Sura 37 · dakika 5 za kusoma

Kugusa Mizizi Yangu

Niliporudi kutoka Scotland mwezi Desemba 2008, nilikwenda kumwona daktari wangu kama ilivyotakiwa, nikiamini kabisa kwamba nilikuwa nimeponywa saratani yangu, kwa hiyo nilishangaa sana alipokuta uvimbe mitatu umetokea ukutani mwa kibofu changu. Kwa kuwa ‘kukwanguliwa’ kule kwa awali kulikuwa kumeonyesha saratani ya daraja la juu, akasema, “ni lazima tuzitoe haraka.” Yaonekana ‘haraka’ yake ilimaanisha majuma matano kwa maana, Krismasi ikikaribia na likizo yake ikiwa imepangwa, nisingelazwa hospitalini hadi mwaka mpya. Upasuaji wa pili ulinisababishia mkakamao wenye maumivu makali kuliko yote niliyowahi kupata, lakini ni dhahiri ulifanikiwa, kwa kuwa sasa sina dalili zozote za saratani ndani yangu.

Katika miezi mitatu iliyofuata nilipata sindano ya kila juma kwenye kibofu changu ya kifua kikuu cha ng’ombe, ambayo yaonekana ndiyo tiba ya kawaida ya saratani ya kibofu. Baada ya tiba ya namna hiyo, ni kawaida mtu kumwona daktari wake kila miezi mitatu kwa miaka miwili kabla haijaongezwa kuwa kila miezi sita, na ndivyo ilivyokuwa nilipotoa ombi la pekee. Steve Evans wa Cardigan, Wales alikuwa akiwasiliana nami kuona jinsi nilivyokuwa nikiendelea na saratani, naye alikuwa amelichukua neno nililolisema nilipokuwa naye. Alinialika nirudi Wales kunena katika kanisa lake katika ‘kongamano la uamsho’ na kubaki nikihudumu katika kanisa lake kwa muda mrefu.

Ningezamishwa katika utamaduni unaozungumza Kiwelisi kama ilivyokuwa ndoto niliyoieleza. Akaongeza kwamba gari lingepatikana kwangu, na kwamba ningeweza kuitunza nyumba ya Dick wakati akiwa katika likizo yake ya masomo ya majuma saba huko Marekani. Ndivyo ilivyokuwa kwamba nilimwuliza daktari wangu kama ingewezekana nibaki Uingereza hadi juma la kwanza la Agosti, wakati Karys, mpwa wake Anne, angetimiza miaka 50, yaani majuma matatu zaidi ya ziara yangu iliyofuata iliyopangwa. Alikubali kwa urahisi akisema, “Gareth, mtazamo wako na mtindo wako wa maisha vinanisadikisha kwamba saratani hii haitarudi, lakini hata ikirudi, tutakuwa na muda wa kutosha wa kuitibu. Nendeni mkajifurahishe.”

Mimi na Anne tuliwasili Cardigan juma la kwanza la Mei 2009, bila kujua kwamba baadaye sote tungeiona miezi hii mitatu kuwa ‘likizo nzuri kuliko zote tuliyopata kuwa nayo!’ Tangu mwanzo, ‘tuliwapenda’ watu wa Mt Zion Baptist Church, ambako hisia yangu ilikuwa kwamba ‘uamsho u karibu.’ Nilinena huko mara nyingi lakini nilibarikiwa zaidi Steve Evans alipohubiri jumbe nne juu ya ‘bonde la mifupa mikavu.’ Upako ulioje juu ya mahubiri yake! (Waweza kuzisikiliza jumbe hizi kwenye tovuti yangu - ‘links’ www.garethevansministries.org) Mikutano ya maombi ilikuwa ya kutia moyo sana, watu zaidi ya 25 wakihudhuria kila juma (kutoka kusanyiko la watu wapatao 100), hali uimbaji ulikuwa... naam, wa Kiwelisi! - wa moyo, wa kuchangamsha, wenye upatano na shauku. Nilikuwa katika hali yangu niipendayo! Nyumba ya Dick ilikuwa kibanda kizuri kilichoelekea korongo ambamo ulipita, kimya na wenye kina, Mto Teifi ukielekea baharini kupita mji wa Cardigan.

Kingo za korongo zilifunikwa na miti, na ishara nyingine pekee ya makazi ilikuwa ngome ya kale ya Kilgerran juu kilimani. Dick na mkewe Mguatemala, Gladys, walikuwa wawili wa ajabu. Walikuwa wamekuja kuyatoa maisha yao katika maombi kwa ajili ya nchi ambayo hakuna hata mmoja wao mwenye mizizi ndani yake, lakini ambayo Bwana ameiweka mioyoni mwao, hadi uamsho utakapokuja tena. Wakati wa kuandika haya, waweza kufuatilia yote wanayoyafanya kwenye tovuti yao, www.walesawakening.org .

Mengi ni mambo makuu ya wakati ule mzuri – kutembea majabalini kando ya pwani yenye miamba, kumtembelea Doreen kipofu, mtakatifu mwombaji, kuzunguka barabara za mji ule mdogo wa soko – na kunena Kiwelisi! Naam, niliweza kuyafanyia mazoezi yote niliyojifunza kwa masomo ya Kiwelisi ya BBC Wales, nikisaidiwa na Steve na Sulwen, na kwa kuhudhuria darasa la ‘wanafunzi wa kati.’

Huko hata nilitoa wasilisho mbele ya darasa, nikinena Kiwelisi tu na, kwa mujibu wa mwalimu, kwa matamshi mazuri sana. Mada yangu ilikuwa pendo langu la sasa – kujifunza lugha. Baada ya Dick & Gladys kurudi kutoka Marekani, tulikaribishwa katika B&B nzuri mbele zaidi kando ya pwani kwa juma moja, kwa sehemu ndogo ya gharama ya kawaida, kabla ya kuitunza ‘jumba’ la hapo kwa majuma mawili – nyumba ya fahari ya mshiriki wa kanisa.

Tulibarikiwa sana na watu hawa wote wa thamani! Siku moja, wanandoa walikuwa wamesimama nje ya Mt Zion wakitazama ubao wa matangazo, ndipo Arlene, mmoja wa washiriki, akatoka kanisani, na alipoona wanaonyesha hamu kubwa hivyo, akaanza kusema nao.

Walikuwa wakipita Cardigan katika safari ya kwenda kaskazini mwa pwani pamoja na mwana wao anayeishi Uingereza. Wakaongeza kwamba walitoka Kanada, kwa hiyo Arlene alipokutana na Anne baadaye, alimweleza juu ya mazungumzo yao na kusema kwamba walikuwa wameingia tu katika duka la vitabu vya Kikristo la hapo, mkabala na kanisa. Anne aliingia dukani na kuanza kusema nao.

Walitoka Brentwood Bay, umbali wa maili chache tu kutoka nyumbani kwetu huko Victoria! Waliposikia jina langu, yule mwanamke akapaza sauti kwa msisimko, “Tumekuwa tukimwombea kwa miezi minne iliyopita!” Ni dhahiri kwamba walikuwa wamesikia juu ya saratani yangu nao wakajitoa kuniombea ingawa hawakunijua mimi binafsi. Ni baraka iliyoje kuwa mmoja wa jamaa ya Mungu, tukijua kwamba hakuna wageni katika jamaa hii, ila ndugu tu ambao hatujapata kukutana nao.

Kabla ya kurudi Loughor kwa wakati wa sherehe ya Karys, tuliamua kufanya safari kuvuka Uingereza ili kumtembelea binamu yangu Christopher na mkewe (Dame) Elsbeth Thomas. Elsbeth alikuwa amepewa heshima ya ushujaa na malkia kwa utumishi wake kwa British Red Cross ambayo alikuwa Rais wake. Pia alimjua Princess Diana vyema kabla ya kifo chake cha ghafla. Christopher na Elsbeth walikuwa wametualika mimi na Anne tukae nao Cambridgeshire kwa siku chache, mwaliko tuliokuwa na hamu ya kuukubali.

Njiani tuliwatembelea Ivor na May Sherwood, Wasomaji wa Maandiko wastaafu tuliokutana nao kwa mara ya kwanza Ujerumani mwaka 1964, Marion (na John) Palmer, rafiki yake Anne tangu siku za shule, na binamu yangu mwingine Cynthia (na Bill Brown), pamoja na binamu yake Anne, Gwilym (na Sue) Edwards. Safari iliyoje ya ajabu, iliyojaa kumbukumbu na mwisho unaostahili wa likizo yetu ya Wales. Kilibaki kimoja tu – kuifurahia sherehe ya miaka 50 ya Karys, tuliyoiadhimisha na marafiki zake wengi katika karamu nzuri. Tulirudi nyumbani kwenye habari njema kwamba saratani haikuonyesha dalili za kurudi.

Ukurasa 1 / 4 · 5 dakika zimebaki katika sura