Sura 35 · dakika 6 za kusoma

Sermonindex.net

Tulirudi nyumbani Kanada mwishoni mwa Juni 2007, bila kujua milango mipya ambayo Mungu alikuwa karibu kunifungulia. Hadithi hii ingeanza mwaka 2004 nilipokutana na wachungaji wapatao kumi na wawili kutoka Washington na Oregon, waliokuwa wamekuja Victoria kwa siku mbili, ili kushirikiana na kuomba pamoja na wachungaji wa hapa. Niliona aibu kama vile wao pengine walivyovunjika moyo kwa wanaume wachache wa hapa waliokuja kukutana nao.

Hata hivyo, tulikuwa na wakati wa thamani pamoja, lakini kilele kwangu kilikuwa mwishoni mwa siku ya pili, walipokusanyika kutuombea. Kiongozi wao alikuwa Mchungaji John Roddam, kasisi mkuu wa St Luke’s Episcopal Church, Seattle, naye ndiye aliyepiga magoti mbele yangu wakati huu wa maombi na kuniomba niweke mikono yangu ndani ya yake. “Mungu amekupa wana na binti wengi,” akasema, akiongeza, “naye yu karibu kukutumia katika kuwaachilia waingie katika upako wake!” Nilifurahi na kushangaa, kwa maana kweli ninao wengi ninaowaita ‘wana na binti zangu’ na ambao nawaombea takriban kila siku.

Hakuna namna yoyote ambayo John angeweza kuwa amejua jambo hili, kwa hiyo nilikuwa na hamu ya kulipokea kama ‘neno kutoka kwa Bwana.’ Nilikumbuka vyema yale ambayo Floyd McClung alikuwa ametufundisha kuhusu kupokea ‘neno kutoka kwa Bwana’ alipoitembelea Anastasis wakati mmoja. “Hupewi neno hilo kwa ajili ya kukuongoza, bali kwa ajili ya kuitegemeza imani yako utakapoliona likitimia.

Liweke neno hilo katika kasha la chini kabisa na ulifunge kwa ufunguo hadi wakati ambapo Mungu atakufunulia kutimia kwake.” Sasa nilijua nilipaswa kufanya nini na ‘neno langu kutoka kwa Bwana.’ Sikumwambia mtu yeyote juu yake bali niliomba mara kwa mara kwamba, kama kweli hili lilitoka kwa Bwana, angenitayarisha, nikitafuta kupatikana, ili kulileta likatimie. Naamini Mungu alikuwa karibu kulizalisha tunda la jambo hili.

Nilikuwa nimevutwa kwenye tovuti fulani kwa sababu ya shauku ya vijana wanne ambao nilipata heshima ya kuomba nao kila juma kwa majuma kadhaa wakati wa ugonjwa wangu wa muda mrefu. Nilikuta www.sermonindex.net imejaa mahubiri ya ajabu, hasa yale yaliyoutia moyo wangu shangwe juu ya somo la ‘uamsho.’ Nilikuwa nimesikia na kusoma juu ya matendo ya ajabu ya Mungu kwa watu wa Wales, nchi yangu ya asili, katika uamsho mkuu wa 1904/5, nami nilitamani kuonja hayo hayo.

Nilikuwa nimepata uamsho wangu binafsi katika chumba changu cha kupanga pale Chuo Kikuu cha Swansea, Mungu aliponibatiza kwa neema yake kwa Roho wake; nilikuwa nimepata furaha ya kuitwa ‘mtoto wa uamsho’ nilipohubiri katika mabonde ya Wales; siku zote nilikuwa nikiona njaa ya ‘mambo ya ndani zaidi ya Mungu’, lakini sasa ningeweza kujiloweka katika kusikiliza mahubiri ya watu wakuu, wenye shauku kama yangu, ili Mungu alivamie kanisa lake, aliamshe na kujiletea utukufu tena.

Kila juma, nilikuwa nikitumia muda kwenye tovuti hiyo, hadi siku moja nikiwa nachunga katika Departure Bay Baptist Church, nilijikuta ‘nimepotea msituni,’ kwa kuwa yalikuwa yameanza kuwapo maandishi mengi mno kwenye mtandao kiasi kwamba haikuwa rahisi kwangu kuwapata wanenaji na mada nilizotamani kuzisikia.

Niliamua kuandika barua pepe kwenye tovuti hiyo, nikiuliza kama ingewezekana kuwapanga wanenaji na ujumbe katika orodha, ili kwamba mtu aliye na shauku ya maisha ya ndani zaidi na ya uamsho asilazimike kupekua mahubiri mengi yenye vichwa vya kuvutia lakini yaliyo na maudhui tofauti, kabla ya kupata moja linalompendeza. Bila kuwa na dharau wala kutaja majina, kwa kweli sina hamu ya kuwasikiliza watu wanaoniambia kwamba siku za miujiza zimepita, au kwamba tunapokea yote yaliyopo wakati wa kuokoka na kwamba hakuna kitu kama ‘baraka ya pili’ ambapo Roho wa Mungu humjia mtu ili kumtia nguvu, kama ilivyokuwa siku ya Pentekoste. Wala sina hamu na ujumbe wenye upendeleo wa kimadhehebu au wenye msimamo wa KJV pekee. Wengi wa hawa ni watu wamchao Mungu, wanaostahili kuwa kwenye sermonindex, lakini mimi sivutiwi sana na baadhi ya ujumbe wao.

Bila shaka, tovuti yaweza kuwa na makao yake mahali popote duniani, kwa hiyo waweza kuwazia mshangao wangu nilipopokea jibu juma moja tu baadaye kutoka Kelowna, umbali wa safari ya siku moja tu kwa gari kutoka nyumbani kwangu British Columbia, likisema kwamba mwanzilishi wa tovuti hiyo, Greg Gordon, alikuwa akihamia Victoria mwishoni mwa mwezi, na kuuliza kama ningekuwa mshauri wake! Heshima iliyoje! Nilikubali mara moja. Ndivyo ilivyokuwa kwamba siku chache baadaye niliitikia kengele ya mlango na kukutana na mtu huyu mkubwa mithili ya jitu, nikamkaribisha katika maisha yangu na nyumbani kwangu.

Greg alikuwa na umri wa chini ya miaka thelathini, lakini Mungu alikuwa amempa shauku ya utakatifu na uamsho tangu alipookoka miaka kumi tu kabla. Ilikuwa heshima iliyoje kushirikiana naye kila siku juu ya Biblia zetu, vikombe vya chai na keki za Kiwelisi.

Mwezi Julai 2007, Greg alikuwa ameandika kwenye tovuti yake kwamba alitamani kuona kongamano la uamsho ambalo lingekuwa tofauti na mengine yote. Hakungekuwa na vikundi vikubwa vya muziki vya kuongoza ibada, wala vitabu au muziki wa kuuza, wala malipo ya kuingia na sadaka. Wanenaji wangekuja kwa gharama zao wenyewe bila ahadi yoyote ya malipo. Lingekuwa ‘kusanyiko takatifu’ la wanenaji na washiriki wenye shauku moja – kumtafuta Bwana kwa ajili ya uamsho, wa binafsi na wa kitaifa.

Kanisa dogo mjini Canton, Ohio liliandika likisema kwamba lingekuwa tayari kuandaa kongamano la namna hiyo na lingefanya matangazo na maandalizi yote. Greg alikubali naye akaanza kuwasiliana na watu ili wanene, akiwajua tu kwa kuwasikiliza kwenye tovuti yake mwenyewe. Kwa mshangao wangu – pengine si kwake – kila mmoja aliyemwomba awe mnenaji alikubali kuja kwa masharti hayo! Hawa walikuwa watu wenye heshima kubwa kila mmoja kwa nafasi yake, na hapa walikuwa wakikubali kuja kwenye kongamano lililoandaliwa na kijana asiyejulikana mwenye ushahidi mchache.

Asiyejulikana kwa wanadamu pengine, lakini ajulikanaye vyema kwa Mungu! Hakika hii ilikuwa ishara ya kwanza ya upako wa Mungu. Hivyo basi, kongamano likaandaliwa, likiwa na wanenaji kutoka Uingereza, Afrika Kusini, Marekani, na Kanada, na washiriki kutoka mbali kama Australia na Ulaya.

Maombi ya kuhudhuria yalipoingia, lile kanisa dogo lililokuwa mwenyeji liligundua kwamba jambo hilo lilikuwa likawa kubwa mno kwao, kwa hiyo wakalifuata kanisa kubwa kuliko yote mjini chini ya uongozi wa Mchungaji ‘Dave’, mzee mwenye heshima kubwa katika eneo hilo. Yeye aliingia mtandaoni kuichunguza sermonindex mwenyewe, kisha akatangaza, “Hili ni la Mungu – tutalikaribisha.” Ndivyo ilivyokuwa kwamba tulipewa majengo mazuri ya kanisa lake, pamoja na ushirikiano kamili kutoka kwa wafanyakazi wake wote, kwa siku tatu za kongamano. Baraka iliyoje waliyokuwa kwetu! Kulikuwa na kamera za televisheni za kurusha mikutano moja kwa moja kwenye mtandao ili Anne aweze kuyatazama mambo yote akiwa nyumbani Kanada.

Anne alikuwa amependekeza nihudhurie ili kumtia moyo Greg, lakini tulipofika kukiwa na maandalizi machache mno ya mikutano, ikawa juu yangu mimi na Don Courville kuwa waendeshaji, bila kupangwa. Tumebarikiwa sana tunapoyaona makongamano haya yakikua, na jinsi Mungu alivyomwongoza Greg kupata kibali mbele zake na mbele ya watu wamchao Mungu duniani kote. Nimepata heshima kubwa ya kuketi katika kundi la watu waliouonja utendaji wa enzi wa Mungu katika uamsho na kuwasikiliza wakisimulia juu ya nyakati hizo. Ni jambo la hakika kwamba mtu akiisha kuuonja uamsho, hawi yule yule tena kamwe! Mtu aweza kuwasikiliza wanenaji wote wa kongamano hili na ya baadaye kwenye tovuti ya Greg www.sermonindex.net.

Ukurasa 1 / 5 · 6 dakika zimebaki katika sura