Sura 31 · dakika 6 za kusoma

Bwana Anaendelea Kuongoza

Nilikuwa na huduma nyingi mwaka 2002, nyumbani na nje ya nchi, nikitembelea Haiti, Manitoba, Uingereza, Portland, Fortaleza na kurudi Australia. Huko Haiti, rafiki yangu mwema Dave Knippel wa Portland, Marekani, na mimi, tulikuwa wageni wa Kevin na Karen Hull waliokuwa wakiendeleza kazi ya watoto magharibi mwa kisiwa kile. Nilipaswa kufundisha mtaala wa Circuit Teaching International katika mikutano kadhaa ya wachungaji lakini kulikuwa pia na fursa nyingine nyingi za kuhubiri. Mmoja hasa unajitokeza, kwani ulikuwa katika kusanyiko kubwa kuliko yote la Kiingereza Haiti, Quisqueya Chapel, Port au Prince, mji mkuu. Tulichelewa kidogo kwa kuwa Kevin alikuwa na matatizo ya gari lake, hivyo nilipata nafasi ndogo ya kukutana na Mchungaji Olsen kabla ya ibada.

Kulikuwa na mamia kadhaa ya watu waliojaa katika ukumbi wa ibada nilipoongozwa kwenda kuketi karibu naye na mkewe safu chache kutoka mbele. Baada ya nyimbo za kufungua za kuabudu, alisimama kuwakaribisha wageni waliokuja ibadani, akiwaalika wasimame ili watambulikane. Nilipoyasikiliza majina na huduma za watu wengi waliokuwa wageni, hasa kutoka Marekani, nikaanza kujiuliza imekuwaje kwamba mimi nimepewa upendeleo wa kuwa msemaji wao asubuhi ile. Nilizungumza kuhusu makwazo na nikahisi upako wa namna hiyo hata nikajua kwamba Bwana alikuwa akizungumza kupitia kwangu kwa wengi waliokuwepo siku ile.

Mwishoni mwa ibada, nilimshukuru Mchungaji Olsen kwa fursa hii na nikampa kimoja cha vitabu vyangu, The Key in My Hand, ambacho ni dhahiri kwamba kilikuwa baraka kwake, kwani baadaye aliniandikia Victoria akiomba nakala kumi na mbili zaidi, kwa kuwa alitaka kuwapa wajumbe wote wa bodi ya Kanisa hili la Kimataifa, wao wakiwa Atlanta, Ga.

Katika safari ya kurudi kituoni kwetu upande wa magharibi, Kevin, Dave na mimi tulisimama kula chakula cha mchana na kushirikiana katika kituo kidogo cha misheni. Pale tulisikia hadithi ya ajabu. Mmoja wa wamisionari alikuwa na mpango wa kuwaleta madaktari watatu kila juma kutoka Marekani. Wangepelekwa katika kijiji cha mbali kuwatibu watu wa huko, kuandika ripoti zao kwa ajili ya daktari mmisionari wa hapo, na kisha kurudi nyumbani. Angefanya hivi kila juma, akiwa na mzunguko wa vijiji kumi na vitatu ambako wangehudumu. Siku hii alikuwa ndio kwanza ametoka uwanja wa ndege kuwabadilisha madaktari kwa ajili ya mpango huu, ndipo alipotuambia jambo la ajabu lililokuwa limetokea punde.

Wale watu watatu walikuwa wamemaliza kazi yao na walikuwa wakiandika ripoti zao, walipoona moto juu kilimani. Wakatambua kwamba ulikuwa kule kijijini walikokuwa wametoka punde. Hivyo, wakapanda gari lao la magurudumu manne, wakarudi na kumkuta mganga wa kienyeji wa kijiji kile amesimama kando ya magofu yaliyoungua ya nyumba yake. Wakaanza kumhurumia hata aliposema, “La! Ndio kwanza nimeyatoa maisha yangu kwa Kristo, hivyo nikaamua kukusanya vifaa vyangu vyote vya uganga ndani ya nyumba yangu na kuviteketeza vyote. Havitakuwa tena na mamlaka yoyote juu yangu!” Mfano wa ajabu kama nini wa toba!

Ziara yangu ya Manitoba, Kanada, ilikuwa ya kuzungumza katika karamu ya mwaka ya Manitoba Bible Society. Pale tulifufua ushirika na John na Eileen Wiebe tuliowafahamu Hamm, nilipofundisha Ujerumani mwaka 1967-67. John wakati ule alikuwa katika Jeshi la Kanada lakini sasa alikuwa padre wa Kanisa la Anglikana la Kanada. Pia, katika karamu ile kama wageni, walikuwepo wanawake wawili waliokuwa wamehusika hivi karibuni katika Uamsho wa Kiroho uliokuwa ukitokea katika eneo jipya la Kanada la Nunavut. Waliweza kusimulia hadithi ya ajabu kama nini – mtu aweza kupata filamu ya hali halisi kuhusu kutembelewa huku na Mungu, iitwayo Transformations #2. Nilipewa fursa nyingine za kuzungumza, tulipofurahia ushirika wa uchangamfu namna hiyo na waaminio wa huko, ijapokuwa halijoto ilikuwa ya baridi mno kwa Aprili!

Safari za Uingereza na miadi mingine mingi ya kuhubiri huko BC zilichukua sehemu kubwa ya mwaka, lakini mwezi wa Oktoba, tulisafiri hadi Portland kuwatembelea Dave na mkewe Ellen. Huu pia ulikuwa wakati wa kufundisha katika kikundi kidogo cha nyumbani walichokuwa wakikiandaa. Mwaka 1982, walikuwa wanachama wa kanisa letu huko Kitchener wakiwa wanafunzi katika kituo cha YWAM cha hapo Cambridge, Ontario. Huko, Ellen alikuwa amehusika sana katika dansi, lakini ajali ya kusikitisha ilimwacha na madhara ya kimwili na ya ubongo, hivyo sasa alikuwa amefungwa nyumbani na angeweza tu kutembea polepole kwa msaada wa ‘kitembezi.’ Ilikuwa furaha kukaa nao, kuiona furaha ambayo ziara yetu ilimletea Ellen na kumsikia akituombea.

Mwezi wa Novemba, nilisafiri tena hadi Fortaleza nchini Brazil, kwa ziara ambayo ingekuwa ya mwisho kwa Tony na Christine, Marcello na Aline, na kwa marafiki wengi niliowapata katika ziara zangu zilizotangulia. Kama nilivyokwisha andika, huu pia ulikuwa wakati wa baraka kuona kwamba kila kanisa nililohudumu lilikuwa na washiriki wengi zaidi kuliko kabla ya kampeni ya uinjilisti ya 1998.

Mwaka uliisha kwa ziara yetu ya kila miaka mitatu kwenda Australia kuwaona Lynette, Philip na watoto wao watatu, Michael, Chloe na Emma. Kama ilivyokuwa desturi yetu, tungekaa miezi sita katika baridi ya Kanada, tukiwa na miadi mingi ya kuhubiri. Miongoni mwa vilele vilikuwa mafungo mawili huko Jindabyne katika Snowy Mountains, na watumishi na wanafunzi wa seminari ya The Christian & Missionary Alliance na kambi ya familia ya kanisa la C&MA la Woden (Canberra). Pia ya pekee mno, yalikuwa mikutano yangu ya kila juma ya kuomba na Ron Williams, mchungaji Mwaborijini, kwenye kumbukumbu aliyoisimika kuwaheshimu wanaume wote wa Kiaborijini waliokufa vitani, wasiotambuliwa na serikali ya Australia ingawa idadi yao ilizidi elfu moja!

Tulipokuwa tukiagana, Ron aliniambia, “Utakapokuja mara ijayo, nitakupeleka ukutane na watu wangu!” Hatukujua kabisa kwamba angekufa kwa saratani kabla mimi sijaweza kurudi, na kwamba angepokea heshima kubwa kutoka kwa serikali, kwa kuwa ibada yake ya kumbukumbu ilifanyika katika ukumbi wa bunge huko Canberra. Ilikuwa heshima kama nini kuitwa rafiki yake. Alikuwa pia amenipa heshima kwa kuingiza ndani ya kifaa chake cha kufundishia, ufunguo uliokiwakilisha kitabu changu The Key in My Hand.

Kifaa hiki cha kufundishia kilikuwa ubao ulioonyesha ‘njia ya emu’, chenye ishara kubwa kwa Waaborijini, ukionyesha safari yao kutoka nyakati za kale, kupitia kuja kwa mzungu, hadi siku hii ya leo. Kilikuwa na hadithi nyingi za ‘damu iliyomwagwa’ kabla Ron hajaonyesha kwamba damu iliyomwagwa msalabani ndiyo dawa pekee ya dhambi ya mwanadamu, na ulazima wa upatanisho kati ya mzungu na Mwaborijini. Katikati ya ubao ulikuwepo ufunguo, uliochongwa kutoka mti wa kigeni, ukiashiria upatanisho ule.

Tulirudi nyumbani Kanada mwaka 2003 tukisimama New Zealand kuwaona marafiki zetu wapendwa, John na Marion Brignall, aliyekuwa zamani injinia katika M/V Anastasis. Tuliruka hadi Wellington, ambako Dave Knipell alikutana nasi, na kisha tukaendesha gari hadi Masterton alikoishi dada yake. Nancy alikuwa mjane wa mtafsiri wa Biblia wa Wycliffe, hivyo nikamwuliza kama naye alifahamu Kiyunani. Nilikuwa nimetoa hivi karibuni muhtasari wangu wa kitabu bora Christ’s Paralysed Church X-rayed, kitabu kilichokoma kuchapishwa tangu zamani, cha mwanachuo wa Kiyunani McCrossan, nami nilitaka kumpa nakala.

Nilihudumu katika kanisa lake Ijumaa Kuu ile na Jumapili ya Pasaka kabla hajatuendesha maili kadhaa kaskazini hadi Lake Taupo ambako tungekutana na akina Brignall waliokuwa wameendesha kusini kutoka Tauranga. Njiani, Nancy alimtembelea rafiki aliyekuwa sasa na duka dogo la zawadi, likiwa na rafu chache za vitabu vilivyotumika. Fikiria mshangao wangu alipopata nakala ya kitabu cha awali karibu katika hali mpya kabisa! Bwana anaendelea kunishangaza kwa ‘sadfa’ zake!

Ukurasa 1 / 5 · 6 dakika zimebaki katika sura