Sura 27 · dakika 7 za kusoma
Njiani Kuelekea Varanasi
Mwaka 1996, nilipokea barua kutoka seminari moja kaskazini mwa India ikiuliza kama ningekubali kuja huko kufundisha katika juma la “Msisitizo wa Kiroho”. Kungekuwa na Mhindi akizungumza katika hema kubwa kila jioni nami nilipaswa kufundisha kwa saa moja kila asubuhi kwa wanafunzi wote, wafanyakazi na waamini wa hapo ambao wangeweza kuja. Mwandishi aliongeza kwamba alikuwa amepewa jina langu na ndugu mmoja huko Uingereza aliyekuwa ametaja kwamba yaelekea ningekuja hata kama wasingeweza kutoa msaada wowote wa fedha. Nilikubali kwenda kwa kuwa nilikuwa tayari nimejitoa kwa Bwana kwamba ningekubali mwaliko wowote maadamu kungekuwa na fedha za kutosha katika ‘akaunti yangu ya huduma’ ambako zawadi zote za shukrani, michango, na kadhalika, zilikuwa zimewekwa.
Safari ilipangwa kwa Februari 1997. Anne alitaja safari hii katika barua yetu ya Krismasi mwisho wa mwaka ule, hivyo hatukushangaa sana barua nyingine ilipofika mapema mwaka mpya ikiuliza kama ningeirefusha safari yangu ya Asia kwa mwezi mmoja zaidi wa huduma na Youth With A Mission (YWAM) huko Nepal. Hili nilikuwa na hamu ya kulifanya kwa kuwa tuna kumbukumbu za joto namna hiyo za ushirika wetu na waamini wa Kinepali miongoni mwa askari wa Ghurka wa Hong Kong. Hivyo safari ikapangwa – majuma mawili Allahabad, India, yakifuatiwa na mwezi mmoja Nepal, ambako kutoka huko ningesafiri hadi Australia na Capernwray School ambapo Anne angenisubiri.
Tiketi yangu ya safari nzima ya miezi mitano iligharimu karibu sawa na nilichokuwa nacho katika ‘akaunti ya huduma.’
Nilizungumza katika madarasa matano madogo ya seminari New Dehli kabla ya kupanda treni ya usiku kwenda Allahabad na seminari. Mzungumzaji mkuu asipofika siku ya Jumapili, niliombwa kuzungumza katika mkutano wa hema kubwa mbele ya mamia kadhaa ya waamini. Kisha kila asubuhi, niliwahutubia wanafunzi mia moja pamoja na wafanyakazi na wageni, wakiwemo wengi kutoka seminari ya wanawake ya hapo – takriban mia mbili kwa jumla. Mambo yalikwenda vizuri sana, na wote waliyapokea mafundisho yangu kwa wema.
Siku ya Jumamosi, kazi yangu ilikuwa imekwisha lakini nilikuwa na tatizo. Jumatatu iliyofuata, nilipaswa kuruka kwenda Kathmandu. Hata hivyo, mawakala wa Air India waliniambia kwamba tiketi yangu (iliyokatwa kwa kompyuta majuma kadhaa awali huko Kanada) haikuweza kupatikana, na kwamba tarehe ya mapema zaidi wangeweza kunipandisha ndegeni ilikuwa Ijumaa, juma moja baadaye. Njia pekee mbadala ilikuwa kupanda basi kwa saa kumi na tano juu ya barabara ya daraja la pili, na kubeba mizigo yangu miwili mizito umbali mrefu kupita mpakani. Uwanja wa ndege wa karibu zaidi ulikuwa Varanasi, kilomita 150 kutoka pale hivyo sikuweza kwenda uwanjani kwa urahisi kuchunguza tatizo.
Katika mwaka uliopita, rais wa seminari alikuwa ameondoka na kiongozi wa muda, mmisionari wa zamani kutoka Marekani, aliyekuwa akiielekeza kazi. Rudy Raby na mkewe Eleanor walikuwa wamefikia miaka ya 70 lakini upendo wao kwa Bwana na kazi yake haukuwa umepungua.
“Gareth, ni lazima niende uwanja wa ndege siku ya Jumamosi, kumchukua mgeni kutoka Australia,” alisema Rudy. “Kwa nini usiende nami ili uone kama unaweza kugundua nini kilichoipata tiketi yako? Labda wamechanganya jina lako katika kumbukumbu zao huko.” Nilipoamka asubuhi ile ya Jumamosi, nilimhakikishia Bwana kwamba nilikuwa tayari kusafiri kwa basi, lakini ningependelea zaidi kusafiri kwa ndege! Hivyo ikawa kwamba muda mfupi baadaye, Rudy, Eleanor nami tulianza safari ya saa tano kutoka Allahabad hadi Varanasi, uwanja wa ndege.
Safari ilikuwa ya polepole kwani barabara nyembamba yenye kupinda ilikuwa imejaa mashimo, watu, na ng’ombe. Kama saa tatu ndani ya safari, Eleanor alihisi uhitaji mkubwa wa kusimama kwa choo. Nchini India hilo mara nyingi humaanisha ‘nyuma ya kichaka cha karibu zaidi’ hivyo Rudy akaagizwa asimame mahali pa kwanza panapofaa. Hapo hapakumfaa Eleanor hivyo Rudy akaambiwa aendeshe mbele kidogo. Hili likarudiwa mara tatu hadi tuliposimama nyuma ya gari lililoegeshwa.
Eleanor alipoingia vichakani vya karibu, dereva wa gari lile, ambaye lazima alikuwa ameona mwendo wetu wa kusimama-na-kwenda wa dakika chache zilizopita, alitoka garini mwake na kutukaribia.
“Kuna tatizo?” aliuliza. “Hapana, ni kusimama kwa choo tu” akajibu Rudy, na kisha, akitazama kwa makini, “Hebu, si wewe ni Simon Job?”
“Ndiyo,” akajibu yule mgeni. “Wewe ni nani?” “Mimi ni Rudy Rabi!” alipaza sauti Rudy aliporuka garini na wote wawili wakakumbatiana. Ni dhahiri kwamba miaka kumi na mitano awali, Simon na mwana wa Rudy walikuwa marafiki wa karibu shuleni huku baba zao wakifundisha seminarini.
Nilitambulishwa na, aliposikia juu ya tatizo langu la tiketi, Simon aliniomba ratiba yangu ya safari, akisema “Niachie hili mimi.” “Je, wewe ni malaika?” niliuliza, nikitazama kuona kama kulikuwa na mabawa yoyote yanayoonekana.
Baadaye jioni ile, tulipokuwa tukipumzika katika hoteli moja ya Varanasi, Simon alipiga simu kuniambia kwamba wakala wake angenipeleka uwanja wa ndege asubuhi. Hakuwa ameweza kunipangia tiketi lakini alinihakikishia kwamba wakala wake angejitahidi kadiri ya uwezo wake wote.
Katika safari ya kilomita 25 kwenda uwanjani asubuhi iliyofuata, ‘wakala’ wake, meneja wa hoteli yangu, aliniambia kwamba katika jiji lile la Kihindu Simon Job alikuwa mmoja wa watu wanaoheshimika kuliko wote, ambaye maadili yake ya Kikristo yalionekana katika biashara zake zote. Aliniambia pia alikuwa amewasiliana na ofisi ya Air India asubuhi ile nao wakanifanya nambari 10 katika orodha yao ya kusubiri ya ‘daraja la biashara’. Nambari 10! Moyo wangu ulizama nilipotambua tumaini dogo nililokuwa nalo la kupata kiti, nikijua kuna viti kama kumi tu katika daraja la biashara.
Ukumbi wa uwanja ulikuwa umejaa wasafiri, wengi wao mahujaji na watalii wa jiji hili la Kihindu kuliko yote ya India. Niliketi juu ya mizigo yangu kona moja huku wakala akienda kutafuta tiketi yangu. Dakika kumi baadaye alirudi. “Bwana Evans, nimelipata jina lako!” alipaza sauti, “lakini wamekutoa katika orodha ya abiria ya Jumatatu kwa sababu wana kundi kubwa la watalii linalopita!” Alipoona kufa moyo kwangu, aliharakisha kuongeza, “Niliwaambia hakuna anayemtoa rafiki wa Simon Job katika orodha ya abiria!”
Saa moja ilipita. Kundi kubwa la wasafiri lilikuwa limeondoka kwenda ukumbi wa kuondokea, nami nilikuwa nikisubiri kwa saburi wakala na dereva wake warudi ili tuweze kurudi jijini. Papo hapo, kijana mmoja alikimbia kunijia akiwa na tiketi mkononi mwake. “Njoo, bwana,” alipaza sauti, “Uko katika ndege hii leo.” Alichukua mizigo yangu yote miwili ya safari na kukimbia kuelekea lango la kuondokea. Nilipomfikia, niliuliza, “Ni wangapi kutoka orodha ya kusubiri waliopanda ndege?” Aliponiambia kwamba wawili tu ndio waliopata tiketi, nilionyesha mshangao, nikijua kwamba nilikuwa nambari 10. Akajibu, “La hasha, bwana, yeyote aliye rafiki wa Simon Job ni nambari 1 hapa juu!” Nilikimbia juu ya ngazi kuingia ndegeni ili tu kugundua kwamba mimi ndiye nilikuwa peke yangu ndani!
Mhudumu aliponiketisha katika kiti cha kwanza, niliogopa kwamba nilikuwa katika ndege isiyo sahihi, hadi nilipoona milango ya jengo la abiria ikifunguka na abiria wengine wote wakitembea kutuelekea. Kila mmoja wao aliniinamishia kichwa alipoingia akidhani kwamba nilikuwa mtu fulani mkubwa! Na, bila shaka mimi ni hivyo – Mwana wa Mfalme - na rafiki wa Simon Job!
Je, yawezekana kwamba Mungu, akijua mtoto wake alikuwa na matatizo ya safari, alimfanya mfanyabiashara kijana asimame kando ya barabara mahali pale pale ambapo, dakika chache baadaye, mwanamke mzee angehitaji kusimama kwa ajili ya choo? Sadfa? Sidhani hivyo!
Kulikuwa na mwezi wa ajabu wa huduma Nepal, ambao humo niliwapata wawili wa askari wa Ghurka niliopata upendeleo wa kuwafundisha Hong Kong. Nilizungumza na vikundi vingi vya YWAM na katika makanisa kadhaa.
Nilipata upendeleo mkubwa wa kukutana na mtu aliyekuwa amechunga kanisa wakati wa mateso makubwa kabla taifa halijaruhusu huduma za Kikristo mapema miaka ya 90. Takwimu zangu hapa chini pengine si sahihi lakini si kwa mbali sana. Alikuwa amekamatwa mara ishirini, ametiwa gerezani mara nane akitumikia hata miaka kumi na miwili nyuma ya nondo. Kila mara alipoachiwa, alirudi kanisani kwake kilichoteketezwa na kuanza kuhubiri tena. Vitisho, kipigo na kukamatwa vikafuata tena.
Kwa kuwa sikuwahi kupitia mateso, nilimwuliza aliwezaje kuwa shujaa namna hiyo katika yote. Jibu lake lilikuwa lenye kuangaza. Alisema, “Gareth, kwa nini niogope wakati najua simba ameshanguruma kwa sauti yake kubwa kuliko zote?” Unyenyekevu wake ulifunuliwa pia wakati, katika mapumziko ya mafundisho yangu ambayo yeye alikuwa mkalimani wake, sisi wawili tuliletewa vikombe vya bati vya Coca Cola kwa burudisho. Alitoa maoni, “Ni upendeleo ulioje kusimama pamoja na nabii – kwa maana hata punda hupata kunywa!”
Ndani ya ndege iliyotoka Kathmandu, nilibarikiwa kupata kiti cha dirishani upande wa kushoto, ambako nilipata mandhari ya ajabu ya milima ya Himalaya, tulipokuwa tukisafiri mashariki kabla ya kugeukia kusini kwenda Singapore na Sydney. Anga lilikuwa buluu ing’aayo, milima ikimetameta myeupe na safi kabisa, yote isipokuwa pembetatu moja ndogo nyeusi – Everest, ambao uso wake wa kusini ni mteremko mkali mno kushika theluji!
Niliruka kwenda Sydney, na kutoka hapo hadi Capernwray Bible School ambako Anne alikuwa akinisubiri. Hapa, niliwafundisha vijana kutoka Australia, Ulaya na Kanada kwa juma moja.
Hii ingekuwa zawadi ya kwanza ya shukrani kwa miezi miwili kwa kuwa kazi zote mbili India na Nepal hazikumudu kusaidia gharama zozote za safari yangu. Yatosha kusema kwamba baada ya miezi mitatu Australia, jumla ya zawadi zangu za shukrani huko zilifikia karibu sawa na gharama ya tiketi ya miezi mitano ya safari hii ya pamoja! Zaidi ya hayo, kanisa la Lynette liliamua kutushtua na kutubariki kwa ‘sadaka ya upendo’ ambayo tena ililingana na gharama ya tiketi ya Brazil, nilikoelekea mwezi mmoja baadaye. Mungu ni mwaminifu!