Sura 25 · dakika 5 za kusoma
Milango Inayofunguka
Mimi na Anne tuliondoka M/V Anastasis mwishoni mwa mwaka 1994. Yalikuwa yamepita miaka minne yenye kuridhisha sana tangu bonde langu la ukosefu wa usingizi, nasi tulikuwa tumebarikiwa kwa mambo mengi ya ajabu na marafiki wapya. Tulikusudia kurudi British Columbia nzuri ili, kwa mara nyingine tena, tushike uchungaji wa kanisa pamoja na Christian & Missionary Alliance. Walikuwa wamenipa heshima kubwa kwa kuendelea kunihifadhi katika usajili wao, ingawa sikuwa tena rasmi katika kazi ya dhehebu lile. Nilipewa cheo cha huduma maalum, kwa kuwa Msimamizi wa Wilaya alitambua thamani ya kazi iliyofanywa na wafanyakazi wa Anastasis katika uwanja wa umisionari wa Afrika Magharibi, eneo ambalo C&MA walikuwa na nafasi maarufu.
Lakini kwanza, tungetumia fursa kumtembelea binti yetu Lynette na familia yake huko Australia. Tuliwezeshwa kufanya hivi kupitia ukarimu wa daktari aliyekuwa akitembelea Anastasis. Jioni moja, tukiwa tunapiga soga, nilitaja kwamba nilikuwa na wajukuu watatu Australia ambao sikuwahi kuwaona. Alasiri ile, alikwenda chumbani kwetu melini na kumwambia Anne, “Wakati wowote mnapotaka kwenda Australia, tiketi zenu zimelipiwa!” Hii ingekuwa safari ya mara moja tu maishani, hivyo tulipanga ziara ya miezi sita.
Fikiria furaha yetu ya ziada Anne alipoarifiwa, karibu kwa kuomba radhi, na wakala wa safari wa Kiingereza kwamba njia ya bei nafuu zaidi ilikuwa kusafiri kupitia Kanada tukisimama Vancouver. “Ndiyo, tungeweza kushuka njiani kama tungependa.” Hivyo ndivyo ulivyokuwa mwezi mmoja uliotumika Victoria, tukiona familia za binti zetu wengine na marafiki, kabla ya kuendelea na safari yetu hadi kwa Lynette na familia yake Canberra.
Mwezi wa kwanza ungekuwa mgumu sana kwangu, nikizoea maisha ya ukosefu wa shughuli na kutokuwa na uhakika juu ya siku zijazo. Kisha nilikwenda kufundisha shule ya kiangazi ya Capernwray Bible School huko Moss Vale, karibu na Sydney. Hili lilikuwa juma la kwanza la Januari 1995, wanafunzi wakija kwa juma moja kutoka kote mashariki mwa Australia.
Mwaliko wangu wa kuzungumza katika shule hii ulikuja kama mshangao mkubwa nao unastahili kusimuliwa. Miaka miwili kabla, nikiwa Afrika, nilikuwa nimepokea barua kutoka kwa wanandoa vijana waliokuwa wamehudhuria Capernwray huko Australia kwa shule ya miezi 6. Waliniambia kwamba mkuu wa shule alikuwa amesema kwamba kama ningewahi kuja Australia, ningekaribishwa kufundisha shuleni hapo (nilisoma hili kama maneno ya kawaida ya kiongozi anayejibu ombi la mwanafunzi la ‘tafadhali mwalike mchungaji wangu aje kufundisha shuleni’ – akijua kwamba ni wachache wao ambao wangewahi kufika ‘kule chini’).
Tulipojua kwamba tulikuwa tunakwenda Australia Oktoba 1995 – Machi 1996, nilimwandikia mkuu wa shule nikimweleza juu ya ziara yetu na kujiuliza kama kungekuwa na nafasi ya kufundisha shuleni kwa juma moja hivi.
Jibu lake lilikuwa zaidi ya nilivyotarajia aliponialika kufundisha katika ‘shule hii ya kiangazi’ ya majuma mawili ambayo watu kutoka kote pwani ya mashariki mwa Australia wangekuja. Nilialikwa kutoa mihadhara kumi ya saa moja kila mmoja juu ya mada ya kuchagua kwangu.
Kama sabini kati yetu tulikusanyika Wongabri, makao mazuri ya Capernwray, usiku wa Mkesha wa Mwaka Mpya 1995. Peter McDonough, mkuu wa shule, alitukaribisha kisha akamwalika kila mmoja asimame na kujitambulisha. Wengi walikuwa wamekuja umbali mrefu kuhudhuria juma hili, kutoka Adelaide, Melbourne na Brisbane, mbali na wale wa karibu zaidi. Mimi nilikuwa wa mwisho kusimama nikaanza kujitambulisha kwa kusema, “Peter McDonough, wewe ni ama mtu shujaa sana, mtu mpumbavu sana au mtu wa kiroho sana!” Nikaendelea kusimulia jinsi alivyonialika kuwa mzungumzaji wao, bila kuniona wala kunisikia.
“Ninaweza kuwa mzungumzaji anayechosha kuliko wote uliyewahi kumsikia, nanyi mmelipa fedha nzuri kusafiri hadi hapa na kuhudhuria shule hii.” Yatosha kusema kwamba juma lile lilikwenda vizuri sana, nami nilikuwa nikitambua daima uongozi wa Bwana huku mafundisho yangu kutoka Kitabu cha Waefeso yakipatana vizuri kiasi hicho na mihadhara mingine iliyotolewa na Peter na mmoja wa wenzake. (Kiini cha mafundisho yangu kikawa ndicho chanzo cha kitabu cha kwanza nilichokiandika, “The Key in My Hand”) Tulipokusanyika ili kuagana, Peter alisimulia jinsi alivyokuja kunialika niwe mwalimu wao. Alikuwa ameingia ofisini kwake siku moja akiwa na orodha ya majina ambayo alipaswa kuyaombea ili aone ni nani ambaye angemwalika. Alimwomba katibu wake asimsumbue kwa kuwa angetumia asubuhi ile yote katika maombi.
Alishangaa kusikia kwamba barua moja tu ilikuwa imefika siku ile badala ya nyingi za kawaida, hivyo akaamua angeisoma kabla ya kuanza maombi yake. Ilikuwa kutoka kwa mgeni asiyejulikana huko Afrika akisema kwamba angeona ni heshima kufundisha katika shule ile (ya kawaida) kama kungekuwa na nafasi. Peter alishangazwa na ukweli kwamba barua moja tu ilikuwa imefika siku ile naye akaanza kujiuliza kama hii ilikuwa kuingilia kati kwa Bwana. Hakuwa na amani juu ya nani wa kumwalika alipokwenda nyumbani kwa chakula cha mchana pamoja na mkewe, Pam. Waliomba pamoja na wakahisi kwamba Bwana kwa kweli alikuwa amewaongoza kwa barua hii peke yake – “hivyo nilimwalika Gareth kwa hofu nyingi.”
Kutokana na juma lile, nilipokea mialiko ya kuzungumza katika makanisa mengi. Mwezi Februari, mimi na Anne tuliendesha gari hadi Melbourne ambako tulihudhuria kongamano la mwaka la C&MA nchini Australia. Mialiko mingi zaidi ilifuata hata kwamba, punde tukajikuta kila wikendi imejaa nafasi za kuzungumza. Kulikuwa na makongamano mawili ya wikendi huko Adelaide, yaliyotenganishwa na siku kumi huko Perth, magharibi mwa Australia. Kisha ziara ya Brisbane ambako tulipata fursa ya kukaa na dada yangu na familia yake.
Kabla ya kuondoka Australia, nilitembelewa na Rais wa Kiaustralia wa C&MA aliyenialika kurudi miaka miwili baadaye kuendesha mafungo kwa ajili ya wachungaji wake, wazee na wake zao huko Melbourne.
“Hili ndilo unalopaswa kuwa unalifanya.” alisema Anne. “Moyo wako hauko katika siasa za kanisa la mtaani, bali katika kuwa pamoja na wachungaji na wamisionari ili kuwatia moyo na kuwahudumia. Chukua muda kuona kama hapa ndipo Bwana atakapokuongoza baadaye.
Tunaweza kuishi kwa mapato ya wanafunzi walio nyumbani kwetu nawe waweza kusafiri kufundisha.” Yatosha kusema kwamba, katika miaka hii iliyofuata, tumeshangazwa tulipoona uongozi wa Bwana katika kunifungulia milango ya kusafiri na kuhudumu katika nchi nyingi kiasi hicho, ambazo hakuna hata moja niliyowahi kuitafuta kwa barua au kwa simu. Ametoa kila senti niliyoihitaji kwa safari, bila kuomba wala kumjulisha mtu yeyote juu ya uhitaji huo. Nimesafiri kwenda Mexico, Peru na Brazil, India na Nepal, Australia na New Zealand, Uholanzi na Uingereza.
Kila mara ninapopanda ndege huwa naeleza mshangao wangu kwa Bwana kwa sala kwamba anilinde nisiwe na mtazamo wa kitalii wala kiburi, na kwamba aniongoze kwa yule mtumishi anayeumia ambaye yeye anataka niseme naye.