Sura 9 · dakika 3 za kusoma
Tusukume, Bwana!
Ilikuwa asubuhi nzuri yenye jua ya Jumapili, nami nilikuwa katika ‘kilele cha kiroho’ kwa majuma matatu yaliyopita. Ingawa maamuzi yalipaswa kufanywa, mwenendo wangu na Bwana ulikuwa wa pekee sana. Kazi ya vijana ilikuwa ikifanikiwa kweli; maisha mengi yalikuwa yakibadilika, watu wapya walikuwa wakija kila juma, na makanisa mengine yalikuwa yameanza kujihusisha nasi, lakini siku hii ingekuwa tofauti!
Mapema katika ibada ya asubuhi, nilihisi kwa kina uwepo wa Bwana, na ile sauti yake ndogo ya ndani ikanena na roho yangu.
“Ni wakati wa kwenda nyumbani,” akasema.
“Siwezi kuinuka na kuondoka sasa hivi,” nikawaza. “Je, kutaniko litafikiri nini? Watadhani kwamba sifurahii ibada hii!”
Ile sauti ya ndani ikaendelea kusisitiza hata, baada ya nusu saa hivi, nikainuka kimyakimya kutoka kitini pangu na kutoka nje ya kanisa. Kulikuwa na umbali wa maili moja hivi hadi nyumbani kwetu, na nilipotembea taratibu kuelekea huko nilizungumza na Bwana. Yeyote aliyepita angedhani nilikuwa nikijinong’oneza mwenyewe, lakini uwepo wa Roho ulikuwa halisi mno nilipomimina kero zangu mbele zake.
Nilipopita Brewery Field - makao ya Bridgend Rugby Club, fahari ya wapenzi wote wa michezo wa eneo hilo - nikamkuta mvulana mdogo akihangaika na baiskeli yake ya magurudumu matatu. Magurudumu yake mawili yalikuwa juu ya kijia cha waenda kwa miguu, lakini gurudumu la mwisho lilikuwa bado barabarani, naye alikuwa akijaribu kwa nguvu zake zote ndogo kuipandisha baiskeli hiyo juu ya kijia. Alipoona ninakaribia, akainua uso wake uliolowa machozi na kusema, “Tusukume, bwana.”
Nikaunyoosha mkono wangu chini, nikashika sehemu ya nyuma ya baiskeli hiyo, na kwa juhudi kidogo tu, nikampeleka mtoto huyo mchanga zake akiwa na furaha. Alipopinda kona, aliangalia nyuma na kupunga mkono wakati uleule nilipokuwa nikimwambia mwenzangu asiyeonekana, “Tafadhali, nisukume, Bwana.”
Nilikuwa nimekuwa nikijihisi hasa jinsi mtoto yule alivyokuwa amejihisi. Njia iliyo wazi kabisa mbele yake, lakini akihangaika kujua namna ya kusonga mbele. Nilipoendelea na safari ile ya miguu, sala iliyozaliwa na Roho ikaanza kutoka midomoni mwangu. Tangu siku ile nimeirudia sala hii mara nyingi kiasi kwamba ninaijua karibu neno kwa neno kama nilivyoinena mara ya kwanza. Siitamki tena sala hii kwa sauti kwa kuwa imekuwa sehemu kubwa yangu kiasi kwamba sasa kwa kweli, ni sala ya moyo.
Muda fulani baada ya haya nilisoma juu ya kitabu, “Desert Fathers.” Watu hawa waliishi katika karne ya nne baada ya Ukristo kuheshimishwa na Rumi, na waaminio hawakuwa tena wakiuawa kwa ajili ya imani. Basi, wangewezaje ‘kuubeba msalaba wao’ na ‘kuifisha nafsi?’
Watu hawa waliamua kwamba maisha ya upweke katika Jangwa la Misri - mbali na vivutio vyote vya ubatili wa ulimwengu huu - yangekuwa ‘kufa kishahidi’ kwa namna hiyo. Walitafakari juu ya mambo mengi, hasa maombi, na jinsi mtu apaswavyo “kuomba bila kukoma” (1 Wathesalonike 5:17).
Miongoni mwa mafundisho yaliyoniteka fikira ni hili: kwamba mtu akiirudia sala mara nyingi za kutosha, sala hiyo huondoka midomoni, na kuwa ‘sala ya moyo.’ Hivyo, ingawa mtu huyo hasemi tena, moyo wake huendelea kumlilia Mungu katika ‘maombi yasiyokoma.’ Sala hii imekuwa sala ya namna hiyo kwangu.
“Bwana, ninatamani kuenenda katika mapenzi yako. Siombi kitu kingine chochote ila hiki: kwamba, nitakapofika mwisho wa safari yangu, nitakusikia ukisema, ‘Vema, mtumishi mwema na mwaminifu.’ Najua kwamba mimi ni mpumbavu na hata mjinga nyakati nyingine, na kwamba nitatoka nje ya mapenzi yako, lakini ninakupa ruhusa ya asilimia 110 ya kunichapa ili nirudi mstarini. Siombi kujua mapenzi yako ni nini wala kuiona njia iliyo mbele yangu bali ninaomba tu, kwamba unihifadhi ndani ya mapenzi yako.”
Njia ambayo Mungu ameitumia kuijibu sala hiyo imeuumba uelewa wangu wa “mwenendo wa imani” na imenisaidia kuelewa baadhi ya magumu ya Waebrania 11 - sura ile kuu juu ya “mashujaa wa imani.” Nitajieleza kwa upana zaidi baadaye itakapodhihirika jinsi Bwana alivyoniongoza katika mapenzi yake.