Sura 21 · dakika 5 za kusoma
Wewe u Nani?
Yafikirini mambo yaliyo juu, siyo mambo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uzima wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu." — Wakolosai 3: 2, 3.
Katika kuingia mbele za uwepo wa Mungu wakati wa asubuhi, mengi hutegemea juu ya Mkristo kutambua si tu Mungu ni nani, bali pia yeye mwenyewe ni nani, na uhusiano gani asimamao nao mbele za Mungu. Kwa swali “Wewe u nani?” aulizwalo, si kwa maneno bali kwa roho, kila mmoja adaiye haki ya kukaribia na kusikilizwa na Aliye Juu Sana, ni lazima pawe na jibu tayari katika fahamu yake ya ndani kabisa; fahamu hiyo ni lazima isiwe kitu pungufu ya utambuzi ulio hai wa nafasi aliyo nayo katika Kristo mbele za Mungu. Namna ya kulieleza yaweza kutofautiana nyakati mbalimbali, lakini katika kiini chake litakuwa lilo hilo siku zote.
Mimi ni nani? Naam, na nifikiri na kusema, mimi ni nani hata nimwombe Mungu akutane nami hapa, atumie siku hii nzima pamoja nami? Mimi ni yeye ajuaye, kwa neno na Roho wa Mungu, ya kuwa nimo ndani ya Kristo, na ya kuwa uzima wangu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Katika Kristo, niliifia dhambi na ulimwengu. Sasa nimetolewa katika hivyo, nimetengwa navyo na kuokolewa kutoka katika nguvu yavyo. Nimefufuliwa pamoja na Kristo na ndani yake naishi kwa Mungu.
Uzima wangu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu, nami naja kwa Mungu ili nidai na kupata uzima wote wa Kimungu uliofichwa ndani yake kwa ajili ya hitaji na riziki ya leo.
Naam, huyu ndiye mimi nilivyo, nalisema hili kwa Mungu kwa unyenyekevu na heshima takatifu, kama ombi langu. Nalisema hili kwa nafsi yangu ili kuwatia moyo wengine, pamoja na nafsi yangu, kutafuta na kutarajia kisicho pungufu — neema ya kuuishi, hapa duniani, uzima uliofichwa wa mbinguni. Mimi ni yeye atamaniye kusema, naam asemaye, Kristo ndiye uzima wangu. Shauku ya nafsi yangu ni kwa ajili ya Kristo, aliyefunuliwa na Baba mwenyewe ndani ya moyo. Hakuna kitu pungufu kiwezacho kuniridhisha. Uzima wangu umefichwa pamoja na Kristo. Hawezi kuwa uzima wangu kwa namna nyingine yoyote isipokuwa apo ndani ya moyo wangu. Naam! Sivyo naweza kuridhika na kitu pungufu ya Kristo ndani ya moyo.
Kristo ni Mwokozi kutoka dhambini. Kristo ni kipawa na mleta wa upendo wa Mungu. Kristo kama Rafiki na Bwana akaaye ndani. Ee! Mungu wangu! Kama waniuliza, “Wewe u nani?” sikiliza kigugumizi changu: Mimi naishi ndani ya Kristo, na Kristo ndani yangu. Wewe peke yako waweza kunifanya nijue na kuwa yale yote lisemayo. Kuna zaidi, itanipasa niseme, kama ombi langu la neema ya uwepo na nguvu ya Mungu mchana kutwa. Naja kama yeye atakaye, atafutaye, kuwa tayari kuuishi uzima wa Kristo leo hapa duniani, kuutafsiri utukufu wake wa mbinguni uliofichwa, kuwa lugha ya maisha ya kila siku, pamoja na tabia zake na wajibu wake.
Kama vile Kristo duniani alivyoishi kwa ajili tu ya kuyatenda mapenzi ya Mungu, ni tamaa yangu kuu kusimama nikiwa mkamilifu na timilifu katika mapenzi yake yote.
Ujinga wangu wa mapenzi hayo, katika utumizi wake wote wa kiroho kuhusu umoja na ulimwengu na wanadamu, ni mkubwa sana. Udhaifu wangu ni mkubwa zaidi. Na hata hivyo naja kwa Mungu kama yeye asiyethubutu kutoa kitu pungufu wala kutafuta maridhiano yoyote, kama yeye ambaye kwa uaminifu wote hukubali wito wa juu wa kuyaishi kwa ukamilifu mapenzi ya Mungu katika mambo yote.
Ni jambo hili linaloniletea kwenye chumba cha faragha. Nifikiripo juu ya kushindwa kwangu kote katika kutimiza mapenzi ya Mungu, nitazamapo mbele juu ya majaribu yote na hatari zote zinizongojeazo, nihisipo kupungukiwa kwangu kabisa na hata hivyo nikimwambia Mungu — naja kudai uzima uliofichwa katika Kristo, ili nipate kuuishi uzima kwa ajili ya Kristo; nahisi kusukumwa na kuvutwa nisitosheke pasipo hakikisho la kimya la kuwa Mungu atakwenda pamoja nami na kunibariki.
Mimi ni nani hata niyaombe mambo haya makuu na ya ajabu kwa Mungu? Je, kweli naweza kutarajia kuuishi uzima uliofichwa pamoja na Kristo katika Mungu, hata kuudhihirisha katika mwili wangu upatikanao na mauti? Naweza; kwa maana ni Mungu mwenyewe atakayeutenda ndani yangu kwa njia ya Roho Mtakatifu akaaye ndani yangu. Mungu yeye yule aliyemfufua Kristo katika wafu, na kisha akamweka mkono wake wa kuume, amenifufua pamoja naye na kunipa Roho wa utukufu wa Mwana wake ndani ya moyo wangu.
Uzima ndani ya Kristo, uliotolewa ili kujua na kuyatenda mapenzi yote ya Mungu, ndio uzima ambao Mungu mwenyewe atautenda na kuuendeleza kwa kuzidi ndani yangu kwa njia ya Roho Mtakatifu. Nami nijapo asubuhi na kujiweka mbele zake ili kuutwaa upya uzima aliouficha ndani yake mwenyewe kwa ajili yangu, mahali alipofichwa Mwana wake, na kuuishi katika mwili, naweza kungoja kwa uthabiti na kwa utulivu, kama yeye ambaye ndani yake Roho akaa, hata Baba anipe upako mpya ufundishao mambo yote, na yeye mwenyewe kuisimamia siku mpya aliyonipa.
Ndugu yangu, nina hakika wahisi umuhimu usio na kifani ulio nao, ikiwa saa ya asubuhi itapata uwepo wa Mungu kwa ajili ya siku nzima, ya kuwa usimame imara juu ya kisicho pungufu ya msingi wa ukombozi kamili.
Amini yale Mungu akuambiayo. Kubali yale Mungu aliyokupa ndani ya Kristo. Uwe kwa fahamu na kwa wazi yale ambayo Mungu amekufanya uwe. Chukua wakati mbele za Mungu ili kuyajua na kuyasema. Ni kiasi gani katika vita hutegemea juu ya nafasi isiyoweza kutekwa. Chukua nafasi yako mahali Mungu alipokuweka.
Jaribio lenyewe la kufanya hivi, laweza nyakati fulani kuingilia kati kujifunza kwako kwa kawaida Biblia, au maombi. Halitakuwa hasara. Litalipwa kikamilifu baadaye. Maisha yako yote hutegemea juu ya kujua Mungu wako ni nani, na wewe u nani kama mtu wake aliyekombolewa ndani ya Kristo. Maisha ya kila siku hutegemea juu yake; mara ile umekwisha jifunza siri hiyo, itakuwa, hata usipoifikiri, nguvu ya moyo wako, katika kumwendea Mungu, na katika kutoka pamoja naye kuuendea ulimwengu.