Sura 30 · dakika 4 za kusoma
Zaburi 119 na Fundisho Lake
Sheria yako naipenda mno ajabu, ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa. “Zaburi 119:97.
Katika Maandiko Matakatifu, kuna sehemu moja iliyowekwa kabisa kutufundisha nafasi ambayo Neno la Mungu lapaswa kuwa nayo katika kuthaminiwa kwetu, na jinsi tuwezavyo kupata baraka yake. Ndiyo sura ndefu kuliko zote katika Biblia, na, isipokuwa nadra sana, katika kila mstari mmojawapo wa mistari yake 176, tunayo, chini ya majina mbalimbali, kutajwa kwa Neno. Yeyote atakaye kweli kujua jinsi ya kujifunza Biblia yake sawasawa na mapenzi ya Mungu, yampasa kuifanya Zaburi hii kuwa somo la makini.
Yapasa uje wakati katika maisha yake ambapo aazimu kujifunza fundisho lake na kulitekeleza katika vitendo. Twawezaje kushangaa ya kuwa kujifunza kwetu Biblia hakuleti faida na nguvu ya kiroho zaidi kama twaupuuza Mwongozo wa Kimungu autuletao kwa kujifunza huko? Yamkini hukupata kuisoma kamwe hata mara moja tangu mwanzo hata mwisho kama nzima. Kama huna wakati, tafuta wakati, saa fulani ya Sabato iliyo huru — au kwa nini si juma, siku, au saa fulani iliyo huru? — Ambamo waisoma tangu mwanzo hata mwisho na kujaribu kuufahamu wazo lake kuu, au angalau kuinasa roho yake.
Kama waona ni vigumu kufanya hivi kwa kuisoma mara moja, isome zaidi ya mara moja. Hili litakufanya uhisi hitaji la kuipa fikira ya makini zaidi. Madokezo yafuatayo yaweza kukusaidia katika kujifunza kwako: 1. Angalia majina yote mbalimbali ambayo kwayo Neno la Mungu husemwa.
2. Angalia vitenzi vyote mbalimbali vinavyoeleza tunayopaswa kuhisi na kutenda kuhusu Neno. Hili na likuongoze kufikiri kwa makini nafasi ilioje ambayo neno la Mungu hudai katika moyo wako na maisha yako, na jinsi kila kipawa cha nafsi yako — tamaa, upendo, furaha, tumaini, utii, tendo — kinavyoitwa kwake.
3. Hesabu na uangalie ni mara ngapi mwandishi asema katika wakati uliopita juu ya yeye kuwa amezishika, amezitunza, ameziambatia, na amefurahia shuhuda za Mungu. Ni mara ngapi aeleza katika wakati uliopo jinsi afurahiavyo, aipendavyo, na kuithamini sheria ya Mungu? Na kisha jinsi, katika wakati ujao, aahidivyo na kuweka nadhiri kuzitunza amri za Mungu hata mwisho. Weka haya yote pamoja na uone jinsi zaidi ya mara mia moja ajiwekavyo nafsi yake mbele za Mungu kama yeye aiheshimuye na kuishika sheria yake. Jifunze hili hasa kama semi hizi zinavyounganishwa na maombi yake kwa Mungu mpaka uwe na taswira dhahiri ya mtu mwenye haki ambaye kuomba kwake, kwenye bidii na nguvu, kwaweza mengi.
4. Kisha jifunze maombi yenyewe na uandike maombi mbalimbali afanyayo kuhusu Neno, ikiwa ya fundisho la kulielewa na nguvu ya kulishika, au ya baraka iliyoahidiwa katika Neno, na ipatikanayo katika kulitenda.
Angalia hasa maombi kama “Ee BWANA, unifundishe njia ya amri zako” na "Nipe akili." Pia, yale ambayo ombi lake ni "sawasawa na neno lako."
5. Hesabu mistari ambamo mna dokezo la mateso, ikiwa kutokana na hali yake mwenyewe au kutoka kwa adui zake au dhambi za waovu au Mungu kukawia "kumsaidia"; na ujifunze jinsi ni wakati wa taabu ndipo twalihitaji Neno la Mungu hasa, na ya kuwa hili peke yake laweza kutuletea faraja.
6. Kisha huja mojawapo ya mambo muhimu kuliko yote. Ona jinsi kiwakilishi kidogo wewe, na wako, kinavyotokea mara nyingi, na jinsi kinavyoeleweka katika kila ombi, "Nifundishe," “Nihuishe," nawe utaona jinsi zaburi nzima ilivyo ombi lililonenwa kwa Mungu. Yote Mtunga Zaburi aliyo nayo ya kusema juu ya Neno la Mungu, ikiwa kuhusu kushikamana kwake nalo, au hitaji lake la fundisho la Mungu na kuhuishwa, husemwa kwenda juu usoni pa Mungu. Aamini ya kuwa kwampendeza Mungu na ni vyema kwa nafsi yake mwenyewe, kuunganisha kutafakari kwake na mawazo yake juu ya Neno, kwa kudumu na kwa ukaribu kadiri iwezekanavyo, kwa maombi, na Mungu aliye hai mwenyewe. Kila wazo la Neno la Mungu, badala ya kumvuta mbali na Mungu, humwongoza kwenye ushirika na Mungu.
Neno la Mungu hugeuka kwake kuwa maada tajiri na isiyokwisha ya kufanya ushirika na Mungu ambaye ni wake na ambaye limekusudiwa kuongoza kwake. Kadiri twapatapo taratibu ufahamu wa ndani wa kweli hizi tutapata maana mpya kutoka katika mistari mmoja mmoja.
Na tunapochukua, mara kwa mara, aya nzima pamoja na mistari yake minane, tutaona jinsi inavyosaidia kutuinua, pamoja na na kwa njia ya neno, kuingia katika uwepo wa Mungu, na katika maisha yale ya utii na furaha yasemayo, "Naliapa, tena nimehakikisha, ya kwamba nitazishika hukumu za haki yako." “Sheria yako naipenda mno ajabu, ndiyo kutafakari kwangu mchana kutwa.”
Na tutafute kwa neema ya Roho Mtakatifu kuwa na maisha ya kiibada, ambayo Zaburi hii huyafunua, yaliyofanyizwa katika saa yetu ya kesha ya asubuhi. Na Neno la Mungu kila siku, na kabla ya kila kitu kingine, lituongoze Kwa Mungu. Na kila baraka iliyomo ndani yake iwe jambo la maombi, na hasa hitaji letu la fundisho la Kimungu. Na kushikamana kwetu sana nalo kuwe ombi letu kama la mtoto na tumaini letu ya kuwa Baba atatusaidia. Na maombi yetu yafuatwe na nadhiri ya kuwa kadiri Mungu atuhuishavyo na kutubariki, tutaipiga mbio njia ya amri zake, na yote ambayo neno la Mungu hutuletea yatufanye kuwa na bidii zaidi katika kutamani kulipeleka Neno hilo kwa wengine, ikiwa kwa kuamsha au kwa kutia nguvu uzima wa Mungu katika nafsi.