Sura 5 · dakika 5 za kusoma

Nenda Mbele, Kijana!

Miaka minne niliyoitumia katika kampasi nzuri ya Brynmill, Swansea ilikuwa yenye faida kubwa. Ingawa nilikuwa nimeingia chuo kikuu kusoma hisabati, nilihamia idara ya fizikia katika mwaka wangu wa pili kwa kuwa nilijikuta nikiwa na shauku iliyokua ndani yake. (Nikitazama nyuma, jambo hili pia laweza kuonekana kuwa ni uongozi wa Bwana.) Hapo mwanzo nilikuwa nimefikiri kwenda Birmingham kwa kuwa chuo kikuu kile kilijulikana kwa idara yake ya hisabati. Sasa nilikuwa nikisoma fizikia huko Swansea, chuo kilichojulikana kwa idara yake ya fizikia! Nilipata shahada bora ya fizikia kuliko mtu yeyote alivyotarajia, na katika mwaka wangu wa mwisho, diploma ya elimu. Nilipoondoka chuoni nilianza kazi yangu ya kwanza ya kufundisha fizikia nikiwa Mkuu wa Idara katika shule mpya ya sekondari.

Nyumba ya akina Evans ikawa mahali pa pekee ambapo nilitendewa kama mmoja wa familia; naam, hata leo hii bado ni familia kwangu. Tulihudhuria kanisa moja, nami nikajiunga na Swansea Gospel Male Voice Choir, ambamo Mary Evans alikuwa mpiga kinanda na Aubrey Evans mtunza vitabu. Mary alihakikisha kwamba nilikula vizuri kabisa, huku mumewe, Aubrey, ingawa hakuwa mtu wa elimu, akinipa vito vingi vya ufahamu vilivyobaki nami miaka yote.

Mara moja, nilipokuwa nimekata tamaa kidogo kwa sababu ya kukosekana kwa bidii miongoni mwa vijana wa kanisa, alinichukua kando, akasema, “Kumbuka mwanangu, kwamba wale wafuatao kwa mbali, bado wanaweza kumwona Bwana, lakini wale wanaotangulia hatua moja mbele ya Nuru ya Ulimwengu, hawawezi tena kumwona. Wanajikuta wakitembea katika kivuli chao wenyewe.”

Russell alisoma sayansi ya madini chuoni kikuu na baadaye akawa profesa mwandamizi katika taasisi hiyo hiyo. Alikuwa mwanafunzi hodari, tena msaada mkubwa kwangu nilipohangaika katika kozi zangu za Honours za fizikia ya nyuklia.

Don Evans alikwenda Chuo cha Biblia, akachunga kwa miaka michache kisha akaingia Swansea University College kusoma Falsafa. Sasa anaishi Dunedin, New Zealand akiwa profesa huko, na mmoja wa wasomi maarufu duniani katika fani ya Maadili ya Kitiba. Amesafiri sana, katika duru za kitaaluma na pia kama mzungumzaji katika vuguvugu la uamsho la kikarismatiki.

Ni wakati wa miaka ile ya ajabu huko Swansea ndipo nilipokutana na Anne, katibu aliyekuwa akihudhuria kanisa lile lile kama mimi. Baba yake alikuwa Mnorwe naye alikuwa mhudumu mwaminifu wa Injili ingawa afya yake ilikuwa dhaifu kwa miaka mingi. Alinipa ufahamu mwingi katika mambo ya ndani zaidi ya Mungu, nami bado navithamini vitabu vya tafakari alivyonipa. Mama yake alikuwa amelelewa katika kanisa ambako Evan Roberts alikuwa kiongozi wa vijana wakati uamsho wa Wales ulipozuka mwaka 1904.

Aliwajua wengi wa ‘watakatifu’ wa wakati ule na baadaye akawa mshiriki wa “Rees Howells’ Prayer Band.” Kwa urithi wa kimungu namna hiyo, si ajabu kwamba Anne ameonyesha tabia ya kina ya Kikristo ambayo nimejifunza kuithamini ndani yake.

Tulichumbiana siku ya mahafali yangu na tukaoana mwaka mmoja baadaye nilipomaliza kozi yangu ya diploma ya ualimu. Tulihamia nyumbani kwetu kwa kwanza kwa wakati wa kuanza kufundisha kwangu katika Cynffig Comprehensive School. Sikuelewa kamwe jinsi nilivyoipata nafasi ile - lazima ilikuwa ni miadi nyingine ya Bwana kwa sababu ilikuwa fursa ambayo sikuitafuta kamwe.

Mmoja wa maprofesa wangu alinijia chuoni siku moja akiniuliza kama nilikuwa nimekwisha kupata kazi. Nilijibu kwamba sikuwa nimepata, lakini bila wasiwasi, kwa kuwa bado kulikuwa na muda kabla chuo hakijaisha. Kisha akapendekeza niandike kwa anwani fulani, aliyokuwa ameiandika kwa ajili yangu, na kuuliza juu ya nafasi zozote zilizokuwepo. Muda mfupi baadaye nilialikwa kwenye usaili wa nafasi ile ya Cynffig. Kadiri niwezavyo kuthibitisha, mimi ndiye peke yangu niliyesailiwa kisha nikapewa kazi ya kufundisha fizikia hadi ngazi ya juu kabisa.

Katika mwaka wangu wa tatu katika shule ile ya kwanza, nilialikwa kufundisha na Majeshi ya Uingereza huko Ujerumani. British Army of the Rhine ilikuwa na shule kadhaa ambako watoto wa wanajeshi walisomeshwa, nami ningefundisha katika Windsor Boys School ambayo, kama shule dada yake ya Wasichana, ilikuwa makao ya wanafunzi zaidi ya 500 wa sekondari.

Nilikuwa mwalimu mdogo kuliko wote aliyewahi kuajiriwa na Ministry of Defense wakati ule, bila kuwa nimefanya “National Service,” wala miaka mitano ya uzoefu wa ualimu uliohitajika kwa kawaida.

Sikuwa nimeyatambua masharti hayo nilipoomba mara ya kwanza, kwa kusitasita, kufundisha na B.O.A.R. hivyo nilivunjika moyo kidogo nilipopokea kukataliwa kwao kwa kwanza. Nilikuwa nimeacha kabisa kufikiria nafasi ya ualimu ya namna hiyo, ndipo miezi michache baadaye, barua nyingine ikafika ikiniambia kwamba kulikuwa na nafasi ya kufundisha huko Hamm, Ujerumani Magharibi. Inaonekana, mwalimu wa fizikia wa shule ile alikuwa amepandishwa cheo kuwa Naibu Mkuu wa Shule, nami nilikuwa mwalimu pekee wa fizikia mwenye sifa zinazofaa waliyekuwa naye katika daftari zao. Mungu aweza hata kuyapindua masharti ya jeshi!

Ile ilikuwa miaka mizuri kwa Anne na mimi. Mungu alikuwa ametubariki tayari na binti mmoja Corinne, aliyezaliwa Wales, na sasa akatupa wengine wawili: Andrea na Lynette kuikamilisha familia yetu. Tulipata marafiki wengi Wajerumani na tukafurahia kuishi kati ya tamaduni mbili.

Siku za Jumapili, tulisafiri hadi kambi jirani ya jeshi la Kanada ambako Salvation Army ilifanya ibada ya jioni. Tulipokuwa tukishirikiana pamoja, moyo wangu uliwapenda watu hawa wakarimu kutoka nchi ya wenyeji wa asili na Wainuit, ‘Mounties’ na wawindaji, dubu na tai, na piza na samoni. Hivyo ndivyo, kwa kutiwa moyo nao, tulianza kufuatilia uwezekano wa kufundisha Kanada.

Punde nilipokea barua ikinijulisha kwamba nilikuwa nimekubaliwa kufundisha Fizikia katika chuo maarufu cha ufundi huko Toronto, Kanada. Ilinipasa kuwatumia nakala za vyeti vyangu vya shahada na diploma ili kuthibitisha sifa zangu, nao wangenijulisha mipango ya safari ya ndege kwenda nchi ile kubwa ya kaskazini.

Nyaraka zetu zilitumwa kwa posta hadi Bloor Street, Toronto, na punde jibu likanijulisha kwamba yaelekea ningestahili “Type-A Specialist Diploma.” Uchunguzi wa kina wa kitabibu ukafuata viza vikapatikana, barua yangu ya kujiuzulu ikatolewa shuleni, nasi tukangoja… Barua ya pili haikupendeza hivyo! Kosa lilikuwa limefanyika! Mkurugenzi wa Elimu wa hapo alikuwa amemteua mwalimu kuijaza nafasi yangu bila kujua kwamba Mkuu wa Chuo alikuwa tayari amenikubali! Walimu watatu walikuwa wameteuliwa kwa nafasi mbili, na kwa kuwa mimi nilitoka nje ya nchi, mimi ndiye niliyepaswa kuvunjika moyo.

Aibu ilikuwa kubwa tulipowaambia rafiki zetu habari za karibuni. Tulikuwa tumetoa ushuhuda wa kung’aa namna ile wa wema wa Mungu kwetu na sasa ilionekana kuwa maneno matupu tu. Hatukuwa na kazi kwa mwaka mpya wa shule na ingetubidi kurudi Wales kutafuta kazi nyingine kwa angalau muhula mmoja. Maombi yetu yalikuwa yamejaa maswali, bila kutambua kwamba Bwana alijua barabara alilokuwa akilifanya!

Siku tatu baadaye barua nyingine ikafika. Hii ilitoka kwa Jeshi la Uingereza wakisema jinsi walivyosikitikia kujiuzulu kwangu na kunialika nifikirie tena. Waliandika, “Tuna nafasi nyingine iliyo wazi ya mwalimu wa fizikia huko Hong Kong. Je, tafadhali unaweza kuifikiria nafasi hiyo na kutujulisha uamuzi wako mapema iwezekanavyo?”

Kwa kuwa rafiki zetu wa karibu zaidi nao walikuwa wakienda Hong Kong, uamuzi ulikuwa rahisi kuufanya. Tungegundua tena kwamba Bwana alikuwa hatua chache mbele yetu.

Ukurasa 1 / 4 · 5 dakika zimebaki katika sura