Sura 11 · dakika 4 za kusoma
Yehova Yire - Mruzuku Wetu
Mapokezi yetu Kanada hayakupendeza. Kwanza, ndege yetu ilibidi irudi nyuma tulipokuwa juu ya Iceland kwa hitilafu iliyohisiwa ya injini, kisha baada ya kungoja saa nne katika ukumbi wa kuondokea Heathrow, tuliondoka tena usiku wa manane kwa ndege ileile - wahudumu tofauti!
Kuchelewa kwetu kulifanya tufike Toronto saa 7:00 usiku kwa saa za huko, na punde ikadhihirika kwamba baadhi ya maofisa wa forodha hawakupendezwa hata kidogo na kulazimishwa kufanya kazi saa mbaya kiasi hicho. Uzoefu wetu haukupendeza kiasi kwamba tukaanza kutamani tungalibaki nyumbani kwetu Wales, lakini hatimaye tulipomaliza kupita, ofisa mmoja wa uhamiaji alitukaribisha na kutuhakikishia kwamba “si Wakanada wote walio kama yeye.”
Tulitazama huku na huko tukitafuta uso wa kutukaribisha, kwa kuwa juma moja kabla tulikuwa tumempelekea telegramu Hazel Weech, mama yake Sharon, iliyomjulisha habari za safari yetu, lakini hapakuwa na uso wa namna hiyo, na punde tukajikuta peke yetu katika ukumbi wa wanaowasili uliokuwa mtupu. Sote tulikuwa tumechoka sana na watoto waliweza kulala juu ya viti vya ukumbi, lakini Anne nami tulikesha, tukilinda mizigo na kumngoja Hazel. Saa 12:30 asubuhi niliamua kumpigia simu, ila nikagundua kwamba hakuwa amepokea telegramu yetu kamwe na alikuwa karibu kuondoka kwenda kazini.
“Chukueni teksi,” akasema, akinipa anwani ambako dereva angepaswa kutupeleka. Hivyo, saa 30 baada ya kuondoka Heathrow mara ya kwanza, tulikuwa tumejifunika katika vitanda vyema vya joto, tumelala fofofo.
Mwezi wetu wa kwanza Toronto ulikuwa wa kusisimua sana. Tulitembelea masoko makubwa, tulihudhuria People’s Church kumsikia Dr. Oswald Smith na Nicki Cruz, mwandishi wa, “The Cross and the Switchblade,” tulifurahia kumsikiliza Dr. John Wesley White akinena katika United Church of Canada ya hapo, na tukanunua nyumba!
Hii ilikuwa nyumba ndogo ya ghorofa moja, chafu, katika kitongoji cha Toronto, iliyokuwa tupu kwa miaka miwili. Mpangilio wa rangi ulikuwa rahisi: kahawia na kijani kibichi cheusi. Siku ya kwanza, nilianza orodha ndefu ya ukarabati kwa kupiga nyundo kilima kikubwa kilichokuwa katikati ya sakafu ya sebule, ambacho ilinibidi nitumie msumari wa inchi nne kukiweka chini, na kupaka rangi nyeupe fremu kadhaa za madirisha. Baada ya siku ndefu ya kufanya kazi hizo, nilikwenda kuoga ili kujiburudisha; lakini, nilipokwenda kufungua maji nilishtuka vigae kadhaa vilipoanguka kutoka kutani kwa bafu na kuingia birikani. Vilikuwa vimeshikamanishwa kwa Scotch Tape!
Labda unajiuliza kwa nini tulinunua nyumba ya namna hiyo, na niamini, ndiyo pekee tuliyoweza kuimudu kwa kuwa bei za Toronto zilikuwa karibu mara tatu ghali zaidi kuliko za Wales, na kupanga kungeyamaliza upesi akiba yetu ndogo. Sasa tuligundua jinsi mshahara wangu ulivyokuwa mdogo ukilinganishwa na gharama za maisha Kanada.
Mwaka wetu wa kwanza ulikuwa wa taabu kubwa kifedha lakini tulimwona Bwana ameitwa kwa haki, Yehova Yire, mruzuku wetu (Mwanzo 22:14).
Mara tatu katika mwaka ule wa shule tulikuwa bila fedha wala mahitaji yoyote kufikia katikati ya mwezi. Hatukumwambia mtu yeyote lakini siku zote tulishangazwa na jinsi Bwana alivyoyakidhi mahitaji yetu.
Mara moja, mwanamke mmoja kanisani kwetu alitupa zawadi ndogo ingawa hakuujua uhitaji wetu. “Natumaini hamjachukizwa,” akasema, “lakini Bwana aliniambia niwapeni hii.” Wakati mwingine, baadhi ya wazazi wa wanafunzi wangu walitupa fedha; lakini, riziki iliyoshangaza kuliko zote ilikuja mapema katika mwaka wetu. Mambo yalikuwa magumu wakati barua ilipoletwa kwa mkono kutoka Wizara ya Uhamiaji ikinialika kutembelea ofisi yao. Nilikuwa na wasiwasi. Je, kulikuwa na tatizo na karatasi zetu? Je, tungerudishwa nyumbani? Ofisini, nilipewa bahasha, ndani yake ikiwa barua ya kutukaribisha Kanada na hundi ya dola 1,000. Hii ilikuwa, kwa jinsi ilivyoonekana, zawadi kutoka Serikali ya Kanada kwa kila mtu anayenunua nyumba yake ya kwanza Kanada. Hundi nyingine mbili za dola 250 zikafuata.
Ni mwaka mmoja baadaye tu ndipo iligunduliwa kwamba kosa lilikuwa limefanyika na kwamba hatukustahili msaada huu kwa kuwa tulikuwa tumemiliki nyumba huko Wales. Serikali ilitaka fedha yao irudishwe, lakini kwa kuwa kosa lilikuwa lao, walikubali tuirudishe, bila riba, katika kipindi cha miaka mitatu. Ni nani mwingine awezaye kujivunia kupokea kiasi kama hicho kutoka serikalini, bila riba? Ni dhahiri kwamba Yehova Yire hutawala hata idara za fedha za serikali!
Kwa miezi ya kiangazi, sikupokea mshahara wowote, lakini tulikuwa na ahadi ya kutimiza. John na Eileen Weibe walikuwa marafiki zetu wazuri tulipokuwa Ujerumani, ambako yeye alitumika katika Jeshi la Kanada. Sasa walikuwa wakifanya kazi Manitoba ya Kaskazini pamoja na Church Army, na waliposikia kuwasili kwetu Kanada, walitusihi tuje kuwatembelea. Mwanzoni tulikuwa tumekubali, lakini tulipoona jinsi mapato yetu yalivyokuwa machache, Anne ilimbidi awaandikie mara mbili kuwaeleza kwamba ingetubidi tuahirishe kuja kwetu. Kila mara alipokuwa karibu kupeleka barua hiyo, barua ingeingia kutoka kwa Eileen ikituambia jinsi walivyokuwa wakitazamia kwa hamu kutuona tena, na hivyo, zikatuzuia kuwapelekea barua zetu hizo.
Hivyo, mwezi Julai, Anne aliwachukua wasichana katika safari ndefu hadi Dauphin, Manitoba, huku mimi nikibaki Toronto nikisomea cheti cha ualimu cha kibobezi, lakini hiyo ni hadithi nyingine.
Ziara ile ilikuwa nzuri sana lakini safari ya kwenda na kurudi ni matukio ambayo Anne angependelea kuyasahau. Jambo la kushangaza katika hadithi hii ni kwamba Anne alipohesabu fedha zetu, salio letu la mwisho wa mwezi lilikuwa sawasawa kabisa na lilivyopaswa kuwa kama safari hiyo isingefanyika!
Tena, ni lazima Bwana alikuwa ameruzuku.