Sura 11 · dakika 6 za kusoma
Mwitikio Wetu
Kipaumbele cha Mungu ni Kipaumbele cha Shetani!
Tunaweza kuwa na uhakika juu ya jambo hili! Yoyote yawe makusudi ya Mungu kwa wanadamu, Shetani atafanya kila awezalo kuizuia kazi hiyo. Ikiwa ni matakwa ya Bwana kwamba waaminio waishi katika umoja, adui hufanya bidii sana kuuzuia umoja huo.
Tunapoichunguza Biblia ni dhahiri kabisa kwamba mahusiano yako juu katika orodha ya vipaumbele vya Mungu. Alituumba kwa ajili yake mwenyewe, na kwa ajili ya mmoja na mwenzake. Tangu mwanzo hadi mwisho, Biblia inasisitiza uhusiano: mtu na Mungu, na mtu na mtu.
Katika Mwanzo, Mungu alimuumba mtu kwa mfano wake mwenyewe - ili wapate kuwa na ushirika pamoja (1 Yohana 1:3). Kisha kwa ajili ya huyo mtu, akamuumba mwanamke, kwa sababu “si vema mtu awe peke yake” (Mwanzo 2:18).
Baadaye, akamchagua mtu mmoja ambaye kutoka kwake lingetokea taifa la pekee. Akajiita mwenyewe, “Mungu wa Abrahamu, Isaka, na Yakobo,” akiwa Baba na mume kwa wazao wao.
Shetani alifanya kila alichoweza kuyavunja mahusiano haya, kwa msaada mkubwa kutoka kwa wanadamu wenyewe! Ujue kwamba hata leo bado anafanya kazi kwa juhudi kubwa kuwavuta watu wamwache Mungu, kuzivunja familia, na kuwaangamiza Wayahudi.
Agano la Kale linamalizika kwa ahadi ya ajabu kuhusu mahusiano, “Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao; ili nisije nikaipiga nchi kwa laana ya uharibifu kabisa” (Malaki 4:6).
Msisitizo wa Agano Jipya ni uleule kama ule wa Agano la Kale, pamoja na wajibu wa ziada kwa waaminio wa kuwa katika umoja kama msingi wa ushuhuda wao.
Sehemu kubwa za Agano Jipya zinasisitiza kweli hii, zikiishia kwa mwaliko wa sura ya mwisho, “Na Roho na Bibi-arusi wasema, Njoo!” (Ufunuo 22:17). “Bibi-arusi,” kama vile “Mwili,” ni neno la uhusiano!
Majeraha Yanayovuruga Maisha Ikiwa Bwana angependa kumkomaza mwanamume au mwanamke awe shujaa hodari mwenye ufanisi katika vita dhidi ya uovu, adui atajaribu ‘kumlemaza’ askari huyo hata kabla hajajiunga na jeshi akiwa mwanafunzi wa kijeshi.
Shetani hajui yote, na kwa hiyo, hayajui maisha yako yajayo. Wala hayupo mahali pote, kushindana nawe kila dakika, hivyo ni lazima atumie mbinu za ‘vita vya msituni’ katika mapambano, huku askari wake (mapepo) wakitumia sera ya ‘kupata au kukosa.’ ‘Ushindi’ wa wazi unaonekana katika idadi kubwa ya watu wanaohesabiwa kuwa wanatoka katika familia ‘zilizovurugika.’
Washauri, wa kilimwengu na wa Kikristo pia, hutumia saa nyingi kujaribu kuwafundisha watu jinsi ya kukabiliana na majeraha yao - uvurugikaji wao. Wanatumaini kuwaleta wagonjwa wao mahali pa ‘kujiendeleza’ ambapo hujifunza kutumia kwa ufanisi ‘magongo’ wanayopewa na washauri. Kwa mfano, lengo la Alcoholics Anonymous ni kuwawezesha wanachama wao kudumisha hali ya kutokunywa pombe badala ya kuwaleta katika uponyaji.
Kwa kusikitisha, washauri wengi wa Kikristo wamezikubali mbinu na nyenzo za kilimwengu katika kushughulikia majeraha haya, mara chache wakiwaleta watu wao mahali pa uponyaji ambapo Yesu aliupata msalabani. “Kwa kupigwa kwake sisi tumepona” (Isaya 53:5).
Hila za Shetani huwajeruhi wengi ambao hawataingia kamwe katika jeshi la kupambana naye, kwa kuwa hawatajipatia kamwe wokovu waliopewa katika Kristo. Lakini, mtu anapotambuliwa kuwa yumo ndani ya Mwili wa Kristo, ndipo Shetani hukaza nguvu zake juu ya mtu huyo, hasa ikiwa ataanza kumshambulia.
Huduma ya Upatanisho Yesu alikuja kuishinda nguvu ya Shetani katika maisha ya wanadamu. Ndani yake, uhusiano wetu mpya unapaswa kudhihirika katika umoja wetu kama waaminio: kama Mwili mmoja. Shetani hana nguvu ya kuuharibu umoja huu wala mahusiano haya, lakini kwa njia ya ujinga, hali ya kimwili, na majeraha yenye kudhuru ya nafsi zetu, tumempa ngome.
Tunaweza kufanya nini kurekebisha hali hii? Bila shaka, tunaweza kuomba! Maana, bila msaada na uongozi wa Roho Mtakatifu, hatuwezi kufanya lolote! Lakini, ni lazima tutambue kwamba Baba mara chache atayajibu maombi katika maeneo yale ambayo tayari ametukabidhi sisi mamlaka na wajibu. Wajibu wa upatanisho kati ya watu, si wake tena, ni wetu. “Lakini vyote pia vyatoka kwa Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho; yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho” (2 Wakorintho 5:18-19).
Tunahitaji kuyashughulikia makosa yetu, kutafuta kuyaelewa ‘majeraha’ yetu, na kutumia kanuni za Kibiblia ili kupata uponyaji, kurejeshwa, na upatanisho. Ikiwa umejeruhiwa, natumaini kwamba sehemu hii ya kitabu itakupa msaada fulani wa kukuleta mahali pa ukamilifu ndani ya Kristo, ukijua kama Daudi alivyojua, kwamba “Hurejesha nafsi yangu” (Zaburi 23:3) na kwamba wale, “ambao Mwana akiwaweka huru, wako huru kweli kweli” (Yohana 8:36).
Kondoo Aliyekwazwa Kwa wale ambao ni washauri, wazee, au wachungaji, ningewasihi kwamba hii ndiyo huduma yenu. Fungu la Maandiko linalonichokoza sana nikiwa mchungaji na mshauri linapatikana katika Mathayo 18. Muktadha wote wa sura hii unahusu kukwazwa, kurejeshwa, upatanisho, na msamaha.
Ninachokozwa hasa na masimulizi ya Mathayo kuhusu mfano wa mchungaji na kondoo mia moja ambapo imeandikwa, “Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akapotea, je! Hataziacha zile tisini na kenda mlimani, akaenda kumtafuta yule aliyepotea? Hata akikutana naye, amin, nawaambia, afurahi kwa ajili yake kuliko kwa ajili ya wale tisini na kenda wasiopotea” (Mathayo 18:12-14).
Ni kondoo aliyeondoka zizini, si mbuzi. Katika Agano Jipya, waaminio kwa kawaida hurejewa kama “kondoo” ilhali neno “mbuzi” hutumiwa kwa wasioamini.
Picha hii ni ya muumini ambaye amekwazwa, na ametoka nje ya kanisa, huenda akiwa na sumu kidogo iliyo tayari kusambaa kwa yeyote atakayemsikiliza. Sisi sote tumeliona jambo hili likitokea katika makutaniko yetu na mara nyingi tunashawishika kupigana vikofi tukisema, “Ni afadhali ameondoka! Alikuwa mtu wa kuudhi kweli!” Badala yake, tunahimizwa kumfuata kondoo huyo, tukitafuta kumuelewa na kumhudumia bila kumhukumu, tukiamini kwamba Bwana ataleta upatanisho na kurejeshwa. Kama tungefanya hivyo, labda tungekuwa na ‘watu wa kuudhi’ wachache zaidi katika kanisa letu!
Wakati mwingine kondoo huondoka akihisi amejeruhiwa vibaya sana. Namkumbuka msichana mmoja aliyekuja kwangu, akiwa ameumizwa sana kwa sababu viongozi wa ‘huduma’ yake walikuwa wamemwadhibu, wakiwa wamepokea taarifa mbaya kadhaa kumhusu; lakini, hakuna aliyekuwa tayari kumwambia taarifa hizo zilisema nini. Nilikwenda kuwaona viongozi wake nikaambiwa na mkuu wa waamuzi wake kwamba walikuwa “wanamwacha achemke katika juisi yake mwenyewe ili kumfundisha somo.” Nikamwambia kiongozi huyo, aliyejiona kuwa mchungaji, kwamba hatuna ruhusa ya kumtendea kondoo namna hiyo.
“Kondoo akinaswa katika kichaka cha miiba, ni lazima nitambae ndani ili nimweke huru, hata ingawa naweza kuchanwa na miiba na huenda kuumwa na kondoo aliyeumia. Kisha namimina mafuta na divai na kuyafunga majeraha, kabla ya kumwachilia kondoo huku nikimuonya asiingie tena katika kichaka cha miiba. Nikisikia tena mlio na kumwona kondoo katika kichaka kingine baada ya muda kidogo, narudia zoezi hilo. Hili linaendelea kwa maonyo zaidi na huenda kutumia kamba, lakini kamwe siwezi kusimama nje ya kichaka, nikitikisa kidole changu nikisema, ‘Umestahili!
Chemka katika juisi yako mwenyewe!’ Mchungaji Mkuu hakunipa ruhusa kama hiyo aliponiita nitumike nikiwa mchungaji msaidizi!”
Msichana huyo alifukuzwa kutoka katika huduma hiyo, ingawa nilikuwa nimewaonyesha viongozi wake waziwazi kwamba taarifa dhidi yake zilijengwa juu ya uongo! Haishangazi kwamba alijeruhiwa vibaya sana na akahitaji ushauri wa kitaalamu wa muda mrefu!