Sura 30 · dakika 6 za kusoma

Kuingia Katika Milenia Mpya

Tuliingia mwaka wa 2000 nyumbani kwa binti yetu huko Canberra, Australia. Kwa kuwa mstari wa kimataifa wa tarehe upo magharibi kidogo ya Australia, nchi ile ilikuwa miongoni mwa za kwanza kuikaribisha milenia mpya. Hofu iliyohisiwa na wengi, kwamba misiba mikubwa ingeufagilia ulimwengu kwa sababu ya kompyuta kuharibika na biashara kutokuwa tayari, haikutokea kamwe, na sherehe kubwa kutoka pande zote za dunia zilishuhudiwa kwenye televisheni. Australia ilijipatia sifa kwa kuwa taifa kubwa la kwanza kutangaza karibu yake.

Bandari ya Sydney ilionyeshwa saa ya usiku wa manane ilipokaribia. Ghafla, kikawa giza kabla ya fataki za ajabu kuliangaza anga la usiku, zikiishia kwa mwonekano wa kupendeza katika upana wote wa daraja maarufu la bandari ya Sydney. Neno moja lilijitokeza – UMILELE. Waaustralia wengi wangeijua maana ya neno lile ingawa wengi wengineo wasingeijua.

Kwa miaka mingi, mtu akitembea katika mitaa ya Sydney, angeweza kulikuta neno hili moja limeandikwa kwa chaki kwenye vijia vya watembea kwa miguu. Ilikuwa kazi ya mzee mmoja, aliyekuwa mlevi wa mitaani zamani, aliyekuwa amejiingiza katika Ukumbi wa Misheni na kumsikia msemaji akitangaza, “Kama kungekuwa na neno moja tu ambalo ningeweza kuliandika mbinguni ili wote walitafakari, lingekuwa neno ‘umilele’ – utaukaa wapi?”

Maisha yake yakabadilika kwa sababu ya kulitafakari swali lile, hivyo akajitoa kuandika ‘umilele’ kila alikokwenda kama ushuhuda kwa wengine. Ilikuwa ajabu kwamba serikali ya Australia ilitumia neno lilo hilo kuikaribisha milenia mpya, ikijua maana yake kwa watu wao wengi kiasi hicho!

Ninapotazama nyuma katika miongo minne ya mwenendo wangu wa Kikristo, hufurahishwa daima na uaminifu wa Mungu kwangu. Amenichukua pamoja naye hadi milima mingi mirefu na kunitumia katika huduma ambazo nisingeweza kamwe kuziota nikiwa mwamini kijana. Kila muongo umekuwa na huduma yake ya pekee, hivyo nikajiuliza karne ya 21 ingekuwa na nini kwa ajili yangu.

Katika miaka ya ‘60’, nilipata pendeleo la kuwahudumia askari wa Ghurka huko Hong Kong; katika miaka ya ‘70’, Bwana alitutumia katika kile wengi walichokuja kukiita ‘uamsho’ miongoni mwa vijana wa Bridgend, Wales; katika miaka ya ‘80’ nilifundisha katika Chuo cha Kiyahudi huko Toronto, kwa fursa yake ya ajabu ya kuwashirikisha Injili wanafunzi na Rabi Saknovich; katika miaka ya ‘90’, nilikuwa ndani ya M/V Anastasis nikiwa na furaha ya pekee ya kuendesha makongamano ya wachungaji Afrika Magharibi, hasa Sierra Leone. Hivi vyote vilikuwa ‘vilele’ katika safu ndefu ya milima. Miaka ya ‘00’ ya milenia mpya ingeleta nini?

Mwaka 2000, nilihusika katika huduma mpya iliyoanzishwa na Ade Ajala, rafiki mpendwa kutoka Nigeria ambaye sasa alikuwa akichunga kanisa huko Denver, Colorado, Marekani. Iliitwa “Hands On” na kusudi lake lilikuwa kupanda makanisa nchini Nigeria.

Nilipaswa kuandaa programu ya mafundisho kwa ajili ya huduma hii, hivyo nilitumia majuma kadhaa Denver nikilifanyia kazi baadhi ya hili. Katika ziara yangu ya pili mwaka 2001, nilialikwa pia kujiunga na watumishi wa kituo cha YWAM huko Colorado Springs kama mchungaji wa kituo. Hii ilionekana kuwa fursa ya ajabu lakini, nilipoyafikiri matokeo yake yote, nilitambua kwamba ndoto za viongozi wale hazikuwa halisi na, nikiwa na kizuizi rohoni mwangu, nilikataa mwaliko ule. Hapakuwa na jinsi ya kuziendesha huduma hizi zote mbili kwa wakati mmoja.

Kwa masikitiko, ndoto za “Hands On” nazo hazikuzaa matunda ingawa Ade bado ana kanisa lenye uhai Denver. Ziara nyingine za Baja California na Brazil zilikuja miaka miwili iliyofuata, kila moja ikitia moyo kama zilizotangulia.

Hata hivyo, kilele cha mwaka 2001 kilikuwa safari ya pili kwenda India, safari hii hadi Chennai kusini, kuhudumu katika kituo kingine cha YWAM. Fikiria mshangao wangu nilipogundua kwamba wanafunzi watano wa shule ile walitoka Vancouver Island, nao hawakufahamiana kabla ya kuja! Nilivutiwa na wanafunzi Wahindi, wengine kutoka jamaa za tabaka la juu na wengine la chini, walioketi na kushirikiana pamoja.

Msichana mmoja alikuwa amewekewa zawadi ya kichwa chake kwa kumgeukia Kristo kutoka katika asili ya jamaa yake ya Kihindu. Msalaba wa Yesu daima huvipinga vizuizi viovu vya kitamaduni kama hivyo. Nilivutiwa hata zaidi na uimbaji wa sauti tofauti wa baadhi ya vijana wa Kihindi, hivyo nikawauliza walikojifunza kuimba hivyo – karibu ilisikika kana kwamba walikuwa Wawelisi! Wakaniambia walitoka Nagaland kaskazini, na kwamba waaminio wa kule walikuwa wamefundishwa kuimba namna hii na wamisionari Wawelisi wa Kipresbiteri walioleta Injili kwao baada ya uamsho wa Wales wa 1904/5.

Nilihudumu katika shule mbili za YWAM wakati wa ziara yangu ya majuma matatu, nilizungumza na uongozi wa YWAM katika seminari ya St Thomas’ Hill, mahali alipouawa shahidi mtume Tomaso, nilitembelea maeneo ya mabanda wanakofanya kazi nyingi, na nikachukua nafasi ya kutembelea na kukaa kwa muda mfupi Ebenezer Home. Kituo hiki cha yatima Martin, binamu yake Anne, hukifadhili kwa fahari nacho kinaongozwa na mtu mwema, Mchungaji VeeJay.

Watoto wadogo wapatao 100 walinizunguka wakijaribu Kiingereza chao kidogo na kunipa furaha kubwa. Nilicheza kriketi nao lakini sikuwavutia. Jambo moja lililokosa kunipa furaha nyingi lilikuwa chakula cha kila siku cha wali na mchuzi wa bizari. Napenda bizari lakini huu ulikuwa mkali ‘mno’ – na, kwa kuwa nilionywa nisinywe maji ya huko, kila mara uliletwa pamoja na Coca Cola, siyo kiungo kizuri kwa bizari!

Miongoni mwa makanisa niliyozungumza ndani yake lilikuwa Maranatha, kanisa la watu wa Kitamil. Mchungaji hapa alikuwa mtu mwema lakini mtu mwenye historia. Alikuwa amejaribu mara mbili kujiua kwa kuwa kwanza mkewe na kisha mwanawe mkubwa walikuwa wamepatwa na saratani, nao wote wawili walikuwa wamepewa muda mfupi tu wa kuishi. Kila mara alishindwa, akikutwa na majirani kabla hajaweza kulikamilisha kusudi lake. Kutokana na kunusurika kwake kwa shida, aligeukia Kristo kutoka katika asili yake ya Kihindu, akilia kwa sauti kuona kama Bwana angeweza kumsaidia. Si kwamba Bwana alimwokoa yeye tu, bali mkewe na mwanawe wote wawili walipona saratani zao. Akaanza kufungua makanisa kila alikoweza, miongoni mwa wale watu aliokuwa akiwaongoza kwa Bwana, na wakati nilipokuwa pale, alikuwa ameanzisha makanisa zaidi ya kumi. Mwanawe mkubwa sasa alikuwa mwinjilisti kusini mwa India huku mwanawe mdogo akiwa mkalimani wangu. Mwishoni mwa ujumbe wangu kuhusu Chumba cha Juu, nilitoa mwaliko ambao baadhi ya watu waliuitikia. Kisha mchungaji akasimama kuzungumza na watu wake.

Wanawake wapatao wanane na wanaume kumi walisimama na kusonga mbele. Nilimwuliza mkalimani wangu baba yake alisema nini hasa na kwa nini watu hawa walikuwa wamesonga mbele, naye akajibu, “Baba yangu alisema kwamba ulikuwa wakati wao wa kushuka uzioni, wakiyumba kati ya miungu yao ya Kihindu na Kristo. Leo ndiyo siku waliyopaswa kuamua watakayemtumikia.” “Hawa wote wamesonga mbele ili kujitoa kwa Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wao.” Moyo wangu ukaruka kwa furaha kwa pendeleo la kuzungumza katika kanisa la namna hiyo.

Mwezi wa Novemba wa mwaka 2001, nilipokea mwaliko wa kuja kuzungumza katika Intervarsity Christian Fellowship (IVCF) ya University of Victoria jioni moja ya Ijumaa. Nilifika pale kwa wakati wangu lakini mwenyeji wangu, mtumishi wa chuo kile, alinisalimu kwa aibu kwa kuwa wanafunzi walikuwa wamemwalika mwanafunzi mwingine kutoka chuo kingine ili ahudumu jioni ile. “Nimemwomba ajiwekee kikomo cha dakika ishirini tu,” mtumishi yule akasema, “ili wewe uwe na muda wa kutosha kabisa kwa ujumbe wako.” Nikamhakikishia kwamba ningependelea zaidi amruhusu yule mwanafunzi ashiriki yote aliyotaka kusema, na kwamba haingenijali hata kidogo mimi kutozungumza jioni ile. Ningefurahi sana kumsikiliza kijana yule.

Kwa kawaida, kutokana na hilo, nilialikwa tena punde baadaye, wa kwanza kati ya mialiko mingi ya kuzungumza na kundi lile la ajabu la wanafunzi.

Zikafuata mialiko ya kuzungumza katika karamu za Krismasi za IVCF, miaka minne kati ya sita iliyofuata. Najiuliza kama ningepata upendeleo kama huo miongoni mwa wanafunzi wale kama ningelisisitiza kuzungumza jioni ile ya kwanza ya Ijumaa! Sikutambua kwamba upendeleo huo ungekuwa na sehemu kubwa katika kunifikisha kileleni cha mlima ambao Mungu alikuwa ameupanga kwa muongo huu!

Ukurasa 1 / 5 · 6 dakika zimebaki katika sura