Sura 33 · dakika 6 za kusoma
Huduma Bondeni
Katika miaka yangu miwili ya udhaifu, nilipata nyakati fulani za huduma zenye maana. Nilialikwa kufundisha katika shule ya kila juma huko Lambrick Park, kanisa kubwa la Ndugu katika mji wangu wa Victoria. Hufurahia daima mialiko ya namna hiyo kwa kuwa msimamo wangu wa kimafundisho na msisitizo unajulikana kutofautiana na wa uongozi wao. Wao ni wa mwelekeo wa mafundisho ya vipindi hali mimi ninajulikana kama ‘Mkarismatiki mhafidhina’, niaminiye kwamba karama na utendaji wa Roho Mtakatifu ni vilevile leo kama siku zote – tena vya lazima vilevile.
A W Tozer inasemekana alisema, “Mafundisho ya vipindi ni hatari zaidi kuliko Uliberali: Uliberali hutunyang’anya ujumbe wetu, mafundisho ya vipindi hutunyang’anya nguvu zetu.” Naamini katika ‘baraka ya pili’ – ubatizo wa Roho, na kwamba hatupokei ‘kila kitu’ wakati wa kuongoka – kama vile wanafunzi wasivyopokea Yesu alipowapulizia ‘pumzi’ mara ya kwanza ndani ya chumba alimotokea kwao mara ya kwanza baada ya ufufuo wake, akisema, “Pokeeni Roho Mtakatifu.” (Yohana 20). Ingekuwa majuma saba zaidi kabla hawajampokea kwa nguvu siku ya Pentekoste. Ni furaha daima kwangu kuwa na marafiki zangu wa karibu zaidi Victoria, watu ambao asili yao ya kiroho ni katika mapokeo ya Ndugu, hali yangu ni katika mapokeo ya Kipentekoste. Wao, kama natumaini mimi nilivyo, ni watu wenye maono makubwa kuliko ya mapokeo yetu.
Nilifundisha kwa majuma kumi huko Lambrick Park, dakika 90 kila juma, juu ya somo la ‘kuachiliwa,’ dhamira ya kitabu changu The Key in My Hand. Ningeombwa kurudi mwaka uliofuata kufundisha mafundisho yaleyale, pamoja na somo la nyongeza la ‘karama za Roho.’ Kwa kuwa watu wengi katika kusanyiko lile walikuwa wakiuliza maswali ambayo uongozi haukuweza kuyajibu kwa umahiri, na kwa kuwa nilikuwa tayari nimekubaliwa kama mwalimu, walinialika kufundisha kozi ile, ambayo, bila shaka, nilifurahi kuifundisha.
Nilialikwa pia kutumia wikendi moja pamoja na wanaume kutoka Reformed Episcopal Church, huko Parksville katika Vancouver Island. Tena, marafiki wapya wengi walipatikana na mawasiliano kwa ajili ya huduma ya baadaye.
Mwezi wa Oktoba tuliweza kuchukua fursa ya nauli rahisi za ndege kusafiri kuwaona marafiki zetu wengi Ontario. Tulitembelea Toronto na tukakaribishwa kwa Lorne na Sandy LeGrow. Waliwaalika wengi mno wa marafiki zetu wa zamani wa mwisho wa miaka ya 70 na jioni ya ajabu ilitumika katika kukumbuka mambo, kucheka, na kula. Kisha tukaendelea Guelph kuwaona Hugo na Jacqui Jiminez, marafiki zangu wapendwa tangu siku za Anastasis, niliowafunga ndoa Mexico City mwaka 1995. Jioni ile, tulikuwa Kitchener nyumbani kwa Ruth Setacci. Walikuwa wamewaita pamoja wengi wa kusanyiko letu – na marafiki – kutoka Hazelglen Fellowship kwa jioni nyingine ya ajabu. Kilele kimoja kilikuwa simu kutoka kwa Ron Smith ambaye hakuweza kuhudhuria kwa kuwa alikuwa nje ya mji.
Nilipomwambia jinsi nilivyomhesabu kuwa yeye ndiye sababu ya kuanzishwa kwa kanisa lile, kwa kuwa alikuwa ametufundisha jinsi ya kuomba, alizibwa koo na machozi. Labda sikuwa nimemjulisha jambo hilo kamwe kabla ya hapo. Siku iliyofuata ilikuwa pendeleo langu kuhubiri tena katika kanisa langu la zamani na kuona, kwa furaha kubwa, kwamba kusanyiko lingali imara.
Mwanzoni mwa vuli ya 2004, nilipokea simu kutoka kwa kijana mmoja huko Lorrane, Oregon. Alikuwa mchungaji wa vijana katika Quisqueya Chapel, Haiti, naye alikuwa amenisikia nikihubiri juu ya Makwazo. Aliuliza kama ningekwenda huko kwa wikendi moja kufundisha mafundisho haya na mengine. Kwa kuwa hili lingetupa nafasi ya kuwatembelea Dave na Ellen Knippel Portland tena, tulikubali kuendesha gari hadi Oregon, tukiwachukua marafiki wawili wema pamoja nasi. Ilikuwa wikendi ya ajabu yenye huduma nyingi katika mazingira haya ya kijijini.
Shane na mkewe Christie wangekuwa wanandoa vijana wa thamani kwetu, nasi tungekuwa na nyakati nyingi za ushirika mwema siku za mbele. Walikuwa na upendo mkubwa kwa Haiti na walikuwa wamewaasili wasichana wawili wadogo walipokuwa wakiishi huko.
Miaka miwili baada ya ziara yetu na safari nyingine iliyofuata ya Oregon, Shane angeanza kazi katika kisiwa kilekile cha Dominica ambapo Haiti ina nusu na Dominican Republic nusu nyingine. Kazi yake inaitwa ‘Mercy League’ nayo inatafuta kutoa makao salama yanayojitegemea kwa yatima wa Kihaiti ng’ambo ya mpaka katika Dominican Republic.
Katika kiangazi cha 2005, nilichukua jukumu la kuhubiri katika kanisa dogo la First Nations kwenye hifadhi ya Tsawout. Mchungaji wao alikuwa amestaafu hivi karibuni, nao walikuwa wakitaka mtu wa kuwachukua. Kanisa liliongozwa na wanandoa vijana wa wenyeji wa asili wa Salish, Peter na Stephanie na jamaa zao. Tuliifurahia sana ibada yao na roho yao, hivyo kwa furaha kubwa tulihudhuria ibada kila juma kulifundisha kusanyiko dogo.
Muda mfupi baadaye, kijana mmoja Mholanzi na jamaa yake walihisi wito wa Mungu wa kusafiri kuvuka Atlantiki kuwahudumia watu hawa wa thamani. Marco na mkewe walitoka kanisa lilelile la Rotterdam ambako marafiki zetu wema sana, Henk na Marta Hempenius wanatumika kama watumishi. Dunia ni ndogo kama nini!
Mwezi wa Oktoba, nilialikwa kufundisha kila jioni ya Jumatano, mfululizo katika New Life Baptist Church, Duncan, juu ya somo la Utatu. Hili ndilo kanisa ambako mkwe wangu Rob angekuwa Mchungaji Msaidizi mwaka mmoja baadaye. Nilizifurahia daima nyakati hizi katika kanisa ambako mwandishi mashuhuri Mark Buchanan ni mchungaji, na kumjua yeye binafsi kama rafiki.
Jioni moja, nilipokea simu ya kuvutia. Ilitoka kwa mwanamke mmoja huko Courtney, safari ya masaa matatu kwa gari kaskazini mwa Victoria. Adele alisema alitoka St George’s United Church; walikuwa wakipanga kuwa na mafundisho fulani juu ya ‘maombi,’ naye alikuwa amepewa jina langu kama mwalimu atarajiwaye.
Ni lazima nikiri kwamba niliposikia maneno ‘United church’ mara moja niliwahukumu kuwa wa kiliberali katika theolojia, kama sehemu kubwa ya United Church ya Kanada ilivyokuwa.
Mtu hujiuliza John Wesley angesemaje juu ya Kanisa la Methodisti sasa, kwa kuwa ni sehemu kubwa ya United Church! Baada ya majadiliano kidogo, nilikubali kuendesha gari kwenda kaskazini Jumamosi iliyofuata ili kukutana naye na wenzake wawili waliohitaji kunihoji kabla hawajaweza kuwasilisha ombi lao mbele ya ‘sinodi’ ya kanisa! Katika mkutano huu, niliwauliza wote watatu ni nini hasa walichokuwa wakipanga kufanya, lakini ilikuwa dhahiri kwamba kwa kweli hawakuwa na mipango yoyote, kwani hili lilikuwa jambo jipya kabisa kwao. Kisha nikawauliza walidhani kusudi la maombi ni nini, ambapo tena hawakuwa na hakika, hivyo nikasema, “Naamini maombi ni kipawa cha Mungu kwetu ili tuweze kujifunza kukuza urafiki wa karibu naye.”
Kwa hili, yule mwanamume aliyekuwepo, Gary, akachangamka sana. “Hicho ndicho ninachotaka,” akasema, “Ukaribu na Mungu!” Moyo wangu ukamwitikia mtu huyu na shauku yake ya kumjua Bwana zaidi, hivyo kwa hamu nilikubali kusafiri kila wikendi hadi Courtney, kufundisha wowote wangeweza kuwashawishi kuja kila asubuhi ya Jumamosi kwa majuma matatu. Katika majuma machache ya katikati Adele angeniandikia barua pepe akinieleza maendeleo – “Nimepata 8 – 9 - 10 waliojiandikisha kwa kozi” angeandika kwa msisimko uliokuwa ukiongezeka.
Kwenda Courtney kwa kozi ya asubuhi ya Jumamosi, mtu anahitaji kuondoka Victoria Ijumaa na kwa kuwa ni safari ndefu hivyo kwa gari, niliamua kusafiri kwa treni moja ya kila siku. Hii ilimaanisha kuondoka Victoria asubuhi na mapema Ijumaa, kurudi jioni sana Jumamosi au Jumapili, kutegemea kama ningezungumza katika ibada ya kanisa asubuhi ya Jumapili. Nikaishia kufanya hivyo kwa Jumapili mbili!
Nilifika St George’s asubuhi ya Jumamosi ya kwanza na kusalimiwa na watu zaidi ya 40, kalamu na madaftari tayari, kwa wakati uliokuwa wa ajabu sana pamoja. Tulipata marafiki wa ajabu katika majuma yale matatu, hasa Gary na mkewe Debbie, waliotukaribisha wikendi ya mwisho kwa kuwaalika wengine kadhaa, wakiwemo rafiki zangu wa karibu Ron na Eunice Freeman (mchungaji wangu wa vijana katika Victoria Alliance Church) na Mchungaji Bill na Joan Hodges (padre wa Kiepiskopali ambaye nilikuwa nimeendesha mafungo ya wanaume kanisani kwake) kwa mlo wa ajabu uliotanguliwa na kuoshwa miguu kwa burudisho tulipowasili. Zawadi ya pekee kama nini!
Muda mfupi baada ya kumaliza wikendi zile tatu za mafundisho, tuliondoka kwa ziara yetu ya Australia. Ulikuwa mwisho wa 2005, nami nilikuwa bado nikijisikia dhaifu sana lakini nikiweza kumtumikia Bwana katika fursa zozote alizonipa.