Sura 14 · dakika 4 za kusoma

Yesu - Mponyaji

Dhambi za Vizazi Katika miaka yangu ya ushauri nasaha, nimejifunza kwamba vidonda vinavyowazuia wagonjwa wangu katika kuenenda kwao na Bwana, mara nyingi vinatokana na visababishi vya miaka mingi iliyopita. Nyakati nyingine, kuna ushahidi wa mfululizo wa vidonda vinavyofanana kupitia vizazi kadhaa vilivyotangulia. Ni ukweli wa Kimaandiko kwamba, “maovu ya baba yaweza kuwapata wana hata kizazi cha tatu na cha nne” (Kutoka 20:5).

Zaidi ya hayo, kulikuwa na kizuizi cha wana wa uzinifu kuingia katika ushirika kamili na kusanyiko la Bwana “hata kizazi cha kumi” (Kumbukumbu la Torati 23:2)! Haya ni mahukumu ya Agano la Kale yanayoonyesha jinsi dhambi iwezavyo kumwathiri, si mwenye dhambi tu, bali wazao wake wengi. Kwa shukrani, Yesu alikuja ili aiondoe laana ya dhambi na kutuweka huru kutoka katika athari zake, kwa hiyo, hatuna budi kuendelea katika utumwa wa vidonda vya dhambi ya wazazi wetu.

Bwana anataka tuenende tukiwa huru, lakini twawezaje kuwaachilia wale walioleta vidonda ikiwa tayari wamekwisha kufa? Ikiwa hatuwezi kuwaachilia, je, sisi wenyewe twaweza kuachiliwa? Haya ndiyo aina ya maswali ambayo mara nyingi naulizwa wanaoshauriwa wanapotambua vidonda vya zamani na mienendo ya sasa. Hatuamini kwamba kuwaombea wafu kutabadilisha kwa namna yoyote hali yao mbele za Mungu, Hakimu Mkuu, kwa hiyo, kwa masikitiko hatuwezi kuwafungulia ufalme wa mbinguni.

Ijapokuwa hatuwezi kutumia ufunguo wa ufalme uliopewa sisi kwa ajili yao, Bwana bado atatuweka huru kwa uponyaji alionunua Kalvari, kwa sababu “kwa kuchubuliwa kwake sisi tumepona” (Isaya 53:5).

Kumbukumbu Zilizofichika Kila ninapomshauri mtu, sikuzote twaanza kwa kumwomba Roho Mtakatifu aziongoze fikira zetu. Twataka Yeye atufunulie maeneo ya nafsi ambako vidonda vyaweza kupatikana.

Hunishangaza daima (ingawa haipaswi kunishangaza) jinsi mara nyingi kumbukumbu za matukio yaliyosahauliwa siku nyingi zinavyorudi kwa wingi! Wakati mmoja, nilikuwa nikimshauri mwanamke wa makamo aliyekuwa na matatizo fulani ya mahusiano. Alianza kulia kimya kimya bila sababu iliyodhihirika.

Msaidizi wangu, Debbie, alisogea na kumkumbatia, ndipo mwanamke huyo akaanza kulia bila kuzuilika.

Debbie akamweka mapajani mwake na kumkumbatia kama mama amkumbatiavyo mtoto mchanga. Baada ya muda mfupi wa machozi ya hisia kali, mgonjwa akaanza kumpiga Debbie kwa ngumi zake, akipiga kelele “Kwa nini ulifanya hivyo? Kwa nini ulifanya hivyo?”

Alipotulia, alituambia kwamba alikuwa amefikiri anampiga mama yake kwa kutupilia mbali mwanasesere wake wa nguo aliyempenda zaidi alipokuwa na miaka minne tu! Msichana mdogo alikuwa amebeba kidonda hicho kwa zaidi ya miaka 40 ijapokuwa hakuwa amekikumbuka! Kilikuwa kimefukiwa ndani ya fahamu zisizojulikana.

Mara nyingi wagonjwa wamerudi kuniambia juu ya kumbukumbu iliyowajia ghafla ya tukio fulani la kutisha la zamani. Sidhani moja kwa moja kwamba kumbukumbu hizi zote ni sahihi. Kuna hatari kubwa siku hizi kwa sababu watu wengi wanataka kuwalaumu wengine kwa dhambi za wazia za zamani, nao wanataka kujiondolea lawama kwa udhaifu na mienendo ya sasa.

Hilo si kusudi langu katika kuandika kitabu hiki. Nataka kuwaona watu wakichukua jukumu la matendo yao wenyewe, kutumia ufunguo wa ufalme wa Mbinguni, kujiweka huru wenyewe, na kuwaachilia wale ambao wamewaumiza. Wote wawili ni wahasiriwa wa Shetani - wote wawili wahitaji kuwekwa huru. Kulipiziana kamwe hakuleti uhuru, msamaha peke yake ndio uletao!

Yeye Yeye Jana, Leo na Hata Milele Roho Mtakatifu anapofunua vidonda, ni lazima tuchukue muda kukiweka kidonda hicho mbele za Bwana, kwa ajili ya kuguswa kwake kuponyako.

Yeye ni “Alfa na Omega, mwanzo na mwisho” (Ufunuo 1:8). Yeye ni “yeye yule, jana na leo na hata milele” (Waebrania 13:8). Anakijua kidonda chako - alikuwepo kilipotokea - naye alikulilia. Tunapomletea kidonda, pamoja na msamaha kwa yule aliyekisababisha, huanza kuponya na kuirejesha nafsi. Ijapokuwa hatuwezi kumwachilia yule aliyetuumiza, Bwana ni mwaminifu kuponya na kutuachilia sisi.

Barua Baada ya mgonjwa na mimi kuzungumza, nao wametambua maumivu, vidonda, na mienendo, ninawaalika kuandika barua kwa mtu aliyewaumiza wakieleza kidonda walichokitambua na maumivu kilichoyaleta. Ninawatia moyo waeleze hisia na shauku zao.

“Laiti ungelielewa jinsi ulivyoniumiza sana ulipo… Ee jinsi nilivyotamani kukusikia ukiniambia kwamba ulinipenda!”

Barua yaweza kuwa na maelezo mengi sana kwa sababu haitatumwa. Kusudi lake ni kuyaleta juu ya uso hisia zote na maumivu yaliyofichika ndani ya fahamu. Wakati wa msamaha na kuachilia (ikiwezekana) unapofika, barua hii huwa ‘mkataba’ wa msamaha. “Je, u tayari kusamehe kwa yote uliyoyaandika hapa?” ninawauliza. Kisha ninapokuwa na uhakika kwamba wameelewa kikamilifu niliyowafundisha, na kwamba wamesamehe kweli (na kumwachilia) yule aliyewakosea, ninawaalika kuiharibu barua hiyo wakikumbuka mahali na tarehe ya tendo lao. Kisha wanatiwa moyo kuwaombea baraka wale waliowakosea, ikiwa bado wako hai.

Ili kukamilisha kuachiliwa kwao, nimewafahamu watu waliochukua barua hiyo hadi makaburini ya karibu, ambako walinyunyiza majivu yake na kuweka maua juu ya kaburi la aliyeondoka. Kwa wengine, hii imekuwa mara ya kwanza kwao kumwomboleza kweli kifo cha mtu wa jamaa, hata mzazi, nao wamejua kuguswa kwa uponyaji kunakofuata maombolezo ya kweli.

Tendo letu la makusudi la msamaha huvunja nguvu ya Shetani.

Bwana afanyapo kazi yake ya uponyaji katika maisha yetu, twajifunza kuenenda katika nguvu za Roho wake.

Tunapojivika silaha zote za Mungu, adui hukuta kwamba hatuna eneo lolote la udhaifu katika maisha yetu ambalo kwalo aweza kutuzuia katika vita.

Bila shaka, msamaha si tukio la mara moja wala hata ahadi ya mara saba. Kama Yesu alivyomfundisha Petro, ni takwa la “mara sabini mara saba” (Mathayo 18:22). Kwa maneno mengine, twapaswa kuwa na moyo wa kusamehe daima.

Ni lazima sikuzote tuwe wepesi kupatana na wale ambao matendo au maneno yao yaweza kuleta mfarakano kati yetu. Mtu ni lazima atambue kwamba yaweza kuwepo haja halisi ya ‘kupoza hasira,’ lakini hakuwezi kuwa na udhuru kwa uadui unaoendelea.

Na tujitoe kikamilifu katika kutumia ufunguo ulio mikononi mwetu hata tutakapojulikana kuwa ‘wapatanishi,’ wale wanaojulikana kuwa wana wa Mungu (Mathayo 5:9).

Ukurasa 1 / 4 · 4 dakika zimebaki katika sura
Ochorus

Kuwawezesha watu vitabu vya Kikristo vya kale — bila malipo, kwa lugha yako.

Chunguza

Dhamira Yetu

Vitabu vya Kikristo vya kale bila malipo mtandaoni — na vitabu vilivyochapishwa tunavyogawa kwenye makongamano, makanisa, shule na magereza kote Afrika Mashariki.

Faragha na Masharti

Huduma tangu 2021 · Victoria BC, Kanada · Kampala, Uganda