Sura 15 · dakika 7 za kusoma
Kutembea Katika Uponyaji Wako
Kwa namna nyingi, hii ndiyo sura ngumu zaidi kuiandika. Nimefundisha kanuni zilizoelezwa katika sura zilizotangulia kwa makundi mengi tofauti ya watu. Kumekuwepo na vikundi vya vijana na wazee, mikutano ya kanisa yenye taratibu za ibada na ile isiyofuata taratibu hizo, vyuo vya Biblia na vikundi vya nyumbani. Katika karibu vyote, kumekuwepo na mwitikio wa kihisia, watu wengi wakinijia wakilia wakitafuta ushauri.
Ninahuzunika kwa kuwa mara nyingi mimi hupita tu, na siwezi kujitoa kwenye mchakato mrefu wa kutembea katika uponyaji ambao wengi wao wanauhitaji. Ninafahamu kwamba mara nyingi nimekuwa niki‘fungua kidonda’ - kumbukumbu iliyofichwa kwa muda mrefu - ambacho sasa kinahitaji uponyaji.
Wakati mwingine mwitikio wao huwa wa kushtukiza kabisa. Nakumbuka kanisa moja la Kiepiskopali lililojumuisha watu wazima waliokomaa, ambao walipiga makofi wakati mchungaji na mimi tulipokumbatiana tukionyesha upatanisho unaofuata baada ya kufungua. Walikuwa wanajua sana hitaji lao la kumsamehe na kumfungua mchungaji wa zamani wa kanisa hilo, na furaha ya ufahamu wao mpya wa jinsi wangeweza kuondolewa maumivu waliyoyabeba, iliwafanya wapige makofi ya ghafla. Mara moja tuliyainua makofi hayo kama sadaka ya sifa kwa Bwana.
Natumaini kwamba kitabu hiki kitawaamsha wachungaji na washauri wengi kutambua jukumu kubwa tulilonalo la kuleta upatanisho na uponyaji katika mahusiano yaliyovunjika na roho zilizojeruhiwa ambazo zimeenea sana katika makanisa yetu. Natumaini zaidi kwamba waumini wengi watajifunza jinsi ya kutumia funguo zinazofungua ufalme wa Mbinguni kwa ajili ya wapendwa wao, na kujiletea uhuru kutoka kwa vidonda ambavyo wamevibeba kwa muda mrefu mno.
Ni wakati muafaka Shetani awekwe mahali pake na watu wa Mungu waweze kutembea katika ukamilifu na nguvu, badala ya kuchechemea kama wanavyofanya wengi!
Kwa wale ambao huenda wamejitambua kuwa wamejeruhiwa walipokisoma kitabu hiki, ninahitimisha kwa miongozo kadhaa itakayowawezesha ‘kutembea’ katika uponyaji wao wenyewe. Ikiwezekana kupata mshauri mzuri atakayepitia jambo hili pamoja nawe, mwenzi wa aina hiyo angekuwa na thamani kubwa mno. Ningekutia moyo umhimize afahamu vyema kitabu hiki kabla hujaanza.
Mwombe Bwana Aongoze Mawazo Yako Uwe na hakika kwamba Bwana anataka kuponya vidonda vya nafsi yako. Anavijua, lakini amekupa ufunguo wa kuponywa, na anataka uutumie! Hatajibu maombi katika maeneo ya maisha yetu ambako tayari ameshinda ushindi msalabani, na ambako ametukabidhi sisi mamlaka au wajibu.
Usiwe na Haraka Uponyaji mara chache huja kwa haraka. Hadithi nyingi ninazoweza kuzisimulia zinahusu miezi mingi ya ushauri. Huchukua muda kuweza kutembea tena baada ya kidonda kibaya.
Kama vile tiba-mazoezi ilivyo muhimu ikiwa tutatembea tena baada ya ajali mbaya iliyosababisha majeraha ya miguu, ndivyo tiba ya kiroho ilivyo muhimu ili kutembea katika uponyaji wetu baada ya vidonda vya nafsi vya muda mrefu.
Zungumza Kuhusu Maisha Yako Yaliyopita Kwa kawaida mimi humtia moyo yule anayeshauriwa kugawanya maisha yake yaliyopita katika vipindi vifupi vya muda. Kwa mfano, kabla ya shule, shule ya msingi, miaka ya ujana, utu uzima wa mapema, na kadhalika. Ninawachochea kwa maswali kuhusu nyumbani kwao, shule, marafiki, mambo wanayoyapenda, na mambo wanayoyachukia, huku nikitathmini mifumo ya tabia au majeraha. “Yule mtoto mdogo aliye ndani yako alihisije?”
Mwombe Bwana akiguse kila kidonda kadiri kinavyofunuliwa.
Andika Chochote Unachohisi Kina Umuhimu Mimi huwa na kalamu na karatasi tayari ili kuandika mifumo yoyote inayoweza kujitokeza au mawazo yoyote yanayonijia. Katika siku ambazo hakuna mshauri wala rafiki aliye pamoja nawe, utashangaa kadiri kumbukumbu za mambo yaliyosahaulika kwa muda mrefu zinavyokujia, lakini kwa nini ushangae ikiwa tayari umeshamwomba Bwana ashiriki kikamilifu katika mchakato wa uponyaji wako? Andika kumbukumbu hizi.
Tambua Kama Umejeruhiwa na Dhambi ya Mtu Mwingine Usimlaumu mwingine ikiwa dhambi ni yako mwenyewe. Ikiwa umeudhika, ni lazima ulishughulikie jambo hilo kama ilivyoelezwa katika sura ya tisa.
Usikatae kukubali ukweli ikiwa yule aliyekukosea ni mtu unayempenda, na hakika usimtafutie visingizio. Mungu anamwona kama mwenye dhambi, kama vile wewe na mimi - na wenye dhambi hutenda dhambi! Hakuna haja ya kupiga danadana - kiite tu kama kilivyo - dhambi! Huenda ni mwenye dhambi aliyekombolewa, lakini bado ana uwezo wa kukujeruhi.
Mara nyingi, vidonda hivyo vilisababishwa bila kukusudia, lakini ni vidonda halisi, na kama mkosaji asingekuwa mwenye dhambi, visingekuwa vimekuumiza hivyo.
Nilipofikia kuielewa kanuni hii, niliona jinsi ambavyo huenda nilikuwa nimemjeruhi binti yangu mwenyewe kwa kutokujua.
Anne alikuwa hospitalini kwa majuma machache kabla ya kuzaliwa kwa binti yetu wa kwanza, Corinne, kwa hiyo alipoanza uchungu wa kujifungua, mimi nilikuwa nyumbani, bila kujua kilichokuwa kikitokea. Marafiki wawili ndio waliokuwa wa kwanza kuniambia kuhusu uchungu wake wa kujifungua kwa kuwa walikuwa wamepiga simu hospitalini muda mfupi kabla ya kuondoka kwenda likizo. Wafanyakazi wa uuguzi waliwaambia kwamba mtoto amezaliwa, lakini hawakutaka kueleza kwa undani habari za uzazi, hasa jinsia ya mtoto - baba ndiye angekuwa wa kwanza kuarifiwa hivyo. Walinisihi nipige simu hospitalini ili wapate kujua habari hizo kabla ya kuanza likizo yao. Niliwaambia kwamba ningefanya hivyo baada ya kumaliza riwaya ya Agatha Christie niliyokuwa nikiisoma! Bila shaka, nilikuwa nikitania tu, ili niwaweke katika mashaka, na haraka tukaenda pamoja kwenye kibanda cha simu cha umma kusikia habari za kufurahisha kwamba sasa nilikuwa baba wa mtoto mzuri wa kike.
Hata hivyo, hadithi hiyo ilirudiwa mara nyingi kwa marafiki waliokuja kututembelea kwa miaka mingi, na wakati mwingine, mbele ya binti yangu. Sikuwahi kufikiria jinsi alivyokuwa akiisikia hadithi hiyo - kwamba baba hakujali sana wakati alipozaliwa. Labda hakumtaka?
Miaka miwili tu baada ya kukichapisha kitabu hiki kwa mara ya kwanza, nilimwandikia Corinne nikiomba msamaha wake kwa vidonda vilivyosababishwa na kutojali kwangu.
Andika Barua, Ukieleza Waziwazi Maumivu Yako Si lazima kumwonyesha barua hii mtu yeyote, ingawa waweza kuchagua kumwaminisha siri mshauri wako. Hata hivyo, hilo liwe tu ikiwa anaweza kuaminiwa kuweka siri, na unajua kwamba hataruhusu habari zako kuathiri mtazamo wake kwako au kwa yule aliyekujeruhi. Jaribu kuwa kamili na wa haki katika barua hiyo, ukiandika jinsi ulivyohisi ulipojeruhiwa: kukataliwa, kudharauliwa, kuaibishwa, na kadhalika.
Jaribu pia kuongeza mambo yoyote mazuri unayoweza kuyasema.
Kuwa mwenye haki kunaweza kuwa vigumu sana kwa kuwa barua hii inaweza kuchochea hisia kali na maumivu. Kusudi lake ni kukuwezesha kuleta juu hisia ambazo umezizuia kwa miaka mingi.
Bandeji zilizogeuka kuwa vifungo lazima ziondolewe! Usiwe na haraka!
Chagua Kusamehe Tambua kwamba yule aliyekujeruhi ni mwenye dhambi anayetembea gizani. Ni kipofu kuhusu alichokitenda dhidi ya nafsi yako. Adui yako halisi ni Shetani ambaye jeshi lake limekulenga tangu kuzaliwa, na mkosaji wako ni chombo tu, asiyejua hila za Shetani. Mkasirikie Shetani, na umsamehe yule kipofu. Hakikisha uko tayari kusamehe kwa kila jambo lililotajwa katika barua uliyoandika.
Usitegemee Bwana aponye mahali ambako hujajiweka tayari kusamehe.
Chagua Kufungua Kwa nini usitumie sala ya Mtakatifu Stefano? “Baba, usiwahesabie dhambi hizi! Leo, ninachagua kuwafungua kutoka hatia yote.”
Baada ya kusali sala hiyo, ninapendekeza uandike tarehe, ukiihifadhi katika kumbukumbu yako kama vile ungefanya kwa siku ya kuzaliwa.
Ichome Barua Moto!
Jambo hilo limeshughulikiwa - kwa nini uliache likining’inia?
Hii inapaswa kuhifadhiwa katika kumbukumbu yako tu kama siku ambayo ulianza kutembea katika uponyaji wako - siku ya kusherehekea!
Mwombee Yule Aliyekujeruhi Jitoe kusali kila siku ili Mungu ambariki yule aliyekujeruhi. Je, watoto wake wako mbali na Bwana? Waombee. Je, biashara yake iko katika shida? Iombee ifanikiwe. Unapoendelea kusali kwa namna hii, Mungu atafanya kazi kupitia mfereji kati yake Yeye na wao - mfereji ambao uliufungua kwa msamaha na kufungua kwako. Kwa kufanya hivi, utakuwa unajikomboa kutoka utumwa wa vifungo vya kihisia vya vidonda vyako na kuwa mtumishi ambaye Yesu alikuita uwe.
Ikiwa mtu anakukosea kwa kuchukua kanzu yako, anakufanya mtumwa wake, lakini kwa kumpa na joho lako pia, unajifanya mtumishi wake. Ikiwa anakukosea kwa kukulazimisha kwenda mwendo wa maili moja, anakufanya mtumwa wake, lakini kwa kwenda maili mbili, unajifanya mtumishi wake (Mathayo 5:40-41). Ikiwa anajeruhi nafsi yako, unakuwa mtumwa wa kihisia, lakini kwa kumwombea, unakuwa mtumishi wake.
Wito wa kwanza wa uanafunzi ni kuwa mtumishi, kama vile Yesu alivyokuwa kwa ajili yako.
Uwe Tayari kwa Upatanisho Ikiwa kutakuwa na nafasi ya kupatanishwa na yule aliyekujeruhi, usiruhusu wasiwasi au woga ukuzuie.
Kipaumbele cha Bwana si uponyaji tu, unaokubariki wewe, bali ni upatanisho unaombariki Yeye!
Tembea Katika Uponyaji Wako Kila siku, jivike silaha zote za Mungu kama zinavyopatikana katika Waefeso 6:10-18. Ufanye hili kuwa tendo la makusudi, hata ukilitamka unapolifanya. “Ninajivika mkanda wa kweli ili ‘mtu wangu wa ndani’ asijeruhiwe na uongo wa adui. Ninajivika dirii ya haki ili adui asisababishe kamwe moyo wangu ugawanyike katika kujitoa na kumpenda Bwana” na kadhalika. Ni wale tu “wenye moyo safi” watakaomwona Mungu - wale ambao mioyo yao haijachanganyika na takataka za ulimwengu huu (Mathayo 5:8).
Mkabidhi Tabibu Mkuu Kila Kidonda Kama vile adui ajuavyo hakika vidonda vyako vilipo, ndivyo na Bwana ajuavyo. Aliyasikia maumivu yako ulipoumia na anatamani sana uponyaji wako; hata hivyo, amekupa wewe ufunguo.
Unapoanza kuutumia, Yeye yu tayari sana kusaidia katika kutembea kwenye uponyaji. Kama alivyokufunulia vidonda, ndivyo anavyoondoa vifungo na kuleta ukamilifu mahali pake, kwani Yeye ndiye “Tabibu Mkuu,” mponyaji, aliyeyachukua udhaifu wetu na kubeba huzuni zetu, na ambaye kwa kupigwa kwake sisi tumepona (Isaya 53:4-5).
Mwishoni, mshukuru kwa uponyaji wake!