Sura 35 · dakika 5 za kusoma
Nguvu ya Maombezi
Ndipo Delila akamwambia Samsoni, “Tafadhali, uniambie nguvu zako nyingi zakaa wapi, na jinsi uwezavyo kufungwa upate kuteswa. “Waamuzi 16:6.
Ni swali ambalo tungependa lijibiwe kuhusu watu ambao zamani za kale, na katika nyakati za baadaye, kama waombezi kwa ajili ya wengine, wamekuwa na nguvu kwa Mungu, na wameshinda. Zaidi ya mmoja, ambaye ametamani kujitoa kwa huduma hii, ameshangaa ya kuwa ameiona ni vigumu hivyo kuifurahia, kudumu ndani yake, na kushinda. Na tujifunze maisha ya viongozi na mashujaa wa ulimwengu wa maombi; huenda baadhi ya vipengele vya mafanikio yao vitagunduliwa nasi.
Mwombezi wa kweli ni mtu ajuaye ya kuwa Mungu anamjua na ya kuwa moyo wake na maisha yake vimetolewa kabisa kwa Mungu na Utukufu wake. Hii ndiyo sharti pekee ambalo kwalo mgeni katika baraza la mfalme wa duniani angeweza kutarajia kutumia ushawishi mkubwa. Musa, Eliya, Danieli, na Paulo huthibitisha ya kuwa ni hivyo katika ulimwengu wa kiroho. Bwana wetu aliyebarikiwa ni yeye mwenyewe uthibitisho wake. Hakutuokoa kwa maombezi, bali kwa kujitoa sadaka. Nguvu yake ya maombezi ina shina lake katika dhabihu yake: hudai na kupokea kile ambacho dhabihu ilikishinda. Kama tunavyoiona iliyowekwa waziwazi hivyo katika maneno ya mwisho ya Isaya 53: “Alimwaga nafsi yake hata kufa, akahesabiwa pamoja na hao wakosao; walakini alichukua dhambi za watu wengi, na” jifunze hili kwa kuunganisha na sura nzima ambayo hili ni taji yake “akawaombea wakosao.” Kwanza alijitoa mwenyewe kwa mapenzi ya Mungu.
Hapo alishinda nguvu ya kuathiri na kuongoza mapenzi hayo. Alijitoa mwenyewe kwa ajili ya wenye dhambi katika upendo uteketezao wote, na hivyo akashinda nguvu ya kuwaombea. Hakuna njia nyingine kwa ajili yetu. Ni mtu atafutaye kuingia binafsi katika mauti pamoja na Kristo, na kujitoa kabisa kwa Mungu na wanadamu, ndiye atakayethubutu kuwa hodari kama Musa au Eliya, ndiye atakayedumu kama Danieli au Paulo. Kujitoa na utii kwa moyo wote kwa Mungu ndizo alama za kwanza za mwombezi.
Walalamika ya kuwa hujihisi uweza kuomba na kuuliza jinsi uwezavyo kufanywa ufae kufanya hivyo. Wanena mengi juu ya udhaifu wa imani yako katika Mungu na upendo kwa roho, na furaha katika maombi. Mtu atakayekuwa na nguvu katika maombezi ni lazima aache malalamiko haya — ni lazima ajue ya kuwa ana asili iliyowekwa kikamilifu kwa kazi hiyo. Mti wa mtofaa hutarajiwa kuzaa tofaa tu kwa sababu una asili ya mtofaa ndani yake.
“Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema.” Jicho liliumbwa ili kuona: ni kwa uzuri ulioje limewekwa kufaa kazi yake! Umeumbwa katika Kristo ili kuomba.
Ni asili yako yenyewe kama mtoto wa Mungu; Roho ametumwa katika moyo wako — kufanya nini? Kulia Aba Baba, kuvuta moyo wako juu katika maombi kama ya mtoto. Roho Mtakatifu huomba ndani yetu kwa kuugua kusikoweza kutamkwa, kwa nguvu ya Kimungu ambayo nia zetu na hisia zetu haziwezi kuielewa. Jifunze, kama utakuwa mwombezi, kumpa Roho Mtakatifu heshima kubwa zaidi kuliko ifanywavyo kwa kawaida. Amini ya kuwa anaomba ndani yako, na kisha uwe na nguvu na moyo wa ushujaa. Uombapo, tulia mbele za Mungu ili kuamini na kujitoa kwa nguvu hii ya ajabu ya maombi iliyo ndani yako.
Lakini kuna dhambi na kasoro nyingi hivyo katika fahamu zetu katika maombi yetu? Ni kweli, lakini je, hukujifunza maana ya kuomba katika jina la Kristo?
Je, jina halimaanishi nguvu iliyo hai? Je, hujui ya kuwa uu ndani ya Kristo naye ndani yako? Ya kuwa maisha yako yote yamefichwa na kufungwa ndani yake? Na maisha yake yote yamefichwa na kutenda kazi ndani yako? Mtu atakayeombea kwa nguvu ni lazima awe dhahiri sana ya kuwa si katika wazo na hesabu tu, bali katika hali halisi kabisa, iliyo hai, ya Kimungu, Kristo na yeye ni mmoja katika kazi ya maombezi. Hutokea mbele za Mungu akiwa amevikwa jina na asili, haki na ustahili, sura na roho na uzima wa Kristo. Usitumie muda wako mkuu katika maombi kurudia-rudia ombi lako, bali kwa unyenyekevu, kwa utulivu, na kwa uthabiti ukidai nafasi yako ndani ya Kristo, muungano wako mkamilifu naye, na njia yako ya kumfikia Mungu ndani yake. Ni mtu ajaye kwa Mungu ndani ya Kristo, akimletea Baba Kristo yule anayependezwa naye, kama uzima wake na sheria yake na tumaini lake pekee, ndiye atakayekuwa na nguvu ya kuombea.
Maombezi ni kwa hakika kazi ya imani. Si imani ijaribuyo tu kuamini ya kuwa ombi litasikiwa, bali imani iliyo nyumbani katikati ya hali halisi za mbinguni. Imani isiyohangaishwa na ubatili wake na udhaifu wake, kwa sababu inaishi ndani ya Kristo. Imani isiyoyafanya matumaini yake kutegemea juu ya hisia zake, bali juu ya uaminifu wa Mungu Watatu-Mmoja, katika kile ambacho kila nafsi imejitwika kufanya katika maombi. Imani iliyoushinda ulimwengu, na kutoa dhabihu kile kinachoonekana ili kuwa huru kabisa kwa ajili ya vya kiroho na vya mbinguni, na kutoa dhabihu vya muda ili kumiliki vya milele. Imani ijuayo ya kuwa imesikiwa na yapokea kile iombacho, na kwa hiyo kwa utulivu na kwa makusudi hudumu katika dua yake mpaka jibu lije. Mwombezi wa kweli ni lazima awe mtu wa imani.
Mwombezi ni lazima awe mjumbe — yeye ajiwekaye tayari, ambaye kwa bidii hujitoa binafsi kupokea jibu na kuligawa. Kuomba na kufanya kazi huenda pamoja. Mfikiri Musa — ujasiri wake katika kumsihi Mungu kwa ajili ya watu haukuwa mkuu zaidi ya kuwasihi watu kwa ajili ya Mungu. Twaona vivyo hivyo katika Eliya — dharura ya maombi yake sirini yalingana na wivu wake kwa ajili ya Mungu hadharani, alipoishuhudia dhambi ya taifa.
Na maombezi yaandamane daima, si sana kwa kazi ya bidii zaidi, bali kwa kumngoja Mungu kwa upole na unyenyekevu ili kupokea neema yake na roho yake, na kujua kwa hakika zaidi tuutende nini na jinsi gani atakavyo tuutende.
Ni jambo moja, ni jambo kubwa, kuanza kuichukua kazi ya maombezi — kuzivuta chini duniani baraka ambazo mbingu inazo kwa ajili ya kila hitaji lake. Ni jambo kubwa zaidi kama mwombezi kupokea binafsi baraka hiyo, na kutoka mbele za uso wa Mungu, ukijua ya kuwa tumepata kitu ambacho twaweza kukitoa. Mungu na atufanye sote kuwa waombezi wa moyo wote, wenye kuamini, wachukuao baraka.