Sura 36 · dakika 9 za kusoma
Ule Ugonjwa Mkubwa
Mwezi Aprili 2008, nilipata mwaliko mwingine wa kulitunza kanisa lililokuwa likitafuta mchungaji. Bethel Baptist Church ya Sidney, BC walikuwa katikati ya mradi wa ujenzi na, mchungaji wao alipostaafu, wakaniita niwasaidie. Huko tulipata wakati mzuri sana tukipata marafiki wapya wengi, lakini pia nilipata heshima ya mashaka ya kusoma maombi zaidi ya 250 ya watarajiwa wa uchungaji! Sidney ni safari fupi kwa gari kutoka nyumbani kwetu, kwa hiyo nilisafiri kwenda huko siku nyingi za juma, wakati wangu huko ukiisha mwezi Oktoba, kwa wakati barabara wa Kongamano la Uamsho la Atlanta.
Katika kiangazi cha 2008, kabla ya kongamano la Atlanta, binamu yake Anne, Bernard, na mkewe Pam, walikuja Kanada likizoni. Tulisafiri kukutana nao Calgary, na kutoka huko tukaendesha gari kupitia Milima ya Rockies ya Kanada hadi Victoria. Tulipata wakati mzuri sana pamoja kwa kuwa walikuwa wamekodi gari zuri la safari (RV). Muda mfupi baada ya kufika nyumbani, mimi na Bernard tulipanda mlima wa hapa, Mount Finlayson. Ilikuwa kupanda kwa taabu, lakini msisimko ulikuwa wa ajabu tulipofika kileleni.
Usiku ule kabla tu ya kwenda kulala, nilitokwa na damu nyingi katika mkojo wangu. Wasiwasi wetu ulitosha kumfanya Bernard anipeleke idara ya dharura ya hospitali yetu, ambako daktari alisema nilikuwa ‘nimepasua mshipa wa damu’ kwa sababu ya kupanda kule kwa taabu alasiri ile.
Hata hivyo, kwa tahadhari, alipanga nimwone daktari bingwa wa mkojo majuma kadhaa baadaye. Ripoti yake tena ilikuwa ya kutia moyo sana – hakuna dalili ya tatizo lolote, lakini alipoona kwamba ningepita mahali pa kupiga picha kwa sauti nikiwa njiani kurudi nyumbani, alishauri niingie kwa uchunguzi mwingine. Hilo likifanyika, nilisahau kabisa juu ya kutokwa damu.
Majuma mawili baadaye daktari wangu alinipigia simu kusema kwamba uchunguzi wa sauti ulikuwa umeonyesha dalili ya vidonda kwenye kibofu changu, kwa hiyo ‘afadhali tuwe salama kuliko kujuta.’ Aliingiza kifaa chake cha uchunguzi, akaangalia, kisha akasema kwa mtindo wa kawaida kabisa, “Ndiyo, una saratani!” Hili halikutarajiwa kabisa kwa kuwa nilijihisi mzima kabisa bila usumbufu wowote. “Ni lazima tuikwangue hii haraka iwezekanavyo,” akaongeza.
Siku mbili baadaye nyumbani, nilimwambia Anne, “Je, tunakataa kuukubali ukweli au ni nini? Sijahisi hata dakika moja ya wasiwasi tangu nipokee habari hii mbaya.” Tena, tulikuwa tumeuonja ule “amani ipitayo akili zote.” Majuma kadhaa baadaye, nilikuwa mnenaji katika kambi ya wazee nami nikapata nafasi ya kuzungumza juu ya amani hii ya ajabu. Sikutambua kwamba jambo hili lingekuwa la wasiwasi mkubwa kwa baadhi ya wasikilizaji wangu, ambao waliinua jeshi la waombezi kwa ajili yangu. Hata nilijisoma mimi mwenyewe katika gazeti la Kikristo la hapa, ambako walikuwa wameandika kwamba nilikuwa ‘nikishindana na saratani.’
Nilimtafuta mhariri ili kumsahihisha kwamba sikuwa ‘nikishindana’ bali nilikuwa nikipumzika katika Bwana. Upasuaji wangu ulipangwa, kisha nikatakiwa kumtembelea daktari wangu kwa ajili ya ziara ya kwanza kati ya ziara nyingi za kila miezi mitatu. Ni kati ya ziara hizi ndipo nilisafiri kwenda Atlanta kwa kongamano lililofuata. Tazama tena hapa, majaliwa makuu ya Mungu yalivyokuwa. Kama nisingeupanda ule mlima, huenda nisingetokwa na damu jioni ile. Kama nisingekwenda idara ya dharura, huenda ningekuwa na saratani hii kwenye kibofu changu bila ya kugunduliwa hadi baadaye sana, wakati ambapo huenda ingekuwa imekwisha kuenea kupita hali ile tuliyoikuta.
Baada ya kongamano la Atlanta, tulikuwa na kongamano jingine lililopangwa kwa ajili ya Greenock, Scotland, mwezi Novemba 2008. Nilimjulisha Greg kwamba nisingekwenda Uingereza kwa ajili ya siku nne tu za kongamano, bali ningetumia nafasi hiyo kuwatembelea marafiki zangu huko Wales njiani, nikifika angalau majuma matatu kabla ya mikutano iliyopangwa. “Kwa nini usije nami?” nikauliza, nikiongeza kwamba ningefurahi kumzungusha katika mahali panapohusiana na uamsho wa Wales wa mwaka 1904.
Greg alikubali upesi, kwa hiyo maandalizi yakafanywa ya kukutana London, pamoja na kijana mwingine mwenye upako, Eli Brayley (www.timothyministry.com).
Tulipowasili, tulisalimiwa na kijana mmoja aliyetupa funguo za gari lake akiwa na maneno haya – “Hili ni lenu kwa muda wote mtakaokuwa Uingereza!” Baraka iliyoje! Hata hivyo, Greg na Eli walipoiangalia zawadi hii, nyuso zao zilibadilika kidogo nao wakasema, “Hatuwezi kuendesha gari hilo! Lina gia ya mkono nasi hatujawahi kuendesha gari la namna hiyo – tena, itatubidi kuendesha upande usio sahihi wa barabara!” Bila shaka, ilinibidi niwe dereva wao kwa majuma matatu yaliyofuata.
Niliendesha gari kwa saa tatu hadi Wales, nikiwapeleka katika mabonde nilikofundisha na ndani ya Bonde la Rhondda (Cwm Rhondda), ambako ‘wana’ wangu wa Kikanada walionja fish & chips halisi pamoja na njegere zilizopondwa. Rafiki yangu mpendwa Rob Ash na familia yake walitupokea usiku mbili huko Bridgend tulipotembelea maeneo yangu ya zamani, tukaiona nyumba ambamo nilizaliwa mara ya pili na ngome nilimocheza, na tukakutana na baadhi ya watakatifu wapendwa wazee wa miaka yangu ya ujana nikiwa mwamini.
Oswald Penry, kwa sasa katibu wa Keswick huko Wales, alikuwa na hadithi nyingi za siku zile za uamsho, kwa kuwa babu yake alikuwa mtu maarufu sana katika huduma wakati ule. Alipokuwa akiwasimulia baadhi ya hadithi hizi kwa marafiki zangu wawili waliokodoa macho, shemeji yake, mchungaji mstaafu wa Kibaptisti aliyeishi jirani, aliingia chumbani na kujiunga nasi katika kusikiliza. Kisha akatualika kwenye karakana yake, ambako aliweka maktaba yake kubwa ya vitabu vya theolojia. “Chagueni mpendacho!” akawaambia wale vijana. Mwanzoni walisitasita, lakini alipowahimiza tena, wakaanza kukichunguza kisanduku hiki cha hazina kwa hamu.
Dakika kumi na tano baadaye, walitoka kila mmoja akiwa na vitabu hata kumi, vya Eli vikiwa hasa vya mafundisho ya Kireformed na vya Greg vya wapuriti wa kale. Tayari walikuwa wakibarikiwa na ukarimu wa nchi yangu ya asili.
Kutoka Bridgend, tulisafiri hadi Swansea na nyumbani kwa shemeji yangu huko Loughor. Huko tulitembelea kanisa la Moriah ambako Evan Roberts alianza huduma yake na Mungu akaanza kuwaingiza roho wengi kanisani.
Mzee mmoja wa hapo, Dyffrig, alikuwa mkarimu sana, akitumia muda mwingi kutuonyesha kumbukumbu na kusimulia hadithi nyingi za wakati ule. Tuliposema tungependa kutumia muda kidogo katika maombi hapo, alikuwa na hamu ya kujiunga nasi, kwa hiyo saa moja ya thamani ilitumika mahali pale ambapo Mungu alitenda kwa nguvu karne moja iliyopita.
Greg alinijulisha kwamba alikuwa amepokea barua pepe kutoka kwa Dick Funnel, Mmarekani anayeishi Wales ya Magharibi, aliyebarikiwa na tovuti ya sermonindex na kutamani tutembelee eneo lake tukiwa njiani kwenda Scotland. Kwa kweli, Wales ya Magharibi iko mbali sana na njia ya Scotland, lakini nililazimika kusafiri magharibi kwa kuwa Greg alikuwa amekubali mwaliko huo, na Dick, akiwa ametuahidi huduma kwa wikendi, angekuwa nyumbani kwake karibu na Cardigan.
Tuliwasili jioni ya Ijumaa baada ya mfumo wetu wa GPS kutuongoza kupitia maili nyingi za vijia vya mashambani ambako tungeweza karibu kuvigusa vichaka vya ua kila upande tulipopita, jambo lililowafurahisha na kuwastaajabisha sana Greg na Eli. Nilipangiwa kukaa kwa mchungaji wa Kibaptisti wa hapo, Steve Evans na mkewe Sulwen.
Katika wikendi ile, walinivuta moyo wangu walipojitaabisha kutubariki kwa ziara na nafasi za huduma. Asubuhi ya Jumapili, nilikuwa nimepangiwa kuhubiri katika Cardigan New Life Church, linaloongozwa na wachungaji Doug & Janice Bell. Wakati wa matangazo, Janice alimtambulisha Tony Nam aliyekuwa na ushuhuda wa ajabu wa kuponywa kutoka, kati ya magonjwa yote, saratani ya kibofu.
Baada ya hayo, mwanamume mmoja alisimama kutangaza kwamba naye alikuwa amegunduliwa na saratani ya kibofu, lakini Bwana alikuwa amemponya pia! Kisha mwanamke mmoja akasimama kusema jambo lilo hilo! Sasa Janice akatangaza, “Ni dhahiri kwamba Bwana anafanya jambo hapa kwa ajili ya saratani za kibofu. Kuna mtu mwingine yeyote mwenye saratani ya kibofu?” Sikuweza kuyaamini masikio yangu nilipoinua mkono wangu polepole. Bila shaka, nilitiwa moyo sana walipokusanyika kunizunguka ili kuniombea kwa kuweka mikono.
Sikumbuki kamwe kumsikia mtu yeyote akitoa ushuhuda wa kuponywa saratani ya kibofu kabla ya hapo, lakini hapa nikawasikia watatu ndani ya dakika chache – hakika Bwana alikuwa akinena tena ili kunihakikishia ukaribu wake wakati wa udhaifu wangu. Hakika, alikuwa amepanga niwe katika kanisa lile kwa ajili ya wakati kama huu!
Siku ya Jumatatu, tulisafiri hadi NewQuay ambako Florrie Evans alipaza sauti (kwa Kiwelisi) “Ninampenda Yesu kwa moyo wangu wote” – jambo linalofikiriwa na wengi kuwa ndilo ‘kichocheo’ kilichoanzisha uamsho wa Wales. Kisha tukaendelea hadi Blaenannarch ambako Evan Roberts alipokea Ubatizo wake katika Roho na kulia kwa uchungu, “Ee Bwana, nipinde!” Kutoka hapo, alirudi Loughor na yaliyofuata ni historia – waamini wapya zaidi ya 100,000 ndani ya majuma machache tu! Tukiwa katika kanisa la Blaenannarch, tuliungwa na watu watatu kutoka Swansea.
Steve aliwajua vyema, kwa hiyo alimwalika mmoja wao, mwimbaji wa opera na mwamini mwenye shauku, Huw Priday, atuimbie. Sauti yake ya fahari ilijaza chumba alipoimba wimbo ulioandikwa wakati ule wa uamsho. “Hapa kuna upendo mpana kama bahari, fadhili zenye upendo kama gharika...”
Ee, mioyo yetu ilifurahi kiasi gani maneno haya ya ajabu yalipotuchochea kuwa na shauku ya Bwana kuudhihirisha uwepo wake katikati yetu tena. Kabla ya kuondoka Wales ya Magharibi, neno moja nililolisema kwa bahati kwa Steve Evans lilichochea jibu ambalo lingeniongoza katika mojawapo ya yale mambo ya baraka ambayo Bwana amenijalia. Nilimwambia jinsi ambavyo ningependa kurudi katika sehemu hii ya nchi, ambayo sikuwa nimeitembelea kamwe kabla, ili nijizamishe katika jamii inayozungumza Kiwelisi ambapo ningepata nafasi ya kujifunza lugha ya baba zangu. Siku zote hili limekuwa mojawapo ya majuto yangu makuu – kwamba sizungumzi Kiwelisi, ingawa nimejaribu kujifunza kwa matangazo ya BBC na mafundisho ya mtandaoni. (Jingine ninalojutia ni kwamba sipigi kinanda vizuri – mama yangu alikuwa mpiga kinanda mashuhuri mwenye herufi kadhaa nyuma ya jina lake, lakini kwa masikitiko alifariki katika miaka ya ujana wangu.)
Niliporudi Kanada, Steve angeandika kunialika nirudi Cardigan, ambako tungepatiwa gari, na nyumba ya kuishi kwa majuma kadhaa, na nafasi za huduma pamoja naye katika kanisa la Mt Zion Baptist. Zaidi juu ya wakati ule mzuri nitasimulia katika sura yangu ifuatayo.
Tulipoondoka Wales ya Magharibi, tuliendesha gari kuelekea Scotland, tukisimama usiku wa kwanza nyumbani kwa Netta Rowland, kitukuu wa David Morgan, aliyetumiwa na Mungu kwa nguvu katika uamsho wa Wales wa mwaka 1859. Husemwa juu yake kwamba usiku mmoja ‘alilala kama mwana-kondoo lakini akaamka kama simba; miaka miwili baadaye alilala kama simba akaamka kama mwana-kondoo.’ Netta na mumewe Wynn, sasa wanafuga farasi wakubwa wa magari ya kukokotwa – wanyama wa fahari.
Kongamano la Greenock lilikuwa tofauti na yale mawili ya Marekani, lakini nalo lilibarikiwa sana. Mmoja wa wanenaji alikuwa rafiki yangu wa zamani Yorrie Richards, mtu wa kawaida mwenye upako mkubwa katika kuhubiri kwake. Akiwa kijana, aliishi maisha ya uhalifu hadi Bwana alipomkamata. Alikuwa na kigugumizi kibaya sana na aliweza kusoma na kuandika kidogo tu. Lakini nilikuwapo katika mkutano ambao kwa mara ya kwanza alinena bila kigugumizi – muujiza mkuu – na baadaye nikamsikia akihubiri mara nyingi kwa upako mkubwa. Greenock nako pasingekuwa tofauti!
Upako ulioje uliomkalia mtakatifu huyu mzee mpendwa alipoumimina moyo wake kwa ajili ya uamsho, na athari iliyoje alipomnukuu mmoja wa wachungaji wake wa zamani – “Ni rehema ya Mungu kwamba HATUMI uamsho – juu ya watu wasiotayarishwa!”
Niliadhimisha miaka yangu 70 ya kuzaliwa katika kongamano lile kwa keki na ushirika mwema wa wenzangu waandalizi. Tena, tulikuwa tukiuona mkono wa Mungu juu ya huduma hii na juu ya Greg alipoenenda mbele za Bwana kwa unyenyekevu.