Sura 12 · dakika 4 za kusoma

Barua Ya Kutambuliwa

Ni katika mwaka ule wa kwanza Toronto ambapo matukio ya kushangaza kuliko yote maishani mwetu yakaanza kuungana, ingawa ilidhihirika kwamba Bwana alikuwa amepanga yote miaka mingi kabla, tena akiwa na kusudi hata zaidi ya wakati ule.

Punde nikatambua kwamba hapakuwa na mustakabali mkubwa kwangu katika French School ambako matumaini ya mshahara wa kutosha kuishi yalikuwa hafifu. Lakini, ili kufundisha katika mfumo wa Kanada ningehitaji sifa zangu za Uingereza zitambuliwe ili niweze kuomba cheti cha ualimu cha “Type-B.” Kwanza, nilihitaji kupata Barua ya Kutambuliwa, lakini ningefanyaje hivyo?

Hakuna aliyeonekana kujua shuleni pale, lakini nilikumbuka kwamba miaka kumi kabla, nilipokuwa nikiomba nafasi katika Danforth Technical College, nilikuwa nimepeleka nakala za shahada yangu na vyeti vya ualimu kwenye ofisi moja iliyoko Bloor Street, Toronto.

“Je, kuna yeyote ajuaye ofisi ya elimu iliyoko Bloor Street?” niliwauliza wenzangu.

“Naam, idara ya elimu ya chuo kikuu iko huko,” mtu mmoja alipendekeza.

Basi, mwisho wa masomo ya alasiri, niliendesha gari hadi katikati ya jiji Bloor Street, nikapata pa kuegesha kwa muda mfupi, na kuingia jengo lenye University Education Department.

Ghorofa ya chini ilikuwa tupu na yenye giza isipokuwa chumba kimoja tu mwishoni mwa ukanda mrefu. Kijana mmoja alikuwa amesimama mlangoni, akizungumza na mtu mmoja mzee zaidi aliyekuwa akiinuka kutoka kitini pake wakati nilipofika hapo mlangoni. Punde nikatambua kwamba ofisi ile ilikuwa ya yule kijana na kwamba yule mzee alikuwa mgeni wa heshima.

Nilipoeleza sababu zilizonileta pale, yule kijana aliniambia kwamba ningalipaswa kuwa katika Mowat Building iliyoko Bay Street, umbali wa vitalu kadhaa kutoka pale. Nilimshukuru nami nilikuwa karibu kuondoka wakati yule mzee aliponisimamisha kwa swali moja.

“Kwa nini ulikuja hapa?”

Nilieleza kwamba miaka kumi kabla nilipokuwa nikiomba nafasi nyingine, nilikuwa nimehitaji kupeleka sifa zangu kwenye ofisi moja iliyoko Bloor Street, nami nilidhani labda ndiyo hii.

“Labda uliandikia ofisi yangu,” akasema, na, akiushika mkono wangu katika wake, akaanza kuniongoza kurudi kando ya ule ukanda wenye giza kuelekea mlangoni.

Nilitaka kujiondoa niende Mowat Building, lakini sikuweza kujivuta kwa kuwa alionekana dhaifu mno, huenda angeanguka bila kunitegemea! Aliniongoza nje ya jengo, tukavuka barabara yenye njia nne yenye shughuli nyingi na kupanda ngazi kadhaa hadi ndani ya jengo lililokuwa mkabala. Nilishangaa mtu huyu alikuwa nani kwa sababu tulisalimiwa kwa heshima na bawabu na kutambuliwa na kila mtu mwingine kabla hatujaingia ‘patakatifu pa ndani’ pa jengo lile.

“Keti hapa,” akasema, akionyesha kiti laini chenye mikono kilichokuwa pale mezani, “wakati mimi ninakwenda kutafuta barua yako!”

Hakuwa amekwenda hata dakika moja kabla ya kurudi kwa ushindi akiwa na barua yangu ya awali iliyobanwa kwenye nakala ya jibu lake. Nilibaki nimeduwaa! Nilikuwa nimeingia jengo lisilo sahihi na kuongozwa hadi ofisi isiyo sahihi ili nikutane na ‘miadi ya kimungu’ ambayo Mungu alikuwa ameipanga miaka kumi kabla.

Kisha akanirudia yale maelekezo ambayo yule kijana alikuwa amekwisha kunipa, huku akiandika kwenye daftari dogo alipokuwa akinena.

“Ulizia Don Anderson utakapofika huko, kisha umpe hii,” akasema, akinipatia karatasi ile ya daftari.

Nilimshukuru nami nikatoka chumbani, nikijua kwamba muda ulikuwa unayoyoma na kwamba ofisi zingefungwa punde. Nilipokimbia kuelekea gari langu - ambalo tayari lilikuwa limeegeshwa kupita muda uliopangwa - nilijaribu kusoma kile alichokuwa amemwandikia Don Anderson.

“Ndugu Don,” ilisomeka, “tafadhali mtunze Bw. Evans kwa niaba yangu. Inaonekana anastahili Cheti cha Ualimu cha Kibobezi cha Type-A.”

Karatasi ile ilikuwa na kichwa, “Prof. Carlisle, Chief Education Officer, Ministry of Education, Toronto.” Huyu ndiye Mkurugenzi wa Elimu aliyefuta miadi yangu miaka minane kabla!

Fikiri tu! Nilikuwa nimefika katika jengo ‘lisilo sahihi’ kwa wakati mwafaka kabisa ili kukutana na yule mtu mmoja aliyeweza kunifanyia jambo la pekee - katika jiji la watu zaidi ya milioni nne!

Mshangao wangu wa siku hii ulikuwa bado haujaisha. Nilifika Mowat Block iliyoko Bay Street wakati uleule walipokuwa wakifunga milango. Nilikimbilia juu hadi ghorofa ambako, kwa mujibu wa bawabu, maombi ya barua za kutambuliwa yalishughulikiwa. Nilipoingia, nilisimama upesi kwa kukata tamaa: kulikuwa na kaunta yenye urefu wa futi 50 hivi na watu wamepanga foleni mbele yake, safu tatu. Nilikuwa nikianza kufikiri kwamba ingekuwa usiku wa manane kabla sijaondoka pale wakati ghafla niligongwa na mtu aliyekuwa akitoka chooni upande wangu wa kulia. Aliomba radhi kisha akaongeza, “Je, kuna lolote ninaloweza kukufanyia?”

Nilimwambia kwamba nilitaka kuonana na Bw. Don Anderson.

“Mimi ndiye Don Anderson,” akajibu.

Nilimpa ile karatasi nami nikaongozwa hadi ndani ya ofisi yake mwenyewe. Alinitambulisha kwa katibu wake, msichana Mwelisi, akimpa maagizo kwamba alipaswa, “kumtunza Bw. Evans.”

Nilifika nyumbani mapema kwa chakula cha jioni nikifurahia njia za ajabu ambazo Mungu alikuwa ameniongoza siku ile.

Ukurasa 1 / 3 · 4 dakika zimebaki katika sura