Sura 2 · dakika 3 za kusoma
Mawe ya Kukanyagia
Kanisa Kuu la Notre Dame katika mji wa kale wa Quebec City limeshuhudia matukio mengi ya kihistoria. Alasiri hii yenye jua ya Juni 1979, nilikuwa nikishuhudia tukio jingine. Nilikuwa ndani kidogo ya mlango mkuu nikichungulia sehemu ya ndani yenye giza ya kanisa, ambako kijana mmoja alisimama mbele ya safu mbili za wanafunzi walioandamana na mwalimu wa kiume. Yule kijana alishika Biblia mkononi mwake na, akionyesha kwa zamu kila kimoja cha ‘vituo vya msalaba’ vilivyokuwa kwenye kuta za kanisa hilo kuu, alikuwa akiwafundisha wanafunzi kuhusu mateso ya Yesu. Walisikiliza kwa umakini mkubwa. Ingawa wote walikuwa na miaka kumi na sita au kumi na saba na walijua vyema utamaduni wa Kanada na historia ya Quebec, mafundisho haya yalikuwa mapya kwao. Mtu akitazama kwa karibu zaidi, angeweza kuona kwamba vijana hao wote walikuwa wamevaa kippah vichwani mwao - ishara kwamba walikuwa Wayahudi.
Nilitazama kwa mshangao na kwa furaha ya pekee ya mshiriki, kwa kuwa wanafunzi hawa walikuwa wametoka shuleni kwetu Toronto kuja kutumia wikendi ya kimasomo katika Quebec ya kihistoria. Toronto Hebrew Academy ni shule mashuhuri ya Kiyahudi ya kiorthodoksi, nami nilikuwa nimepata heshima ya kufundisha huko kwa miaka miwili iliyopita. Wanafunzi hawa arobaini walikuwa darasa letu la kumi na moja, nami pamoja na mwenzangu, Ari Barchi, tulikuwa tumeombwa kuongoza safari hii maalum ya kimasomo. Hakuna hata mmoja wa wanafunzi hawa aliyejua kwamba muda si mrefu uliopita nilikuwa nimetoa taarifa kwamba ningeondoka shuleni mwishoni mwa muhula huu, ili kuupokea ‘wito’ mpya - ule wa uchungaji wa wakati wote. Tangu uamuzi ule ulipofanywa, Mungu alikuwa ameniongoza katika mambo ya ajabu, na wikendi hii ilikuwa ikithibitika kuwa baraka yake iendeleayo.
Nilipoziangalia kuta za kale na za fahari za kanisa lile kuu, pamoja na vile vituo kumi na vinne ambavyo mbele yake waaminifu hupiga magoti katika maombi wakikumbuka njia Yesu aliyoipita kutoka Gethsemane hadi Kalvari, akili yangu ilirudishwa kwenye vituo vya maisha yangu ambavyo kwavyo Mungu alikuwa ameniongoza. Nilitazama nyuma zaidi ya miaka ishirini, nikaiona ile kweli aliyoitangaza Mtunga-Zaburi.
“Hatua za mtu zimethibitishwa na BWANA, anapoipenda njia yake; ajapoanguka, hatatupwa chini kabisa, kwa maana BWANA humshika mkono wake” (Zaburi 37:23-24).
Naona vituo vingi sana au ‘mawe ya kukanyagia’ katika maisha yangu vilivyoniongoza kuingia katika mambo ya ndani zaidi pamoja na Bwana, na ambavyo bila hivyo nisingekuwa na habari hii ninayotaka kuisimulia. Kila jiwe la kukanyagia liliongoza hadi lile lingine, kila moja likiwa ni kuingilia kwa Bwana moja kwa moja katika mipango yangu. Ni kwa kutazama nyuma tu ndipo naweza kuona kiasi fulani cha makusudi aliyokuwa nayo tangu mwanzo kabisa. Sasa naweza kuelewa ni kwa nini ‘aliufunga mlango ule,’ wakati mimi nilidhani ungefunguliwa. Sasa naweza kuona jinsi alivyofanya kazi katika maisha ya watu wengine, hata wasioamini, ili kutimiza mipango yake kwa ajili yangu. Sasa naweza kusema kwamba najua masikitiko yangu mara nyingi ni miadi yake. Sasa naweza kumtumaini kwa kila sehemu ya maisha yangu yajayo, kwa maana amejithibitisha katika yaliyopita. Najua mawe ya kukanyagia yapo ingawa siwezi kuyaona bado. Kama yaliyopita yameweka mfano wa yatakayokuja, sitayaona kabla ya kuyapitia.
Nimekuja kuelewa kwamba ‘mwenendo wa imani’ hautegemei ‘kuamini’ kwangu kukubwa, bali kunyenyekea kwangu anapobadilisha mkondo wa maisha yangu kwa kuingilia kwake moja kwa moja. ‘Imani’ ya namna hiyo inahusiana zaidi na utii kuliko inavyohusiana na kuamini. Utii huzaliwa kutokana na kutegemea. Kama imani yangu ingepimwa kwa vipimo vitumiwavyo na baadhi ya ‘walimu wa imani’ wa siku hizi, ningefeli vibaya sana. Kwao, imani ni kitu ninachoweza kujichochea, hivi kwamba nikiwa na kiasi cha kutosha chake, naweza kumshawishi Mungu afanye nitakalo. Nikiwa mgonjwa, ni kwa sababu sina ‘imani’ ya kutosha, na nikiwa mhitaji, ni kwa sababu sina ‘imani’ ya kutosha. Lakini, ninaposoma Maandiko, yananifundisha kwamba siwezi kuizaa imani wala kuiongeza ndani yangu mwenyewe. Hiyo ni kazi ya enzi ya Bwana, naye huifanya kazi hiyo ninapojinyenyekeza kwa uongozi wake na kulifanya Neno lake kuwa msingi wa maisha yangu. Ninaposoma sura ile kuu ya imani katika Waebrania 11, sioni wanaume na wanawake wa ajabu wakisifiwa kama mashujaa kwa sababu waliamini, bali naona simulizi la Mungu kuingilia na kuongoza maisha ya watu wa kawaida ili kutufundisha kweli kuu na kanuni za maisha ya Kikristo, lakini yatosha theolojia kwa sasa! Tuendelee na habari yenyewe!