Sura 21 · dakika 6 za kusoma
M/V Anastasis
Tulikaa miaka minane katika Victoria Alliance Church — miaka mizuri ambamo tulipata rafiki wengi wema na kuona mkono wa Bwana ukitenda kazi katika maisha kadhaa. Nikawa mwenye bidii katika baraza la wachungaji na, mwaka mmoja baadaye, nikateuliwa kuwa katibu wa kundi hilo. Kila mwezi tungekutana kwa chakula cha mchana na kutiana moyo. Ilikuwa masika ya 1985 ndipo nilipopokea simu kutoka San Pedro, California.
Yule aliyepiga simu akaniuliza kama nilikuwa nimesikia habari za meli iitwayo M/V Anastasis. Nikasema sikuwa nimesikia, hivyo akaendelea kunieleza juu ya meli hii kubwa ya bahari kuu iliyokuwa imenunuliwa na Youth With A Mission. Ndoto yao ilikuwa kusafiri hadi sehemu zenye uhitaji duniani ikiwa imebeba wafanyakazi wa afya na wa ujenzi pamoja na timu za uinjilisti. Ilihitajika kufanya kazi kubwa juu ya chombo hicho kabla hakijakidhi matakwa ya usalama ya walinzi wa pwani wa Marekani, hivyo walikuwa wakikileta katika gudi kavu za Victoria. “Mhandisi wetu mkuu, John Brignall, atakuwa Victoria siku ya Jumanne,” akasema yule aliyepiga simu. “Je, waweza kutusaidia kwa kupanga mtu wa kumchukua uwanja wa ndege na kumpeleka kwenye gudi?” Nikasema ningefurahi kufanya hivyo mimi mwenyewe, hivyo, siku ya Jumanne ya wiki iliyofuata, nikaanza urafiki wangu mrefu na John Brignall na Anastasis.
Meli ilipofika hatimaye Victoria mwezi Septemba wa 1985, mimi ndiye niliyekuwa wa kwanza kupanda. John akanitambulisha upesi kwa familia yake, rafiki kadhaa na hatimaye, Don Stephens, mwanzilishi na Rais wa Mercy Ships. Don alikuwa mkarimu sana katika kunikaribisha melini kisha akaanza kunieleza ndoto zake kwa muda ambao Anastasis ingekuwa Victoria, muda aliotarajia kuwa miezi mitatu au minne.
“Tutahitaji nafasi ya ofisi yenye simu,” akasema, “na ukumbi wa mazoezi ambapo timu zetu za maigizo zinaweza kufanyia mazoezi.” “Mnavyo,” nikasema, “Kanisa letu liko wazi kwenu.” Alipouliza kama kulikuwa na orodha ya namba za simu za wachungaji wa eneo lile, nikamweleza juu ya wadhifa wangu kama katibu wa baraza la wachungaji, nikiwa na ofisini kwangu yote aliyoyahitaji. Bila shaka alifurahi sana! Makanisa yakawakaribisha Don na wafanyakazi wake kwa uchangamfu, urafiki wetu ukakua, nami nikajulikana kama ‘mwana wa amani’ wao (Luka 10:6). Wafanyakazi wote walijihusisha na makanisa ya eneo lile, bila kuruka-ruka wakitafuta wanalolipenda zaidi, bali wakibaki wakfu kwa kusanyiko moja. Kanisa letu wenyewe likabarikiwa sana kwa kuwa na familia ya Brignall na wengine kama kumi wakihudhuria mara kwa mara. Muda ulipojinyoosha kutoka miezi michache iliyotarajiwa hadi miezi kumi na minne kamili, wafanyakazi wakaanza kuhisi kwamba Victoria ilikuwa nyumbani kwao — nasi sote tukahisi vivyo hivyo.
Mnamo Novemba 1986, Anastasis iliyokuwa imepewa leseni mpya na kusajiliwa na Lloyds ilisafiri kutoka Victoria kuanza huduma yake. Ilikuwa siku ya baridi kali, lakini mioyo yetu ilikuwa na joto tulipoimba maagano yetu ya kwaheri. Mimi na Anne tulikuwa tumealikwa kusafiri na meli hadi bandari yake ya kwanza.
Hii ilikuwa ziara ya heshima hadi Olympia, mji mkuu wa jimbo jirani la Washington, Marekani. Wiki moja baadaye, ikawa zamu yetu kuwakumbatia na kuwabusu rafiki wengi tuliokuwa tumewapata, walipong’oa nanga kuelekea kusini hadi Mexico na kwa wenye uhitaji wa taifa lile. Hatukufikiri kwamba M/V Anastasis ingekuja kuwa sehemu kubwa ya wakati ujao ambao Bwana alikuwa akituandalia. Kabla ya hilo kutokea, yalikuwapo mawe kadhaa zaidi ya kukanyagia ambayo ilimbidi ayaweke mbele yetu. Bila hayo, tusingeweza kuufuata uongozi wake alipotuita baadaye.
Tulipofika Canada mwaka 1975, ilikuwa kama ‘wahamiaji waliopokelewa’ tukiwa na haki karibu sawa na raia yeyote wa nchi ile. Tuliweza kupiga kura lakini hatukuweza kugombea ubunge. Tulifurahia kuwa katika nchi hii nzuri nasi tulijivunia kuitwa ‘Wakanada.’ (Wakanada Wawelisi!!) Hata hivyo, mojawapo ya matatizo ya kuwa mhamiaji aliyepokelewa ni kwamba waweza kuwa nje ya nchi kwa wakati mmoja, kwa muda usiozidi miezi sita. Ukiwa nje kwa muda mrefu kuliko huo, ni lazima uombe tena hadhi ya uhamiaji — nalo si jambo la hakika.
Nilipoingia Canada mara ya kwanza, nilikuwa na kazi ya uhakika ya kwenda na mdhamini katika Toronto French School. Ungefika wakati ambapo nisingekuwa na kipato wala uhakika wowote wa kuionyesha ofisi ya uhamiaji. Wakati wa namna hiyo, ingekuwa vigumu sana kuingia tena Canada hata ingawa nilimiliki nyumba Victoria na binti zetu waliishi huko.
Bila shaka, sikuwa nikifikiri juu ya hili mwaka 1989 wakati binti yetu mdogo, Lynette, alipokuwa akipanga harusi yake na Phillip, Mwaustralia, akikusudia kuondoka Canada aende kuishi ‘kule chini.’ Alitaka kuwa raia wa Canada kabla ya harusi yake ili, kama angewahi kutaka kurudi Canada, angeweza kufanya hivyo. Mimi na Anne hatukulifikiria sana lakini tukaamua kwamba ingekuwa vyema sisi pia tufanye hivyo. Hatukuona wakati wowote ambapo tungehitaji kuutumia uraia wetu, wala hatukuona sababu ya kutokuwa raia. Tumebadili mawazo yetu tangu wakati ule na tunatambua jinsi ambavyo, hata katika hili, Bwana alikuwa akituandaa. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwamba mwezi Juni 1989 mimi na Anne tulipokelewa kuwa raia wa Canada.
Jiwe la pili la kukanyagia lilihusu nyumba yetu. Mwaka 1986, tulimiliki nyumba nzuri viungani mwa Victoria, lakini ilikuwa na kasoro mbili kubwa. Nikiwa mchungaji, mara nyingi niliwapokea watu nyumbani kwetu kwa ajili ya ushauri, jambo lililohitaji kiasi fulani cha usiri. Hili lilikuwa gumu kwa kuwa nyumba yetu ilikuwa ya ‘wazi’ yenye milango michache ya kugawa sehemu za kuishi.
Pili, kulikuwa na nyasi tatu zilizohitaji kutunzwa mara kwa mara nami si mtu apendaye kazi ya bustani. Daktari wangu alipogundua kwamba nilikuwa na tatizo dogo la moyo, tulijua ulikuwa wakati wa kuhamia nyumba nyingine, ifaayo zaidi mtindo wetu wa maisha. Tukatangaza nyumba yetu iuzwe nasi tukastaajabu tulipopata mnunuzi ndani ya wiki moja. Yule mama angelipa kile tulichotaka kwa fedha taslimu, kwa sharti moja — kwamba tuiache nyumba kufikia mwisho wa mwezi, wiki tatu tu baadaye.
Kwa kweli, hilo lilimaanisha siku kumi tu kwetu kwa kuwa tulikuwa tuondoke kwenda likizo wakati ule, tukiwa tumepanga kumtembelea dada yangu Australia na, kutoka huko, kwenda Kuala Lumpur kuwatembelea Vincent Cheah, mkewe Shirley na wanafunzi wengine waliokuwa sehemu ya huduma yetu ya uchungaji wa Wamalaysia tulipokuwa Kitchener. Tukakubaliana masharti na kuanza kufunga mizigo. Samani zetu ziliwekwa katika nyumba za washiriki wa kanisa hali masanduku yote madogo yakahifadhiwa katika ofisi za kanisani. Tulitarajia kuhamia nyumba ya kupanga tutakaporudi, jambo ambalo lingelitupa muda wa kutafuta nyumba nyingine. Hata hivyo, haikuwa hivyo, kwani Lynette alikuwa ameiona ‘nyumba kamilifu’ katika safari zake za kwenda na kurudi kazini.
Hatukushangaa kuikuta ikiwa nje ya uwezo wetu wa bei ikiwa na thamani ya dola 50,000 zaidi ya nyumba tuliyoiuza, lakini tulishangaa sana wakala wetu wa nyumba alipoeleza kwamba ingewezekana kupata mkopo wa nyumba wenye malipo yanayofanana na yale tuliyokuwa tukiyalipa tayari. Zaidi ya hayo, nyumba ile ilikuwa na fleti ya ghorofa ya chini, ambayo kodi yake ingepunguza sehemu ya mkopo. Kisha muuzaji akashusha bei yake, nasi tukanaswa. Mkopo mpya ulikuwa wa aina ya ‘kufikia thamani,’ maana yake tungeweza kulilipa deni lote wakati wowote bila adhabu. Pia, tungeweza kutoa fedha kutoka humo wakati wowote tungehitaji fedha za ziada — hata nilipokuwa sipati kipato chochote!
Tukaondoka kwenda likizo, tukimpa binti yetu mdogo, Lynette, ‘mamlaka ya uwakili’ ya kuinunua nyumba, hali sisi tukiota jua katika fukwe za Malaysia. Tuliporudi wiki tano baadaye kwa kivuko cha mwisho kutoka Vancouver, tulishindwa na hisia kukuta kwamba rafiki zetu wa kanisani walikuwa wamehamishia samani zetu zote katika nyumba mpya, hata wakitandika vitanda na kuweka vyombo vya mezani katika makabati! Nyumba ile imekuwa baraka kubwa kwetu tangu tuinunue. Tulipokuwa mbali baada ya 1991 — hadithi ambayo bado itakuja — tuliipangisha kwa wanafunzi wa chuo kikuu ambao, si kwamba tu waliitunza katika hali njema bali pia walilipa deni letu lote la nyumba — jambo ambalo sikuwahi kulitarajia tulipoinunua nyumba mara ya kwanza. Sasa imekuwa njia pekee ya kipato kwetu tunapowahifadhi wanafunzi kutoka vyuo vya Victoria nayo imezidisha thamani yake maradufu katika miaka minane iliyopita. Tuna hakika kwamba Bwana alituongoza, katika kupata uraia wetu na katika kununua nyumba hii. Bila mojawapo ya hayo, tusingeweza kamwe kufanya yaliyofanyika — nasi twamshukuru.