Sura 7 · dakika 4 za kusoma
Shughuli! Shughuli! Shughuli!
Punde, mawazo yote ya Kanada yakatuacha nilipotulia katika kazi yangu mpya ya Mkuu wa Idara ya Fizikia. Pia nilichapisha gazeti la shule, nikaendesha umoja wa Kikristo, na kuongoza mikutano ya shule. Nilianzisha kikundi cha ushirika wa vijana nyumbani kwetu nikatazama Mungu akikichanua kuwa kazi kubwa iliyofunika makanisa saba na eneo pana kuzunguka mji wetu. Nilitoa ‘gazeti’ la vijana lililounganisha kazi za vijana za hapo na kuunda kwaya ya sauti 50 iliyoimba kantata za Pasaka na Krismasi katika kumbi, vikanisa, na magereza. Tuliendesha kambi za kiangazi na jioni za vijana za wikendi.
Jioni moja nilipata simu kutoka YMCA ya hapo, klabu kubwa na yenye shughuli nyingi za michezo; mpigaji simu alisema walikuwa wakitafuta damu changa katika Bodi yao na walijiuliza kama ningepatikana, kwa kuwa nilikuwa nimependekezwa kwao kwa kazi yangu miongoni mwa vijana wa hapo. Nilikubali na muda mfupi baadaye nikahudhuria Mkutano wangu wa kwanza wa Bodi ambapo nilikaribishwa sana. Nilipoketi pale, nilitazama majengo haya makubwa ambayo hayakutumika kamwe siku za Jumapili (hizi zikiwa siku kabla ya michezo ya Jumapili). Niliuliza ingenigharimu kiasi gani kukodi vifaa hivi.
“Hakuna kitu chochote!” niliambiwa, “Wewe sasa ni Mjumbe wa Bodi, hivyo unastahili kupata ufunguo wako. Mwambie tu katibu kwamba unataka mmoja na kwamba unauhitajia kwa nini, na hakutakuwa na tatizo lolote.”
Hivyo, jioni za Jumapili niliingia bila kizuizi YMCA, baa yake ya vitafunio na ukumbi wa burudani, na punde, vijana wengi kutoka makanisa ya hapo wakaja kwa ushirika wa saa mbili usiku. Zile zilikuwa siku za pekee za baraka ya Bwana ambapo wengi walimjia. Wazee wa kanisa langu walinipa ‘carte blanche’ ya kuendesha kazi ya vijana ya kanisa, na makanisa mengine mengi yaliniona kuwa mfanyakazi wao wa vijana. Kwa kweli nilikuwa mchungaji-msimamizi wa vijana, nikiwa na watu wengi wazuri wakifanya kazi nami kuendesha kambi, mikaango ya nyama, huduma za kufikia watu, programu za YMCA, na kadhalika! Kupitia huduma hizi, wengi waliongozwa kwa Bwana!
Nilikuwa na shughuli, shughuli, shughuli! Kwa kweli: shughuli nyingi mno!
Nilikuwa nimeanza kukimbia mbele ya ile Nuru!
Hatimaye, mwendo wangu wa kasi ulinifikia nami nikaanza kipindi kirefu cha kukosa usingizi. Nilitembea kwa saa nyingi nikijaribu kujichosha vya kutosha ili nilale, lakini kisha nilalie macho usiku kucha nikiyaishi upya matukio yote ya siku ile. Pindi moja, ilionekana nilikumbuka kila mwendo wa mpira katika mchezo wa kimataifa wa raga niliokuwa nimeutazama siku ile kwenye televisheni. Daktari wangu alikuwa ameniandikia dawa na mmoja wa rafiki zangu alikuja mara kwa mara, nyakati za jioni, ili anicheke huku nikiyumbayumba chumbani nikielekea kitandani. Ni nani atakaye rafiki wa namna hiyo?! Shuleni, wanafunzi wangu waliambiwa wasinisumbue kama nisingetoka katika chumba cha giza kilichoungana na maabara yangu ya fizikia mwishoni mwa mapumziko.
Walijua nilikuwa nimelala ili kupumzika na walipaswa kumwita mkuu wa shule ambaye angeniwakilisha! Baada ya miezi sita usingizi wangu ulirudi katika hali ya kawaida, lakini nilikuwa nimeziacha shughuli zangu zote isipokuwa kusimamia kazi ya vijana.
Baada ya miaka mitano katika Ogmore Grammar School, nilikuwa nikiifurahia kazi yangu na urafiki wa wenzangu. Hata hivyo, sikuwa nimejiandaa kwa mkondo uliofuata wa mambo. Sera mpya ya serikali iliagiza kwamba shule yetu iungane na Nantymoel Secondary School kuunda Comprehensive School mpya, ambayo ingekuwa na jengo lililojengwa maalum chini ya bonde, karibu na nyumba yetu mpya huko Bridgend. Kwa kuwa kazi ya vijana ilikuwa imekua, tulikuwa tumeiuza nyumba yetu ndogo na kuhamia mji huu, katikati ya bonde zuri la Glamorgan. Kuunganisha shule kulimaanisha kuunda Chama kipya cha Wafanyakazi kisha kumchagua mwakilishi wa kuwahudumia katika Bodi ya Wadhamini.
Wakati ule, hakuna mwalimu aliyeruhusiwa kutumika kama mdhamini wa shule, hivyo kumchagua mwakilishi kulipaswa kufanywa kwa uangalifu. Nilihudhuria mkutano wa pamoja wa wafanyakazi nikiwa na mawazo fulani ya nani ningemuunga mkono. Kwa hakika sikuwa na wazo lolote kwamba mimi ningeweza kufikiriwa. Sikuwa mtu aliyechangamana mara kwa mara na wafanyakazi wengine, wala sikuwa na miaka mingi katika shule zile za mabondeni kama wenzangu wengi. Saa mbili baadaye, niliondoka katika mkutano ule nikitikisa kichwa kwa mshangao kiasi. Nilikuwa nimechaguliwa kwa kauli moja kuwa rais wa Chama kipya cha Wafanyakazi na pia mwakilishi wake katika Bodi ya Wadhamini!
Nilimgeukia Alan, mwalimu wetu wa jiografia, aliyekuwa akitembea kando yangu. “Siamini jambo hili,” nikasema. “Kwa nini isiwe hivyo?” akajibu, “sote twajua kwamba wewe ndiye peke yako ambaye angesema kweli sikuzote,” Nikanong’ona sala ya kimya moyoni.
“Asante, Bwana, kwako wewe uwe Utukufu wote!” Kisha nikamgeukia Alan tena na kuongeza, “Ngoja tu nifike nyumbani nimwambie Anne! Naye pia hatasadiki!”