Sura 32 · dakika 7 za kusoma

Bonde Refu La Udhaifu

Nimekuwa daima na afya njema ingawa si mwenye mwili wenye nguvu. Hata hivyo, Septemba ya 2003 ingekuwa mwanzo wa kipindi kirefu cha udhaifu kilicholetwa na kufanyiwa kwangu upasuaji rahisi wa ngiri ya kiwambo. Daktari wangu alikuwa ameupendekeza kama suluhisho la maumivu ya koo niliyoyapata baada ya kuimba.

Niliingia Hospitali ya Victoria Royal Jubilee kwa upasuaji rahisi wa athroskopi, nikaruhusiwa baada ya siku mbili nikitazamia kupona kabisa na haraka. Hata hivyo, Anne alikuwa ameanguka karibuni na kuvunjika kifundo cha mguu, hivyo nilijiandalia chakula cha mchana siku ya kwanza nyumbani. Niliambiwa nile chakula laini tu kwa muda, hivyo nikaandaa mlo wa tambi za Kichina, ‘jambo baya kuliko yote’ kwa mujibu wa daktari wangu baadaye.

Inaonekana tambi hutanuka katika umio, kama hizi zilivyofanya, zikinisababishia kuziba kwa kumeza, jambo ambalo ningelipitia mara nyingi katika miezi michache iliyofuata. Nilipatwa na wasiwasi mkubwa hivyo nikampigia simu daktari wa upasuaji jioni ile. Aliniambia nirudi katika chumba cha dharura ambako angekutana nami ili kuondoa kizuizi kile. Hivi ndivyo alivyofanya, akitumia mrija wa endoskopi kusukuma chakula hadi tumboni mwangu ambako kingeweza kunyonywa nje. Hiyo ilikuwa mateso makubwa, na ilikuwa kwa faraja kwamba hatimaye nilipata usingizi usiku ule hospitalini.

Kama madhara fulani yalifanyika katika umio wangu wakati ule sijui, lakini kwa majuma kadhaa yaliyofuata nilipata shida kubwa ya kumeza karibu katika kila mlo, ingawa daktari wa upasuaji aliendelea kuniambia kwamba lingepita hivi karibuni.

Mwezi wa Desemba, nilikwenda kumwona daktari wangu tena kwa kuwa nilijisikia dhaifu mno. Alinitazama mara moja tu, akaniweka juu ya mizani na kisha akaniambia niende mara moja katika idara ya dharura ya hospitali, ambako kitanda kingekuwa kikinisubiri. Nilikuwa nimepungua uzito zaidi ya pauni ishirini, kutoka 160 hadi 139 lb., hivyo nikawekewa mrija wa maji ya chumvi mshipani kwa siku tatu.

Sasa daktari wa upasuaji akawa na wasiwasi, hivyo akanipangia nifanyiwe vipimo zaidi. Katika miezi michache iliyofuata, nilitembelea hospitali mara kwa mara kwa vipimo vya damu, bariamu, X-ray, CT scan na MRI, hata kutiwa nusukaputi kwa vipimo vya endoskopi, lakini bila suluhisho lolote kwa vizuizi vyangu na udhaifu.

Nilikuwa nikifanyiwa kipimo kingine tena cha bariamu mwezi wa Aprili 2004 nilipochukua kijiko kimoja cha kimiminika kilichokuwa na marshmallow mbili ndogo. Nilipokimeza, nikaziba. Hatimaye, mafundi walikuwa wamelipata tatizo. Ni dhahiri kwamba umio ulikuwa umepinda ulipoingia tumboni, jambo ambalo mrija wa endoskopi haungeweza kuliona, na chakula changu kilikuwa kikikwama katika pindo hili. Iliamuliwa kufanya upasuaji zaidi, hivyo mwezi wa Mei, niliingia tena katika hospitali ya Royal Jubilee.

Upasuaji ulionekana kuwa umefanikiwa, ingawa ‘ulikuwa mgumu sana kwa kuwa kulikuwa na tishu nyingi za kovu za upasuaji uliotangulia’, kwa mujibu wa msaidizi wa daktari.

Sasa matatizo mengine yakaanza nilipopatwa na mabonge ya damu katika mapafu yangu, jambo lililohitaji dawa za kulainisha damu kwa mwaka uliobaki. Nilikuwa hospitalini kila siku kwa majuma machache walipokuwa wakikokotoa kiasi changu cha Coumadin (dawa ya kulainisha damu), wakichukua na kupima sampuli za damu yangu. Kisha ikanibidi kuhudhuria kila juma kwa miezi michache, na kisha mara moja tu kwa mwezi hadi Desemba nilipoachwa kusitisha matibabu. Wakati uo huo, nilikuwa nikilalamikia maumivu katika mapafu na ubavu wangu, nikidhani haya ni matokeo ya mabonge ya damu, ila kuambiwa na daktari wangu kwamba nilikuwa nimepatwa na uvimbe wa utando wa mapafu na mawe ya nyongo!

Nimeamini daima kwamba kazi ya upatanisho ya msalaba inajumuisha afya ya miili yetu ipatikanayo na mauti (iliyo hai) pamoja na wokovu wa nafsi. Hata hivyo, ninaamini pia kwamba “mawe ya kukanyagia” ya Bwana yaweza kuongoza mabondeni ambako aweza kuturudi na kutufundisha zaidi juu ya asili yake mwenyewe ya ajabu. Ingekuwa kosa kwangu kuzungumza juu ya ugonjwa wangu wa muda mrefu kama nisingesimulia pia tukio la kusisimua wakati wa upasuaji.

Daktari alikuwa akinifanyia uchunguzi kabla ya upasuaji, akipima shinikizo la damu na mapigo ya moyo na kutumia stethoskopu sana juu ya kifua na mgongo wangu. Kwa kuwa alichukua muda mrefu kiasi nilisema, “Labda unasikia kulegea kwa vali ya moyo wangu kukiguna,” naye akajibu, “La! Hilo ndilo tatizo hasa. Siwezi kusikia kulegea kokote ingawa chati yako inasema ningepaswa kusikia!” Nilipokuwa mchungaji katika Victoria Alliance Church, ilikuwa desturi yangu kucheza raketiboli kila juma na mtumishi wa vijana. Jioni moja, tukiwa tukicheza, nilipatwa ghafla na udhaifu mkubwa na kukosa pumzi.

Asubuhi iliyofuata daktari wangu alinipeleka kwa mtaalamu wa moyo ambaye ofisini kwake nilitazama skrini ya mawimbi ya sauti, ambapo kulegea kwa vali yangu kulionekana wazi. Mama yangu alifariki mwaka 1952 baada ya ugonjwa wa muda mrefu uliosababishwa na vali ya moyo wake kulegea, hivyo nikawa mwangalifu mno juu ya hali yangu, nikijilinda nisiulemee moyo kwa michezo au shughuli za kupita kiasi. Sasa, zaidi ya miaka ishirini baadaye, ni dhahiri kulegea kule kulikuwa kumeponywa! Nilikumbuka kwenda mbele kuombewa katika Kongamano la Wilaya la Wachungaji miaka kadhaa kabla lakini sikutambua kamwe kuwa nimeponywa hadi sasa.

Katika mwaka 2004, ilinibidi kufuta mikutano fulani, hasa ile iliyohitaji safari nyingi, ingawa tulichukua fursa ya nauli rahisi za ndege kuwatembelea marafiki zetu wa Ontario huko Toronto na Kitchener. Nilijua nilikuwa mgonjwa lakini kwamba ningepona kama ningejitunza, hivyo nilitumia muda mwingi katika chumba changu cha kusomea, nikisoma na kuandika mashairi. Maisha yangu ya maombi yakawa na maana zaidi, wala sikujisikia hatia kwa kutokufanya jambo lingine lolote!

Nilikuwa nimeyapita matatizo haya yote 2005 ulipoanza, lakini nilikuwa bado sijaurudisha uzito wangu, hivyo nilikuwa bado dhaifu kiasi.

Mwishoni mwa Agosti, rafiki mmoja alitujengea baraza dogo nje ya chumba chetu cha kulala likishuka hadi bustanini. Niliketi nikimshikilia skurubu na zana zake wakati akiimaliza kazi ile, kisha akasema maneno yaliyonirudisha nyuma kweli. “Mvua itanyesha Jumamosi hivyo lazima ulipake dawa jukwaa hili kesho ili kulizuia maji.” Kazi ya namna hiyo hakika ilikuwa juu ya uwezo wangu kabisa.

Siku iliyofuata nilikwenda kununua galoni moja ya dawa ya kupaka na, nikiwa nimeketi sakafuni, nikaanza kulipaka jukwaa lile. Ilinichukua masaa kadhaa lakini hatimaye niliweza kuegemea nyuma na kusema, “Nimefanikiwa! Nimefanikiwa!” Hili lilikuwa jambo kubwa la kwanza nililolitimiza katika muda wa miaka miwili!

Ingekuwa Septemba ya 2005, miaka miwili tangu upasuaji wangu wa kwanza, ndipo nilipoanza kuona nafuu katika hali yangu ya jumla. Rafiki mwema alinishauri nitumie BioK, bidhaa ya mtindi yenye nguvu ambayo ingerudisha bakteria wenye afya niliowapoteza kwa sababu ya nusukaputi ya upasuaji na vipimo vyangu vya endoskopi. Sitasema hicho ndicho kilichoniponya, lakini uhusiano kati ya kukitumia kila siku na kupata nafuu kwangu ulikuwa wa ajabu kiasi.

Mwishoni mwa mwaka, tulifanya safari yetu ya kawaida kwenda Australia. Huko nilipumzika juani, nilisafiri kuvuka Great Western Desert, nilipanda baiskeli karibu kila siku na kuogelea katika bwawa la binti yangu. Nguvu zangu zilikuwa zikirudi, nami nilikuwa nikiirudisha hali yangu ya kujisikia mzima.

Safari ya majuma matatu kuvuka Great Western Desert ilikuwa wakati wa kuburudisha sana. Nilikuwa pamoja na rafiki yangu mwalimu wa Canberra, John Coman, na wenzake na wanafunzi wake kadhaa, waliokuwa wakienda kukaa juma moja katika jamii ya Waaborijini kwa programu ya watoto wa huko. Hii ilijumuisha kuendesha pikipiki za vumbini, michezo mingi na mafundisho ya Biblia. Tulipiga hema chini ya anga la usiku lililong’aa ambako ‘emu’ – sehemu ya anga lenye giza inayoenea juu ya eneo kubwa katika umbo la emu, lilionekana wazi.

Nilikwenda matembezi marefu juani. Safarini, tulisimama katika vijiji kadhaa vya Waaborijini ambako nilitambulishwa kama ‘guda Ron’ kuonyesha kwamba nilikuwa rafiki wa Ron Williams, yule mchungaji Mwaborijini kutoka Canberra. Hilo lilinifanya rafiki papo hapo. Marafiki zetu walitupeleka safarini kutafuta vidimbwi vingi vya maji walivyokuwa wakivitegemea, na kutafuta kangaruu na emu kwa ajili ya chakula chetu cha jioni.

Kwa bahati mbaya, hawakupatikana lakini tulimpata, tukampika na kumla iguana, mjusi mkubwa. Alikuwa na ladha kama kuku lakini alikuwa ‘mgumu kutafuna’ zaidi. Hii ilikuwa katika eneo ‘pengine ambalo halikuwahi kuonwa na mzungu’ kwa kuwa lilikuwa na michoro ya mapangoni iliyochorwa na mababu wa waongozaji wetu miaka mingi iliyopita. Nilijua jinsi tulivyokuwa na pendeleo kukubaliwa hivyo na watu hawa wa ajabu. Safari yetu iliishia Ayers Rock katikati ya nchi hii kubwa, ambako nilipanda ndege kurudi Brisbane na nyumba mpya ya binti yangu.

Niliporudi Kanada majira ya kuchipua ya 2006, nilijua kwamba afya yangu ilikuwa njema tena, kwa kuwa nilihisi nguvu mpya na nilikuwa nikila vizuri.

Ukurasa 1 / 5 · 7 dakika zimebaki katika sura