Sura 3 · dakika 5 za kusoma

Safari Yaanza

Ibada ilikuwa imekwisha katika kanisa lile dogo, na kikundi kidogo cha vijana kikakusanyika kumzunguka yule mhubiri kijana. Tulikuwa tumekwenda jioni ile kumtia moyo kwa kuwa alikuwa mgeni katika kazi ya uhubiri wa walei, kazi iliyo ya lazima sana kwa vikanisa vingi vidogo vya Wales. Ujumbe wake umesahaulika tangu zamani, lakini mazungumzo yaliyofuata hayajasahaulika. Tulizungumza kuhusu shule yangu, Cowbridge Grammar, ambako yeye alikuwa mwanafunzi miaka miwili tu kabla yangu, kisha Aneurin akauliza swali lililoyabadili maisha yangu.

“Niambie, Gareth,” akasema, “utafanya nini na Bwana Yesu Kristo?”

Ni wiki tano tu zilizopita nilipoingia kwa mara ya kwanza nyumbani kwa Vince na Betty Bishop. Walifanya mikutano ya vijana ambayo dada yangu Barbara aliihudhuria kila jioni ya Ijumaa. Huko waliimba nyimbo za shangwe, wakacheza maswali ya Biblia na, mara kwa mara, kuwa na mzungumzaji mgeni. Nilihudhuria Shule ya Jumapili hadi mama yangu alipofariki nilipokuwa na miaka kumi na minne, lakini sasa sikuwa na shauku sana katika mambo ya kiroho. Hata hivyo, kwa mwaliko wa Barbara, nilijikuta nimeketi katika kiti cha pembeni chenye starehe sebuleni kwa akina Bishop, na ilinibidi nikiri kwamba nilifurahia. Utaelewa kwamba hilo lilikuwa rahisi, kwa kuwa nilikuwa mvulana pekee pale na wasichana 15! Nilidhani hiyo ndiyo sababu ya Betty kuniita jikoni mwishoni mwa jioni ile wakati vinywaji baridi na biskuti vikiandaliwa.

Bila shaka, angetarajia mimi niingize ile trei nzito ya vinywaji.

Sikutarajia kwamba angesema alilolisema alipogeuka na kunitazama. “Niambie, Gareth,” akasema, “utafanya nini na Bwana Yesu Kristo?”

Katika shughuli nyingi za jikoni ile, kulikwepa swali lile kulikuwa rahisi, lakini haikuwezekana kuliondoa akilini mwangu hadi yule mhubiri kijana aliponipa changamoto tena. Wakati huo huo, nilikuwa nimekuja kutambua kwamba Ukristo hautangazi kifo cha Yesu msalabani tu, bali pia kufufuka kwake kutoka kwa wafu. Nikaanza kufikiri kwamba kama kweli amefufuka kutoka kwa wafu, basi yu hai; kwa hiyo, inawezekana kumjua yeye binafsi. Kila wiki nilikuwa nimefanikiwa kuepuka kuwa peke yangu na Betty kwa kuwa nilijua angeliuliza tena swali ambalo sikuwa na jibu lake, lakini sasa swali lile lilikuwa limenifikia. Wengine walipotembea pamoja na Aneurin hadi kituo cha mabasi, mimi nilipanda kilima kuelekea nyumbani. Nilipoingia chumbani mwangu, nilipiga magoti kando ya kitanda na kuomba sala rahisi.

“Bwana Yesu, kama wewe ni halisi, tafadhali ingia katika maisha yangu, uiondoe dhambi yangu na unifanye kuwa wako.” Sikujua la kusema zaidi, hivyo niliendelea na maneno ya wimbo mmoja rahisi niliokuwa nimeujifunza karibuni. “Moyoni mwangu, moyoni mwangu, njoo moyoni mwangu, Bwana Yesu. Njoo leo, njoo ukae, njoo moyoni mwangu, Bwana Yesu. Amina.” Sikutambua hata kidogo safari ya kusisimua ya imani niliyokuwa nimeianza.

Wengine wanaweza kusema kwamba ilikuwa ni sadfa tu kwamba Aneurin angeuliza swali lile lile nililokuwa nikilikwepa, lakini nimekuja kuona mifano mingi sana ya Mungu kuingilia maisha yangu kwa njia hizo za ‘kibahati,’ hata sasa nayatambua kuwa ni miadi ya Mungu; mawe ya kukanyagia katika mwenendo wangu wa imani. Kusudi langu katika kitabu hiki ni kukutambulisha kwa Mungu anayejishughulisha kumwongoza kila mmoja wetu kuingia katika mwenendo wa karibu naye mwenyewe. Yeye hufungua milango na kuifunga; huongoza katika mabonde na juu ya vilele vya milima; huyachukua masikitiko yetu na kuyafanya kuwa miadi yake.

“Mungu anapotaka kumzoeza mtu...

na kumsisimua mtu...

na kumpa mtu ustadi; Mungu anapotaka kumfinyanga mtu ili acheze fungu lililo tukufu kuliko yote; anapotamani kwa moyo wake wote kumuumba mtu mkuu na jasiri kiasi kwamba ulimwengu wote utashangaa, Tazama mbinu zake! Tazama njia zake!

Jinsi anavyowakamilisha bila huruma - wale anaowachagua kifalme; jinsi anavyompiga nyundo na kumwumiza na kwa mapigo makuu kumgeuza kuwa mabonge ya udongo ya majaribu ambayo Mungu peke yake aweza kuyaelewa!

Huku moyo wake uliolemewa na mateso ukilia naye akiinua mikono ya kusihi!

Jinsi anavyowainamisha, lakini hawavunji kamwe wale ambao mema yao anayachukua; jinsi anavyowatumia wale anaowachagua, na kwa kusudi la upendo huwayeyusha, kwa nafsi iliyolemewa humshawishi kuujaribu utajiri wa Mungu.

Mungu anajua analolifanya!”

-Bila jina Katika miezi iliyofuata sala yangu ile rahisi, nilikua sana katika kuzielewa kweli za msingi za Biblia. Nilibarikiwa kuwa na walimu wazuri waliompenda Bwana na Neno lake. Nilikuwa nimejiunga na kanisa nami nilikuwa mwenye bidii katika kikundi chao cha vijana kilichoitwa, “The Crusaders.” Nilianza kuugundua utajiri wa urithi wetu ndani ya Kristo - tunda la Roho wake. Kweli, “Mbingu juu ni buluu laini zaidi, dunia kotekote ni kijani tamu zaidi. Kitu fulani chaishi katika kila rangi ambacho macho yasiyo na Kristo hayajapata kukiona” (G Wade Robinson). Zile zilikuwa siku tulizoonyesha utii wetu kwa kuvaa ‘vibamba’ vya kifuani. Vingine vilitangaza kuunga mkono klabu ya soka ya hapo, vingine nyota mpya wa burudani. Changu kilisema tu, “Elim Crusader.” Si cha kutia moyo sana, lakini chenye maana kubwa.

Kiangazi kilichofuata, nilisimama nikitazama timu yetu ya kriketi ikicheza na mmoja wa wapinzani wao wakali - shule ya sekondari ya Swansea. Wageni walipiga mpira wakihangaika mbele ya warushaji wetu, nami nilizama sana katika mchezo ule.

“Naona wewe ni wa Elim Crusaders,” ilisema sauti iliyokuwa karibu. “Nadhani unamjua Bwana.”

Niligeuka nikaona kwamba mtu aliyekuwa akizungumza nami alikuwa mchezaji kutoka timu ya wageni. Alionekana kama mwanariadha hodari katika ‘nguo zake nyeupe za kriketi,’ na tabasamu lake la kuvutia lilialika urafiki.

“Nda-ndiyo,” nikagugumia, kwa kuwa nilikuwa bado sijakutana na mtu aliye wazi hivyo katika kuidhihirisha imani yake. “Ndiyo, ninamjua.”

Punde tukaanza kutembea kuzunguka ukingo wa uwanja wa kriketi. Tukafahamiana na kuzungumzia urafiki wetu mpya ndani ya Kristo. Tulipofika tu kwenye lango la viwanja vya michezo vya shule, mwalimu wangu wa zamani wa Kilatini, mtu mkali wa kazi ambaye pia alikuwa mteuzi wa timu ya kriketi ya Welsh Schoolboys, akaingia. Rafiki yangu mpya alikuwa akiangaliwa kwa nafasi katika timu ya Wales, hivyo mwalimu wangu alimjua kweli. Mimi pia nilijulikana, si kwa ustadi wangu uwanjani mwa kriketi, bali kwa ujinga wangu katika darasa la Kilatini! Alijua pia kwamba majina yetu ya ukoo yalikuwa sawa - Evans.

“Habari, Don! Habari Gareth!” akasema, kisha akaongeza, “Je, ninyi wawili ni ndugu?”

Swali lile lilisikika la kipumbavu sana kwa kuwa tuliishi umbali wa zaidi ya maili thelathini, hivyo nilishtuka kumsikia Don akijibu, “Ndiyo bwana! Ndugu katika Bwana!”

Ile ilikuwa mara ya kwanza kwangu kumsikia mtu akiisema imani yake kwa ujasiri, nami niliona aibu kubwa sana.

Hapa kuna dokezo la kuvutia; miaka mingi baadaye ningetembelea kanisa moja huko Cardiff nikiiwakilisha Anastasis. Huko, mzee mmoja wa kanisa lile alijua kwamba nilikuwa nimesoma katika Cowbridge Grammar School, akaniuliza kama nilimjua Sid Harris, yule mwalimu wa Kilatini. Ndipo nikagundua kwamba Sid alikuwa amefariki hivi karibuni, akiwa amekuwa mzee mwaminifu katika kanisa lile kwa miaka mingi. Najiuliza, je, ushuhuda wa Don siku ile ulikuwa na athari yoyote kwa Sid baadaye katika kuwa mwamini?

Ukurasa 1 / 4 · 5 dakika zimebaki katika sura