Sura 2 · dakika 8 za kusoma

Waabuduo wa Kweli

“Lakini saa inakuja, tena sasa ipo, ambapo waabuduo wa kweli watamwabudu Baba katika roho na kweli; kwa maana Baba awatafuta watu wa namna hiyo wamwabudu. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.” Yohana 4:23-24.

Maneno haya ya Yesu kwa yule mwanamke wa Samaria ni fundisho lake la kwanza lililoandikwa juu ya jambo la maombi. Yanatupa mianzo kadhaa ya ajabu ya kuchungulia ndani ya ulimwengu wa maombi. Baba awatafuta waabuduo: kuabudu kwetu huukidhi moyo wake wa upendo nako ni furaha kwake. Yeye awatafuta waabuduo wa kweli lakini huwakuta wengi wasio kama vile angependa wawe.

Ibada ya kweli ni ile iliyo katika roho na kweli. Mwana amekuja kufungua njia kwa ibada hii katika roho na katika kweli na kutufundisha. Na hivyo mojawapo ya masomo yetu ya kwanza katika shule ya maombi lazima liwe kuelewa maana ya kuomba katika roho na katika kweli na kujua jinsi tuwezavyo kuipata.

Kwa yule mwanamke wa Samaria, Bwana wetu alinena juu ya ibada ya namna tatu. Kwanza, kuna ibada ya ujinga ya Wasamaria: ‘Ninyi mnaabudu msichokijua’ Yohana 4:22. Ya pili ni ibada ya maarifa ya Myahudi, aliye na ujuzi wa kweli wa Mungu: ‘Sisi tunaabudu tukijua; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.’ Yohana 4:22. Na kisha ibada mpya, ya kiroho, ambayo yeye mwenyewe amekuja kuiingiza: “Lakini saa inakuja, tena sasa ipo, ambapo waabuduo wa kweli watamwabudu Baba katika roho na kweli.” Yohana 4:23. Kutokana na muktadha, ni dhahiri kwamba maneno ‘katika roho na kweli’ hayamaanishi, kama inavyofikiriwa mara nyingi, kwa bidii, kutoka moyoni, kwa unyofu.

Wasamaria walikuwa na vitabu vitano vya Musa na ujuzi fulani wa Mungu; bila shaka alikuwako zaidi ya mmoja miongoni mwao ambaye kwa unyofu na bidii alimtafuta Mungu katika maombi.

Wayahudi walikuwa na ufunuo kamili wa kweli wa Mungu katika neno lake, kwa kadiri ulivyokuwa umetolewa hata wakati ule; walikuwako miongoni mwao watu wacha-Mungu, waliomwita Mungu kwa moyo wao wote. Lakini bado si ‘katika roho na kweli,’ kwa maana kamili ya maneno hayo.

Yesu asema, ‘Lakini saa inakuja, tena sasa ipo’ Yohana 4:23. Ni ndani yake na kwa njia yake peke yake ambamo ibada ya Mungu itakuwa katika roho na kweli.

Miongoni mwa Wakristo, bado mtu hukuta madaraja yale matatu ya waabuduo. Wako wale ambao katika ujinga wao hawajui vema wanaloomba: huomba kwa bidii, lakini hupokea kidogo tu. Wako wengine, walio na ujuzi sahihi zaidi, wajaribuo kuomba kwa akili zao na mioyo yao yote na mara nyingi huomba kwa bidii nyingi, lakini bado hawaifikii heri kamili ya ibada katika roho na kweli. Ni katika daraja hili la tatu ambamo lazima tumwombe Bwana wetu Yesu atupokee; lazima tufundishwe naye jinsi ya kuabudu katika roho na kweli. Hii peke yake ndiyo ibada ya kiroho; hii ndiyo hutufanya kuwa waabuduo kama vile Baba anavyowatafuta.

Katika maombi, kila kitu kitategemea kuelewa vema na kutenda ibada katika roho na kweli. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli” Yohana 4:24. Wazo la kwanza linaloonyeshwa hapa na Bwana ni kwamba lazima pawe na upatano kati ya Mungu na waabuduo wake; jinsi Mungu alivyo, ndivyo ibada yake itakavyokuwa. Hii ni kwa kadiri ya kanuni itawalayo katika ulimwengu wote: twatazamia kufanana kati ya kitu na kiungo ambacho kwacho kitu hicho hujidhihirisha au hujitoa. Jicho lina ufaao wa ndani kwa nuru na sikio kwa sauti.

Mtu ambaye angependa kumwabudu Mungu kweli, ambaye angependa kumpata na kumjua na kumwmiliki na kumfurahia Mungu, lazima awe katika upatano naye, na lazima awe na uwezo wa kumpokea. Kwa kuwa Mungu ni Roho, lazima tuabudu katika roho. Kama Mungu alivyo, ndivyo alivyo mwabuduo wake.

Na hii yamaanisha nini? Yule mwanamke alikuwa amemwuliza Bwana wetu kama Samaria au Yerusalemu ndipo mahali pa kweli pa kuabudia. Yeye ajibu kwamba tangu sasa ibada haitafungwa tena mahali fulani: “Mwanamke, niamini, saa inakuja ambapo hamtamwabudu Baba katika mlima huu wala kule Yerusalemu” Yohana 4:21. Kama Mungu alivyo Roho, asiyefungwa na nafasi wala wakati, bali katika ukamilifu wake usio na mwisho ni yeye yule sikuzote na kila mahali, ndivyo ibada yake tangu sasa haitafungwa tena mahali wala umbo, bali itakuwa ya kiroho kama Mungu mwenyewe alivyo wa kiroho. Somo la umuhimu mkubwa. Jinsi Ukristo wetu unavyoteseka kutokana na hili, kwamba umefungwa nyakati na mahali fulani.

Mtu atafutaye kuomba kwa bidii kanisani au chumbani hutumia sehemu iliyo kubwa ya juma au ya siku katika roho iliyo kinyume kabisa na ile aliyoomba nayo. Ibada yake ilikuwa ni kazi ya mahali au saa iliyowekwa, si ya nafsi yake yote. Mungu ni Roho: yeye ni yule wa Milele na Asiyebadilika; alivyo, yu hivyo sikuzote na kwa kweli. Ibada yetu vivyo hivyo lazima iwe katika roho na kweli: ibada yake lazima iwe roho ya maisha yetu; maisha yetu lazima yawe ibada katika roho kama Mungu alivyo Roho.

‘Mungu ni Roho: nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli’ Yohana 4:24. Wazo la pili litujialo ni kwamba ibada hii katika roho lazima itoke kwa Mungu mwenyewe. Mungu ni Roho: yeye peke yake ndiye aliye na Roho wa kutoa. Ni kwa ajili ya hili alimtuma Mwana wake, atufae kwa ibada ya namna hiyo ya kiroho, kwa kutupa Roho Mtakatifu. Ni juu ya kazi yake mwenyewe ambayo Yesu asema anapotamka mara mbili, ‘Saa inakuja,’ Yohana 4:23 na kisha aongeza, ‘tena sasa ipo.’

Alikuja kubatiza kwa Roho Mtakatifu; Roho hakuweza kububujika mpaka yeye atukuzwe (Yohana 1:33, 7:37-38, 16:7). Ni pale alipokwisha kuikomesha dhambi, na kuingia Patakatifu pa Patakatifu kwa damu yake, akiisha kupokea humo kwa niaba yetu Roho Mtakatifu (Matendo 2:33), ndipo alipoweza kumshusha kwetu kama Roho wa Baba. Ni pale Kristo alipokwisha kutukomboa, nasi ndani yake tukiisha kupokea cheo cha watoto, ndipo Baba alimtuma Roho wa Mwana wake mioyoni mwetu akilia, ‘Aba, Baba.’ Ibada katika roho ni ibada ya Baba katika Roho wa Kristo, Roho wa Uana.

Hii ndiyo sababu Yesu hapa alitumia jina la Baba. Hatumkuti hata mmoja wa watakatifu wa Agano la Kale akijichukulia binafsi jina la mtoto au akimwita Mungu Baba yake. Ibada ya Baba yawezekana tu kwa wale ambao Roho wa Mwana amewapa. Ibada katika roho yawezekana tu kwa wale ambao Mwana amewafunulia Baba, na waliopokea roho ya Uana. Ni Kristo peke yake afunguaye njia na kufundisha ibada katika roho na katika kweli. Hilo halimaanishi tu, kwa unyofu. Wala halimaanishi tu, kwa kadiri ya kweli ya Neno la Mungu. Usemi huu una maana ya kina na ya Kimungu. Yesu ni ‘mzaliwa wa pekee wa Baba, amejaa neema na kweli.’ Yohana 1:14. ‘Kwa maana torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo’ Yohana 1:17. Yesu asema, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima.” Yohana 14:6.

Katika Agano la Kale, yote yalikuwa kivuli na ahadi; Yesu alileta na kutoa uhalisi, kiini, cha mambo yaliyotarajiwa. Ndani yake, baraka na nguvu za uzima wa milele ni miliki na uzoefu wetu halisi. Yesu amejaa neema na kweli; Roho Mtakatifu ni Roho wa kweli; kwa njia yake, neema iliyo katika Yesu ni yetu kwa hakika, na kweli ni mawasiliano hasa yatokayo katika uzima wa Kimungu. Basi, ibada katika roho ni ibada katika kweli; ushirika hai halisi na Mungu, mawasiliano na upatano halisi kati ya Baba, aliye Roho, na mtoto aombaye katika roho.

Yale Yesu aliyomwambia yule mwanamke wa Samaria, hakuweza kuyaelewa mara moja. Pentekoste ilihitajika ili kudhihirisha maana yake kamili. Sisi hatujaandaliwa vema tunapoingia mara ya kwanza katika shule ya maombi kufahamu fundisho la namna hii. Tutalielewa vema baadaye. Na tuanze tu na kulichukua somo kama yeye alivyolitoa. Sisi ni wa kimwili nasi hatuwezi kumletea Mungu ibada aitafutayo. Lakini Yesu alikuja kutoa Roho: ametupa yeye. Na hali tunayojiweka nayo tuombapo iwe ile ambayo maneno ya Kristo yametufundisha. Na kuwe na ungamo la ndani la kutoweza kwetu kumletea Mungu ibada impendezayo; utii wa kitoto wa kufundishika unaomngoja atufundishe; imani rahisi ijitoayo kwa pumzi ya Roho.

Zaidi ya yote, na tushike sana kweli hii yenye baraka—tutaona kwamba Bwana ana zaidi ya kutuambia juu yake—kwamba ujuzi wa Ubaba wa Mungu, ufunuo wa Ubaba wake usio na mwisho mioyoni mwetu, imani katika upendo usio na mwisho utupao Mwana wake na Roho wake ili atufanye watoto, kwa hakika ndiyo siri ya maombi katika roho na kweli. Hii ndiyo njia mpya na hai ambayo Kristo alituvunulia. Kuwa na Kristo Mwana, na Roho wa Mwana, akikaa ndani yetu, na akitufunulia Baba, hutufanya waabuduo wa kweli, wa kiroho.

Bwana Mbarikiwa! Nauabudu upendo ambao kwao ulimfundisha mwanamke, aliyekunyima kikombe cha maji, ibada ya Mungu inavyopasa kuwa. Nafurahi katika uhakika kwamba hutampungukia sasa kumfundisha mwanafunzi wako, ajaye kwako na moyo utamaniao kuomba katika roho na katika kweli. Ee, Bwana wangu Mtakatifu! Nifundishe siri hii yenye baraka.

Nifundishe kwamba ibada katika roho na kweli si ya mwanadamu, bali yatoka kwako peke yako; kwamba si jambo la nyakati na majira tu, bali ni bubujiko la maisha ndani yako. Nifundishe kumkaribia Mungu katika maombi chini ya hisi la kina la ujinga wangu na kutokuwa na kitu ndani yangu cha kumtolea, na wakati huo huo la maandalizi uyafanyayo wewe, Mwokozi wangu, kwa ajili ya pumzi ya Roho katika kigugumizi changu cha kitoto. Nakuhimidi kwamba ndani yako mimi ni mtoto, na nina uhuru wa mtoto wa kukaribia; kwamba ndani yako nina roho ya Uana na ya ibada ya kweli. Nifundishe, zaidi ya yote, Ee Mwana Mbarikiwa wa Baba, jinsi ufunuo wa Baba ndio utoao ujasiri katika maombi; na Ubaba usio na mwisho wa Moyo wa Mungu na uwe furaha yangu na nguvu yangu kwa maisha ya maombi na ya ibada.

Amina.

Ukurasa 1 / 6 · 8 dakika zimebaki katika sura
Ochorus

Kuwawezesha watu vitabu vya Kikristo vya kale — bila malipo, kwa lugha yako.

Chunguza

Dhamira Yetu

Vitabu vya Kikristo vya kale bila malipo mtandaoni — na vitabu vilivyochapishwa tunavyogawa kwenye makongamano, makanisa, shule na magereza kote Afrika Mashariki.

Faragha na Masharti

Huduma tangu 2021 · Victoria BC, Kanada · Kampala, Uganda