Sura 23 · dakika 4 za kusoma

Kulishwa kwa Neno

Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu" — Yeremia 15: 16.

Hapa una mambo matatu. Kuonekana kwa neno la Mungu. Hili huwajia tu wale wanaolitafuta kwa bidii. Kisha kula. Hii yamaanisha kujitwalia binafsi kwa ajili ya kujilisha kwetu wenyewe, kuyachukua maneno ya Mungu na kuyaingiza katika nafsi yetu. “Naye akajibu akasema, Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Mathayo 4:4 na kisha kufurahi, “Tena ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, akaificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile.” Mathayo 13:44 hapo tuna kuonekana, kujitwalia, na kufurahi. “Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu.”

Kula hapa ndilo wazo kuu la katikati. Hutanguliwa na kutafuta na kuonekana: huandamana na kufuatwa na kufurahi. Ndilo lengo pekee na matumizi ya kile kimoja; ndilo chanzo pekee na uzima wa kile kingine. Katika siri ya chumba cha ndani ni mengi kiasi gani hutegemea juu ya hili — mimi niliyala!

Ili kutambua tofauti kati ya hili na kuonekana kwa maneno ya Mungu, linganisha nafaka ambayo mtu aweza kuwa amehifadhi ghalani mwake, na mkate alio nao mezani pake. Kazi yote ya bidii aliyoitoa katika kupanda na kuvuna na kutunza nafaka yake, thawabu yote tajiri aliyoipata kwa uangalifu wake, haiwezi kumfaa, isipokuwa apo alishwapo na fungu la kila siku la mkate autakao mwili wake. Katika kuonekana, kuvuna na kutunza, kiasi kikubwa zaidi na kazi ya haraka zaidi — hivi ndivyo vilivyokuwa vitu vya kuangaliwa. Katika kula, hutokea kinyume kabisa — hapa ni kiasi kidogo, na mwendelezo wa polepole na usiokoma, ndivyo vinavyodhihirisha kujitwalia.

Je, waona utumizi wa hili kwenye kujifunza kwako Maandiko katika saa ya kesha ya asubuhi? Wahitaji kuyaona maneno ya Mungu, na kwa fikira ya makini kuyamudu, ili uwe umeyahifadhi akilini na kumbukumbuni kwa matumizi yako mwenyewe, na furaha kuu, furaha ya mavuno au ya ushindi; furaha ya hazina iliyopatikana, au ya magumu yaliyoshindwa: na hata hivyo ni lazima tukumbuke kuonekana huku na kuyamiliki maneno ya Mungu bado si kule kuyala ambako peke yake huleta uzima na nguvu ya Kimungu kwa nafsi.

Kule kushughulika na, na kumiliki nafaka njema na bora, hakutamlisha mtu. Kule kupendezwa sana na ujuzi wa neno la Mungu hakutailisha nafsi kwa kutokana nako kwenyewe. “Maneno yako yalionekana” hilo ndilo lililokuwa jambo la kwanza. “Nami nikayala” ambako kulileta furaha na shangwe.

Na kule kula ni nini? Nafaka ambayo mkulima aliikuza na kuifurahia kama yake mwenyewe, isingeweza kuulisha uzima wake mpaka pale alipoitwaa na kuila, na kuiingiza kabisa katika nafsi yake, hata ikawa sehemu yake mwenyewe, ikiingia katika damu yake, ikiumba mifupa yake na nyama yake yenyewe. Hili lapaswa kufanywa kwa kiasi kidogo kwa mara moja, mara mbili au tatu kwa siku, kila siku ya mwaka. Hii ndiyo sheria ya kula. Si kupendezwa au kufanikiwa kwa kujifunza kwangu Biblia; si kuongezeka kwa uwazi wa mtazamo au ukubwa wa uelewa ninaoupata, ndivyo vihakikishavyo afya na ukuaji wa uzima wa kiroho. Hasha. Yote haya mara nyingi huiacha asili bila utakaso mwingi na bila kiroho, ikiwa na utakatifu kidogo sana au unyenyekevu kidogo wa Kristo Yesu: kitu kingine chahitajika. Yesu alisema: Chakula changu ndicho hiki, niyatende mapenzi yake yeye aliyenipeleka.

Kuchukua fungu dogo la neno la Mungu, amri fulani dhahiri au wajibu wa uzima mpya, kwa utulivu kulipokea katika utashi na upendo wa moyo, kuitoa nafsi nzima chini ya utawala wake, na kuweka nadhiri, kwa nguvu ya Bwana Yesu, kulitenda: hili, na kisha kwenda kulitenda, hivi ndivyo kula neno, kuliingiza katika nafsi yetu ya ndani kabisa, hata likawa sehemu thabiti ya uzima wetu wenyewe. Vivyo hivyo na kweli, au ahadi; kile ulichokwisha kula sasa chakuwa sehemu ya nafsi yako, nawe wachukua pamoja nawe kila uendako kama sehemu ya uzima uishio.

Waona mara moja jinsi zile pointi mbili za tofauti kati ya nafaka iliyo ghalani na mkate ulio mezani zinavyofunika kujifunza kwako kote Biblia. Kukusanya ujuzi wa maandiko ni jambo moja. Kula neno la Mungu, kulipokea ndani ya moyo wako kwa nguvu ya Roho atoaye uzima, ni jambo tofauti kabisa.

Nawe waona jinsi zile sheria mbili za kula chakula, kinyume na zile za kukipata, zipaswazo kutiiwa daima. Waweza kukusanya na kuhifadhi nafaka ya kutosha miaka mingi. Huwezi kumeza kiasi kikubwa cha mkate cha kutosha siku nyingi. Siku kwa siku, na zaidi ya mara moja kwa siku, wachukua chakula chako cha siku. Na hivyo kula neno la Mungu ni lazima kuwe kwa mafungu madogo, kadiri tu nafsi iwezavyo kupokea na kuyeyusha kila mara. Na hili, siku kwa siku, tangu mwanzo wa mwaka hata mwisho wake.

Ni kulishwa huku kwa neno kutakakoniwezesha kusema: “Maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu” George Muller asema ya kuwa alijifunza ya kuwa haimpasi kuacha kusoma Neno mpaka pale ahisipo furaha katika Mungu: ndipo alipojisikia amefaa kutoka kwenda kwenye kazi yake ya siku.

Ukurasa 1 / 3 · 4 dakika zimebaki katika sura
Ochorus

Kuwawezesha watu vitabu vya Kikristo vya kale — bila malipo, kwa lugha yako.

Chunguza

Dhamira Yetu

Vitabu vya Kikristo vya kale bila malipo mtandaoni — na vitabu vilivyochapishwa tunavyogawa kwenye makongamano, makanisa, shule na magereza kote Afrika Mashariki.

Faragha na Masharti

Huduma tangu 2021 · Victoria BC, Kanada · Kampala, Uganda