Sura 16 · dakika 5 za kusoma

Kumbe Hiyo Ndiyo Maana Yake!

Asubuhi iliyofuata sisi watatu tukaingia darasani. Chumba kilikuwa kikivuma kwa shauku huku Ari akiketi kitini kwake kwenye kona na Rabbi S. akaanza kusema kwa Kiebrania. Nikatazama chumba kizima nikatambua kwamba hawa hawakuwa wanafunzi wale wale wa awali. Kulikuwa na wanafunzi 50 katika darasa la 13, na hawa walikuwa ‘nusu ile nyingine’ ya kundi hilo. Rabbi akaongea nao kwa dakika chache kwa Kiebrania kisha akanigeukia na kunialika nizungumze. Akaketi kiti mbele yangu kabisa… ndani ya ‘umbali wa kutemewa mate’ endapo ningetatiza maneno!

“Kwa kuwa ninyi ni kundi tofauti na wale niliozungumza nao mara iliyopita, hebu niwaambie kile nilichowaambia wao,” nikaanza. Mwanafunzi mmoja akanikatiza.

“Tafadhali mwalimu, sisi sote tumekwisha sikia Mkristo si nini, jinsi ulivyokuwa Mkristo, na jinsi ulivyokuwa Myahudi. Ndicho tulichokuwa tukikizungumza siku hizi mbili zilizopita. Tafadhali, je, utaturuhusu tukuulize maswali?”

Wanafunzi hawa walikuwa na shauku sawa na wale wa darasa lile lingine — ingawa walikuwa wamejiandaa vizuri zaidi. Maswali machache yalikusudiwa kunitega, lakini mengi yalionyesha hamu ya kweli. Msichana mmoja akauliza ingewezekanaje mimi, mwanasayansi, kuamini kuzaliwa kwa mtoto na bikira. Nilipotaja katika kujibu kwangu kwamba mmoja wa manabii wao alikuwa ametabiri tukio la namna hiyo, akadai kujua ni wapi. Ni Rabbi ndiye aliyemgeukia na kumshauri asome Isaya 7.

Kisha Rabbi S. akasema, “Je, naweza kukuuliza swali?”

Nikahisi nywele zikisimama nyuma ya shingo yangu. Huu ndio wakati wenyewe! Huu ndio ungekuwa ufunuo mkubwa! Kila mwanafunzi chumbani akajiinamisha mbele ili alinase kila neno lililokuwa likaribia kunenwa huku ‘shujaa’ wao akimwonyesha yule Mtu wa Mataifa jinsi alivyokuwa mpumbavu kuamini hadithi ile ya Kikristo. Mtu angeweza kuwa na hakika kwamba kila neno lingerudiwa juu ya meza 25 za chakula cha jioni usiku ule.

“Bwana Evans,” akaanza, “nimelisoma Agano lenu Jipya mara nyingi. Nami, pamoja na Wayahudi wengine wengi, ninaamini kwamba mtu mkuu kuliko wote aliyewahi kutembea juu ya dunia hii alikuwa Yesu wa Nazareti. Ninajivunia kwamba alikuwa Myahudi. Yeye na wafuasi wake walikuwa watu wenye haki, wakiwaita watu kwenye utakatifu na mafundisho sahihi. Walikuwa waaminifu katika ibada yao nao waliadhimisha sikukuu zote na siku takatifu. Kwa kweli, Biblia yenu inaniambia kwamba ‘aliitimiliza Sheria katika matakwa yake yote’ (Mathayo 5:17). Nisichokielewa ni hiki: ikiwa unadai kuwa mfuasi wake, kwa nini nawe usiwe Myahudi?”

Nilistaajabishwa na ungamo lake mbele ya wanafunzi hawa, nilipoanza jibu langu.

“Nami pia nimeyasoma maandiko yenu, yaani Agano letu la Kale, nikaona jinsi Mungu alivyomwambia Musa kwamba kwa kila namna ya unajisi kati ya watu, kulikuwa na dawa moja — kutoa dhabihu ya damu. Ingeweza kuwa damu ya mbuzi au ya mwana-kondoo au ya ndege lakini, katika hali zote, damu ilihitajika. Nilisoma pia kwamba, mara moja kwa mwaka katika siku ya Upatanisho, Yom Kippur, mwana-kondoo dume, wa mwaka mmoja na asiye na waa lolote, alipaswa kuchukuliwa na kuchinjwa.

Damu yake ilipaswa kuchukuliwa na Kuhani Mkuu hadi Patakatifu pa Patakatifu pa hekalu na huko kunyunyizwa juu ya Kiti cha Rehema mahali Mungu alipokaa.”

Rabbi akatikisa kichwa.

Nikaendelea, “Siku hiyo, hakuna mtu aliyefanya kazi katika Israel yote walipokuwa wakingoja, huku wakizuia pumzi zao, kuona kama Mungu angeikubali sadaka hii kuwa kifuniko cha dhambi zao kwa mwaka mwingine. Kila mtu alishangilia Kuhani Mkuu aliporudi kutoka mbele za Mungu. Dhabihu ilikubaliwa! Dhambi zao zilifunikwa kwa mwaka mwingine! Kwa hiyo, ingeweza kusemwa kwa kweli kwamba ‘pasipo kumwaga damu hakukuwa na kifuniko cha dhambi.’”

Tena, Rabbi akatikisa kichwa akasema, “Marabi wetu wa kale wote wawili, Hillel na Shimei, walikubaliana kwamba Sheria yote yaweza kufupishwa katika kauli hiyo.”

Ilikuwa zamu yangu kutikisa kichwa nikikubaliana naye.

“Mwalimu, alikuwepo Myahudi mwingine aliyekuja kabla ya Yesu, akiwaita watu kwenye toba. Jina lake aliitwa Yohana. Watu walipotubu dhambi zao na upotovu wao, aliwabatiza katika Mto Yordani. Aliwaambia watu kwamba aliye mkuu kupita yeye kwa mbali alikuwa akija — ambaye hakustahili hata kulegeza gidamu za viatu vyake. Sioni kuwa ni jambo la ajabu kwamba alipomwona Yesu akikaribia, aliuambia umati, ‘Tazama, Mwana-Kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu’ (Yohana 1:29). Alitambua kwamba dhabihu zote za Sheria zilikuwa kivuli tu cha siku ambayo mwana-kondoo mkamilifu angepatikana ili kuiondoa dhambi yote kwa nyakati zote. Wewe mwenyewe ulisema kwamba Yesu alikuwa mtu mkamilifu kuliko wote waliowahi kuishi.

Yeye ndiye mwana-kondoo ambaye, peke yake, angeweza kuyatosheleza matakwa ya Sheria. Aliitimiliza Sheria katika matakwa yake yote. Kwa kifo chake, alizifunika dhambi zetu zote kwa nyakati zote. Ndiyo maana, siku moja, kijana huyu mdogo wa Mataifa aliweza kupiga magoti kando ya kitanda chake, kutazama kuelekea msalaba mmoja huko Yerusalemu, na kumwomba Mungu wa Kiyahudi aikubali dhabihu ile kwa ajili ya dhambi zangu pia.”

Rabbi S. alikuwa ameinamisha kichwa chake wakati huu. Kila kitu kilikuwa kimya, nami sikuwa na jingine la kusema. Kisha nikaisikia sauti yake kana kwamba alikuwa akijisemea mwenyewe.

“Kumbe hiyo ndiyo maana yake! Kumbe hiyo ndiyo maana yake!” Kisha akiniinulia macho akasema, “Sasa naiona. Sasa naiona.”

Sijui kama nimewahi kupitia wakati wenye furaha kuu kuliko ule. Mara nyingi nimejiuliza kwa nini Bwana angenipa mimi onjo hilo la Mbinguni hali wengine wamemtumikia kwa muda mrefu sana kati ya watu wake wateule bila kuona jambo kama hilo. Zaidi ya hayo, ni dhahiri kwamba alikuwa amepanga haya yote miaka mingi kabla, wakati nilipozihoji sababu zake za kuufunga mlango wa kuja kwetu Canada.

Masikitiko yetu yalikuwa yakidhihirika kuwa miadi yake! Kulikuwa na mfuatano ulio wazi wa ‘mawe ya kukanyagia’ kutoka masikitiko yetu huko Germany, kupitia Ogmore Grammar School, Toronto French School, Profesa Carlisle na barua ile ya hadhi, hadi diploma ya ‘Type-A,’ hadi uteuzi wangu katika Hebrew Academy, na hadi siku hii hasa!

Siamini kwamba Bwana hufanya jambo lolote pasipo kusudi, na kwa kujua kwamba “neno lake halitamrudia bure,” (Isaya 55:11) nina hakika kwamba baadhi ya wale waliokuwa darasani mle, na Rabbi pia, watakuwa pamoja nami Mbinguni.

Ukurasa 1 / 4 · 5 dakika zimebaki katika sura