Sura 8 · dakika 3 za kusoma
Nafasi Zilikuwa Tele
Mwaka uliofuata ulikuwa wa kuvutia mno! Mipango ya shule mpya ilikuwa ikiendelea, nasi sote tulitazama kwa hamu kuona kwamba wasanifu majengo waliyachukulia mapendekezo yetu kwa uzito walipochora michoro yao. Sisi wa Grammar School tulihofia kupoteza baadhi ya shughuli za kitaaluma zaidi tulizokuwa nazo, badala yake tupewe shughuli zilizolenga wanafunzi wa kawaida. Nina hakika walimu kutoka shule ya awali walikuwa na wasiwasi vivyo hivyo kwamba wanafunzi wao wangetendewa kama wa ‘daraja la pili.’ Ilikuwa jukumu langu kuwakilisha makundi yote mawili.
Nilialikwa kujiunga na kikundi kidogo cha walimu wa fizikia katika jopo kazi, ili kuandaa mtaala mpya kwa wanafunzi wa ngazi ya juu: wale waliojiandaa kuingia chuo kikuu. Tulikutana kila juma katika Cardiff University kutengeneza na kupima vifaa vya kielektroniki na pia kujadili mtaala. Transista zilikuwa uvumbuzi mpya, na kama uwezavyo kuwazia, sote tulikuwa ‘wanagenzi’ wa elektroniki tukichezea vitu vipya. Miaka 15 tu kabla ya hapo nilikuwa nimehitimu sekondari, lakini sayansi ya elektroniki ilikuwa tayari ikileta athari kubwa, hata katika elimu.
Kuelekea mwisho wa mwaka wa shule, nilipewa fomu ya kuomba kuhudhuria kozi ya muda wote ya elektroniki katika chuo kikuu - ambayo mwishoni mwake ningetunukiwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi.
Hili lilikuwa la kushawishi sana kwani niliona somo hilo la kuvutia, na kozi hiyo ingeongeza tu ujuzi wangu wa ufundishaji.
Tayari nilikuwa na lengo la kuifanya shule yetu kuwa kinara anayetambulika katika kufundisha fizikia. Zaidi ya hayo, siku zote nilikuwa nimebeba majuto kidogo kwamba sikuwa nimekubali mojawapo ya nafasi mbili nilizopewa za kusomea shahada ya uzamivu katika fizikia. Wakati wa mahafali yangu, nilikuwa nimealikwa kubaki Swansea University kufanya utafiti, na pili, nilikuwa nimealikwa kujiunga na timu ya utafiti ya British Geographical Society huko Antarctica kwa miaka mitatu, na baadaye shahada ya uzamivu ‘iliyohakikishwa’ katika Oxford University; lakini, nilikuwa Mwelisi wa kawaida, mwenye ile tabia ya kitaifa ya kujiona duni, nisiyeamini kwamba kweli niliweza kulifikia lengo la uzamivu. Tena, nilikuwa nimekutana na Anne - nami nilikuwa katika mapenzi!
Niliifikiria nafasi hii mpya kwa makini. Nilipanga apatikane mwalimu wa kunibadili kisha nikaomba likizo ya masomo ili kuendeleza elimu yangu mwenyewe. Bw. Price, mwalimu mkuu wangu, aliiunga mkono ombi langu, nalo likapelekwa kwa Bodi ya Wasimamizi. Mkutano wetu ujao wa Bodi ulikuwa bado majuma mawili mbele, kwa hiyo nilishangaa siku chache tu baadaye mwalimu mkuu aliponiambia kwamba Bodi ilikuwa imelikataa ombi langu. Nilipouliza zaidi, niligundua kwamba alikuwa ni mwenyekiti peke yake aliyefanya uamuzi huo bila kushauriana na wenzake, kwa hiyo nikamweleza Bw. Price kutoridhika kwangu. Vitendo vya namna hiyo vilikuwa vya kawaida kabisa kwa Bodi za Shule zilizojulikana kwa kukosa huruma kwa walimu waliowaajiri.
Hii ilikuwa mojawapo ya sababu zilizoifanya Wizara ya Elimu kusisitiza kwamba mwalimu aliye kazini lazima ateuliwe kuwa mjumbe katika kila Bodi ya Wasimamizi. Nashuku kwamba mwenyekiti hakutambua kwamba mwalimu aliyekuwa ameomba likizo ya masomo alikuwa ni yuleyule aliyeketi katika mkutano wa Bodi!
Mwalimu mkuu aliniambia nisikate tamaa sana kwa kuwa alikuwa na pendekezo lililo bora hata zaidi. “Gareth, ninatafuta mkuu wa shule ya kati, nami nadhani wewe ndiwe mtu wa nafasi hiyo, na kurudi chuo kikuu kunaweza kuiharibu nafasi hiyo.”
Mambo yalikuwa yakivutia sana! Maamuzi yalipaswa kufanywa nami sikujua ni yapi ya kufanya. Je, niishinikize Bodi ya Wasimamizi iniachilie kwa kozi ya shahada ya uzamili? Je, nilirudishe ombi hilo na kutumaini kwamba mwalimu mkuu angelifuatilia pendekezo lake? Je, kweli nilitaka kuacha kufundisha fizikia kwa ajili ya nafasi ya kiutawala? Pamoja na haya yote kulikuwa na kazi ya ziada ya kuendeleza Chama cha Wafanyakazi, katiba yake, na uhusiano wake na Bodi ya Wasimamizi.
Anne nami tulizungumza juu ya uwezekano huo na tukaomba bila kuona mwongozo wowote ulio wazi. Hatukuelewa hata kidogo kwamba Bwana alikuwa tayari ameshiriki kwa bidii sana katika yote yaliyokuwa yakitendeka. Tena, kukatishwa tamaa kwangu kwa kunyimwa likizo baadaye kulionekana kuwa uteuzi wake wa jambo kubwa na bora zaidi.