Sura 4 · dakika 5 za kusoma
Nitatangulia Mbele Yako
Niliifurahia siku ile pamoja na Don Evans na mara nyingi nilimfikiria katika miezi iliyofuata, bila kudhania hata kidogo jinsi njia zetu zingekutana tena.
Niliendelea na masomo yangu ya hisabati na Fizikia nikiwa na tumaini la kwenda chuo kikuu mwaka uliofuata. Masharti ya kuingia chuo kikuu yalikuwa kwamba ilibidi uchague vyuo vinne, uvipange kwa mpangilio wa upendeleo, na kuwasilisha orodha ile kwa wakala mkuu. Kisha wangekujulisha kiwango cha kitaaluma ulichohitaji kufikia katika kila somo, ili kila kimoja cha vyuo hivyo kikupokee kuwa mwanafunzi. Birmingham kilihesabiwa kuwa na kitivo bora zaidi cha Hisabati - somo langu hodari - hivyo kikawa cha kwanza katika orodha yangu, kikifuatiwa na Cardiff, Swansea, na Aberystwyth.
Saa nyingi za kusoma kwa bidii zilitangulia zile wiki mbili za kutisha za mitihani ya ngazi ya juu katika masomo yangu matatu: hisabati safi, hisabati tumizi, na fizikia. Ilikuwa kwa furaha kubwa (na mshangao kidogo), niliposikia wiki kadhaa baadaye kwamba nilifaulu katika masomo yote kwa alama za kutosha kufikia viwango vyote vilivyohitajika. Hadi wakati ule sikuwa na shaka kwamba Birmingham ndicho kilikuwa lengo langu, lakini sasa mawazo mengine yakaanza kujitokeza. Mahali papya palikuwa pakija akilini. Birmingham kilikuwa “cha kiwanda mno” Cardiff kilikuwa “karibu mno,” na Swansea kikawa “bora kuliko vyote.”
Hivyo nilimwandikia mchungaji wa Elim Church huko Swansea nikiomba msaada wake katika kutafuta mahali pa kukaa kwa mwanafunzi mpya wa chuo kikuu. Nilikuwa mjinga kiasi kudhani kwamba mchungaji alikuwa na wakati wa kutafuta nyumba namna hiyo, hivyo nilikuwa bado sina anwani wakati barua ilipofika iliyonitikisa hata nikachukua hatua.
“Tunasikitika kwamba hatutaweza kukutumia ruzuku kwa ajili ya gharama za masomo, vitabu, na malazi kwa mwaka ujao ikiwa hutaweza kutupatia anwani yako huko Swansea. Tarehe ya mwisho ya kutoa taarifa hizo ni…” Tarehe hiyo ilikuwa Jumatano iliyofuata, siku tano tu mbele!
Ingawa Swansea ilikuwa maili 30 tu kutoka nyumbani kwangu, nilikuwa nimefika huko mara moja tu maishani mwangu kwa ziara ya alasiri pamoja na mjomba wangu kutazama mchezo wa kriketi. Siku ile barua ilipofika nilikuwa njiani tena, nikitumaini kulipata Elim Church na mchungaji wake. Niliteremka basi katikati ya mji nikaingia kibanda cha simu nikitumaini kupata anwani na namba ya simu ya ofisi ya Elim Church. Ingawa nilitafuta kwa makini katika kila njia iwezekanayo, sikupata Elim Church yoyote iliyoorodheshwa katika kitabu kile. Wasichana wawili waliokuwa wamesimama nje ya kibanda waliona wasiwasi wangu wakajitolea kunisaidia. Nilitilia shaka kama wangeweza kunisaidia nilipowaeleza tatizo langu; hata hivyo, kwa mshangao wangu mkubwa, si tu kwamba walijua mahali nyumba ya mchungaji ilipo na basi ambalo ningelihitaji kufika huko, bali pia waliweza kunitia moyo, kwa kuwa wote wawili walikuwa waaminio pia! Nilikumbuka kwamba Biblia ilinena juu ya uwezekano wa sisi ‘kuwakaribisha malaika bila kujua.’
Mchungaji alipotambua kusudi la ujio wangu, aliomba radhi kwa dhati kwa kuwa alikuwa amesahau kulifuatilia ombi langu. Kikombe cha chai hakikufanya lolote kutuliza wasiwasi niliokuwa nikianza kuuhisi alipokuwa akipekua meza yake akitafuta orodha ya wenye nyumba ambao wangeweza kunipokea. Alikuwa ameiandaa orodha hii wakati barua yangu ilipofika wiki kadhaa mapema, lakini shughuli nyingi za ofisi ya uchungaji zilikuwa zimemlemea, na ombi langu likawa limemtoka akilini. Dakika chache baadaye, akiwa na ile orodha mkononi mwake, tuliingia katika gari lake tukaanza safari kuelekea zile nyumba nane ambako alidhani ningeweza kupata mahali pa kukaa. Tulipokuwa tukipita Singleton Park, ambako chuo kikuu kipo, ghafla alikanyaga breki akageuza kuingia kijia kembamba kando ya bustani ile.
“Kuna mama mmoja hapa aliye na wavulana mapacha,” akasema. “Mmoja wao anakwenda Chuo cha Biblia, na mwingine ataanza chuo kikuu pamoja nawe. Sina jina lake katika orodha yangu, lakini heri tuanze utafutaji wetu kwa kumwuliza yeye, kwa kuwa tunapita karibu sana na nyumbani kwake.”
Nikafikiri moyoni, “Upumbavu ulioje! Hakuna mama atakayemruhusu mtu mgeni achukue nafasi ya mmoja wa wanawe mapacha!”
Kwa moyo uliokata tamaa, niliketi ndani ya gari huku mchungaji akizungumza na yule mama nyumbani. Hakuonekana na matumaini mengi aliporudi. Mimi nilihisi matumaini machache hata zaidi.
“Karibu ndani. Anataka kukutana nawe,” akasema bila shauku kubwa.
Niliingia ndani ya nyumba ile nikasikiliza huku mama wa nyumba akieleza shaka yake kwamba wanawe wasingekubali yeye kumruhusu mgeni akodishe chumba chao; hata hivyo, alisema angewauliza kisha anijulishe. Bila shaka, hilo halikuwa na faida kubwa kwangu kwa kuwa nilikuwa tayari nimefika tarehe ya mwisho ya kuamua makazi yangu ya chuo kikuu. Akijibu swali la mchungaji kuhusu mahali walipo wanawe, alisema, “Russell yuko chuo kikuu na Don yuko juu mtaani katika duka la hapa.”
“Don?” nikasema, kumbukumbu yangu ikirudi kwenye mchezo wa kriketi wa karibu mwaka mmoja uliopita, “Umesema Don? Alikuwa nahodha wa timu ya kriketi ya Swansea Grammar School mwaka jana?”
“Ndiyo!” likaja jibu huku sura niliyoifahamu ikiingia kupitia mlango wa mbele. Siku ile hakuwa katika nguo nyeupe za kriketi, lakini uso wake ulikuwa na tabasamu lile lile la kupendeza nililolikumbuka.
“Mama, huyu ni Gareth. Ndiye yule kijana niliyekutana naye Cowbridge. Yule niliyekuambia habari zake. Yule Mkristo mpya!”
Nilimwambia kwamba nilikuwa nikitafuta mahali pa kukaa kwa muda wote wa masomo yangu katika Swansea University, ndipo akanikumbatia na kwa shauku kubwa akasema, “Mama, na achukue chumba changu!”
Kupitia bega la Don, nilimwona mama yake akininyooshea mikono yake, akinikaribisha katika nyumba ile ya ajabu. Nilikuwa nimepata nyumbani papya na familia ambayo punde ingekuwa karibu nami kama vile familia yoyote ya damu ingavyoweza kuwa.
Nikaanza kujiuliza, “Je, Mungu alikuwa kwenye mchezo ule wa kriketi? Je, alikuwa tayari akipanga makazi haya?”
Nina hakika kwamba alikuwepo! Wakati mimi nilipokuwa nimepanga kuhudhuria Birmingham University, yeye alikuwa akiniandalia nyumbani huko Swansea, na sasa alikuwa ameniongoza kwa mtu pekee niliyemjua katika mji ule wote - mji wenye watu zaidi ya 100,000!