Sura 6 · dakika 4 za kusoma

Lulu ya Mashariki

Hong Kong, “Lulu ya Mashariki” ilitimiza jina lake. Tangu tulipowasili katika Uwanja wa Ndege wa KaiTak, tuliipenda rangi, harufu, kelele, na watu wake. Anne alinunua katika masoko yake ya barabarani, mara nyingi usiku wa manane, bila hofu, nami niliyafurahia maeneo yake ya michezo kwa tenisi mara mbili kwa wiki na kuogelea katika Forces Club.

Punde tukajikuta tumeshiriki katika maisha ya Kikristo ya jamii ile. Nilipata heshima ya urafiki na Jackie Pullinger wakati alipokuwa akianza tu ile kazi iliyokuwa na matokeo makubwa miongoni mwa waraibu wa dawa za kulevya wa Hong Kong. Ilikuwa pamoja naye nilipoingia katika ‘mji wenye ukuta’ wa Kowloon na kuonja darasa la Biblia katika ‘pango la joka.’

Kila mwezi Anne na mimi tulivuka mashambani hadi kituo cha yatima ambako tulisimulia hadithi za Yesu, ikifuatiwa na supu ya miguu ya kuku na wali. Niliimba katika kwaya ya Kichina, hata nikithubutu kuchukua sehemu za peke yangu katika kantata ya Pasaka… kwa Kikantoni!

John Bechtel alikuwa mmisionari huko Hong Kong tangu kabla ya Vita vya Pili vya Dunia. Alikuwa ameanzisha ofisi ya uchapishaji na kuichunga Waterloo Road Alliance Church. Sasa alikuwa amestaafu, na mwanawe John Jr. alisimamia kazi ile pamoja na shule kadhaa za juu ya paa.

Bechtel mzee hakuwa amestaafu kumtumikia Bwana, kwa sababu kila wiki sebule yake ilipokea hadi wanajeshi 30 wa Uingereza kwa funzo la Biblia. Miongoni mwao walikuwa askari kama kumi na wawili wa Nepal - Gurkhas - waliojulikana kwa ujasiri wao, na kuheshimiwa sana na wenzao. Ilikuwa heshima yangu kila wiki kulifundisha funzo hili, mara nyingine nikipokezana na mama mzee mpendwa aliyekuwa amemtumikia Bwana huko China kabla ya uvamizi wa Wajapani.

Sikutambua kwamba kuwa Hong Kong, na kuwa sehemu ya kikundi hiki cha Funzo la Biblia, kungeyaathiri sana maisha yetu yajayo - miadi nyingine ya kimungu ya Mungu!

Wakati huu, tuliomba tena viza za kuingia Kanada ingawa nafasi za ualimu hazikuwa zikitangazwa nje ya nchi tena. Badala yake, nilipokea barua kutoka kwa Msimamizi Mkuu wa Shule huko San Francisco. Mpwa wake alikuwa ametembelea nyumbani kwetu huko Hong Kong akiwa likizoni kutoka uwanja wa vita wa Vietnam, na aliporudi kwao, alikuwa amemwomba mjomba wake anialike ili nifundishe huko California. Aliandika kwamba, kama tungewahi kufika San Francisco, angefanya awezavyo kunitafutia nafasi ya kazi.

Kwa hiyo, katika kiangazi cha 1969, tulikuwa tayari kabisa kuruka hadi pwani ya magharibi ya Marekani, lakini badiliko la sera ya serikali katika njia za Westminster liliyabadili yote hayo. Ilikuwa ni sera kwamba wafanyakazi wote wa jeshi la Uingereza wangeweza kugharimiwa gharama zote za kujitafutia njia yao wenyewe ya ‘kwenda nyumbani’ kutoka nchi yoyote ya ugenini, maana yake tungeweza kusafiri mahali popote na kugharimiwa na Uingereza.

Kwa njia hii, gharama zetu zote za kwenda San Francisco au Kanada zingelipwa. Mwezi Mei 1969, kwa sababu ya gharama za kijeshi zilizopanda, sera ilibadilishwa ili wote warudishwe nchini kwa ndege za kijeshi, bila malipo ya fedha. Kwa kuwa hatukuweza kumudu safari ya kubahatisha hadi California au magharibi mwa Kanada, bila kazi ya uhakika, mipango yetu ikasimama tena. Mlango mwingine ukafungwa! Kuvunjika moyo kwingine!

Kwa haraka niliomba nafasi za ualimu huko Great Britain nikijua kwamba kama ningepata ushahidi wa ‘kukataliwa’ mara tatu Jeshi la Uingereza lingelipa mshahara wangu kwa muhula mmoja (hadi mwaka mpya). Kukataliwa kukaja nasi tukarudi kwa ndege Wales kwa familia yetu.

Muhula mpya wa shule ulipoanza, tulikuwa tunakaa nyumbani kwa wazazi wa Anne huku nyumba yetu wenyewe ikiachwa na wapangaji waliokuwa wameishi ndani yake tulipokuwa ng’ambo.

Nilipojaribu kuwatafutia binti zetu shule za kuhudhuria, yule mama katika ofisi za Glamorgan Education Board alijibu maswali yangu kwa urahisi.

“Ndiyo, itakuwa sawa kwa binti zako kubaki nje ya shule kwa muda wa zile wiki mbili ambazo zingehitajika ili kuhamia tena nyumbani kwenu.”

“Hapana, hawana haja ya kujiandikisha hapo kisha kulazimika kuhamishwa baada ya wiki mbili.”

Nilikuwa karibu kuweka simu chini wakati aliponiuliza swali la kushangaza, “Samahani, bwana. Je, yawezekana kwamba jina lako ni Bw. Evans, Gareth Evans kutoka Hong Kong?”

Nilipomjibu, nikiwa bado najiuliza ni jinsi gani alilijua jina langu, aliniambia kwamba kama ningekwenda Ogmore Grammar School, kazi ingekuwa ikinisubiri huko.

Ogmore Grammar ilikuwa shule iliyoheshimiwa sana mwanzoni mwa mojawapo ya mabonde yaelekeayo kaskazini kutoka nyumbani kwetu. Mwanawe maarufu kuliko wote alikuwa Lynn “The Leap” Davies. Mwenye rekodi ya dunia ya kuruka umbali hadi Bob Beamer alipoivunja katika Olimpiki za Mexico City za 1968. Vijia vya waenda kwa miguu huko Nantymoel, kijiji cha Lynn, vilipakwa rangi mbalimbali, kila kimoja kikipima urefu kamili wa ruka lake la rekodi.

Ingenichukua dakika 15 tu kuendesha gari hadi huko kila siku, mara tu tulipokuwa tumerudi ‘nyumbani’ katika nyumba ile ndogo tuliyoinunua muda mfupi baada ya arusi yetu.

Nilipokutana na mkuu wa shule siku yangu ya kwanza nilimwuliza alitaka nifundishe hapo kwa muda gani kwa kuwa nilikuwa na uhakika wa mshahara wa miezi minne bila kufanya kazi! Niliuliza kama mwalimu aliyekuwepo alikuwa mgonjwa au yuko likizoni kwa sababu nyingine, kwa kuwa nilikuwa nimeiomba nafasi hii nikiwa Hong Kong na nikadhani ilikuwa imejazwa kwa sababu sikuwa nimepata jibu lolote. Aliniambia kwamba Bodi ya Wadhamini ilikuwa imetaka kuniteua, lakini haikuweza kwa kuwa walikuwa na sera ya kutoteua mtu kutoka ng’ambo. Badala yake, walikuwa wamewaambia waombaji wengine wote kwamba nafasi ile ilikuwa imejazwa, wakitumaini kwamba kwa namna fulani ningewasiliana nao niliporudi Wales – kama nilivyofanya kabisa!

Ukurasa 1 / 4 · 4 dakika zimebaki katika sura