Sura 31 · dakika 7 za kusoma
Utatu Mtakatifu
Kwa sababu hii naipiga magoti yangu mbele za Baba, ambaye kwa jina lake jamaa yote ya mbinguni na ya duniani inaitwa, apate kuwajalia, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani; Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani; mkiwa na shina na msingi katika upendo; ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wa Kristo upitao ufahamu; mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu. Basi yeye aliye na uweza wa kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu, yeye na atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina. Waefeso 3: 14-21.
Maneno haya mara nyingi, na si bila sababu njema, yamehesabiwa kuwa mojawapo ya semi za juu kabisa za yale ambayo maisha ya mwamini yaweza kuwa duniani. Na hata hivyo mtazamo huu si bila hatari zake kama unakuza wazo la kuwa kufikia uzoefu kama huo yapaswa kuhesabiwa kama jambo la kipekee na lililo mbali, na kunaficha kweli iliyobarikiwa ya kuwa, ijapokuwa kwa kiwango kinachotofautiana, hata hivyo umekusudiwa kuwa urithi wa hakika na wa papo hapo wa kila mtoto wa Mungu.
Kila asubuhi kila mwamini ana haki kama alivyo na hitaji la kusema: Baba yangu atanitia nguvu leo kwa uweza, ananitia nguvu hata sasa, katika utu wa ndani kwa njia ya Roho wake.
Kila siku twapaswa kutosheka na kisicho pungufu ya Kristo kukaa ndani yetu kwa imani, maisha yenye shina katika upendo na kufanywa imara ili kuujua upendo wa Kristo. Kila siku twaamini ya kuwa kazi iliyobarikiwa ya kujazwa kwa utimilifu wote wa Mungu inaandaliwa na kuendeshwa na kutimizwa ndani yetu. Na kila siku yatupasa kuwa imara katika imani ya nguvu ya Mungu, na kwa kumpa yeye utukufu katika Kristo, kama awezaye kufanya juu ya tuyaombayo na tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu ya Roho itendayo kazi ndani yetu.
Maneno haya, miongoni mwa mambo mengine mengi, ni ya ajabu kwa jinsi yanavyowasilisha kweli ya Utatu Mtakatifu katika uhusiano wake na maisha yetu ya vitendo. Wakristo wengi hufahamu ya kuwa ni sawa na ni lazima nyakati mbalimbali katika kufuata maisha ya Kikristo, kuzipa uangalifu wa pekee zile Nafsi tatu za Utatu Uliobarikiwa. Mara nyingi huhisi ni vigumu kuunganisha kweli mbalimbali kuwa moja, na kujua jinsi ya kuwaabudu Watatu walio Mmoja.
Andiko letu hufunua uhusiano wa ajabu na umoja mkamilifu. Tunaye Roho ndani yetu kama nguvu ya Mungu, na hata hivyo hatendi kwa mapenzi yetu wala yake mwenyewe. Ni Baba ambaye, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, hutujalia kufanywa imara "kwa Roho katika utu wa ndani.”
Ni Baba afanyaye mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo "kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu" Kwa kiasi hicho, mbali na kuwepo kwa Roho ndani yetu kuwa kwetu badala ya Mungu, hutufanya kuwa tegemezi kabisa na bila kukoma kwa Baba ili atende kazi kwa njia yake. Roho aweza tu kutenda kadiri Baba atendavyo kazi kwa njia yake. Twahitaji kuunganisha kweli hizi mbili — fahamu iliyo ya heshima kuu na ya tumaini ya Roho Mtakatifu akaaye ndani, pamoja na kumngoja Baba daima na kwa kutegemea ili atende kazi kwa njia yake.
Vivyo hivyo na Kristo. Twampigia magoti Mungu kama Baba katika jina la Mwana. Twamwomba atutie nguvu kwa njia ya Roho kwa lengo lile moja ili Kristo akae mioyoni mwetu. Hivyo Mwana huongoza kwa Baba naye Baba tena humfunua Mwana ndani yetu. Na kisha, tena, kadiri Mwana akaavyo moyoni, nao ukiwa na shina na msingi katika upendo, ukivuta uzima wake katika upendo wa Kimungu kama udongo wake, ukizaa matunda na kufanya matendo ya upendo, twaongozwa mbele hata kujazwa utimilifu wote wa Mungu. Moyo mzima pamoja na maisha ya ndani na ya nje huwa uwanja wa ubadilishano uliobarikiwa wa kazi ya Watatu Watakatifu. Kadiri mioyo yetu iaminivyo hili twampa utukufu kwa njia ya Kristo yeye awezaye kufanya zaidi ya tuwezavyo kuwaza kwa Roho wake Mtakatifu.
Ni wokovu wa ajabu jinsi gani huu ambao moyo wetu ndio uwanja wake; Baba akipuliza Roho wake ndani yetu daima, na kwa kufanya kwake upya kwa kila siku akiufanya kuwa makao ya Kristo; Roho Mtakatifu akimfunua na kumfanyiza Kristo ndani yetu daima, hata asili yake yenyewe, tabia, na sifa vikawa vyetu; Mwana akitoa uzima wake wa upendo, na kutuongoza mbele hata kujazwa utimilifu wote wa Mungu.
Hii imekusudiwa kuwa dini yetu ya kila siku. Ee! Na tumwabudu Mungu Watatu-Mmoja katika utimilifu wa imani kila siku. Katika mwelekeo wowote ambao kujifunza kwetu Biblia na maombi yetu hutuongoza, hili na liwe daima kitovu ambacho kutoka kwacho twaenda nje na ambacho twarejea kwacho. Tuliumbwa katika sura ya Mungu Watatu-Mmoja. Wokovu ambao kwao Mungu hutuurudisha ni wokovu wa ndani; si kitu kwetu kama haujafanyika katika mioyo yetu na kufurahiwa humo. Mungu atuokoaye hawezi kufanya kwa namna nyingine yoyote isipokuwa kama Mungu akaaye ndani, akitujaza utimilifu wake wote. Na tuabudu na tungoje; na tuamini na tumpe utukufu.
Je, umepata kuona katika Waefeso jinsi zile Nafsi tatu za Utatu zinavyotajwa pamoja daima?
1. 3. Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani yake Kristo.
1. 12, 13. Ili sisi tuliokuwa tumemtumaini Kristo kwanza tuwe kwa sifa ya utukufu wake. Nanyi katika yeye mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu.
1. 17. Ili Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye.
2. 18. Kwa maana katika yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja.
3. 22. Ndani yake ninyi nanyi mnajengwa pamoja kuwa maskani ya Mungu katika Roho.
4. 4-9. mkiyasoma haya, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri ya Kristo, ambayo katika vizazi vingine haikujulishwa wanadamu, kama ilivyofunuliwa sasa mitume wake watakatifu na manabii katika Roho. Ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi, na wa mwili mmoja, na washiriki wa ahadi yake ndani ya Kristo Yesu kwa njia ya Injili. Ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake. Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii, kuwahubiri Mataifa utajiri wa Kristo usiopimika; na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, iliyositirika tangu zamani zote katika Mungu aliyeviumba vitu vyote.
5. 4-6. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu; Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja; Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote. 5. Mkijazwa Roho, mkimshukuru Mungu, katika jina la Kristo.
6. 10-18. hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.
Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. Basi simameni, hali mmefungwa kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani.
Zaidi ya yote mkitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu; tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; kwa sala zote na maombi, mkisali kila wakati katika Roho. Tena mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote, Ukijifunza na kulinganisha vifungu hivi, na kutafuta kukusanya fundisho lake katika dhana fulani ya kweli na ya unyenyekevu ya utukufu wa Mungu wetu, angalia hasa ni kweli yenye vitendo kiasi gani hii ya Utatu Mtakatifu. Maandiko hufundisha kidogo juu ya siri yake katika asili ya Kimungu, karibu yote yaliyo nayo ya kusema huhusu kazi ya Mungu ndani yetu, na imani yetu na uzoefu wetu wa wokovu wake.
Imani ya kweli katika Utatu itatufanya kuwa Wakristo wenye nguvu, wenye mng'ao, waliomilikiwa na Mungu. Roho wa Kimungu akijifanya mmoja na maisha yetu na nafsi yetu ya ndani; Mwana Aliyebarikiwa akikaa ndani yetu, kama njia ya ushirika mkamilifu na Mungu; Baba, kwa njia ya Roho na Mwana akitimiza siku kwa siku kusudi lake — ya kuwa twajazwa utimilifu wote wa Mungu. Na tumpigie magoti yetu Baba! Ndipo siri ya Utatu itajulikana na kuonjwa.