Sura 28 · dakika 8 za kusoma
Huduma Nchini Brazil
Majira ya pukutiko mwaka 1997, nilifanya safari yangu ya pili kwenda Fortaleza, jiji zuri la pwani la Ceara kaskazini-mashariki mwa Brazil. Hii tena ilikuwa kwa mwezi mmoja na safari hii niliandamana na Anne. Nilikuwa nimepata marafiki wengi katika ziara yangu ya kwanza, hivyo ilikuwa furaha yangu kumtambulisha kwao wote na kufurahia tena ladha ya vinywaji vya matunda mabichi na kinywaji nikipendacho zaidi, Guarana. Nilikuwa na huduma nyingi, pamoja na YWAM na katika makanisa ya hapo. Tulikaa katika kituo cha YWAM, umbali mfupi kutoka jijini, lakini tuliweza kusafiri kwenda maeneo mengi kwa huduma, manunuzi, fukwe, na kadhalika.
Anne alimwagiwa upendo na marafiki zangu, naye punde akajisikia yuko nyumbani, ingawa si wote waliweza kuwasiliana kwa Kiingereza, naye kwa hakika hakuweza kuwasiliana kwa Kireno. Mimi angalau nilikuwa na Kihispania kidogo cha kutegemea kwani kadhaa waliweza kuelewa Kihispania kama si Kiingereza.
Tulirudi Kanada kupitia Rio kwa kuwa wanandoa vijana kutoka ziara yangu ya kwanza ambao nilikuwa nimewaoza walikuwa wamehamia huko. Claudia na JudeClair walikuwa wakifanya kazi katika favella – eneo la mabanda lililosongamana la jiji - hivyo tulikaa nao usiku mbili. Walitupeleka katika mvua kubwa, hadi kwenye ghorofa ya vyumba viwili katikati ya mlima uliobeba favella ile.
Hapo tulikuwa na magodoro sakafuni nasi tukaonywa kwamba tukisikia milio ya risasi au kelele za watu usiku, TUSIINUKE kuchungulia nje kwani pengine tungekuwa sisi ndio wahanga wafuatao wa risasi! Kisha wakatuonyesha picha iliyokuwa imepigwa usiku uliopita ya mwili wa mtu uliokuwa umetupwa kutoka juu, ukatua kizingitini pao. Eneo hili lilikuwa limejaa magenge na mabwana wa madawa ya kulevya.
Asubuhi iliyofuata, nilimwuliza JudeClair kama ningeweza kupanda hadi kilele cha mlima ili nipige picha ya mlima wa jirani ambako sanamu maarufu ya Christo Rey (Kristo Mfalme) ilikuwa imesimikwa kwa fahari. “Je, una kitambulisho chochote?” aliniuliza kisha, akichukua kadi yangu ya kitambulisho ya Kanada niliyoinyoosha, akatembea nje ya mlango, mikono yote miwili juu ya kichwa chake, akiinua juu kadi yake na yangu. “Huku, wanapiga risasi kwanza na kuuliza maswali baadaye” lilikuwa neno lake la fumbo.
Nilipofika kileleni mwa mlima nilikuta kituo kingine cha YWAM kilichowahudumia watoto wa favella. Kilikuwa jirani na uwanja mdogo wa mpira wa changarawe wa mita 50 kwa 30 hivi, uliozungukwa na uzio wa waya. Upande mmoja kulikuwa na vile nilivyodhani vilikuwa vyumba vya kubadilishia nguo vya matofali ya majivu. Sasa vilikuwa vimeanguka na havikufaa kitu. JudeClair aliniambia kwamba muda mfupi kabla ya hapo, baadhi ya wanaume kutoka favella walikuwa wakicheza hapa wakati kikundi cha polisi kilipopanda mlima kwa njia nyingine, kikatokea ghafla juu na kuanza kupiga risasi, kikawaua wanaume wote. ‘Sababu’ yao ilikuwa kwamba miongoni mwa wanaume hao walikuwepo baadhi waliojulikana sana kuwa wahalifu na wasafirishaji wa madawa!
Tulithamini kweli kazi ambayo vijana hawa wanaifanya kwa ajili ya Bwana katika mahali pa hatari kuliko yote Uongozi wa kimataifa wa YWAM ulipangwa kukutana mwaka uliofuata nchini Brazil kwa kuwa rais wao wa wakati ule alikuwa mmisionari Mbrazil. Kituo cha Tony huko Fortaleza kilichaguliwa na vituo vingine vyote vya Brazil kuwa mahali pa mkutano huu wa viongozi wa YWAM kutoka duniani kote, hivyo alianza kupanga tukio hili kwa shauku. Aliamua kuwaita pamoja wachungaji wote wa hapo ili kujadili uwezekano wa kuandaa kongamano la umisionari sanjari na wamisionari hawa wa YWAM kuteremkia jiji lao, naye alitarajia kuwahifadhi kituoni – ambako kungeweza kuchukua mia moja hivi katika kanisa lake dogo – hadi hoteli moja ya hapo (nyota 5) ilipojitolea kuandaa chakula cha mchana kwa gharama nafuu.
Fikiria mshangao na furaha yetu wanaume zaidi ya 250 walipokutana na kuunga mkono kwa shauku wazo la Tony la kuandaa si kongamano la umisionari tu bali pia kampeni ya uinjilisti ya jiji zima. Kikubwa kiasi hicho kilikuwa kibali cha kijana huyu kwa viongozi wa makanisa!
Kwa kuwa Tony angekuwa na shughuli nyingi sana za kuandaa matukio haya mawili, pamoja na kupanga kongamano lao la viongozi wa kimataifa wa YWAM, alinialika kurudi mwaka uliofuata, kwa miezi mitatu, kuwasimamia wa-YWAM wote walipokuwa wakiratibu mikutano.
Mimi na Anne tulikubali kurudi na hivyo ikawa kwamba majira ya pukutiko mwaka 1998 tulirudi Fortaleza kwa miezi mitatu. Wenyeji wetu walikuwa Marcello na Aline Ramos, wanandoa vijana wamchao Mungu ambao hawakuchoka kutubariki.
Ghorofa yao ilikuwa katika orofa ya tano ya jengo la makazi karibu na ufukwe na matembezi ya kupendeza yalitupeleka hadi ofisi kubwa ya katikati ya jiji iliyokuwa kitovu cha maandalizi yote. Hali ya hewa huwa ya joto siku zote Fortaleza lakini, kila jioni, upepo wa baridi ulipuliza kupitia ghorofani ukiangusha picha zote ukutani kama tungekuwa wapumbavu wa kuacha madirisha yote wazi!
Nilijifunza kuwasiliana kwa Kireno na kutatua baadhi ya migogoro iliyozuka ofisini, hasa kutokana na tofauti za tamaduni kati ya wafanyakazi wa hapo na wa-YWAM wa nje ya nchi waliokuja kushiriki katika huduma ya uinjilisti, wakifanya kazi mitaani na shuleni kabla ya siku tatu ambazo tungekuwa katika uwanja wa mpira wa hapo kuhitimisha kampeni.
Mfano mmoja waonekana wa kuchekesha tukiutazama nyuma. Kikundi cha vijana kutoka Marekani kilikuwa kimetengeneza fulana za rangi zenye nembo “No comprommiso,” wakiamini hii ilimaanisha “Hakuna maridhiano.” Marafiki zangu Wabrazil walichanganyikiwa kwa kuwa maneno hayo kwa Kireno yanamaanisha kweli “hakuna kujitoa” – kinyume cha kile kilichokusudiwa!
Msisimko jijini ulikuwa wa kushikika kwani kila mahali mtu alipokwenda, kulikuwa na ushahidi wa ‘uvamizi wa Injili.’ Kongamano la Uongozi la YWAM lilikuwa bora kabisa nalo lilinipa fursa ya kukutana tena na kadhaa niliokuwa nimewafahamu wakati wangu ndani ya Anastasis.
Wamisionari kutoka nchi nyingi walikuja kuzungumza katika Kongamano la Umisionari, lililohudhuriwa na mamia mengi ya Wabrazil – mafanikio makubwa ambayo yangewatambulisha wamisionari wengi wapya kwa ulimwengu. Rafiki yangu Marcello ni mkalimani bora kabisa hivyo ni yeye aliyetafsiri kwa sehemu kubwa ya kampeni ya uinjilisti. Hii pia ilikuwa mafanikio makubwa katika athari yake na katika idadi ya kadi za wanaotafuta ambazo tungewakabidhi wachungaji wa hapo baadaye ili wazifuatilie. Nilipomwuliza Jon, aliyehusika na kadi hizi, tulikuwa tumepokea ngapi, maneno yake hayatasahaulika kamwe. “Gareth” alisema, “tuliacha kuhesabu tulipofika 45,000!”
Nilivutiwa sana na kikundi cha muziki kilichoongoza ibada katika kila moja ya jioni tatu uwanjani. Walikuwa kikundi cha kaka na dada, wakiwa na wanamuziki wasaidizi kutoka kanisa kubwa la Belo Horizonte. Ilionekana wazi kwamba, kila mara vijana walipokuwa na shauku katika kuitikia muziki, ama kaka au dada mara moja angewarudisha katika utulivu kwa kupiga magoti kimya kwenye kipaza sauti na kuomba.
Nilikutana na yule kaka nilipokuwa nikitembea na Marcello ufukweni siku iliyofuata nikamweleza maoni yangu juu ya hili. Jibu lake lilikuwa lenye kutia moyo sana aliposema kwamba walitambua jinsi nyakati kama hizo zingeweza kuwa za ‘kinafsi’, hivyo yeye na dada yake waliazimia kuelekeza shauku yote kurudi kwa Mwokozi ambaye peke yake anastahili sifa. Haishangazi wanamwona Bwana akifanya mambo ya ajabu namna hiyo kupitia huduma yao!
Ningerudi Fortaleza mwaka 2002, miaka minne baadaye, nikafurahi kuona kwamba kila kanisa nililotembelea lilikuwa limeongezeka angalau maradufu tangu ziara yangu ya mwisho. Tena, nilizungumza katika makanisa mengi na kuwahudumia watu wengi walioguswa na mafundisho yangu juu ya ‘Kuachiliwa’ (ona kitabu changu The Key in My Hand). Miongoni mwa mambo makuu, ni kuzungumza katika kongamano la wachungaji wa Assembly of God la Kaskazini-Mashariki mwa Brazil. Hili lilikuwa tukio la siku tatu lililohudhuriwa na wachungaji kama 150.
Jambo lingine kuu lilikuwa kuwahudumia wanandoa vijana waliokuwa wameoana miezi sita tu iliyopita lakini sasa walikuwa katika uhusiano mbaya usio na ukaribu. Maria mfupi alinijia kwa huzuni kubwa akisema kwamba Alfonse alikuwa amejitenga naye (si majina yao halisi). Hadithi yake ilipofunuka, niliumia kusikia tena juu ya unyanyasaji ambao wengi kiasi hicho wanaupokea kutoka kwa baba zao. Sitaingia katika siri zote ambazo Maria alishirikiana nami lakini yatosha kusema kulikuwa na unyanyasaji mwingi wa maneno kutoka kwa baba yake. Alipokuwa katika miaka yake ya mwisho ya ujana alimjia Kristo, akakutana na kijana mmoja (Alfonse) na wakaoana.
Kwa kuwa mchungaji aliamini uvumi kwamba alikuwa kahaba, uvumi ambao yeye aliukana, alikataa kuwaoza kanisani, badala yake akachagua sherehe ndogo nyumbani kwa bwana harusi, iliyohudhuriwa na wazazi wake tu. Muda mfupi baadaye walikuja Fortaleza kufanya kazi na YWAM. Nilimfundisha Maria kwamba baba yake na mchungaji walikuwa wametenda dhambi dhidi yake na kwamba alihitaji ‘kuwaachilia’ ili Mungu aweze kuanza mchakato wa uponyaji ndani yake.
Alipaswa kuandika barua akiyaorodhesha malalamiko yake yote dhidi ya baba yake ili awe na kumbukumbu ya yote ambayo alikuwa tayari kumwachilia kutoka kwayo. Usiku uliofuata alikesha hadi usiku wa manane akiiandika barua ile (ambayo isingetumwa kamwe) naye alikuwa amemaliza tu kuiandika wakati Alfonse alipoamka usingizini, akaingia chumbani na kumpokonya barua ile kwa hasira. Aliingia tena chumbani dakika chache baadaye akilia na kusema, “Sikujua! Sikujua!” Wakakumbatiana na usiku ule ukaishia katika ukaribu. Asubuhi, walikuja pamoja ili kunionana, wakiwa wameamua ‘kumwachilia’ baba yake na kumwombea baraka juu yake.
Siku iliyofuata Christine, mke wa Tony akanijia akisema, “Gareth, kila mwezi wanandoa wa kituoni hukutana pamoja kwa jioni ya ushirika na furaha, na baada ya hapo huchukua sadaka ili wanandoa wamoja waweze kuwa na jioni ya kimapenzi katika hoteli ya hapo mbali na kituo.”
“Mwezi huu, fedha hizo zilitolewa kwa Maria na Alfonse, lakini walizikataa.” Nilijua kwa nini. “Sasa wamekuja na kuziomba hivyo wataondoka kituoni mwishoni mwa juma hili. Je, unajua kwamba hawakuwahi kuwa na harusi ya kweli, hawana picha zozote za harusi na hawakuwahi kuwa na sherehe ya mapokezi? Nilikuwa nikijiuliza wewe unafikiriaje juu ya wazo hili. Nina gauni langu la harusi hapa nami nina umbo sawa na la Maria. Je, unadhani wangeudhika kama ningewapa gauni langu ili wapate kupiga picha nzuri kabla ya kwenda hotelini?”
Ingawa Christine hakuwa na wazo lolote juu ya ushauri niliokuwa nimewapa wanandoa hao, nilimhakikishia kwamba hilo lingekuwa wazo zuri, hivyo tulikwenda pamoja kuwaambia, jambo lililonipa pia fursa ya kuwahakikishia kwamba bado nilizishika siri zao.
Siku iliyofuata nilikuwa naondoka kwenda Kanada, Tony aliponipeleka uwanja wa ndege, nilimpendekezea kwamba angeweza kuwaita wote wa kituoni pamoja wikendi na kufanya sherehe ya ‘maadhimisho ya upendo’ kwa ajili ya Alfonse na Maria, ambapo wangeweza kuvaa ‘mavazi yao ya harusi’, kuweka nadhiri na kupiga picha za kumbukumbu. Alifikiri hilo ni wazo zuri. Kisha akaongeza lake mwenyewe. Kwa kuwa alipangwa kuwapeleka hotelini, angejifanya ‘kupotea njia’ akiishia katika nyumba ya ufukweni, iliyokuwa na bwawa lake la kuogelea, iliyomilikiwa na Romeo rafiki aliyekuwa ameitoa bure kwa ajili ya wikendi. Wengine wote wa kituoni wangekuwepo na ‘keki ya harusi’ na sherehe ya mapokezi kwa ajili ya wanandoa hao. Hivyo, ndani ya siku mbili tangu ‘kumwachilia’ baba yake, Maria angefurahia baraka zote za harusi, sherehe ya mapokezi pamoja na marafiki na picha. Niliruka nyumbani nikishangilia wema wa Mungu wetu!