Sura 20 · dakika 4 za kusoma
Sidney, B.C.
Siku mbili kabla ya kuondoka Kitchener, nilikuwa nimeketi nikifurahia kinywaji baridi pamoja na Uli, katika kituo cha YWAM cha Cambridge. Tulikuwa tukizungumza juu ya mambo mengi mema ambayo Bwana alikuwa akiyafanya katika maisha yetu sote wawili. Tulipoanza kuzungumzia mipango ya baadaye, nikasema, “Uli, kama utawahi kuhitaji mtu wa kuwasiliana naye kwa ajili ya YWAM upande wa pwani ya magharibi, usisite kunipigia simu.” Sikutambua jinsi mwaliko huo rahisi ungeyaathiri maisha yetu ya baadaye. Husemwa kwamba ili uwe Mkanada halisi lazima ufanye mambo mawili; lazima ujenge nyumba yako mwenyewe na lazima usafiri kuivuka nchi nzima. Sikuwa nimejenga nyumba yangu mwenyewe lakini nilikuwa nimeona kanisa likijengwa. Nadhani lazima niligusa kila tofali la saruji na kila kipande cha mbao katika jengo lile, wakati mmoja au mwingine! Sasa ulikuwa wakati wa kuendesha gari kuvuka sehemu kubwa ya Canada.
Lori kubwa la kukodi lilijazwa mali zetu zote, gari letu likafungwa kwa kamba ya kuvuta, nasi tukaanza safari ndefu. Tukiendesha zaidi ya maili mia tano kila siku, tulifika Sidney katika kisiwa cha Vancouver Island, siku sita baadaye. Tulikaribishwa kwa uchangamfu na kusanyiko lile dogo na punde tukatulia katika kazi mpya. Sidney Alliance Church lilikuwa tawi la kanisa la Victoria, mji mkuu wa ‘British Columbia nzuri.’ Kusanyiko lilikuwa na ujali mkubwa, likitamani kwenda katika upya wa kile ambacho Roho Mtakatifu alikuwa akikifanya eneo lile. Walikuwa wamepiga ‘hatua ya imani’ kwa kumwalika mchungaji wa mshahara awasimamie, lakini punde ikawa dhahiri kwamba msingi wa kifedha wa kanisa ungehitaji kupanuliwa kama wangeweza kutimiza ahadi zao. Sote tulifanya kazi na kuomba kuelekea lengo hilo lakini, baada ya miezi mitatu niliweza kuona kwamba punde tungeingia katika hali ya upungufu. Nikafikiria kuomba kazi ya kufundisha ya muda ili mshahara wangu, ingawa mdogo, usiwe mzigo kwa kanisa. Ilikuwa jioni ya Jumapili yenye manyunyu, nami nilikuwa na maumivu kidogo ya kichwa. Anne akawachukua binti kwenda kanisa lingine kwa kuwa hatukuwa na ibada yetu wenyewe ya jioni. Nikatoka kutembea ili kutumia muda zaidi katika maombi kuhusu hali yetu kanisani. Baada ya dakika ishirini, nilikuwa nimefika kilele cha Bear Hill, mahali pa kupendwa pa kutazamia. Hakukuwa na mtu mwingine karibu wa kusikia nilipomlilia Bwana anipe uongozi wake.
Mimi huwa na mashaka watu wanaposema, “Bwana aliniambia…” Siku zote nataka kuwauliza ni jinsi gani hasa alisema nao. Inakera hasa wanapokujia kutafuta ushauri kisha wakaanza kwa kusema “Bwana aliniambia…” Nitathubutuje kutoa ushauri unaoweza kuwa kinyume na kile Bwana alichokisema? Bila shaka, ninaamini kwamba Bwana husema nasi. Kondoo wanapaswa kuijua sauti yake. Hata hivyo, ushahidi mwingi wa sauti ya Mungu ambao watu wameuitikia unanitia wasiwasi mkubwa — na nyakati fulani unakuwa kinyume kabisa na Maandiko. Yeye husema kwa njia nyingi tofauti. Bear Hill ulikuwa mmoja wa nyakati adimu nilipomsikia akisema kwa sauti iliyo wazi, isikikayo!
“Usiogope! Mimi nimekuleta hapa nami nitaendelea kutimiza mapenzi yangu ndani yako. Utakaa katika kanisa la Sidney hadi nitakapokuita uendelee. Kisha utalichunga kanisa la Victoria Alliance.” Nilistaajabu! Sauti ilikuwa wazi sana wala hakukuwa na shaka juu ya kile kilichonenwa. Hata hivyo, matumaini ya karibu ya jambo hilo kutokea yalikuwa madogo mno. Kulikuwa na wachungaji watatu wakati ule katika kanisa mama la Victoria, na yule mkuu alikuwa amekaa pale mwaka mmoja tu. Zaidi ya hayo, hili lilikuwa kanisa la mji mkuu nami nilikuwa nimewekwa wakfu punde tu wala sikuwahi kuhudhuria seminari. Ni dhahiri kwamba ingepita miaka mingi kabla ya mimi kukubalika kuwa mchungaji wa kanisa lile. Hata hivyo, sauti ilikuwa wazi kabisa hivyo nikashuka kutoka kilele kile nikiwa na furaha ya kuwa nimeisikia sauti ya Mungu, na amani ya kujua kwamba nilipaswa kubaki Sidney Alliance Church huku yeye akitupatia mahitaji yetu.
Sikumwambia mtu yeyote isipokuwa Anne yaliyotokea jioni ile juu ya Bear Hill, lakini sikushangaa sana mwezi mmoja baadaye, habari zilipoenea mjini kwamba mchungaji wa Victoria Church alikuwa ametangaza ghafla kujiuzulu kwake. Wachungaji wasaidizi wake pia walikuwa wamejiuzulu nyadhifa zao na Msimamizi wa Wilaya akaitwa ili kusaidia baraza la wazee kutafuta mchungaji mwingine. Sifahamu yote yaliyotokea katika miezi iliyofuata lakini nilipambana na kishawishi cha kupaza sauti wote wasikie kwamba mimi ndiye mtu waliyekuwa wakimtafuta! Badala yake, mimi na Anne tukajitenga na kanisa lile la katikati ya mji ili tusije tukajaribiwa kuyageuza mambo hata wazee wakajihisi kulazimika kunialika niwe mchungaji wao.
Miezi minne ikapita kabla sijapokea simu kutoka kwa Msimamizi wetu wa Wilaya. “Gareth, Victoria Alliance Church wameniomba nikualike uwe mchungaji wao. Je, ungependa nafasi hiyo?” Alishangazwa na haraka ya jibu langu na hata zaidi nilipomwambia kwamba nilijua juu ya jambo hili, miezi kadhaa mapema. Nilikuwa nimemsikia Bwana akisema lakini sikuwa nimetenda lolote kujaribu kulifanya litokee. Anenapo, yeye ana uwezo kamili wa kuyatimiza maneno yake!
Mnamo Septemba 1984, niliwekwa kuwa mchungaji katika Victoria Alliance Church, mwaka mmoja tu baada ya kuja katika kanisa lao binti huko Sidney. Ni lazima kuongeza hapa sifa ya dhati kwa watu wa Sidney waliokuja kuwa wategemezi wetu wakubwa kuliko wote katika miaka ile. Masikitiko yao yalishindwa na upendo wao kwetu na kujua kwamba Bwana alikuwa katika hatua hii. Bado ni miongoni mwa rafiki zetu wa karibu zaidi na wategemezi wetu hata baada ya miaka hii mingi.