Sura 24 · dakika 4 za kusoma
Likizo
Lakini jueni neno hili, kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja mwivi, angekesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.” Luka 12: 39.
Katika hotuba juu ya Elimu, Edward Thring asema: "Saa zenye nguvu za mapumziko pamoja na shughuli zake ni zenye uwezo mkuu… Swali kubwa la saa za mapumziko lapaswa kuwa swali muhimu kuliko yote kwa kuwa laathiri tabia kuliko yote… Saa za mapumziko ndizo bawaba ambazo elimu ya kweli huzunguka juu yake” Bingwa huyu mkuu wa sayansi ya elimu alikuwa ameona, ya kuwa tabia bora, na ukweli wa nafsi, huja kwanza, na kisha baada ya hayo, kama la pili, kuzoezwa kwa ustadi na nguvu. Alikuwa ameona, tena, ya kuwa ijapokuwa mwalimu aweza kutenda mengi kwa neno na tendo kwa imani ya juu na kazi ya kweli ili kuchochea na kuongoza, kila mvulana lazima ajitendee tabia yake mwenyewe. Na kwa sababu ni katika saa za mapumziko, apo huru kutoka katika lazimisho na uangalizi, ndipo mvulana huonyesha kile kilicho juu kabisa ndani yake, ndipo aliponena juu ya saa za mapumziko kama zenye umuhimu wa juu kabisa na uwezo wa juu kabisa, bawaba ambazo elimu ya kweli huzunguka juu yake. Katika dini, hili ni kweli kwa nguvu sana.
Maelfu ya wanafunzi wameihisi, bila kujua jinsi ya kuieleza au kuifafanua.
Chuoni au shuleni, saa yao ya kesha ya asubuhi imekuwa na nafasi yake katika ratiba yao. Akili nzima huimarishwa kwa kazi ya kawaida na yenye mpangilio, na wakati wa ibada hutunzwa kwa uangalifu kama ule wa darasa au kujifunza faragha.
Wakati wa mapumziko ufikapo, na mtu awapo huru kufanya sawasawa apendavyo, mmoja baada ya mwingine hukuta ya kuwa saa ya kesha ya asubuhi na ushirika wake na Mungu havikuwa vimekuwa vya asili hivyo, hitaji kama hilo la uzima wa kiroho na furaha kama hiyo, hata kutunzwa kwake kusingeweza kuingiliana na anasa yetu ya likizo. Likizo hiyo huwa jaribio la tabia, uthibitisho wa jinsi mtu awezavyo kusema pamoja na Ayubu, "Nimeyathamini maneno ya kinywa chake kuliko fungu langu la chakula.” Swali la saa za mapumziko kwa kweli ni la umuhimu wa juu kabisa. Katika hizo nageukia kwa uhuru na kwa asili kwenye kile nikipendacho zaidi. Katika hizo, nathibitisha na kuongeza nguvu ya kushika nilicho nacho.
Mwalimu mmoja katika shule kubwa nchini Amerika hunenwa kuwa alisema, "ugumu mkubwa kuliko yote tunaopambana nao ni likizo ya kiangazi. Wakati ule ule tunapokuwa tumemfikisha mvulana kwenye kiwango kizuri cha nidhamu, naye huitikia maadili yaliyo bora, twampoteza, na arudipo majira ya vuli, twapaswa kuanza na kuyafanya yote tena upya.
Likizo ya kiangazi humharibu tu maadili." Kauli hii, ikirejea masomo ya kawaida na wajibu, ni yenye nguvu: ndani ya mipaka fulani, yatumika vivyo hivyo kwa maisha ya kidini.
Kulegezwa kwa ghafla kwa mazoea ya kawaida, na wazo la hila la kuwa uhuru kamili wa kufanya apendavyo mtu wamaanisha furaha kamili, humrudisha nyuma mwanafunzi kijana mmoja baada ya mwingine katika maisha yake ya Kikristo.
Hakuna mahali ambapo ni pa lazima zaidi kwa wanachama wazee na wenye uzoefu zaidi wa Chama cha Wanafunzi kuwasaidia na kuwalinda wanachama wao vijana kuliko hapa. Yale yaliyofikiwa kwa miezi yaweza kupotezwa kwa kupuuza kwa juma moja. Hatujui saa atakayokuja mwivi. Roho ya saa ya kesha ya asubuhi yamaanisha uangalifu usiokoma mchana kutwa na kila siku.
Kuna nyanja mbalimbali ambazo hatari, na usalama kutoka kwayo, yaweza kuwekwa mbele ya mwanafunzi. Pamoja na likizo twawekwa huru kutoka katika sheria za shule ambazo chini yake twaishi wakati wa kukaa kwetu humo. Lakini kuna sheria nyingine: sheria za maadili, na sheria za afya, ambazo hakuna kulegezwa kutoka kwazo. Mwanafunzi na aonywe ya kuwa wito wa ushirika wa kila siku na Mungu si wa kundi la kwanza bali wa la mwisho. Kama vile ahitajivyo kila siku wakati wa likizo kula na kupumua, ahitaji Kila Siku Kula Mkate na Kupumua Hewa ya Mbinguni.
Weka wazi ya kuwa saa ya kesha ya asubuhi si tu wajibu bali pia pendeleo na anasa isiyoelezeka. Ushirika na Mungu, kukaa ndani ya Kristo, kulipenda Neno, na kulitafakari mchana kutwa — kwa asili mpya mambo haya ni uzima na nguvu, afya na furaha.
Yatazame katika nuru hii; amini nguvu ya asili mpya iliyo ndani, na uitendee kazi; ijapokuwa huihisi, itakuja kuwa kweli. Ihesabu kuwa furaha, nayo itakuwa furaha kwako.
Zaidi ya yote, tambua ya kuwa ulimwengu wakuhitaji na wakutegemea wewe kuwa nuru yake. Kristo akungoja wewe kama kiungo cha mwili wake, siku kwa siku, ili kuifanya kazi yake ya wokovu kwa njia yako. Wala yeye, wala ulimwengu, wala wewe, hawawezi kumudu kupoteza hata siku moja. Mungu amekuumba na kukukomboa, ili kwa njia yako apate, bila kukoma kama vile kwa jua aangazavyo ulimwengu, kuiacha nuru yake na uzima wake na upendo wake vimulike juu ya wanadamu.
Wahitaji kila siku kuwa katika mawasiliano na chemchemi ya nuru yote. Usifikiri kuomba nafuu ya likizo kutoka katika umoja huu. Sembuse, kuichukua. Ithamini likizo kwa ajili ya wakati wa pekee ikupao wa kujifunza yale yaliyokuwa nje ya mtaala wako wa kawaida wa kujifunza Biblia. Ithamini likizo yako kwa ajili ya fursa ya pekee ya ushirika zaidi na Baba na Mwana. Badala ya kuwa mtego, badala ya nguvu zako zote kuchoka katika kujiweka tu usipoteze ardhi, ithamini likizo kama wakati uliobarikiwa wa neema na ushindi juu ya nafsi na ulimwengu, wa kuzidi kukubwa kwa neema na nguvu, wa kubarikiwa na kufanywa baraka.