Sura 26 · dakika 4 za kusoma
Kufanywa Upya Kwa Kila Siku — Nguvu Yake
Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku. 2 Wakorintho 4:16.
"Alituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili, na kufanywa upya na Roho Mtakatifu" Tito 3: 5.
Kwa kila siku mpya, uzima wa asili hufanywa upya. Kama vile jua lichomozavyo tena pamoja na nuru yake na joto lake, maua hufunguka, ndege huimba, na uzima kila mahali huchochewa na kutiwa nguvu. Tuinukapo kutoka katika mapumziko ya usingizi wetu na kula chakula chetu cha asubuhi, twahisi ya kuwa tumejikusanyia nguvu mpya kwa ajili ya wajibu wa siku. Chumba cha ndani ni ukiri usimamao wa hitaji ambalo uzima wetu wa ndani unao la kufanywa upya kwa kila siku pia. Ni kwa lishe mpya kutoka katika Neno la Mungu, na umoja mpya na Mungu mwenyewe katika maombi, peke yake ndipo nguvu ya uzima wa kiroho iwezavyo kudumishwa na kukua.
Ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, ijapokuwa mzigo wa ugonjwa au mateso, mkazo wa kazi, na uchovu vyaweza kutuchosha au kutudhoofisha, utu wa ndani waweza kufanywa upya siku kwa siku.
Wakati na mahali pa utulivu, pamoja na Neno na maombi, ndizo njia za kufanywa upya. Lakini hivi tu pale, kama njia, vinapohuishwa na nguvu ya Kimungu itendayo kazi kwazo. Nguvu hiyo ni Roho Mtakatifu, nguvu kuu ya Mungu itendayo kazi ndani yetu. Kujifunza kwetu chumba cha ndani na uzima wa ndani unaokiwakilisha kungekuwa na kasoro kama tusingelipa nafasi yake ipasayo kufanywa upya kwa kila siku kwa utu wa ndani, ambako ni kazi ya Roho aliyebarikiwa kutenda daima. Katika kifungu kile cha Tito, twafundishwa ya kuwa "Alituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili, na kufanywa upya na Roho Mtakatifu.” Semi hizi mbili hazikusudiwi kuwa marudio.
Kuzaliwa kwa pili ni tendo moja kuu, mwanzo wa maisha ya Kikristo; kufanywa upya kwa Roho Mtakatifu ni kazi iendeleayo daima na isiyoisha kamwe. Katika Warumi 12: 2, twasoma juu ya kugeuzwa kwa hatua kwa hatua kwa maisha ya Kikristo, ya kuwa ni kwa "Kufanywa Upya kwa Nia." Katika Waefeso 4: 23, neno "vueni utu wa zamani" (katika hali ya aoristi) laonyesha tendo lililotendwa mara moja kwa ajili ya wote, neno, "Mkafanywe Wapya katika Roho ya Nia Yenu" liko katika wakati uliopo, na laelekeza kazi ya hatua kwa hatua. Vivyo hivyo katika Wakolosai 3:10 twasoma, "Na mkavaa utu mpya, unaofanywa upya upate ufahamu sawasawa na mfano wake yeye aliyeumba.” Ni Roho aliyebarikiwa ndiye tunayepaswa kumtazama, ambaye twaweza kumtegemea, kwa ajili ya kufanywa upya kwa kila siku kwa utu wa ndani katika chumba cha ndani.
Kila kitu hutegemea, katika ibada zetu za siri, juu ya sisi kudumisha uhusiano wa kweli na nafsi ya tatu inayostahili kuabudiwa ya Utatu uliobarikiwa, ambaye kwa yeye peke yake Baba na Mwana waweza kufanya kazi yao ya upendo wa kuokoa, ambaye kwa yeye peke yake Mkristo aweza kufanya kazi yake. Uhusiano huo waweza kuelezwa katika maneno mawili rahisi sana, imani na kujisalimisha. Imani. Maandiko yasema, "Mungu alimtuma Roho wa Mwana wake mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba.”
Mtoto wa Mungu, hata aliye dhaifu kabisa, ambaye katika ibada yake ya asubuhi angetoa ombi, litakalompendeza Baba, na kuwa baraka kwake mwenyewe, ni lazima akumbuke ya kuwa amempokea Roho Mtakatifu kama roho wa maombi, na ya kuwa msaada wake ni wa lazima ili kutuwezesha kuomba kwa ufanisi. Vivyo hivyo na Neno la Mungu. Ni kwa Roho Mtakatifu peke yake ndipo kweli katika maana yake ya Kimungu na nguvu yake yaweza kufunuliwa kwetu, na kuifanya kazi yake mioyoni mwetu. Kama kufanywa upya kwa kila siku kwa utu wa ndani katika saa ya asubuhi kutakuwa hali halisi, chukua wakati wa kutafakari, kuabudu, na kuamini kwa moyo wako wote ya kuwa Roho Mtakatifu amepewa kwako, ya kuwa yumo ndani yako, na ya kuwa kwa njia yake Mungu atatenda ile baraka aitoayo kwa njia ya maombi na Neno.
Kujisalimisha. Usisahau ya kuwa Roho Mtakatifu ni lazima awe na uongozi kamili. "Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.”
Waenenda kwa kadiri ya Roho, si kwa kadiri ya mwili. Ni uwepo wa Roho usiohuzunishwa uwezao kulipa Neno nuru yake na nguvu yake, na kutuweka katika ule uzima uliobarikiwa wa tumaini kama la mtoto na utii kama wa mtoto uliompendeza Mungu.
Na tumsifu Mungu kwa kipawa hiki cha ajabu, Roho Mtakatifu katika nguvu yake ya kufanya upya, na tutazame kwa furaha na tumaini jipya kwenye chumba cha ndani kama mahali ambapo utu wa ndani waweza kweli kufanywa upya siku hata siku. Hivyo uzima utawekwa daima mpya; hivyo tutakwenda mbele toka nguvu hata nguvu, hivyo tutazaa matunda mengi, ili Baba atukuzwe.
Kama haya yote ni kweli, ni jinsi gani ni ya lazima kwamba tumjue Roho Mtakatifu ipasavyo. Kama Nafsi ya Tatu, ni kazi na huduma yake kutuletea uzima wa Mungu, kujificha katika kina cha nafsi yetu na kujifanya kuwa mmoja nasi, kumfunua huko Baba na Mwana, kuwa Nguvu kuu ya Mungu itendayo kazi ndani yetu, na kuutwaa uongozi wa nafsi yetu nzima. Yeye huomba jambo moja tu, utii wa unyofu kwa uongozi wake. Nafsi iliyojitoa kweli itapata katika kufanywa upya kwa kila siku kwa Roho Mtakatifu siri ya ukuaji na nguvu na furaha.