noti ya juu ndani ya kiitikio ambako alikuwa dhaifu kidogo na mwenye kutetemeka. Ilikuwa ni sauti ndogo tu iliyonong’ona sikioni mwake ikimwambia, “Umejifanya mpumbavu,” lakini ulikuwa ni mngurumo wa simba. Akaapa kutoimba tena hadharani kamwe.
Mchungaji John alikuwa na matumaini makubwa mno alipoanza huduma katika kanisa la St. Peter. Sasa, miaka miwili tu baadaye, alikuwa akiondoka.
Kikundi cha vijana kilikuwa hakijaongezeka idadi kama mchungaji mkuu alivyotazamia, hivyo John akaombwa aondoke. Simba akanguruma, “Hutafanikiwa kamwe kuwa mchungaji. Wewe ni mtu uliyeshindwa!” Wiki moja baadaye, akaomba tena ile kazi ya kilimwengu aliyokuwa ameiacha alipoanza kuamini kwamba Mungu amemwita katika uchungaji.
Alec alikuwa ameanguka tena. Alitamani sana kuwa huru kutoka katika tabia hii chafu ya kuvuta sigara, lakini ilikuwa ni jaribu kubwa mno alipopewa sigara hii. Sasa alikuwa akijisikia na hatia, na simba akanguruma, “Mungu hawezi kukutumia. Daima unamwangusha!”
Simba hangurumi tu kwa kila kujikwaa au kushindwa, bali pia anajua ni hisia zetu zipi zenye uwezekano mkubwa wa kuathiriwa na mngurumo huo. Kwa wengine ni hisia ya hatia, kwa wengine ni hofu. Wengi huitikia mngurumo wake kwa hisia za kujidharau na kukosa kujiamini. Wewe hujiitikia wapi?
Ni jambo la kusikitisha kiasi gani wakati mngurumo wa simba unapokuja kupitia neno lisilo na fikira la mwamini mwingine! Ni muhimu katika Mwili wa Kristo kutiana moyo sisi kwa sisi ili kupinga uongo - mngurumo wa Ibilisi!
Mpiga Mishale Mtu anapokuwa karibu kupigana vita, ni vyema kuchukua mahali pa juu. Hii hukuwezesha kuona mienendo yao ili uweze kuchukua hatua zifaazo kuipinga. Sisi kama waumini tunahitaji kuelewa pendeleo kuu tulilo nalo la kuwa “ndani ya Kristo.” Paulo anatangaza kwamba Mungu “amemtukuza Yesu, juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani” (Waefeso 1:21).
Kwa Wayahudi, haya ni majina ya vyeo vya jeshi la kipepo la Shetani, lakini vyote viko chini sana ya miguu yake. Ameliponda kichwa cha bwana wao naye ana mamlaka yote juu yao. Anatutakia sisi tuutumie mamlaka huo ili tujifunze kuwa washindi. Wale watakaotawala pamoja naye lazima wastahili kuvaa taji, na taji hutolewa tu kwa washindi.
“[Kristo] ametufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu” (Waefeso 2:6).
Ni lazima tuishi juu ya ardhi hiyo iliyo juu, ambapo njia pekee ambayo Shetani anaweza kutufikia ni kwa kutupiga mishale yake yenye moto. Pia tumepewa ngao ya uhakika dhidi ya makombora hayo yenye moto, kama Paulo aandikavyo, “Zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu” (Waefeso 6:16). Adui anapotupigia uongo na mashtaka yake, tunaiinua ngao yetu ya imani, tukikumbuka kwamba “imani huja kwa kusikia… neno la Mungu” (Warumi 10:17).
Tunahitaji kujua sisi ni nani na mapendeleo ya kuwa “ ndani ya Kristo .”
Mimi ni… ● Mtoto wa Mungu (Yohana 1:12).
● Rafiki wa Yesu (Yohana 15:15).
● Mrithi pamoja na Kristo (Warumi 8:17).
● Nimeungwa na Bwana (1 Wakorintho 6:17).
● Kiungo cha Mwili wake (Waefeso 5:30).
● Nimepatanishwa na Mungu (2 Wakorintho 5:18).
● Kazi ya mikono ya Mungu (Waefeso 2:10).
● Raia wa Mbinguni (Wafilipi 3:20).
● Kiumbe kipya (2 Wakorintho 5:17).
● Niliyechaguliwa na Mungu (Wakolosai 3:12).
● Mtakatifu (Waefeso 1:1).
● Mgeni katika ulimwengu huu (1 Petro 2:11).
● Kile nilicho (1 Wakorintho 15:10).
● Adui wa Shetani (1 Petro 5:8).
● Nimevikwa haki (Waefeso 4:24).
● Makao ya Mungu (1 Wakorintho 3:16).
● Mmoja wa mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, na watu wa milki ya Mungu (1 Petro 2:9- 10).
Ndani ya Kristo mimi… ● Nimesamehewa kabisa (Warumi 5:1).
● Nimebarikiwa sana (Waefeso 1:3).
● Nimechaguliwa niwe mtakatifu (Waefeso 1:4).
● Nimetiwa muhuri kwa Roho wake (Waefeso 1:13).
● Nimekusudiwa tangu asili niwe mtoto wake (Waefeso 1:5).
● Nina Kristo ndani yangu (Wakolosai 1:27).
● Nimekamilishwa (Wakolosai 2:10).
● Nimekombolewa kutoka kwa Shetani (Waefeso 1:7).
● Nimeketishwa katika ulimwengu wa roho (Waefeso 2:6).
● Nimewekwa huru mbali na hukumu ya adhabu (Warumi 8:1).
● Nina njia ya kumfikia Mungu moja kwa moja (Waefeso 2:18).
● Naweza kumkaribia Mungu kwa ujasiri (Waefeso 3:12).
Kwa orodha kamili zaidi, soma Biblia yako!
Zamani kulikuwa na dawa rahisi kwa magonjwa madogo mengi, “Meza tu aspirini mbili kisha ulale!” Leo, nina dawa rahisi ya kutoa kwa mashambulizi madogo mengi ya adui.
Chukua mistari miwili kati ya Maandiko yaliyotajwa hapo juu kila siku na uyatafakari. Imani yako itakuwa na nguvu punde, na mishale yenye moto haitakuwa na nguvu sana dhidi yako.