Sura 17 · dakika 4 za kusoma

Neno Langu Halitanirudia Bure

Katika wiki nne zilizofuata, nilifundisha madarasa sita zaidi pamoja na wanafunzi wa darasa la 13. Hakukuwa na kizuizi chochote dhidi ya kuzungumza kwangu juu ya Bwana na juu ya imani yangu. Siwezi kutoa taarifa kwamba yeyote kati ya wanafunzi alifikia imani ya wokovu ndani yake, lakini nikiamini kwamba Mungu hazipandi mbegu zake bure kamwe, nina hakika alikuwa na kusudi la milele katika kuniruhusu pendeleo la namna hiyo — na katika kulipanga miaka mingi hivyo kabla.

Nina imani kwamba Bwana atarudi tena hivi karibuni kulingana na ahadi yake aliyowapa mitume. Wakati huo kutakuwa na dhiki kuu na huzuni juu ya dunia; hata hivyo, Mungu ameagiza kwamba Wayahudi 144,000 watalindwa katika kipindi hicho, wakiwa mashahidi wake, wenye jukumu la kutangaza utukufu wake ulimwenguni kote. Kutokana na ushuhuda wao, wengi wataamini, hata hadi kufa: watakatifu wa dhiki (Ufunuo 7 na 14). Naamini baadhi ya wanafunzi wale wanaweza kabisa kuwa miongoni mwa wale 144,000, na kama sivyo, watakuwa miongoni mwa wale watakaomkiri Mwokozi wakati huo. Naomba kwamba Rabbi S. atakuwa miongoni mwao.

Muhula wa masika ulimalizika na wikendi ya Canada Day. Ilikuwa desturi kwamba katika wikendi hii ndefu, wanafunzi wote walikwenda kwenye ‘safari za mafunzo.’ Baadhi ya wanafunzi wa darasa la 11 wakanijia na kuniuliza kama ningekwenda nao hadi Quebec City.

Nikasema kwamba ningefurahi kufanya hivyo lakini nilitilia shaka kama ningeruhusiwa kwenda kwa kuwa sikuwa nikijua barabara kuhusu Kashrut (sheria za Kiyahudi zinazohusu desturi, ulaji, na maombi). Bwana Diamond aliporudia mwaliko ule asubuhi iliyofuata, nikamweleza hofu zile zile. Ningefurahia kuiongoza safari lakini nikijua jinsi wanafunzi wote wapendavyo kuwatumia vibaya walimu wasiojua, nisingeweza kukubali jukumu la kusimamia utekelezaji wa taratibu mahususi za Kiyahudi. Akanihakikishia kwamba mwalimu mwingine Myahudi naye angekwenda ili kuniondolea wasiwasi huo, hivyo nikaukubali mwaliko nami nikafurahi Ari Barchi alipouliza baadaye kama angeweza kuwa mwenzangu.

Tuliondoka Toronto punde tu baada ya kuzama kwa jua jioni ya Jumamosi (baada ya Sabato) tukasafiri usiku kucha kuvuka Ontario hadi kuingia Quebec. Mimi na Ari tuliketi nyuma ya dereva kabisa. Shauku ya awali ya wanafunzi wetu 40 ilipofifia taratibu hadi kimya cha usingizi, tulizungumza juu ya imani zetu tofauti. Huko Montreal, tulisimama kuchukua chakula cha kosher kwa ajili ya siku iliyofuata na hatimaye tukawasili katika mji mzuri wa Quebec City asubuhi na mapema ya Jumapili. Nilikuwa nimechoka sana tulipokula na kuketi katika bustani kabla ya kupelekwa hadi Chateau de Frontenac Hotel.

Kijana mmoja akanijia akauliza, “Je, ninyi ndilo kundi kutoka Toronto? Mimi nitakuwa kiongozi wenu wa ziara kwa siku hizi chache zijazo.”

Nikamkaribisha na kumpa sandwichi nikisema, “Ni sandwichi za kosher — tamu sana. Pengine unajua kwamba tunatoka shule ya Kiyahudi,” kisha nikaongeza, bila kufikiri, “Lakini mimi mwenyewe si Myahudi. Mimi ni Mkristo aliyezaliwa mara ya pili.” Waweza kuwazia furaha yangu alipojibu kwa shauku kwamba naye pia alikuwa mwamini.

Nikamgeukia Ari nikamwambia, “Unaona jinsi Bwana alivyo mwema. Anajua jinsi nilivyochoka na jinsi ulivyo na maswali mengi, hivyo amemtuma mtu mwingine ili akujibu wewe!”

Tulikuwa na wikendi ya ajabu pamoja. Jean Mark Deneau, kiongozi wetu, alijidhihirisha kuwa mwenzi wa kupendeza naye alipendwa na wote. Alipata wakati wa pekee pamoja na wanafunzi tulipoingia Notre Dame Cathedral. Wanafunzi walikuwa kimya, lakini walishtushwa na sanamu zilizokuwa katika vituo vya msalaba, hivyo akawaalika waketi katika viti vya mbele huku yeye — akiwa na Biblia wazi — akiwapitisha katika Mateso ya Yesu.

Ilikuwa imepita saa sita za usiku kwa mbali asubuhi ya Jumanne tuliporudi viungani mwa Toronto. Tulikuwa tunakwenda kupita karibu na nyumba yangu, jambo ambalo lingeniokolea safari ya kutoka shuleni kwenda nyumbani, lakini nikaamua kubaki na Ari na wanafunzi endapo jambo lisilopangwa lingetokea. Punde tukawa tumerudi shuleni ambapo mizigo yote ilihifadhiwa, wanafunzi wakachukuliwa, nami nikaachwa peke yangu na basi pamoja na dereva wake. Nilikuwa na safari ya saa nyingine moja kabla sijaweza kufika kitandani kwangu, na hakika sikuwa nikitazamia kwa hamu mabasi mawili na treni mbili za chini kwa chini ambazo ningezihitaji.

“Unakwenda upande wangu?” akauliza Al, dereva wetu. Alikuwa alipeleke basi katikati ya mji, jambo ambalo lingeniokolea nusu ya safari yangu. Tulipokuwa tukisafiri pamoja, akaongeza nyongeza ya ajabu kwenye wikendi yetu.

“Nimekuwa nikiwasikiliza wewe na Ari,” akasema. “Je, ulijua kwamba mimi ni nusu Myahudi na nusu Mkatoliki? Nimekuwa nikiitafuta kweli kwa wiki chache zilizopita, nikitazama vipindi vya televisheni vya Kikristo, na kujiuliza kama wanachokisema ni kweli. Je, ni kweli hasa kwamba naweza kujua dhambi zangu zimesamehewa na kwamba Yesu aweza kuwa Mwokozi wangu binafsi?”

Sikuweza kuyaamini masikio yangu ingawa kufikia sasa ningepaswa kuwa nimezizoea njia za Bwana. Katika dakika kumi zilizofuata, nikamtia moyo aitegemee kazi ya Kalvari, na nilipomwacha, akanihakikishia kwamba sasa alikuwa akianza mwenendo mpya wa imani pamoja na Mwokozi.

Nilipoketi katika treni ya chini kwa chini, nikamsifu Bwana wetu kwa wema wake nami nikafurahi mno kwamba nilikuwa nimeutii msukumo wake wa kutoshuka basini mapema mno.

Ukurasa 1 / 3 · 4 dakika zimebaki katika sura