Sura 13 · dakika 3 za kusoma

Mbobezi Wa Type-A

Siku chache baadaye, kabla barua yangu ya kutambuliwa haijafika, nilipata mgeni darasani kwangu. Aliingia bila kutangaziwa naye akaketi huko nyuma. Kwa kuwa French School ilikuwa shule binafsi na walimu wengi walikuwa vijana wasio na uzoefu kutoka Ufaransa, wengi wao wakitafuta kukwepa utumishi wa kijeshi kwao kwa kufanya kazi Kanada, baadhi ya wazazi waliona ni haki yao, au ni wajibu wao, kuchunguza yale yaliyokuwa yakifundishwa kwa wana wao na binti zao. Walimu hawakupinga kwa kuogopa kurudishwa Ufaransa; lakini, mimi sikuwa na hofu ya namna hiyo. Basi, nikidhani huyu ni mzazi asiyealikwa, nilisimamisha somo nililokuwa nikifundisha, nikawapa wanafunzi kazi ya kuendelea nayo, na kumwendea yule mgeni. Aliomba radhi kwa kuingia bila mwaliko lakini alikuwa amedhani kwamba nilijua kuja kwake. Hakuwa mzazi, alikiri akicheka kidogo, bali alikuwa mkaguzi kutoka Wizara ya Elimu. Tena, nikamwambia kwamba kwa kuwa sikuwa nimearifiwa kuja kwake, sikuwa tayari kufundisha kwa ajili yake. Alicheka na kusema, “Bw. Evans, sijaja kukupima wewe, bali kuona kwamba mtaala wa Ontario unafundishwa kwa uaminifu katika shule hii.” Nilitulia na punde tukawa tunazungumza kwa urafiki alipokuwa akitazama daftari la mwanafunzi mmoja. Tulizungumza juu ya ‘nyumbani’ kwa kuwa yeye alikuwa amehama kutoka Scotland miaka kadhaa kabla ya hapo.

“Je, tayari umeomba barua yako ya kutambuliwa?” aliuliza. Nilimjulisha kwamba nilikuwa nimekwisha kuomba.

“Barua hiyo itakapofika,” akasema, “nipigie simu nami nitakuja kukutathmini ili uweze kupokea cheti cha ualimu cha Type-B.” Akasita kidogo. “Afadhali zaidi, barua yako ya kutambuliwa itakapofika, tuma nakala yake ofisini kwangu nami nitakutumia cheti chako.” “Ni dhahiri kabisa kwa jinsi unavyoliendesha darasa hili kwamba wewe ni mwalimu mwenye uwezo!”

Mwaka wa shule ulipoisha Anne alijiandaa kuwapeleka wasichana wetu safari ya Manitoba kuwaona akina Wiebe, lakini mimi nilikuwa nikifikiria jambo lingine kwa nafsi yangu; nilikuwa nimeona tangazo la kozi ya kiangazi ya majuma sita kwa wale waliopendezwa na waliostahili kupokea cheti cha ualimu cha Kibobezi cha Type-A.

Wote wanaotamani kuwa Wakuu wa Idara katika shule ya sekondari ya Ontario wanapaswa kuwa na cheti hiki, ingawa wengi hawana.

Wakati ule nilikuwa na rafiki aliyekuwa amefanya kozi za kiangazi kwa miaka kadhaa ili tu astahili kozi hii. Prof. Carlisle alikuwa ameonyesha kwamba ningestahili cheti hiki, kwa hiyo niliandika nikiomba fomu ya maombi. Ilipofika, nilijaza maelezo yaliyohitajika na kukusanya pamoja karatasi zote muhimu - isipokuwa moja. Cheti changu cha Type-B kilikuwa bado hakijafika ingawa yule mkaguzi alinihakikishia kwamba kilikuwa “ndani ya kompyuta.” Siku ya mwisho ya kupokea maombi, nilipiga simu chuo kikuu nikieleza kwamba cheti changu cha Type-B kilitarajiwa kufika “siku yoyote sasa,” na kuuliza kama ombi langu lingeweza kucheleweshwa kidogo.

Yule katibu alisikiliza kwa huruma, akasema alisikitika lakini, “tarehe za mwisho ni tarehe za mwisho.” Nilipokuwa karibu kuweka simu chini, nikihuzunika kwa kuwa karibu hivyo na kupata Type-A ndani ya mwaka mmoja tangu kufika Kanada, alinena tena. “Samahani, bwana. Je, yawezekana jina lako ni Bw. Evans?” Nilikumbuka kusikia hivyo hapo awali kutoka kwa katibu mwingine! Deja Vue? Kisha akaniambia kwamba jina langu lilikuwa tayari limeandikwa kuhudhuria kozi hiyo! Nilisema haingewezekana kwa kuwa sikuwa nimeomba bado. Aliniambia kwamba Prof. Carlisle ndiye aliyeliingiza jina langu! (Labda aliona haya kwa kuwa miaka kadhaa kabla alinisababishia kukatishwa tamaa kukubwa.)

Sasa nilikuwa nimeanza kweli kuelewa ni kwa nini Bwana alikuwa amefunga mlango ule Ujerumani, miaka mingi hivyo kabla.

Niliifurahia sana kazi ya kiangazi kile, nikahitimu nikiwa Mbobezi wa Type-A katika fizikia. Ndipo Anne aliporudi nyumbani kutoka majuma manne mazuri ajabu Dauphin, Manitoba na akina Wiebe. Yeye na wasichana watatu walikuwa wamesafiri zaidi ya maili 2,000, na walikuwa wamenunua fungu lao la vyakula, na bado tukakuta kwamba akaunti yetu ya benki mwisho wa mwezi haikuwa tofauti kabisa na kama wasingekwenda!

Tena, ni lazima Bwana alikuwa ameruzuku!

Ukurasa 1 / 3 · 3 dakika zimebaki katika sura