Safari ya Msafiri kwa Watoto ·Msalaba na Mzigo Uliopotea

Sura 4 · dakika 3 za kusoma

Msalaba na Mzigo Uliopotea

Ndipo nikaona katika ndoto yangu ya kuwa njia kuu ambayo Mkristo alipaswa kuikanyaga, ilikuwa na ukuta kila upande, na jina la ukuta ule ni Wokovu. Katika njia hii kuu Mkristo alikimbia, lakini kwa taabu nyingi kwa sababu ya mzigo uliokuwa mgongoni mwake. Alikimbia hivyo hata alipokaribia mahali palipokuwa na msalaba, na chini yake kaburi. Mkristo alipoukaribia msalaba tu, mzigo wake ukateleza kutoka mgongoni mwake, karibu na mdomo wa kaburi, ukaanguka humo, nami sikuuona tena.

Ndipo Mkristo akafurahi, akasema kwa moyo wa shangwe: Yeye ananipa raha kwa huzuni yake, na uzima kwa kifo chake.

Lakini alisimama kimya kwa muda, kwani alishikwa na hofu ya kicho kufikiri ya kuwa kuuona msalaba kumemwondolea hivyo mzigo wake. Mara tatu au nne aliutazama msalaba na kaburi, na machozi yakampanda machoni. Alipokuwa akisimama hivyo na kulia, tazama, Wenye-Kung'aa watatu wakamjia, na mmoja wao akasema: Amani iwe kwako! umepata neema ya kusamehewa dhambi zako. Na mmoja akamkaribia kumvua matambara yake na kumvika vazi jipya, hali wa tatu akatia alama usoni pake, akampa kitabu cha kukunjwa chenye muhuri, akamwambia akitazame njiani aendako, na akikabidhi kwenye Lango la Mbinguni; kisha wakamwacha.

Mkristo akaruka mara tatu kwa furaha, akaimba alipokwenda: Ee, mahali hapa ni pa namna gani! Msalaba uliobarikiwa! Kaburi lililobarikiwa! La, amebarikiwa Bwana aliyeaibishwa kwa ajili yangu!

Akaendelea hivyo hata akafika bondeni ambako aliwaona watu watatu waliokuwa katika usingizi mzito, wenye minyororo miguuni mwao. Jina la mmoja aliitwa Mpumbavu, mwingine Mvivu, na wa tatu Kiburi. Mkristo alipowaona wamelala katika hali hii, akaenda kuwaamsha, akasema: Mnafanana na wale walalao juu ya mlingoti wa merikebu, kwa maana Bahari ya Chumvi iko miguuni mwenu. Amkeni, ondokeni, mje pamoja nami. Nitumainini, nami nitawasaidia kuvua minyororo yenu. Kwa hayo wakainua macho yao kumtazama, naye Mpumbavu akasema: Ningependa kulala usingizi zaidi. Kiburi akasema: Kila mtu na aangalie yake mwenyewe. Nao wakalala tena kupata usingizi.

Ndipo nikaona katika ndoto yangu ya kuwa watu wawili wakaruka kutoka juu ya ukuta, wakafanya haraka nyingi kumfikia. Majina yao yalikuwa Mwenye-Desturi na Unafiki.

Mkristo.—Mabwana, mnatoka wapi, nanyi mwenda wapi?

Mwenye-Desturi na Unafiki.—Tulizaliwa katika nchi ya Majivuno-Batili, nasi tuko safarini kwenda Mlima Sayuni ili kupata sifa.

Mkristo.—Mbona hamkuingia kwa kupitia Lango? Je, hamjui ya kuwa yeye asiyeingia kwa mlango, bali hupanda ili kuingia, huyo ni mwivi?

Wakamwambia ya kuwa kupita langoni ni kuzunguka mno; ya kwamba njia iliyo bora ni kufupisha, na kupanda ukuta, kama walivyofanya wao.

Mkristo.—Lakini je, Bwana wa mji tuendako atafikiri nini juu ya hilo, kama hatuendi kwa njia ya mapenzi yake?

Wakamwambia Mkristo ya kuwa hakuwa na haja ya kujali juu ya jambo hilo, kwa maana desturi ya muda mrefu ilikuwa imeifanya kuwa sheria, nao wangeweza kuthibitisha ya kwamba imekuwa hivyo kwa miaka mingi. Mkristo.—Lakini je, mna hakika kabisa ya kuwa namna yenu itasimama mbele ya hukumu ya sheria?

Naam, wakasema, hapana shaka juu yake. Nasi tukiingia njiani hata kidogo, basi kuna tofauti gani? Tukiwa ndani, tu ndani; wewe u njiani tu, uliyeingia langoni, na sisi pia tu njiani tuliochagua kupanda ukuta. Je, hali yetu si njema kama yako?

Mkristo.—Mimi natembea kwa kanuni ya Bwana wangu, bali ninyi mnatembea kwa kanuni ya tamaa zenu wenyewe. Bwana wa njia atawahesabu ninyi kuwa wevi, wala hamtaonekana kuwa watu wa kweli mwishoni.

Yaliyomo

Safari ya Msafiri kwa Watoto John Bunyan

Ukurasa 1 / 1 · 3 dakika zimebaki katika sura