Sura 12 · dakika 10 za kusoma

Ufunguo wa Kuachilia

Sehemu kubwa ya ushauri niutoao ni kuwasaidia watu kukabiliana na makosa waliyotendewa. Ni saa ngapi zingeokolewa kama wangalijua wajibu wao binafsi na kutenda kulingana na kanuni za Kimaandiko!

Mimi naamini kwamba mojawapo ya hila kuu azitumiazo adui kutuzuia katika vita, ni wingi wa saa zitumiwazo na wachungaji (hasa katika Amerika ya Kaskazini) kushughulikia mambo ya ushauri ambayo waumini wangeweza kuyashughulikia wenyewe kama wangelikuwa na bidii zaidi katika kujifunza Neno.

Kazi ya mchungaji inapaswa kuwa ni kuondoa mahitaji mengi ya ushauri miongoni mwa watu wake, kwa kuwafundisha kanuni za Kimaandiko. Ni jukumu lake, kama mchungaji, kuwaongoza hadi ‘malisho mema’ ambako kondoo hujilisha wenyewe; lakini tumefikia mahali ambapo kondoo bado wanahitaji kunyweshwa kwa chupa (kushauriwa), kila mara kunapotokea ‘dharura!’ Shetani amelinyang’anya kanisa wachungaji wake wengi kwa kuwalemea kwa ‘mahitaji’ ya ushauri.

Mfano wa kawaida ni kwamba, tukila na kufanya mazoezi ipasavyo, tutabaki na afya njema; hata hivyo, mtu hutambua kuwa zitakuja nyakati, iwe kwa ajali au ugonjwa sugu, ambapo mtu huhitaji msaada wa mwingine. Palipo na majeraha mabaya na mgonjwa amelemazwa kwa namna fulani, huruma, faraja, na msaada wa mwingine huthaminiwa. Vivyo hivyo ndivyo ilivyo kwa majeraha ya kiroho.

Kuna vitabu vingi vya Kikristo sokoni vinavyoshughulikia majeraha ya nafsi. Vinazungumzia ‘kuponya kumbukumbu’ za familia zenye matatizo na utegemezi wa kupindukia. Vingi vyao ni vizuri sana na vimewasaidia sana watu wanaotafuta mtazamo mpya wa maisha na wa nafsi zao. Mpango wa ‘hatua 12’ wa Alcoholics Anonymous umekuwa msingi wa mafundisho mengi haya, ukiwa na lengo la kumleta mtu aliyejeruhiwa katika hali ya ‘kuendeleza hali.’ Kisha wanaweza kukabiliana na tatizo lao kwa njia ya vitendo, kwa kutumia vikundi vya kutegemezana, ushauri unaoendelea, na mipango iliyowekwa au ‘kanuni’ ya kutenda. Kila siku, wanapata maagizo ya ‘kuutembea’ uponyaji wao. Nimevitumia vitabu hivi na naendelea kuvitumia kwa sehemu. Kinachonisumbua kuhusu vingi vyao ni kwamba ni vichache vinavyotaja athari ya kuachilia iletwayo na msamaha.

Siamini kwamba nia ya Bwana ni kuwaleta watu wake waliojeruhiwa katika hali ya ‘kuendeleza hali’ tu, bali kwamba anataka kuzirejesha nafsi zao, na kuwaletea uponyaji. Kusudi kuu la kitabu hiki ni kufundisha jinsi tuwezavyo kuwekwa huru kutoka utumwa wa majeraha yetu, ili tuwe na ufanisi mkubwa katika vita dhidi ya adui yetu, Shetani. Ufunguo wa uponyaji hupatikana katika msamaha.

Funguo za Ufalme → Mathayo 16:19 Kwa muda wa miaka mitatu wanafunzi walikuwa wametembea pamoja na Bwana katika sehemu za Yudea, Samaria, na Galilaya. Walikuwa wamemwona akifanya miujiza mingi na wamemsikia akiwafundisha makutano, lakini mara chache alikaa chini ili kuzungumza nao tu. Sasa, baada ya kipindi cha shughuli nyingi, anawaongoza mpaka kaskazini mbali mwa nchi, hadi sehemu zilizoizunguka Kaisaria-Filipi, kwenye miteremko ya chini ya Mlima Hermoni. Wakiwa wanatembea, Bwana anawageukia wanafunzi wake na kuwauliza maswali mawili.

Swali la kwanza linahusu maoni ya watu kuhusu Yesu, hali swali la pili linahusu maoni ya wanafunzi kuhusu Yesu.

Baada ya wanafunzi kujibu swali la kwanza, anawageukia tena, na kuuliza, “Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?” (Mathayo 16:15). Je, walikuwa wamefikia kuelewa kwamba Yesu alikuwa zaidi ya mtu mwema tu au mtenda miujiza?

“Simoni Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” Naye Yesu akamjibu, “Heri wewe Simoni Bar-Yona! Kwa maana mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu, wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa funguo za ufalme wa mbinguni, na lo lote utakalolifunga duniani litakuwa limefungwa mbinguni, na lo lote utakalolifungua duniani litakuwa limefunguliwa mbinguni” (Mathayo 16:16-19).

Kwa karne nyingi, Kanisa Katoliki la Roma lilifundisha kwamba huu ndio mamlaka waliopewa mapapa wote, kama warithi wa Petro, kichwa cha kanisa, wa kuwatenga na ushirika wafalme, nchi, na watu wasiounga mkono amri zao, au kutoa maghfira ya dhambi.

Je, isingekuwa jambo la ajabu kama ungekuwa na ufunguo wa ufalme kwa ajili ya wapendwa wako? Kwa ajili ya mwenzi wako wa ndoa? Kwa ajili ya mtoto wako ambaye hajaokoka? Kwa ajili ya wazazi wako? Laiti ungeweza kuwafungulia njia ya uzima wa milele! Basi, naamini tunayo nafasi hiyo!

Ni hakika kwamba wengi wanazuiliwa mbali na furaha ya kuuona na kuuingia ufalme kwa sababu ya kushindwa kwetu kuwa mashahidi tunavyopaswa kuwa. Sehemu kubwa ya kushindwa huko ipo katika mitazamo yetu ya kutosamehe. Wapo wazazi wengi leo ambao huomba, kwa kilio, kwa ajili ya mtoto wao mkaidi, bila kutambua kwamba kutosamehe wanakouhifadhi dhidi ya mtoto huyo ndicho kizuizi kikuu cha Mungu kuyajibu maombi!

Yesu alimaanisha nini kwa sehemu ya mwisho ya mstari ulio hapo juu? Nimepewa maelezo mengi, kuanzia ‘mamlaka’ ya mapapa, hadi ‘ukombozi kutoka kwa pepo wachafu,’ lakini sioni lolote kati ya hayo hapa.

Ni ufafanuzi mzuri wa Maandiko, unapotafakari mstari usiofahamika, kutafuta mistari inayofanana, hasa kutoka kwa mwandishi yule yule. Katika hali hii, hatuhitaji kwenda mbali sana, kwa maana sura mbili tu baadaye, Mathayo anauandika tena.

“Amin, nawaambia, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni” (Mathayo 18:18).

Wakati huu Bwana anazungumza na wanafunzi wote, si Petro peke yake. Ikiwa funguo zilitolewa ili kufungua na kufunga (matumizi ya kawaida ya funguo!), basi zilitolewa kwa wanafunzi wote - wewe na mimi tukiwemo!

Kanuni ya pili ya ufafanuzi mzuri ni kuchunguza muktadha, hivyo tutatafakari kile Bwana alichokuwa akifundisha katika sehemu iliyobaki ya Mathayo 18. Punde tunaona kwamba sura nzima inashughulikia urejesho, upatanisho, na msamaha. Mifano midogo inazungumzia kuwa kama watoto, wasio na hila wala uchungu moyoni - waumini kama hao hawakosei wala kujeruhi, nasi tunapaswa kuwa waangalifu tusiwasababishie kosa wala jeraha.

Jambo la pili ninaloliona ni kwamba ikiwa mtu amejeruhiwa au ameumizwa, na kwa sababu hiyo, anaondoka, mchungaji mwema atawaacha wale wengine ili kumrejesha ‘kondoo’ huyo zizini. Angalia tena, kwamba hadithi hii inahusu ‘kondoo’ si ‘mbuzi.’ Inahusu waumini, si ‘waliopotea.’ Mara ngapi, ‘mtu wa matatizo’ anapoondoka kanisani, tunakung’uta mikono yetu tukisema, “kwaheri ya kuonana!” Takwa la Mungu kwa wachungaji watumishi, na kondoo wengine wote, ni kwamba tutafute urejesho wao, si kutengwa kwao na ushirika.

“Na ndugu yako akikukosa, unapaswa kwenda kwake, kwanza faraghani, ukiwa na kusudi moja tu la kutafuta maelewano na upatanisho” (Mathayo 18:15). Angalia neno “kukosa.” Mara nyingi mno huondoka tunapokwazwa, jambo ambalo, kwa upande wake, huzalisha kosa kubwa zaidi. Hatuna agizo kama hilo la kwenda kwao tunapokwazwa - ila tu tunapotendewa dhambi. Isipokuwa peke yake ingekuwa, pale mchungaji wa kanisa au wazee wanapoona ni lazima kumwendea mtu ambaye wanaamini kwamba mara kwa mara ni chanzo cha kukwaza, au ambaye amewatenda wengine dhambi. Katika hali hiyo, kusudi la kumwendea daima ni kwa ajili ya upatanisho.

Wakati Yesu anatoa fundisho la Mathayo 18:18-20, swali linamjia Petro akimwuliza Bwana ni mara ngapi anapaswa kusamehe. “Hata mara saba?” (Mathayo 18:22). Yamkini Petro alidhani swali lake lingekuwa zuri, lakini Bwana aliitumia kusisitiza kwamba msamaha unapaswa kuwa usio na kikomo.

Upendo hudai kwamba tusamehe daima.

Muktadha wote wa sura ya 18 unahusu urejesho, upatanisho, na msamaha, yote bila wewe mwenyewe kusababisha kosa… ndiyo dhamira ya kitabu hiki!

Yohana 20:23 Mstari huu ni mstari mwingine unaofanana na ile miwili iliyo hapo juu, ingawa umeandikwa na Yohana katika Yohana 20:23.

Katika mstari huu, wanafunzi wote wako ndani ya chumba kilichofungwa kwa sababu wanaogopa kwamba viongozi wa Kiyahudi wangekuja punde kuwakamata, kama vile walivyokuwa wamemkamata Bwana wao. Hisia zao zimepanda juu, na baadhi yao waliokuwepo walidai kwamba wamemwona Bwana, amefufuka kutoka kwa wafu! Habari ilikuwa ikienea kwamba Yesu alikuwa amemtokea Petro na Mariamu Magdalene pamoja na wengine wawili njiani kwenda Emau. Wengine hawakutaka kuamini isipokuwa nao wamwone Bwana aliyefufuka.

Ghafula, ingawa milango ilikuwa imefungwa, Yesu alisimama katikati yao! Akasema, “Amani iwe kwenu! Kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka ninyi… Pokeeni Roho Mtakatifu” (Yohana 20:21-22).

Kauli ya Kiyunani ya “pokeeni,” ni kauli ya amri ya aoristi ambayo daima hudai jibu la papo hapo. Wakati ule, wanafunzi walipokea uzima wao mpya katika Roho. Kisha baadaye, siku ya Pentekoste, wangepokea ukamilifu wake ili kuwatia nguvu kwa ajili ya huduma. Walikuwa wamepewa mamlaka mpya! “Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa” (Yohana 20:23). Niruhusu nifafanue, “Wale unaowafungua (kuwaweka huru) wamefunguliwa; wale unaowafunga, wamefungwa.”

“Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu?” (Marko 2:7) waliuliza Mafarisayo. Kwa namna fulani, walikuwa sahihi kwa sababu mamlaka aliyotupa Bwana hayasamehi dhambi kwa kipimo kile kile kama msamaha wake. Anaposamehe ni “kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, hata vilindi vya bahari, zisikumbukwe tena kamwe” (Zaburi 103:12). Wewe na mimi hatuwezi kufanya hivyo - kwa dhambi zetu wenyewe, sembuse za mtu mwingine. Dhambi pekee tuwezazo ‘kusamehe’ ni zile tulizotendewa sisi wenyewe - dhambi ambazo yamkini ndizo zilizosababisha majeraha ya nafsi tuyabebayo, ambayo kwayo Shetani ametuzuia.

Kuondoa Kizuizi cha Dhambi Nikikutenda dhambi wewe, ninamtenda dhambi Mungu pia. Mara moja, kizuizi kinajitokeza kati yangu na Bwana wangu. Naona ni vigumu zaidi kuomba, Neno linapoteza mvuto wake, na ushirika si mtamu sana - dhambi yangu imekuwa wingu juu ya kichwa changu!

Kuna njia mbili ambazo kwazo ‘wingu’ hilo laweza kuondolewa.

Kwanza, ni “kuiungama dhambi yangu, [kwa sababu] Yeye ni mwaminifu na wa haki hata aniondolee dhambi yangu, na kunisafisha na udhalimu wote!” (1 Yohana 1:9). Haleluya! Nimeliona ahadi hiyo kuwa ya kweli.

Hata hivyo, nimegundua pia kwamba Bwana ana ‘tabia’ hii ndogo ya kuzungumza nami kuhusu ile dhambi. Baada ya kunisamehe, kisha ananong’oneza nafsi yangu, “Sasa, nenda kwa ndugu yako ili naye akusamehe. Sitamani tu kukusafisha na dhambi, bali nataka kukuona umepatanishwa.” Kipaumbele chake si msamaha - ni upatanisho! Kuungama hakukamiliki isipokuwa kuleta upatanisho. Hilo si jukumu lake - ni langu, kwa maana “Kristo alitupatanisha sisi na nafsi yake na kutupa huduma ya upatanisho” (2 Wakorintho 5:18-19).

Njia ya pili ambayo kwayo ‘wingu’ langu laweza kuondolewa, ili mbingu ifunguliwe kwangu tena, ni ikiwa wewe unaliondoa kwa msamaha wako. Tafsiri ya King James ya Biblia hutumia neno la pekee katika tafsiri yake ya Yohana 20:23, isemayo, “Kila mtu mtakayemwondolea dhambi zake…” Neno “kuondolea” linazungumzia ‘kuweka kando.’ Waweza kuiondoa dhambi yangu, iliyotendwa dhidi yako, na kwa kufanya hivyo, kunifungulia mbingu. Unapoiweka ‘kando’ dhambi yangu, unaliondoa ‘wingu’ mbali, na njia inafunguka ili Baba anene nami kama vile nilipoutafuta msamaha wake kwa ajili yangu mwenyewe. Atatenda tena juu ya moyo wangu, ili kuleta upatanisho wetu!

Waweza kuchagua kunisamehe kwa sababu wajua Maandiko yanadai hivyo, lakini ni muhimu ikiwa tutapatanishwa, kwamba pia unifungue kutoka hukumu ya Mungu iliyo juu yangu kwa kutafuta kuweka kando ‘wingu’ la dhambi lililo juu yangu.

Mimi daima nazungumzia “msamaha na kuachilia” - lazima vihubiriwe pamoja! Mfano mzuri ungekuwa Stefano, shahidi wa kwanza. Alikuwa amekwisha teuliwa kuwa kiongozi katika kanisa la kwanza wakati viongozi wa Kiyahudi walipomchukua na kumpiga mawe hata kufa. Sauli wa Tarso alisimama karibu, akikubaliana kwa moyo wote na matendo yao, kwa maana alikuwa na chuki kubwa dhidi ya hawa wafuasi wa Yesu.

Stefano alipokuwa akifa, alilia kwa sauti kuu, “Bwana, usiwahesabie dhambi hii!” (Matendo 7:60). Hakuomba kwa ajili yake mwenyewe kwa ajili ya ujasiri, nguvu, wala hata kuachiliwa, bali, aliwaachilia kutoka hatia yao.

Najiuliza, je, Sauli angaliwahi kuwa mtume mkuu Paulo, kama Stefano asingaliomba ombi lile? Ni imani yangu kwamba yeye ‘aliifungua Mbingu’ kwa ajili ya Sauli! Yesu naye aliomba ombi kama hilo alipolia, “Baba, uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo” (Luka 23:34) alipokufa kwa ajili yako na yangu.

Tokeo moja la ajabu la kuwaachilia wengine ni kwamba nasi twaachiliwa pia! Ni kama kuwa na farasi mwishoni mwa kamba - twaweza kusema kwamba farasi amefungwa anapokimbia kutuzunguka uwanjani; hata hivyo, farasi akiamua kukimbia mbio kuvuka shamba lenye matope, tutaburutwa kupitia matope isipokuwa tuiache kamba!

Ile fundo uhisiyo tumboni mwako baada ya mtu kukutenda dhambi, ni kama ile kamba tu. Umefungwa kihisia kwa wale waliokuumiza. Maumivu hayo ni sehemu ya jeraha waliolisababisha. Ingawa umewasamehe, fundo lipo kila unapokutana nao au kumsikia mtu akizungumza juu yao.

Wewe, na wao, mnahitaji kuachiliwa!

Yesu Katikati Ni jambo la kusikitisha jinsi Mathayo 18:18-20 inavyonukuliwa nje ya muktadha mara nyingi! Mistari hii inarejelea msamaha, kuachilia, na upatanisho, si uwepo wa Mungu wakati watu wengi wanapokusanyika pamoja! Ahadi za Yesu zilizotolewa pale, ni kwa ajili ya wale wanaotafuta kwa bidii kupatanishwa.

“Tena nawaambia, ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo kati yao” (Mathayo 18:19-10). Msisitizo hapa si uwepo wake, kwa maana yu pamoja nasi sikuzote sisi tulio waumini, bali baraka yake kwa ajili ya upatanisho - kipaumbele chake!

Tumepewa ufunguo ambao utaifungua Mbingu kwa ajili ya wengine na ambao utatuweka huru kutoka majeraha, vifungo walivyovisababisha katika nafsi zetu! Na tujifunze jinsi ya kuutumia ufunguo huo!

Ukurasa 1 / 8 · 10 dakika zimebaki katika sura
Ochorus

Kuwawezesha watu vitabu vya Kikristo vya kale — bila malipo, kwa lugha yako.

Chunguza

Dhamira Yetu

Vitabu vya Kikristo vya kale bila malipo mtandaoni — na vitabu vilivyochapishwa tunavyogawa kwenye makongamano, makanisa, shule na magereza kote Afrika Mashariki.

Faragha na Masharti

Huduma tangu 2021 · Victoria BC, Kanada · Kampala, Uganda