Sura 11 · dakika 5 za kusoma
Kuzishika Amri za Kristo
“Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda.” — Yohana 13:17.
Baraka na neema ya Neno la Mungu vyaweza kujulikana tu kwa kulitenda. Somo hili ni la umuhimu wa juu mno katika maisha ya Kikristo, na kwa hiyo katika kujifunza kwetu Biblia, hata lazima nikuombe urudie kwalo tena mara moja zaidi. Na wakati huu na tuchukue tu usemi ule mmoja, kulishika neno, au kuzishika amri. Na tuuchukue kwanza katika ile hotuba ya kuaga. Waweza kuzifahamu sehemu hizi, lakini itakuwa na faida kuziangalia pamoja.
“Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine.” (Yohana 14:15, 16).
“Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake.” (mstari 21). “Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake.” (mstari 23). “Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote, nanyi mtatendewa.” (15:7). “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. (15:10). “Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. (15:14).
Yachunguze na kuyalinganisha mafungu haya, hadi maneno yataingia moyoni na kufanya sadikisho la ndani kwamba kuzishika amri za Kristo ndilo sharti lisiloepukika la baraka yote ya kweli ya kiroho. Kwa kuja kwa Mungu Roho Mtakatifu, na ukaaji wake halisi wa ndani, kwa kuufurahia upendo wa Baba, kwa udhihirisho wa ndani wa Kristo, kwa makao ya Baba na Mwana moyoni, kwa nguvu ya maombi, kwa kukaa katika upendo wa Kristo, na kwa kuufurahia urafiki wake, kuzishika amri ndilo hitaji moja.
Na kwa nguvu ya kudai na kufurahia baraka hizi kwa imani siku baada ya siku, ufahamu wa kitoto kwamba kweli twazishika ni jambo lisiloepukika pia. Na si lisiloepukika kidogo, kwa kujifunza Biblia kwa matunda, ile hakika ya utulivu ithubutuyo kutarajia mwanga na nguvu ya Kimungu kwa kila neno la Mungu kwa sababu ajua kwamba tuko tayari kutii kabisa hata mwisho.
Kwa njia ya mapenzi ya Mungu, yaliyofurahiwa, na kutendwa, ndipo njia yetu pekee ya kuufikia moyo wa Baba, na njia yake pekee ya kuufikia moyo wetu.
Zishike amri: hii ndiyo njia ya kila baraka. Ona jinsi haya yote yanavyothibitishwa kwa namna ya kushangaza na tuyapatayo katika waraka wa kwanza wa Yohana.
“Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake. Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu umekamilika kweli kweli.” (1 Yohana 2:3-5). Uthibitisho pekee wa ujuzi wa kweli, ulio hai, uokoao wa Mungu; uthibitisho pekee wa kutokujidanganya wenyewe katika dini yetu; wa upendo wa Mungu kutokuwa mawazo tu, bali umilikaji, ni, kulishika neno lake.
“Mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye.” (3:21, 22, na 24). Kuzishika amri ndiyo siri ya ujasiri mbele za Mungu, na ushirika wa kweli wa ndani naye.
“Kwa maana huku ndiko kumpenda Mungu, kwamba tuzishike amri zake. Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu.” (5:3, 4).
Ungamo letu la upendo halina thamani, isipokuwa linavyothibitishwa kuwa la kweli kwa kuzishika amri zake katika nguvu ya uzima uliozaliwa na Mungu. Kumjua Mungu, kuwa na upendo wa Mungu umekamilishwa ndani yetu, kuwa na ujasiri kwa Mungu, kukaa ndani yake, kuzaliwa naye, na kumpenda—yote yategemea jambo moja—KUZISHIKA AMRI.
Ni kadiri tunavyotambua umaarufu ambao Kristo na Maandiko wanautoa kwa kweli hii ndipo tutakapojifunza kuutoa umaarufu ule ule katika maisha yetu. Itakuwa kwetu mmojawapo wa funguo za kujifunza Biblia kwa kweli. Mtu asomaye Biblia yake kwa shauku na kusudi thabiti la kuchunguza na kutii kila amri ya Mungu na ya Kristo, yuko katika njia sahihi ya kupokea baraka yote ambayo neno lilikusudiwa kuleta. Atajifunza hasa mambo mawili. Jinsi anavyohitaji kungoja mafundisho ya Roho Mtakatifu ili kumwongoza katika mapenzi yote ya Mungu, na baraka iliyoje iliyopo katika kutimiza kazi za kila siku, si tu kwa sababu ni sahihi, au anazifurahia, bali kwa sababu ni mapenzi ya Mungu. Atagundua jinsi maisha yote ya kila siku yanavyoinuliwa, asemapo kama Kristo alivyosema: “Agizo hili nalipokea kwa Baba yangu.” Neno litakuwa nuru na mwongozo ambao kwao hatua zake zote zitaongozwa.
Maisha yake yatakuwa shule ya mazoezi ambamo nguvu itakasayo ya Neno hudhihirishwa, na ile faraja. Na hivyo kuzishika amri kutakuwa ufunguo wa kila baraka ya kiroho.
Fanya jitihada thabiti kufahamu maana ya maisha haya ya utii kamili. Chukua baadhi ya amri za wazi kabisa za Kristo: Pendaneni: kama vile mimi nilivyowapenda ninyi; imewapasa kuoshana miguu; nanyi imewapasa kufanya vivyo kama mimi nilivyowatendea: na uukubali upendo na unyenyekevu ufananao na wa Kristo kama sheria ya maisha ya kimuujiza uyapaswayo kuishi. Mbali na hisi ya kushindwa au kutokuwa na uwezo kukuongoza kwenye kukata tamaa, au kuridhika na kile ufikiriacho chaweza kupatikana, na ikutie moyo tu kuweka tumaini lako kikamilifu zaidi juu yake, atakayefanya kazi ndani yako kwa Roho wake kutaka na kutenda.
Tena, lengo letu moja lazima liwe maelewano kamili kati ya dhamiri na mwenendo. Kila sadikisho lazima litekelezwe katika tendo. Amri za Kristo zilikusudiwa kutiiwa. Kama hili halifanyiki, mrundikano wa maarifa ya Maandiko huleta giza tu na kufanya moyo mgumu, na hufanya ile hali ya kuridhika na furaha iletwayo na kupata maarifa, ambayo hutufanya tusifae kwa mafundisho ya Roho.
Naomba usichoke kwa kurudia kwangu mara nyingi hivyo ujumbe huu wa baraka na wa dhati. Katika chumba chako cha ndani, ndipo swali litakapoamuliwa kama utazishika amri za Kristo mchana kutwa. Na pale pia litaamuliwa kama katika maisha yajayo utabeba tabia ya mtu aliyejitoa kabisa kujua na kutenda mapenzi ya Mungu.