Sura 23 · dakika 4 za kusoma

Mwito wa Kwenda Afrika

Nifanye nini sasa nikiwa na wakati mwingi mikononi mwangu? Dawa zangu zilikuwa zikifanya kazi, nami nilikuwa nikilala saa chache kila usiku. Kimwili, nilijisikia vizuri lakini akili yangu ilikuwa bado imechoka. Taratibu shauku nne zilianza kujitokeza.

Ningependa kufanya kazi fulani ya kujitolea; ndani ya Anastasis. Meli hiyo sasa ilikuwa Afrika Magharibi, lakini ingekuwa vyema kuchukua muda kando nikiwa ‘nakwangua kutu’ - au kufanya kingine chochote kilichohitajika. Labda ningeenda Hawaii. YWAM walikuwa wamefungua University of the Nations huko nami ningeweza kwenda katika Crossroads School kwa muda wa miezi mitano. Ingependeza ‘kupokea ndani’ badala ya ‘kutoa nje’ wakati wote.

Ningeweza kwenda Amerika ya Kusini kuwa pamoja na wamisionari wa huko. Nilikuwa tayari nimekwenda Mexico na kuona kwa macho yangu uhitaji wa mchungaji kwa ajili ya wamisionari. Labda ningeanzisha shule mjini Victoria ya kufundisha misingi ya Neno na kuwafunza wanafunzi kwa ajili ya umisionari.

Miaka miwili kabla, niliombwa kutumika katika Bodi ya Kanada ya Mercy Ships, tawi la baharini la YWAM lenye jukumu la M/V Anastasis. Hili lilikuwa takwa la kisheria tu la kuwawezesha wafadhili wa Kanada kupokea risiti za kupunguziwa kodi.

Tulipaswa kufanya mikutano ya mwaka ambayo ingeweza kuendeshwa kwa simu ya ‘mkutano wa pamoja’. Hivyo ikawa, katikati ya mwezi Oktoba, kwamba Don Stephens, rais wa Mercy Ships, aliendesha mkutano wa simu wa saa moja, na mwishoni mwake nikamwomba anipigie simu kwa jambo la binafsi. Nilikusudia kumwuliza maoni yake juu ya mawazo mawili ya kwanza niliyoyaandika. Je, ningeweza kuwa na manufaa yoyote ndani ya meli?

Je, kulikuwa na faida yoyote kwangu kuhudhuria Crossroads School? Alisema angenipigia baadaye. Muda mfupi baadaye Don aliondoka kwenda kutembelea Asia ya Kusini-Mashariki na ombi langu likasahaulika. Haikuwa hadi mwezi mmoja baadaye ndipo hatimaye alipopiga simu, na wakati huo mazingira mengine yalifanya isiwezekane kwangu kusafiri ama kwenda Afrika Magharibi au Hawaii - angalau kwa miezi mitatu. Aliomba radhi kwa kusahau kwake kisha akasikiliza nilipoeleza kwa nini nilikuwa nimeomba anipigie.

Kisha Don akasema, “Nina sababu nyingine ya kupiga simu. Jana jioni, Baraza letu lilikutana, na kasisi aliyepo sasa akaomba likizo ya kutokuwepo. Je, wewe na Anne mngekuwa tayari kuja melini kuwa makasisi wetu? Hii hapa namba yangu ya faksi. Nirudie mara tu wewe na Anne mtakapofanya uamuzi wenu!”

Nilimpigia Anne simu kazini, nikitarajia kabisa jibu la kukataa. Hakukuwa na njia yoyote ambayo angekubali kuacha nyumba yetu, binti zetu na wajukuu ili kuishi katika jumuiya ndani ya meli katika joto la Afrika Magharibi. Sikuweza kuamini masikio yangu aliposema, “Tunaondoka lini?” Nilikuwa na hakika nilikuwa nimepiga namba isiyo sahihi! Yeye alishangazwa na jibu lake kama nilivyoshangazwa mimi, lakini tumegundua kwamba Bwana hutoa neema siku zote pale tu inapohitajika. Mipango ilifanywa ili tuungane na meli huko Rotterdam mwezi Mei wa mwaka 1991, punde tu iliporudi kutoka safari yake ya kwanza ya kuhudumu Ghana, Afrika Magharibi.

Tukiwa tunaisubiri meli, tulitumia fursa kuhudhuria Crossroads School huko Lindale, Texas, makao ya Mercy Ships. Tulikuwa na miezi mitatu ya ajabu, ya kupumzika, tukifurahia mafundisho na ushirika. Baadaye, katika juma letu la kwanza melini, nilialikwa kufundisha katika Discipleship Training School (DTS) na ndipo nilipotambua kwamba ndani ya miezi minne nilikuwa nikifanya mambo yote manne niliyokuwa nimeyatamani. Hata hivyo, nilikuwa pamoja si na mmisionari mmoja bali zaidi ya mia tatu! Najua jinsi nilivyokuwa na upendeleo wa kutumika ndani ya meli hii lakini naweza tu kutazama nyuma kwa mshangao jinsi Bwana alivyoniongoza katika kila hatua ili kunileta hapo. Najua bonde la mwaka 1990 lilikuwa refu sana, lakini sasa alikuwa amenileta juu ya kilele cha mlima kilichokuwa kirefu sana. Ni kweli siku zote kwamba mabonde marefu hutangulia milima mirefu.

Nimewaona watu wakija melini wakiwa na ulemavu wa kutisha wa uso, wenye kujithamini kidogo na waliohesabiwa kuwa laana katika jamii zao wenyewe. Nimewaona watu hao hao wakiondoka wakiwa wameinua vichwa vyao juu baada ya madaktari wetu wa upasuaji kuwapa heshima. Nimekwenda katika kliniki za matibabu na za meno na kutazama kukata tamaa kukigeuzwa kuwa tumaini huku wajitoleaji waliojitoa wakihudumia mahitaji ya watu wasio na fursa ya kupata huduma ya matibabu ambayo sisi tunaidharau kwa kuizoea.

Naweza kutazamia baraka tulizoacha katika nchi ambako tulijenga shule au tawi la hospitali au kliniki, ambako maji safi na vyoo vya usafi husaidia kukomesha magonjwa yauayo. Hata hivyo, furaha yangu kuu ilikuwa katika fursa ya kuwahudumia wamisionari na wachungaji katika semina na makongamano ya kila juma.

Nilipoona umoja ukikua kati yao na kusikia maneno yao ya shukrani kwa mafundisho, nilijua nimebarikiwa kweli na Bwana. Katika Sierra Leone, kwa mfano, niliweza kuwafundisha zaidi ya viongozi 150 wa kanisa, saa tatu kila juma, kwa jumla ya majuma kumi na moja! Ingawa sikuwahi kwenda katika Chuo cha Teolojia, niliwafundisha viongozi wote wa madhehebu makuu ya nchi ile - wanaume 23 - kwa siku mbili.

Mbadilishe mchungaji nawe utalibadilisha kanisa; wabadilishe wachungaji 100 nawe utalibadilisha taifa!! Ni upendeleo ulioje wa kileleni mwa mlima!

Ukurasa 1 / 3 · 4 dakika zimebaki katika sura