Sura 25 · dakika 3 za kusoma

Ya Ndani na Ya Nje

Enyi wapumbavu! Yeye aliyeumba ya nje, si ndiye aliyeumba na ya ndani pia?” Luka 11: 40.

Kila roho hutafuta kujiumbia umbo au sura ambamo uzima wake unadhihirishwa. Ya nje ni usemi unaoonekana wa uzima uliofichwa wa ndani. Ya nje kwa kawaida hujulikana kabla ya ya ndani; kwa njia yake, ya ndani hukuzwa na kufikia ukamilifu wake wote, kama mtume asemavyo katika 1 Wakorintho 15: 46. "Lakini hakikuwa kwanza kile cha roho, bali kile cha asili; baadaye kile cha roho." Kuelewa na kudumisha uhusiano ulio sahihi kati ya ya ndani na ya nje ni mojawapo ya siri kubwa kabisa za maisha ya Kikristo.

Kama Adamu katika bustani asingemsikiliza mjaribu, jaribu lake lingaliishia katika kuukamilisha uzima wake wa ndani. Ilikuwa dhambi yake na maangamizi yake, na chanzo cha taabu yake yote ya kuwa alijitoa kwa nguvu ya ulimwengu unaoonekana wa nje. Badala ya kutafuta furaha yake katika uzima uliofichwa wa ndani wa moyo ambamo amri ya Mungu iliheshimiwa, katika tabia za ndani za upendo na imani, za utii na kutegemea, aliweka tamaa yake juu ya ulimwengu ulio nje yake, juu ya anasa na ujuzi wa mema na mabaya ambao ungeweza kumpa.

Dini zote za uongo, tangu ibada ya sanamu iliyo ya kudhalilisha zaidi hata upotovu wa Dini ya Kiyahudi na ya Kikristo, ina msingi wake katika hili, ya kuwa kile kilicho cha nje, kile kiwezacho kupendeza jicho, au kuvutia akili, au kuridhisha ladha, huchukua nafasi ya ile kweli katika sehemu ya ndani, ile hekima iliyofichwa katika moyo na maisha ambayo Mungu huitafuta na kuitoa.

Alama kuu ya Agano Jipya ni kuwa ni maongozi ya uzima wa ndani. Ahadi ya agano jipya ni: "Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika." “Nami nitawapa moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu.” Ahadi ya Bwana wetu Yesu ilikuwa "Siku ile ninyi mtajua ya kuwa mimi ni ndani ya Baba yangu, nanyi ndani yangu, nami ndani yenu.” Ni katika hali ya moyo ndimo dini yakaa, katika moyo ambamo Mungu ametuma Roho wa Mwana wake, moyo ambamo upendo wa Mungu umemiminwa, ndimo wokovu wa kweli upatikanamo.

Chumba cha ndani, pamoja na umoja wake wa siri na Baba, aonaye sirini, ndicho ishara na shule ya mazoezi ya uzima wa ndani. Matumizi ya kweli na ya uaminifu ya kila siku ya chumba cha ndani yataufanya uzima uliofichwa wa ndani kuwa wenye nguvu na wenye furaha.

Katika dini zetu zote hatari kubwa ni kutoa muda na kupendezwa zaidi kwa njia za nje kuliko kwa hali halisi ya ndani. Si uzito wa kujifunza kwako Biblia, si mara nyingi au moto wa maombi yako au matendo yako mema, ndivyo hakika vifanyavyo uzima wa kiroho wa kweli.

Hasha! Kile tunachohitaji ni, kutambua ya kuwa, kama vile Mungu alivyo Roho, ndivyo ilivyo na roho ndani yetu iwezayo kumjua na kumpokea na kufanywa mfano wake, na kuwa mshiriki wa zile tabia zenyewe zimhuishazo yeye kama Mungu katika wema na upendo wake.

Weka imara hili akilini mwako ya kuwa wokovu wetu wote wakaa katika dhihirisho la asili, uzima, na roho ya Kristo Yesu katika mtu wetu mpya wa nje na wa ndani. Hili peke yake huufanya upya na kuurudisha ule uzima wa kwanza wa Mungu katika nafsi ya mwanadamu. Kila uendako, lolote ulitendalo, nyumbani au ugenini shambani, tenda yote katika tamaa ya kuungana na Kristo, katika kuiga tabia zake na maelekeo yake, na usitamani kitu, usitake kitu kwa nguvu kama kile kiuzoezao na kuuongeza roho na uzima wa Kristo katika nafsi yako, na kuwa na yote yaliyo ndani yako yamegeuzwa kuwa tabia na roho ya Yesu mtakatifu.

Fikiri hazina uliyo nayo ndani yako, Mwokozi wa ulimwengu, Neno la milele la Mungu, lililofichwa moyoni mwako kama mbegu ya Asili ya Kimungu ambayo itashinda dhambi na mauti ndani yako, na kuzalisha tena uzima wa mbinguni katika nafsi yako. Geukia moyo wako, na moyo wako utampata Mwokozi wake, Mungu wake, ndani yake mwenyewe. Huoni wala huhisi lolote la Mungu, kwa sababu wamtafuta huko nje, katika vitabu, kanisani, katika mazoezi ya nje; lakini huko hutampata mpaka pale utakapokwisha mpata kwanza moyoni mwako. Mtafute moyoni mwako nawe hutatafuta bure kamwe, kwa maana humo akaa, humo ndipo makao ya nuru yake na Roho wake Mtakatifu.

Ukurasa 1 / 3 · 3 dakika zimebaki katika sura
Ochorus

Kuwawezesha watu vitabu vya Kikristo vya kale — bila malipo, kwa lugha yako.

Chunguza

Dhamira Yetu

Vitabu vya Kikristo vya kale bila malipo mtandaoni — na vitabu vilivyochapishwa tunavyogawa kwenye makongamano, makanisa, shule na magereza kote Afrika Mashariki.

Faragha na Masharti

Huduma tangu 2021 · Victoria BC, Kanada · Kampala, Uganda