Sura 4 · dakika 7 za kusoma
Watu wa Agano
The Agape Feast “Karamu ya Agape “Yesu akatwaa mkate, na alipokwisha kushukuru, akaumega, akasema, ‘Huu ndio Mwili wangu, uliomegwa kwa ajili yenu. Twaeni, mle!’”
(1 Wakorintho 11:23-24). Wote walifanya hivyo, na kwa kufanya hivyo, walijitambulisha na Mwili wa Kristo.
“Vivyo hivyo akakitwaa kikombe pia, baada ya kula, akisema, ‘Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu; fanyeni hivi kila mnywapo, kwa ukumbusho wangu’” (1 Wakorintho 11:25-26). Nashangaa kwamba hakuna hata mmoja kati ya waliokuwepo aliyemuuliza alichokimaanisha aliposema haya. Naweza tu kudhani kwamba wote walielewa.
Agano ni mapatano kati ya pande mbili. “Wewe unifanyie hivi, nami nitakufanyia vile!” Leo, watu wafanyapo maagano ni lazima ushahidi upatikane katika mfumo wa saini zilizoambatanishwa na mapatano yaliyoandikwa. Kwa masikitiko, neno la muungwana halikubaliki tena. Katika wakati wa Yesu, maagano yalitiwa muhuri kwa kinywaji cha pamoja. Isingekuwa damu, kama ilivyokuwa hivi karibuni miongoni mwa Wenyeji Wahindi wa Amerika ya Kaskazini na wanakabila wa Afrika, ingawa maagano yote ya siku za Agano la Kale yangeashiriwa kwa kumwaga damu katika kuchinja mnyama wa dhabihu. Kwa kweli, mtu alisemekana ‘kukata agano’ badala ya kulifanya.
Kuna hadithi ya kuvutia inayosimuliwa kuhusu Dr. Livingstone, mmisionari mkuu aliyekuwa mwanzilishi wa kazi barani Afrika. Yeye, pamoja na waongozaji na wachukuzi wake, mara nyingi walitekwa na wanakabila wapiganaji walipokuwa wakisafiri katika bara hilo lenye giza.
Wakati mmoja, wafungwa hao waliletwa mbele ya chifu mkali aliyeanza kuwakemea kwa kuingilia eneo lake. Alipokuwa akizidi kukasirika kwa sababu ya kimya cha Livingstone, mwongozaji mmoja alimwinamia mmisionari na kumhimiza ‘akate agano.’ Livingstone hakuelewa kilichokuwa kikiombwa, lakini punde si punde alirudi nyuma kwa mshangao alipomtazama mtumishi wake Mkristo na kijana aliyechaguliwa kutoka kabila hilo la uadui, wakifanya kitendo ambacho kwake kilikuwa cha kipagani. Walijikata kidogo kwenye mikono yao ya juu, wakakusanya damu ndani ya bakuli na kuinywa pamoja!
Kisha chifu akasogea mbele na kushika kamba ambayo kwayo Livingstone alikuwa akiongoza mbuzi, chanzo cha maziwa aliyoyapenda sana. Livingstone alishtuka kisha akashangaa chifu alipomkabidhi zawadi mkononi mwake - ile fimbo yenye ncha ya shaba ambayo kwayo alikuwa amewakabili wale walioingilia eneo lake. Kisha waliongozwa hadi kwenye kibanda ambapo wangelala usiku baada ya kupokea chakula kutoka kwa wale waliowateka.
Baada ya muda, alipokuwa akisafiri katika eneo lingine la Afrika, Livingstone alitekwa tena na kuletwa mbele ya chifu mwingine mkali. Lakini wakati huu, chifu alipiga magoti mbele ya mmisionari. Ni hapo tu ndipo ufahamu ulipokuja. Kijana yule mwongozaji alipokuwa ‘amekata agano’ kwa niaba ya Livingstone, na kulitia muhuri kwa kunywa damu, mapatano yalifanyika kati yao na kabila, hasa kati ya Livingstone na chifu.
Kama ishara ya mapatano hayo ya agano, chifu alikuwa ametoa fimbo yake, alama ya kujitoa na kuunga mkono kwake. Chifu wa pili mkali aliitambua fimbo, akaelewa kwamba Livingstone alikuwa na ndugu wa damu na akajisalimisha kwa nguvu na mamlaka hiyo iliyo kuu zaidi.
Yesu amefanya agano kama hilo pamoja nasi! Sasa tunaweza kutembea kwa kujiamini katika ulimwengu huu uliolemaa kwa mamlaka yake! Tuna ndugu wa damu aliyeimwaga damu yake, akainywa hadi tone la mwisho lenye uchungu kwa niaba yetu, na akatupa mamlaka ya jina lake (Matendo 3:16)!
Adui yetu, Shetani, na wasaidizi wake, dhambi na mauti, hawapaswi kuwa na mamlaka juu yetu (Warumi 6:14)!
Yesu alipowaalika wanafunzi wake kunywa ‘kikombe cha agano,’ walijua walikuwa wakionyesha kukubali kwao masharti ya agano jipya. Ndivyo ilivyo kila tunapopokea alama katika meza ya Bwana. Tunapokula mkate, tunajitangaza kuwa mwili wa Kristo . Tunapokunywa kikombe, tunaingia tena katika agano la kuwa watumishi kila mmoja kwa mwenzake, wapendanao, na watii kwa Neno lake .
Kwa Namna Isiyostahili Katika waraka wake kwa Wakorintho, Paulo anatuhimiza tuwe waangalifu sana katika kupokea alama hizi. Tukikinywa kikombe cha Bwana “kwa namna isiyostahili” twaweza kabisa kujiletea hukumu sisi wenyewe, tusiupambanue mwili wa Bwana. “Kwa sababu hiyo wako wengi kwenu (waamini) walio hawawezi na wagonjwa” (1 Wakorintho 11:30).
Ikiwa nabeba uadui moyoni mwangu kwa mwingine, au siishi kama mtumishi , mpendaji , au katika utii , kupokea kwangu mkate na kikombe ni unafiki. Ninashindwa kumtambua mwenzangu kuwa ni mmoja pamoja nami katika Mwili wa Kristo. Jambo hili laweza kabisa kunisababishia udhaifu na ugonjwa. Haya hayatoki kwa Bwana - yeye si mwanzilishi wa ugonjwa, bali mimi nimempa shetani nafasi (2 Wakorintho 2:11), na hakika yeye anajua jinsi ya kutumia nafasi kama hizo kwa faida yake!
Kuwaombea Wagonjwa Sasa nina ufahamu wa kile Yakobo alichokimaanisha alipoandika, “Mtu wo wote miongoni mwenu amekuwa hawezi? Na awaite wazee wa kanisa, nao wamwombee, na kumpaka mafuta kwa jina la Bwana. Na kule kuomba kwa imani kutamwokoa mgonjwa, naye Bwana atamwinua; hata ikiwa amefanya dhambi atasamehewa” (Yakobo 5:14-15).
Mara nyingi nilijiuliza kwa nini wazee walipaswa kuhusishwa. Je, si kila mtu angeweza kuomba? Je, wazee wana nguvu za maombi zaidi kuliko rafiki na jamaa wapendao? Sasa siamini kwamba kuwaita wazee kuna uhusiano wowote na nguvu zao za maombi, bali na mamlaka yao . Fungu hili ni lazima liunganishwe na onyo la Paulo lililotangulia, kwa kuwa ndiyo mafungu pekee yanayotoa dokezo lolote la sababu zinazoweza kuwafanya waamini kuwa wagonjwa au wadhaifu. Bila shaka, sisi pia twaweza kupatwa na vijidudu, magonjwa, na maradhi kama vile mtu ye yote ulimwenguni, lakini onyo la Paulo ni lazima lielezwe kwa nguvu kwa waamini.
Iwapo wazee watatambua kwamba ugonjwa wa mwamini waweza kuhusiana na mtazamo mbaya kwa wengine katika Mwili wa Kristo, ni lazima watumie mamlaka yao kama wazee wa kanisa, kumwagiza huyo apatane. Ndipo tu wanaweza kuomba, wakimpaka mafuta (alama ya baraka na ulinzi wa Roho Mtakatifu) kwa jina la Bwana. Mgonjwa huyo - mwenye hatia - atarejeshwa na kusamehewa.
Maombi ya Bwana Baada ya kuwafundisha wanafunzi wake mambo ya kwanza ya moyo wake, Bwana wetu aliinua macho yake kuelekea Mbinguni na kusema na Baba yake.
Yafaa mtu achukue muda kusoma Yohana 17 ili kusikia kilio cha moyo wa Yesu usiku ule kabla ya kufa kwake. Acha nitembee nawe katika maneno haya ya ajabu, nikisisitiza wazo moja kuu.
“Baba, nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye… Nimelidhihirisha jina lako (sifa zako) kwa watu hawa… nao wamelishika neno lako. Ninawaombea hao… kwa kuwa hao ni wako. Wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni. Siwaombei hao tu, bali na wale wote watakaoniamini kwa sababu ya neno lao (ambao ni pamoja nawe na mimi). Ili wote wawe na umoja … ili ulimwengu upate kusadiki. Nami utukufu wako nimewapa … ili wawe na umoja … kama sisi tulivyo Umoja. Ili wakamilishwe katika umoja , ili ulimwengu ujue ya kuwa wewe ndiwe uliyenituma, na ya kuwa umewapenda wao kama ulivyonipenda mimi… Nimewajulisha jina lako (sifa zako)… ili pendo lile ulilonipenda liwe ndani yao, nami niwe ndani yao” (Yohana 17).
Jina la Mungu lilifunuliwa kwa Musa walipokutana katika Mlima Sinai; kwa hiyo, twaweza kuwa na hakika kwamba yeye ni “ BWANA, Mungu mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli; mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi” (Kutoka 34:6-7).
Kwa kweli, Yesu alidhihirisha sifa hizo hizo kwa wote aliokutana nao.
Kijitabu cha Injili cha Mungu Siwezi hata kuchukua ukurasa mmoja kutoka katika Biblia na kuutumia kama kijitabu cha uinjilisti cha kumpa rafiki asiyeamini. Naweza kunukuu kutoka Yohana 3 au kufuata “Njia ya Warumi” inayowaeleza njia ya wokovu. Naweza kuwapa “Hatua Nne” au “Mpango wa Ajabu wa Mungu wa Wokovu,” lakini siwezi kurarua ukurasa mmoja kutoka katika Biblia na kuutoa kama kijitabu cha injili.
Hata hivyo, naweza kuchukua sura nzima na hata vitabu vizima, ili kumwonyesha mwamini mambo ya kwanza ya Mungu: njia yake ya wokovu. Amesema kwamba watu wake watakapokuwa wakitembea katika umoja kama watumishi , kama wapendaji na katika utii , ulimwengu utajua na kuamini !
Sisi ndio kijitabu chake cha Injili! Ni wakati wa kuweka mambo yetu ya kwanza sawasawa na kupatana na mambo ya kwanza yake! Tuko wepesi kusema tunapogundua uzushi wa mafundisho kwa mwenzetu - je, si wakati wa kuwa wepesi vivyo hivyo kutenda dhidi ya uzushi wa matendo, tukiona migawanyiko mingi miongoni mwa waamini, iliyo dhahiri sana kwa ulimwengu?
“Kwa maana viumbe vyote pia vinatazamia kwa shauku nyingi kufunuliwa kwa wana wa Mungu” (Warumi 8:19).