Sura 14 · dakika 3 za kusoma

Ombi Lile

Mwaka wangu wa pili katika Toronto French School ulikuwa mzuri. Mshahara wangu ulipandishwa hadi dola 17,000 ambao sasa ulitosha kuishi kwa kuwa gharama kubwa za mwaka wa kwanza katika nchi mpya zilikuwa zimepita. Lakini, pamoja na nyongeza hii, nilitarajiwa kubaki shuleni hadi saa 1:00 usiku usiku mbili kwa juma ili kuwapatikania wanafunzi waliohitaji msaada wa ziada katika hisabati na fizikia. Sasa pia nilikuwa na jukumu la kupanga shughuli zote za nje ya mtaala za wanafunzi, zilizojumuisha: mashindano ya muziki na ngoma, mashindano ya sataranji, mbio za magari, na kadhalika.

Mwaka wa shule ulipokaribia mwisho, nilianza kusoma magazeti kuona ni nafasi zipi za ualimu zilizotangazwa katika mfumo wa shule za umma za Kanada. Zilikuwepo mbili zilizoniteka fikira: Upper Canada College na The Toronto Hebrew Academy. Upper Canada College ni shule binafsi ya kihistoria katikati ya Toronto yenye rekodi bora ya mafanikio kitaaluma na kimichezo pia; walikuwa wakitafuta mwalimu mwandamizi wa fizikia. The Toronto Hebrew Academy ilikuwa ikitafuta mtu wa kuwa Mkuu wa Idara ya Sayansi, ingawa nafasi hii ilihitaji cheti cha kibobezi cha Type-A.

Mtu anapoomba nafasi mpya za kazi, ni muhimu kuomba zote zilizotangazwa. Kwa njia hii, jina lako huanza kujulikana, na, mara nyingi majina na sifa za waombaji ambao hawakufanikiwa hupelekwa kwa shule nyingine.

Basi, nilipeleka maombi yangu kwa kila shule. Niliingizwa katika orodha fupi kwa nafasi ya Upper Canada College, jambo lililonifurahisha, lakini pia nilialikwa kwenye mahojiano katika Hebrew Academy. Hili lilinishangaza kwa kuwa ilikuwa dhahiri kutokana na ombi langu kwamba mimi si Myahudi.

Mahojiano yalipangwa yafanyike siku ya Jumatatu pamoja na mkuu wa shule na Rabi wao mwandamizi. Walinihoji kwa saa moja kisha wakauliza kama nilikuwa na maswali yoyote. Wakati ule sikuwa na swali lolote la kuuliza, lakini niliwaambia, “Mnatambua kwamba mimi si Myahudi? Kwa kweli, mimi ni Mkristo ‘aliyezaliwa mara ya pili’! Bila shaka, nitafundisha fizikia tu katika maabara yangu, lakini nikiulizwa na mwanafunzi juu ya imani zangu kuhusu mambo fulani, nitaona ni vigumu kutokujibu.”

Nilifikiri haingedhuru kusema hivi kwa kuwa sikuwa na tumaini la kuipata nafasi hiyo hata hivyo, ingawa wanaume hao walionekana kupendezwa na ombi langu! Mkuu wa shule, Gary Diamond, alijibu, “Naam, tunaelewa. Tunadhani huenda ikawa vyema kwa wanafunzi wetu kupewa changamoto na mtu wa imani nyingine!”

Niliendesha gari maili 20 kurudi nyumbani nikivuka jiji lote nikiwa katika hali ya mshangao mkubwa. Je, ingewezekana kwamba nifundishe katika chuo cha Kiyahudi cha kiorthodoksi? Siku zote nilikuwa nimewapenda watu wa Kiyahudi tangu wakati ule baba yake Anne aliponitambulisha kwa “Shepherd of Israel” - jarida alilolipokea mara kwa mara kutoka Amerika. Nilikuwa nikisema “Kama nisingekuwa Mwelisi, ningependa kuwa nimezaliwa Myahudi!”

Ijumaa iliyofuata adhuhuri, Keith aliniita ofisini kwake kuniambia kwamba Hebrew Academy ilipendezwa sana na ombi langu na ilikuwa imepiga simu kuthibitisha kama sifa zangu zilikuwa halisi. Nadhani ni jambo la kuzingatiwa kwamba mtu pekee Toronto aliyejua - hasa kuhusu vipengele viwili vya mwisho katika wasifu wangu wa kazi - “Rais wa Chama cha Wafanyakazi; Mjumbe wa Bodi ya Wasimamizi” - alikuwa ni Keith mwenyewe! Jioni ile nilipokea simu. Ilitoka kwa Bw. Diamond akinialika kuichukua nafasi katika The Toronto Hebrew Academy kuanzia Septemba kwa mshahara wa dola 33,000! Nilinong’ona kukubali kwangu, na baada ya dakika chache za mazungumzo ya kawaida, mara moja nikampigia Anne simu kumwambia habari hizo!

Tulizidiwa kabisa na furaha. Tulipozipata tena akili zetu, tukaanza kumsifu Bwana kwa njia zake za ajabu. Je, hii ndiyo ingekuwa sababu iliyomfanya aufunge mlango ule Ujerumani zamani hizo ili apate kujithibitisha kwangu kwa kutuleta Kanada? Alikuwa ameniruzuku cheti cha Type-A katika muda usiosikika wa mwaka mmoja tu, na sasa, akaufungua mlango kwa watu wake wateule! Nilikuwa nimefanya nini ili kustahili hili zaidi ya kuomba kando ya Brewery Field huko Bridgend?

Baadaye niligundua kwamba wengine saba walikuwa wameomba nafasi ileile katika The Toronto Hebrew Academy, kila mmoja akiwa na diploma za kibobezi na wote wakiwa Wayahudi. Naam, wawili kati yao walikuwa tayari shuleni pale, wote wawili wakiwa na Type-A katika masomo mawili! Ni sifa yao kwamba Andy na Marty wakawa marafiki zangu wazuri nilipoyazoea maisha katika jumuiya ya Kiebrania.

Kulikuwa na walimu 50 shuleni pale, ni wawili tu kati yetu tuliokuwa si Wayahudi, lakini walijitahidi sana kuhakikisha kwamba nilijua nilikuwa mmoja wao.

Ukurasa 1 / 3 · 3 dakika zimebaki katika sura