Sura 24 · dakika 5 za kusoma
Kugusa Mizizi Yetu
Mambo makuu ya miaka minne tuliyoitumia melini, Anastasis, yalikuwa mengi. Ulikuwa wakati wa pekee kwa Anne na kwangu. Hata hivyo, ninapofikiria ‘mawe ya kukanyagia’ naweza kuona si tu jinsi Mungu alivyokuwa akiniandaa kwa ajili ya huduma ya baadaye, bali pia jinsi alivyokuwa akituwezesha ‘kugusa mizizi yetu.’ Nitasimulia baadhi ya ‘sadfa’ za ajabu zilizoendelea katika kipindi hicho.
Tuliungana na meli huko Amsterdam nasi tukakaribishwa kwa uchangamfu na watu kadhaa tuliowakumbuka tangu siku za Victoria. Miongoni mwao alikuwa Odd Neilson aliyehudhuria kanisa langu kwa miezi kumi na minne ambayo meli ilikuwa katika gudi kavu, mwaka 1986. Aliniambia kwamba angeoa baada ya majuma sita meli itakapofika Oslo, Norwei, akauliza kama ningeongoza sherehe hiyo. Kwa kawaida, nilifurahi sana.
Harusi ilipangwa kufanyika katika Salem Pentecostal Church. Hivyo, meli ilipowasili, tulihudhuria ibada ya Jumapili juma moja kabla ya harusi iliyopangwa. Mchungaji alinialika kuwasilisha salamu kwa kusanyiko lake na kuleta habari kuhusu Anastasis. Hili nilifanya kisha nikaongeza, “Nawaletea pia salamu kutoka kwa mama mkwe wangu aliyehudhuria kanisa hili zaidi ya miaka hamsini iliyopita pamoja na mumewe na watoto wawili.” Mchungaji aliuliza jina la baba yake Anne endapo mtu fulani pale angeweza kuwakumbuka.
Mwishoni mwa ibada, mwanamke mmoja alimwendea Anne kwa maneno haya, “Namkumbuka mama yako na baba yako, na dada yako Betty, na kaka yako David. Baba yako ana dada; Paula anayeishi sasa Karlskoga, Uswidi, naye ni rafiki yangu wa karibu zaidi. Zaidi ya hayo, sasa hivi yuko akinitembelea, nyumbani kwangu, jengo moja tu kutoka kanisa hili!” Kwa kawaida, Anne alifurahi kuandamana na mwanamke yule baada ya ibada kukutana na Shangazi Paula na, kupitia kwake, ndugu wengine wote walioishi Oslo. Katika majuma matatu yaliyofuata, tulikutana na zaidi ya ndugu ishirini na watano wa Anne, tukila nyumbani kwa mtu tofauti kila jioni.
Kabla meli haijaondoka Ulaya kwenda miezi sita ya Afrika, tulipata fursa ya kuwatembelea marafiki wengine wengi tuliowafahamu miaka yetu ya Hamm pamoja na Majeshi ya Uingereza. Ilionekana kwamba wale pekee ambao tungewakosa wangekuwa Lars na Marion Friedner, na marafiki wa familia huko Stocklholm. Kwa hiyo tulipokea kwa furaha mwaliko wa kufundisha katika kambi ya YWAM ya huduma yao ya vijana KING’S KIDS, huko Laxo, saa nne kusini-magharibi mwa Stockholm. Mara moja tuliwaandikia Lars na Marion tukiwaeleza mipango yetu ya kuendesha gari hadi kwao katika mojawapo ya siku za mapumziko za kambi lakini hatukupokea jibu kabla ya kuondoka melini. Hatukujua kwamba walikuwa mbali likizoni juma lile lile la kambi yetu, na kwamba nyumba yao ya likizo ilikuwa safari fupi tu kutoka Laxo.
Siku ya Alhamisi, binti yao Ingemo na mumewe walisafiri kwenda kuwatembelea wazazi wake wakichukua pamoja nao barua zao zote za karibuni, ikiwemo barua yetu. Waliposimama kwa chakula cha mchana safarini mwao, Ingemo alitambua majina yetu nyuma ya bahasha hivyo akaifungua na kusoma kwamba tungekuwa Laxo wakati ule. Alikaa akiwa amefungua kinywa kwani walikuwa wamesimama katikati ya Laxo kwa mapumziko yao. Alasiri ile, Lars alitupigia simu nasi tukapanga kukutana nao wote siku iliyofuata.
Huduma yetu ya mwisho na Anastasis ilikuwa kuongoza Advance Team kabla ya ziara yake Cardiff, Wales mwezi Septemba 1994. Niliongoza timu ya vijana watano wa ajabu tulipowasiliana na vyombo vya habari, makanisa, biashara, shule, na kadhalika, tukiwajulisha na kuwaandaa kwa kuja kwa meli.
Kwa kawaida, nikiwa mvulana wa hapa, nilikuwa na mawasiliano mengi makanisani na ratiba yangu ilikuwa imejaa nafasi za kuzungumza. Nilialikwa kuzungumza katika Sikukuu ya Mavuno ya alasiri huko Zoar, kanisa la Kipresbiteri la ujana wangu na la Shule ya Jumapili, ambako mama yangu alipiga kinanda na amezikwa. Nilipotembelea kaburi lake, mzee mmoja alinikaribia kwa maneno haya, “Iliwezekanaje mtundu kama wewe kuwa mchungaji?” Baadaye, tukiwa na sandwichi za tango na chai ya moto, nilitambulishwa kwa kijana mmoja, aliyerudi nyumbani kutoka Madagascar ambako anatumika kama mmisionari. Niligundua kwamba alikuwa mwana wa mpenzi wangu wa kwanza nilipokuwa na miaka kumi tu. Lo, nilipokea viboko vingi kutoka kwa mwalimu mkuu wangu siku zile kwa kuandika barua za mapenzi kwa Barbara!
Baadaye, meli ilipokuwa bandarini na wanawake wengi walipokuja melini kwa ajili ya mikutano ya wanawake, nilitazama bure kuona kama Barbara alikuwa miongoni mwa wageni. Hata hivyo, siku kadhaa baadaye, nilipewa barua fupi kutoka mapokezi yetu iliyosema, “Kasisi mpendwa, ni kukujulisha tu kwamba mpenzi wa sasa wa mpenzi wako wa kwanza alikuja melini leo!”
Juma moja baada ya Zoar, nilipaswa kuzungumza katika mkutano wa wazee wa kanisa dada lake, maili tano kutoka pale. Nilipoketi katika benchi ya mbele nikiandaa mada yangu, mchungaji alikuja na mwanamke mzee akauliza kama angeketi kando yangu kwa kuwa “Dolly ni mwanachama wetu mkongwe kuliko wote naye anahitaji kuketi mbele ili asikie.” Nilimwuliza kama alikuwa vizuri kisha yeye akaniuliza mimi ni nani. Nilipomwambia, alisema, “Lo, wewe na mimi ni ndugu!” Niligundua kwamba Dolly Hallett alikuwa binamu ya mama yangu naye aliishi jirani kabisa katika Railway Terrace, Peterston-super-Ely, mahali pa utoto wa mama yangu.
Kwa hakika, nilikuwa nimegeuza gari langu katika njia yake ya kuingilia alasiri ile ile nilipozunguka maeneo niliyoyazoea ujanani na kwenda kuona nyumba ya zamani ya babu na bibi yangu. Nilimwahidi kumtembelea mchana wa siku iliyofuata, nikiwa na Anne. Tulipokelewa na Dolly pamoja na binti zake wawili Dorothy na Thelma ambao, waliponiona, walipaza sauti, “Lo, wewe ni Lovelock kweli kweli!” Kisha wakanisimulia hadithi za ajabu kama nini juu ya mama yangu akiwa msichana, hadithi ambazo sikuwahi kuzijua. Walikumbuka huzuni yao alipokufa akiwa “mwanamke kijana mzuri kama nini.”
Niliwaambia juu ya meli iliyokuwa ikija baada ya majuma mawili na nikaongeza kwamba George Thomas, Lord Tonypandy, spika wa zamani wa House of Commons na mmoja wa watu mashuhuri kuliko wote katika historia ya Wales, angekuwa mgeni wetu siku moja melini. “Lo, tunamjua George vizuri,” wakasema wale dada, “Alikuwa akija Railway Terrace kumtembelea dada yake aliyeishi hapa. Tumekwenda nyumbani kwake mara nyingi.”
Siku iliyopangwa, Lord Tonypandy alikuja akatumia kama saa mbili na baadhi ya viongozi wetu, akishiriki imani yake mwenyewe katika Bwana na kututia moyo kazini kwetu. Baadaye, nilipomsindikiza chini ya ngazi ya meli hadi garini mwake, nilimwuliza alikumbuka nini juu ya Dolly Hallett na binti zake. Kumbukumbu zake zilikuwa tele lakini kisha akauliza niliwajuaje. Nilimwambia kwamba Dolly alikuwa binamu ya mama yangu na kwamba waliishi jirani kabisa huko Peterston. Aliposikia kwamba mama yangu alikuwa Ethel, alipaza sauti, “Ethel! Je, wewe ni mtoto wa Ethel?” Ni dhahiri kwamba yeye pia alikuwa na kumbukumbu ya joto sana juu ya binti mdogo kuliko wote wa ‘familia ile kubwa.’ (Mama yangu alikuwa mdogo kuliko wote kati ya kumi na watatu).
Nikipanda tena ngazi ya meli, nilitambua kwamba angekuwa na umri sawa na mama yangu - labda yeye alikuwa mpenzi wake wa kwanza! Najiuliza kama alipokea viboko vingi kwa kuandika barua za mapenzi. Ilikuwa vizuri sana kugusa mizizi hii na kupokea maoni ya joto namna hiyo juu ya mama.