Sura 15 · dakika 7 za kusoma

Toronto Hebrew Academy

Miaka miwili niliyoitumia katika Hebrew Academy ilikuwa ya kufurahisha sana kwa sababu wanafunzi wa pale walikuwa na hamasa kubwa nao walijibidiisha katika masomo yao. Zaidi ya kazi yangu ya idara, pia niliifundisha timu ya soka ya shule hadi ikapata msimu wake wa kwanza wa ushindi katika ligi ya mtaa. Kwa mara ya kwanza katika uzoefu wangu wa ualimu, nilikuwa nikipokea mshahara mzuri (labda ulio bora kuliko yote katika Toronto nzima, kwa kuwa Hebrew Academy ilikuwa imejitolea kuwalipa walimu wake ‘angalau’ kile ambacho shule za serikali zilikuwa zikilipa). Binti zetu walikuwa wakizungumza juu ya nyumba mpya tuliyokuwa tunakwenda kununua — yenye bwawa la kuogelea, bila shaka! Kulikuwa na kasoro moja tu! Katika shule zangu nyingine zote, nilikuwa huru kuchukua hatua ya kuwaeleza wanafunzi wangu juu ya imani yangu. Katika kila mojawapo yao, nilikuwa nimeweza kuanzisha Umoja wa Kikristo au mikutano kama hiyo kwa ajili ya wanafunzi, ambayo wazungumzaji mashuhuri wangeifikia au mimi mwenyewe ningeongoza majadiliano. Bila shaka, hili halikuwezekana katika Hebrew Academy.

Hivyo basi, nikamwendea Msimamizi wa Wilaya wa kanisa ambalo familia yangu ilihudhuria, ili kutafuta nafasi ya kuhubiri nikiwa mtu wa kawaida. Aliniambia kwamba haikuwa kawaida nchini Canada kwa watu wa kawaida kuhubiri, lakini baada ya kusikia juu ya uzoefu wangu wa kuhubiri huko Wales, akaniuliza kwa nini nisifikirie kuingia katika huduma.

Nikamwambia kwamba hakuna jambo ambalo ningelipenda zaidi kuliko kuwa mchungaji, lakini nisingeweza kumudu kutumia miaka mitatu nikisoma seminari; zaidi ya hayo, ningehitaji kweli kuwa na wito ulio wazi kutoka kwa Bwana kabla ya kuacha ualimu ili niwe mchungaji wa wakati wote. (Naona kwamba wako wanaume wengi mno katika huduma wasioonyesha dalili yoyote ya upako kutoka kwa Mungu; watu wema, lakini hawakuitwa kuwa wachungaji.) Jibu lake lilikuwa kwamba hangenilazimu kuhudhuria seminari kwa kuwa alifahamu kazi yangu kama mzee katika kanisa la mahali hapo. Kuhusu ‘wito,’ alisema kwamba angetafuta ‘Ushuhuda wa Ndugu.’

Wiki chache baadaye, mchungaji wetu akajiuzulu wadhifa wake ili kuanza huduma ya kuimba ya kuzunguka, na kwa kuwa nilikuwa mzee pekee mwenye uzoefu wa kuhubiri, nikaalikwa kuzungumza katika ‘kuagana’ kwake. Baada ya ibada, wanaume wawili wa kusanyiko, wote wawili wakiwa wachungaji wa zamani, wakanijia (bila kujua chochote juu ya mkutano wangu na Msimamizi wa Wilaya) wakiniambia, “Hupaswi kuwa ukifundisha: unapaswa kuwa katika huduma!”

Je, huu ndio ulikuwa ‘Ushuhuda wa Ndugu’? Jambo hilo likafungua mwelekeo mpya kabisa katika maisha yangu. Matokeo yake yalikuwa kwamba baada ya miaka miwili ya kufundisha katika The Toronto Hebrew Academy, nikatoa taarifa ya kuondoka shuleni kwa kuwa nilikuwa nikienda kuwa mchungaji katika Christian and Missionary Alliance, lakini hiyo ni hadithi nyingine.

Zilikuwa zimebaki wiki nne kabla ya mwisho wa muhula wa masika kwa wanafunzi wetu wa darasa la 13, ambao wangetumia muhula wao wa mwisho wa shule katika kibbutz nchini Israel. Nilikuwa katika chumba cha walimu wakati Ari Barchi aliponijia.

Ari alikuwa mhitimu wa University of Jerusalem na alikuwa Toronto kufundisha masomo ya Kiebrania yaliyojumuisha pia mafundisho fulani juu ya dini linganishi.

“Gareth,” akasema, “niko karibu kufundisha somo juu ya Ukristo, nami nikaona ingekuwa upumbavu kidogo kwangu kufanya hivyo hali wewe unajua mengi zaidi juu ya Ukristo kuliko mimi! Je, ungekuwa tayari kuingia darasani pamoja nami?”

Bila shaka, nikasema kwamba ningefurahi sana, hivyo, asubuhi iliyofuata nikaenda naye kwenye darasa la ‘dini’ la kidato cha 13. Wale wanafunzi 25 wenye umri wa miaka 17 hadi 19, hawakuonyesha hamu kubwa tulipoingia. Baada ya yote, walijua mimi ni nani — waliniona kila siku katika maabara ya fizikia. Ari akaongea kwa Kiebrania kisha akasema, “Bwana Evans sasa atawapa mhadhara juu ya Ukristo!”

Nikameza mate! Nilidhani nilikuwa pale kama mtu wa kutoa msaada tu wa kujibu maswali yoyote. Sikuwa nikitegemea kufundisha somo lenyewe.

“Labda niwaeleze Ukristo si nini.” Nikaanza, nikijitahidi kwa nguvu kufikiri la kusema. “Si Ireland ya Kaskazini na vita vyake vya kimadhehebu. Si Vita vya Msalaba na umwagaji wake wa damu. Wala si siasa za sehemu kubwa ya ulimwengu wa Magharibi. Bali ni kukiri kwamba Yesu ndiye Masiya wa Mungu, ajaye kuziondoa dhambi za wanadamu. Hebu niwaambie jinsi nilivyokuwa Mkristo. Kisha nitawaambia jinsi nilivyokuwa Myahudi!” Kila mtu akaamka! “Kisha nitajibu swali lolote.”

Nikatoa ushuhuda wangu kwa kifupi (kama ulivyoandikwa katika sura ya pili), kisha nikawafundisha jinsi ulivyonifanya kuwa mtoto wa Mungu. Kwamba kwa imani, kama vile imani ya Ibrahimu ilivyomfanya kuwa mwenye haki mbele za Mungu (Mwanzo 15) na ‘baba wa waaminio,’ sasa nilikuwa nikimwabudu Mungu wa Kiyahudi, nikiwa nimekwisha ‘kufanywa mwana’ katika jamaa yake. Nikazungumza kwa muda wa dakika kumi hivi kisha nikauliza, “Kuna maswali?”

Kila mkono chumbani ukainuka. Nakumbuka nilianza na kijana aliyekaa katika kona ya nyuma upande wa kulia wa chumba. Aliuliza ingewezekanaje Yesu kuwa Masiya hali kila mtu alijua kwamba Masiya angeleta amani duniani, na ni vita tu vilivyofuata baada ya kuja kwake Yesu. Nikajibu kwa kuonyesha unabii wa Agano la Kale juu ya Masiya ateseaye na pia Masiya ashindaye. Vita ni matokeo ya kukataa kwa mwanadamu kuukubali uwezo wa dhabihu aliyoitoa pale Kalvari; hata hivyo, atarudi, wakati huu akiwa Mfalme, ili kuisimamisha “amani yake duniani.”

Maswali mengi yakafuata, wanafunzi wakipunga mikono na kupiga kelele ili maswali yao yasikike.

“Tafadhali, mwalimu! Tafadhali mwalimu! Ni zamu yangu, mwalimu!”

Msichana mmoja akauliza, “Je, unaamini Masiya atakuja katika kizazi chetu?” Nikajibu kwa kukubali, nikiongeza kwamba nilitumaini tungekuwa pamoja atakapokuja. Aliponiuliza, “Kwa nini?” nikajibu, “Kwa sababu hapo nitaweza kukuonyesha alama za misumari katika mikono yake na miguu yake!”

Somo likaendelea hivyo kwa dakika 40 kabla ya kengele ya shule kuashiria kwamba ulikuwa wakati wa kwenda darasa lililofuata; hata hivyo, wanafunzi hawa hawakuwa tayari kuniachia kwa kuwa walikuwa na maswali mengi mno yasiyojibiwa waliyokuwa na shauku ya kuyauliza. Punde nikagundua kwamba muda mrefu mno ulikuwa umepita na kwamba haingekuwa na maana kwangu kuondoka kwenda darasa lililofuata. Kufikia wakati huo, wanafunzi wangekuwa wameshaondoka katika maabara ya fizikia nao wangekuwa wametulia kusoma maktabani. Hii ndiyo ilikuwa taratibu ya kawaida ikiwa mwalimu hakufika kwa wakati kwa ajili ya somo. Hivyo, nikaendelea kujibu maswali hadi kipindi kingine kikapita. Wakati huu, ilinibidi kuondoka, lakini tu baada ya kuahidi kwamba ningekuja tena ikiwa mwalimu wao angependa hivyo.

Nilipokuwa nikiendesha gari kurudi nyumbani jioni ile, nilifurahi mno kwa pendeleo nililopewa la kuzungumza juu ya imani yangu na vijana hawa wa pekee. Sikuwahi kuota kwamba jambo hili lingewezekana, wala sikuweza ila kustaajabia njia za ajabu za Mungu. Nikaomba kwamba maneno niliyoyanena yangezaa tunda fulani katika maisha ya wanafunzi wale, nikiwa na hakika kwamba Bwana hazipandi mbegu zake bure kamwe.

Asubuhi iliyofuata ujumbe ulikuwa ukiningoja katika sanduku langu la barua shuleni. Ulisomeka, “Bwana Evans, tafadhali njoo unione ofisini kwangu saa 4:00 asubuhi ya leo. - Rabbi S.” Moyo wangu ukazama. Ni dhahiri kwamba Rabbi mkuu alikuwa amesikia juu ya muda niliokaa na wanafunzi wa darasa la 13, nami nilikuwa karibu kukemewa. Labda hata ningeambiwa niondoke shuleni!

Nilijihisi mnyonge sana, lakini nikajifariji kwa kukumbuka kwamba nilikuwa nimewaonya wakati wa usaili wangu kwamba jambo hili lingeweza kutokea. Nilipoikaribia ofisi yenye kuta za vioo, niliweza kumwona Ari Barchi ameketi ndani, akizungumza na Rabbi.

“Ah, Gareth, karibu ndani!” akasema Rabbi S. “Mimi na Ari tumekuwa tukijadili somo ulilokuwa nalo na wanafunzi wa darasa la 13 jana.” Akaendelea, “Kama ujuavyo, shule hii ilianzishwa ili kuwapa watoto wetu Wayahudi elimu bora kabisa, na sehemu muhimu sana ya jambo hilo ni kuwapandikiza upendo kwa mambo yote ya Kiyahudi, hivyo tunawafundisha historia yetu, mashairi yetu, utamaduni wetu, na dini yetu. Nimefundisha hapa kwa miaka kadhaa na lazima nikiri kwamba mojawapo ya masikitiko yangu makubwa kuliko yote ni kwamba ni wachache mno wanaofikia imani ya kweli katika Mungu; hata hivyo, nilipoingia darasani kwangu asubuhi ya leo, niliwakuta wote wakitaka kuzungumza juu ya imani na juu ya Mungu. Gareth, sijawahi kuwaona wakiwa na shauku kiasi hicho! Tatizo pekee ni kwamba, yote yamo vichwani mwao wala si mioyoni mwao. Tulikuwa tunajiuliza kama ungeweza kutusaidia kuiingiza imani hiyo mioyoni mwao!”

“Njia pekee ninayoijua ni kwa kukiri kwamba Yesu ndiye Masiya,” nikasema, huku kichwa changu kikianza kuzunguka.

“Naelewa hilo,” akasema Rabbi, “lakini unatambua kwamba itatubidi tukubaliane kutofautiana, lakini… tulikuwa tunajiuliza kama ungekuwa tayari kuingia katika madarasa mengine zaidi ili kuwafundisha wanafunzi wetu.

Wanastaajabu kumkuta mtu wa sayansi ambaye pia ni mtu wa imani. Hasa mtu ayajuaye maandiko yao vizuri kama unavyoyajua wewe. Tafadhali, je, utakuja?”

Haraka nikaonyesha utayari wangu, na mipango ikafanywa ili nihudhurie somo la darasa la 13 siku iliyofuata. Nadhani ningeweza kusikika ‘wa kiroho’ kwa kusema, “Hebu niliombee jambo hili,” lakini nadhani Bwana alinisamehe kwa haraka yangu ile!

Ukurasa 1 / 5 · 7 dakika zimebaki katika sura