Sura 3 · dakika 9 za kusoma

Vipaumbele

Karamu ya Agano Ilikuwa siku ya joto na vumbi wakati Petro na Yohana, wanafunzi wa Yesu, walipoingia mji wa Yerusalemu. Walikuwa wamekuja kuadhimisha Pesaki, Sikukuu ya Pasaka, na hata sasa walikuwa wakimfuata mtu aliyechukua mtungi wa maji, ambaye angewaongoza mpaka mahali karamu ilipopaswa kuandaliwa.

Kama vile Bwana alivyokuwa amewaambia, haikuwa vigumu kumpata kiongozi wao, kwa maana kumwona mwanamume akichukua mtungi wa maji lilikuwa jambo lisilo la kawaida. Hiyo ilikuwa kazi ambayo mara nyingi ilifanywa na wanawake.

Aliwaongoza mpaka nyumba nzuri ya ghorofa mbili, ambako mwenyeji aliwakaribisha kwa uchangamfu. Walipomweleza shughuli yao, waliingizwa katika chumba kikubwa kilichopambwa kilichokuwa ghorofani.

Haikuwachukua muda mrefu kuandaa meza ya chini, kwa kuwa mahitaji ya karamu yalifahamika vyema kwa wote wawili. Mabakuli ya mboga chungu yaliwekwa kwa kupokezana na sahani za matofaa, mdalasini, na lozi. Chupa ya maji ya chumvi na mayai kadhaa ya kuchemshwa viliwekwa kando ya vyombo vya divai, na kulikuwa na vipande kadhaa vya mkate usiotiwa chachu walioita “matzah.” Punde saa ikawadia, naye Yesu akaja pamoja na wanafunzi wengine.

Kulikuwa na mnong’ono wa shangwe na mazungumzo yaliyojaa hamasa walipoingia katika chumba cha ghorofani. Huu ulikuwa wakati wa kusherehekea, wakati wa furaha kuliko yote katika mwaka mzima kwa Wayahudi wote; walipokumbushwa tena uaminifu mkuu wa Yehova. Je, hakuwa amewakomboa kutoka utumwa wa Misri miaka mingi iliyopita? Je, hakuweza kuwakomboa tena kutoka udhalimu wa sasa wa Warumi?

Kwa wanafunzi wa Yesu wakati huu labda ulikuwa wa kusisimua hata zaidi. Walikuwa wakijiuliza kama siku ilikuwa karibu ambapo bwana wao angejidhihirisha kwa taifa kuwa ndiye Masihi aliyengojewa kwa muda mrefu, aliyekuja kuwaweka huru kama walivyotabiri manabii wa zamani. Walihisi kwamba walikuwa katika wakati muhimu sana katika historia ya watu wao. Kwa kweli, juma hili lililopita lilikuwa la ajabu kiasi, na mambo yalikuwa yakifikia kilele. Ilikuwa dhahiri kwamba viongozi wa dini walitikiswa sana na mafundisho na umaarufu wa Yesu.

Naweza kuwazia kwamba mazungumzo ya wanafunzi yalihusu kabisa matukio ya juma hili lililopita, wakijiuliza yalikuwa na maana gani. Nina hakika Petro hakuweza kuacha kuzungumza juu ya kuingia kwa ushindi katika Yerusalemu siku tano tu zilizotangulia, wakati makutano walipotandaza mavazi yao barabarani penye vumbi, na kukata matawi ya mitende ili kuyapunga, huku wakipiga kelele, “Ndiye mbarikiwa yeye ajaye kwa jina la Bwana, naam, Mfalme wa Israeli” (Yohana 12:13).

Naweza kumwazia, kichwa juu, kifua nje, alipomwongoza mwana-punda ambaye juu yake bwana aliketi. Yohana na Yakobo, wenye bidii (wana wa ngurumo), huenda walivutiwa zaidi na jinsi bwana wao alivyozipindua meza za wabadili fedha na kuwafukuza kutoka hekaluni. “Je, uliona sura ya Kuhani Mkuu? Ndugu, alikasirika kweli!”

Wote wakajishusha hata wakaegemea kando ya meza, wakiwa bado na furaha katika hali yao ya sherehe: ulikuwa wakati wa karamu. Yesu aliwatazama kwa furaha rafiki zake wakisherehekea, lakini alijua jambo ambalo lilikuwa limewapita ufahamu wao: kesho angekufa.

Ungefanya nini kama daktari wako angekuambia kwamba umebakiwa na muda mfupi tu wa kuishi? Bila shaka, ungetafuta maoni ya pili! Na kama hayo pia yangethibitisha kwamba karibu ungeuacha ulimwengu huu, wenzako wa daima, na rafiki zako? Ninajua ningefanya nini. Ningemaliza haraka shughuli zangu za sasa na kupanga kuwa pamoja na wale walio wa thamani zaidi kwangu: mke wangu, binti zetu, na jamaa zao.

Ningetaka kuwaambia jinsi ninavyowapenda na jinsi ninavyojivunia. Ningewatia moyo waendelee na Yesu, wakimtumikia na kuishi maisha ya kumsifu utukufu wake.

Ningewauliza kama kuna jambo lolote ambalo ninapaswa kuwaomba msamaha, majeraha yoyote, maneno yoyote yasiyo na huruma au ukosefu wa kufikiri. Ningetaka kuhakikisha kabisa kwamba hakuna lililobaki bila kufanyika ambalo lingeweza kufanywa ili kuimarisha uhusiano wetu sisi kwa sisi.

Ningepata muda mchache sana wa kuzungumza mambo madogo kama matokeo ya michezo au uvumi, ambayo hujaza muda wangu mwingi vinginevyo. Kwa kweli, ningekuwa nikishughulikia vipaumbele tu. Na usiku ule, katika karamu ya Pasaka, hicho ndicho hasa Bwana alichokusudia kukifanya na wanafunzi wake - kushughulikia vipaumbele!

Matakwa Yake Kama ilivyokuwa desturi, wote walikuwa wamevua viatu vyao walipoingia katika chumba hiki cha ghorofani. Miguu yao ilikuwa na vumbi, na mchanga kati ya vidole vya miguu yao uliwafanya wasistarehe kabisa.

Punde mnong’ono wa manung’uniko ukasikika. Mabakuli ya maji yalikuwa juu ya meza karibu na mlango, na kulikuwa na taulo, lakini alikuwa wapi yule mtumishi msichana ambaye kazi yake ilikuwa kuwaosha miguu ili kuwaburudisha? Alipaswa kuwa hapa walipowasili!

Naweza kuwazia kwamba lazima alikuwa Petro ambaye angekuwa wa kwanza kusema waziwazi kile ambacho wote walikuwa wakikifikiria. Anafanana nami sana - siku zote akijitia matatani kwa maneno yake! “Yuko wapi yule msichana? Miguu yangu inawashwa. Je, mtu amefanya kosa na kusahau kumwambia? Ni nani aliyepanga karamu hii? Ni nani aliye kwenye kamati?” Mnong’ono wa aibu ungesikika huku wengine wakijaribu kumwambia anyamaze. Kwani, ni Bwana mwenyewe ndiye aliyefanya mipango! Naye hafanyi makosa; hata tunaposhindwa kuelewa makusudi yake.

Yesu akainuka mezani na kuelekea kwenye mabakuli ya maji.

“Vyema,” Petro akawaza, “Anaenda kumwita yule msichana.”

Yesu akavua vazi lake la nje, akajifunga taulo, akachukua bakuli la maji, akageuka… kumwelekea Petro!

“La hasha,” Petro akawaza, “Ataniomba mimi nifanye hivyo!”

Badala yake, Yesu akaiosha miguu yenye vumbi ya Petro na kisha ya wengine wote, pamoja na Yuda Iskariote ambaye angemsaliti na kuleta mateso aliyokuwa akiyatazamia usiku ule. Je, waweza kuwazia Bwana akitazama juu machoni pa Yuda alipokuwa akimwosha miguu? Aliona nini katika macho hayo?

Hofu? Au hatia? Yuda aliona nini katika macho ya bwana wake? Nashangaa, je, aliweza kutazama? Upendo wa namna hiyo!

Yesu akalirudisha bakuli na taulo mahali pake kando ya mlango, akavaa vazi lake la nje, akageuka kuwaelekea wanafunzi.

“Nimewapa kielelezo,” akasema, “kama mimi nilivyowatendea ninyi, nanyi mtende vivyo” (Yohana 13:1-20).

Kipaumbele cha kwanza cha uanafunzi ni utumishi. Tumeagizwa na Bwana kuwa watumishi. Ni jambo la lazima kama tunatamani kuwa kama yeye, aliyekuja si kutumikiwa, bali kutumika (Mathayo 20:28). Ni sharti la ukuu katika Ufalme wa Mbinguni na ushahidi wa kujazwa Roho (Waefeso 5:18,21).

Sidhani kwamba Bwana alikusudia tumfuate kihalisi kwa kuoshana miguu (ingawa hilo ni baraka kubwa kuipata), bali kwamba tunapaswa kutafuta kuburudishana kutoka vumbi na uchafu wa kutembea katika ulimwengu huu. Haiwezekani kuishi katika ulimwengu huu bila baadhi ya uchafu wake kukupaka. Ni mara chache mno mtu aweza kusoma gazeti, kutazama televisheni, au kupiga soga na majirani au wafanyakazi wenzake bila kuambukizwa sumu yake. Kusengenya na kunung’unika, ambako ni kwa kawaida hata miongoni mwa waumini, punde hutunyang’anya furaha ya kutembea katika njia ya Kikristo. Tunahitaji maneno ya kutakasa, kuburudishwa na kutiwa moyo na waumini wenzetu. Tunahitaji kuoshwa miguu yetu! Hicho ndicho kusudi la ushirika wa Kikristo; hata hivyo, mara nyingi kuna ‘uchafu’ mwingi unaotupwa miongoni mwa waumini kama ulivyo miongoni mwa watu wa ulimwengu!

Si kwamba tumeitwa kutumikiana tu katika Mwili wa Kristo, bali pia tunapewa changamoto kuwa watumishi kwa wale ambao hata wangemsaliti Bwana wetu wala si miongoni mwa wafuasi wake.

Yesu aliiosha miguu ya Yuda akijua yote yaliyokuwa moyoni mwake. Aliona mashaka yake na kukata tamaa kwake, alijua hila zake na udanganyifu wake, lakini hakusita kuiosha miguu yake.

Alipomaliza kazi hii aliwaalika wale wote ambao wangemtambua kuwa bwana, wafanye vivyo hivyo.

Kuwa na moyo wa mtumishi si rahisi katika ulimwengu wetu wenye kujifikiria wenyewe. Kunahitaji unyenyekevu - kujijua jinsi mtu alivyo kweli - na kujikubali. Tunapojiona ‘ndani ya Kristo’ hatutishwi na yale ambayo wengine wanaweza kutufikiria. Ni nani ajaliye wengine watasema nini tunapojua kwamba tunampendeza Bwana? Ujasiri wetu u ndani yake na katika ahadi zake.

Yesu alijua utume wake ulikuwa nini, alikotoka, na hatima yake ilikuwa nini (Yohana 13:3). Ujasiri huu ndio uliokuwa msingi wa utumishi wake. Baba alikuwa amempa mamlaka, alikuwa amemtuma ulimwenguni, na angempokea tena.

Sisi tuna utume ule ule na hatima ile ile! Ulimwengu waweza kutuita dhaifu au wanyonge, ukijaribu kuutumia vibaya moyo wetu wa utumishi kwa faida yao wenyewe. Watakuchukua koti lako, watakulazimisha uende nao maili moja, na kukufanya mtumwa wao.

Yesu alituambia, kama hilo litatokea, wape pia shati lako na uende maili ya pili! Kwa kufanya hivyo, unajiondoa katika utumwa wao na kujifanya mtumishi wa kujitolea (Mathayo 5:40-41).

Muda mfupi baada ya Yuda kutoka chumbani kwenda kufanya kazi yake chafu, Yesu aliwafundisha wanafunzi wake takwa la pili. “Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi” (Yohana 13:34-35). Angalia kwamba hii ni amri, si hiari! Je, umewahi kujaribu kupima ni kiasi gani anakupenda? Hicho ndicho kipimo pekee ambacho kwacho atapima ni kiasi gani unavyopendana “ninyi kwa ninyi!”

Ingekuwa jambo lisilowezekana kama isingekuwa kwa ajili ya neema yake na Roho Mtakatifu akaaye ndani ambaye huyatoa.

“Kuishi juu pamoja na wale niwapendao, lo, hiyo itakuwa utukufu! Kuishi hapa chini pamoja na wale niwajuao - basi, hiyo ni hadithi tofauti!”

(Mwandishi Hajulikani).

Huenda tusipendane, lakini tumeamriwa kupendana! Hilo lamaanisha kutokusengenya na kutokusalitiana, bali badala yake kuheshimiana, kupendeleana, kuchukuliana mizigo, na mengi zaidi… Takwa la tatu liliwekwa mbele ya wanafunzi. “Mkinipenda, mtazishika amri zangu” (Yohana 14:15). Anatuita tuwe watiifu kwa neno lake. Nabii wa Agano la Kale, Samweli, alimkemea Mfalme Sauli asiyetii akisema, “Je! Bwana huzipenda sana sadaka za kuteketezwa na dhabihu, kama kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, na kusikia kuliko mafuta ya kondoo waume.

Kwa maana kuasi ni kama dhambi ya uganga, na ukaidi ni kama uovu na kuabudu sanamu. Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme” (1 Samweli 15:22-23).

Kwa sababu Sauli hakulitii neno la Bwana Mungu, alipoteza ufalme wake na mamlaka yake. Yesu alipozungumza na makutano, wale waliomsikia walijawa na mshangao kwa maana alinena kama mwenye mamlaka makuu (Mathayo 7:28-29).

Sisi tunaomtambua kuwa Mwokozi ni lazima pia tukiri kwamba yeye ni Bwana. Analosema lina mamlaka makuu kuliko yote.

Tunahitaji kuwa wepesi kusikia na kuitambua sauti yake siku kwa siku. Alisema kwamba sisi, kondoo wake, twapaswa kuitambua sauti yake. Zaidi ya yote, twapaswa kumsikia akinena nasi kupitia Maandiko na kutii analosema. Waumini wote wanapaswa kuwa wanafunzi wa Neno lililoandikwa, wakiishi kwa kutii maagizo yake.

Matakwa ya Yesu kwa wanafunzi wake ni kwamba tutumikiane, tupendane, na kulitii Neno lake.

Ahadi Zake Mbali na matakwa matatu aliyoyaweka mbele ya wanafunzi wake, Yesu pia aliwaahidi baraka tele. Angekuja tena na kuwapokea kwake mwenyewe akiisha kuwatengenezea mahali “nyumbani mwa Baba yangu” (Yohana 14:2). Wangefanya kazi kubwa kuliko alizozifanya kwa kuwa angewapelekea Msaidizi mwingine, naye angezijibu sala walizoziomba sawasawa na mapenzi yake. Wangepaswa kuijua baraka ya kuwa ndani ya Kristo, na kuupata upendo wa Baba.

Yule Msaidizi, Roho Mtakatifu, angekuja kukaa ndani yao na angewaongoza kwenye kweli na maarifa ya mapenzi ya Mungu; angewakumbusha yote waliyofundishwa na Yesu.

“Msifadhaike mioyoni mwenu; mnamwamini Mungu, niaminini na mimi” (Yohana 14:1).

“Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga” (Yohana 14:27).

“Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe” (Yohana 15:11).

Aliwaahidi wao - na sisi - amani ambayo ulimwengu hauwezi kuitoa wala kuiondoa, furaha ambayo kipimo chake ni ukamilifu, na uwepo ambao si mwingine ila Roho mwenyewe, asiyetuacha kamwe wala kututupa (Kumbukumbu la Torati 31:6).

Je, umeyapata haya katika kutembea kwako na Bwana? Mimi hakika nimeyapata, lakini natamani zaidi!

Kuyapata ahadi hizi kwategemea sisi kuwa watumishi, wapendaji, na watiifu kwa Neno lake.

Ukurasa 1 / 7 · 9 dakika zimebaki katika sura
Ochorus

Kuwawezesha watu vitabu vya Kikristo vya kale — bila malipo, kwa lugha yako.

Chunguza

Dhamira Yetu

Vitabu vya Kikristo vya kale bila malipo mtandaoni — na vitabu vilivyochapishwa tunavyogawa kwenye makongamano, makanisa, shule na magereza kote Afrika Mashariki.

Faragha na Masharti

Huduma tangu 2021 · Victoria BC, Kanada · Kampala, Uganda