Sura 9 · dakika 5 za kusoma
Unyenyekevu na Imani
“Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamuutafuti?” Yohana 5:44.
Katika hotuba niliyoisikia hivi karibuni, msemaji alisema kwamba baraka za maisha ya juu ya Kikristo mara nyingi ni kama vitu vilivyoonyeshwa dirishani mwa duka: mtu aweza kuviona waziwazi lakini asiweze kuvifikia. Akiambiwa anyoshe mkono atwae, angejibu, Siwezi. Kuna kioo kinene kati yangu nayo. Vivyo hivyo, Wakristo waweza kuziona waziwazi ahadi zilizobarikiwa za amani na raha kamili, za upendo na furaha ifurikayo, za ushirika udumuo na kuzaa matunda, lakini wakahisi kwamba kuna kitu katikati kikizuia kumiliki kwa kweli. Ahadi zitolewazo kwa imani ni huru na za hakika mno, mialiko na vitia-moyo ni vyenye nguvu mno, nguvu kuu ya Mungu ambayo imani yaweza kuitegemea i karibu na i huru mno. Kwa hiyo, kiburi ndicho kitu pekee kiizuiacho imani na baraka isiwe yetu.
Katika andiko hili, Yesu atufunulia kwamba ni kiburi hasa kifanyacho imani isiwezekane. Yohana 5:44 lasema: “Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi?” Tuonapo jinsi kiburi na imani vilivyopingana kiasili pasipo upatano, tutajifunza kwamba imani na unyenyekevu ni kitu kimoja shinani, na kwamba kamwe hatuwezi kuwa na imani ya kweli kuliko kadiri ya unyenyekevu wa kweli tulio nao. Tutaona kwamba twaweza kuwa na sadikisho thabiti la akili na uhakika wa ile kweli hali kiburi kimetunzwa moyoni, lakini hufanya ile imani iliyo hai, yenye nguvu kwa Mungu, isiwezekane.
Yatupasa tu kufikiri kwa kitambo juu ya imani ni nini. Je, si ungamo la kutokuwa kitu na kutokuwa na uwezo, kujisalimisha na kungoja ili Mungu atende kazi? Je, yenyewe si jambo linyenyekezalo kuliko yote, yaani kuikubali nafasi yetu ya utegemezi, tusioweza kudai wala kupata wala kufanya cho chote ila kile neema itoacho? Unyenyekevu ndiyo hulka iiandaayo roho kuishi kwa kutegemea. Hata pumzi ya siri kabisa ya kiburi—katika kujitafutia nafsi, kujitakia, kujiamini, au kujikweza—ni kuitia nguvu tu ile nafsi isiyoweza kuingia wala kumiliki mambo ya ufalme, kwa kuwa yakataa kumwacha Mungu awe kile alicho na kile ambacho lazima awe, Yote katika yote. Imani ni chombo au hisi ya kutambua na kushika ulimwengu wa mbinguni na baraka zake. Imani hutafuta utukufu utokao kwa Mungu, nao huja tu pale Mungu alipo yote.
Maadamu tunapokeana utukufu sisi kwa sisi, tukiutafuta na kuupenda na kuulinda kwa wivu utukufu wa maisha haya, heshima na sifa itokayo kwa wanadamu, hatuutafuti wala hatuwezi kuupokea utukufu utokao kwa Mungu. Kiburi hufanya imani isiwezekane. Wokovu huja kwa njia ya msalaba na ya Kristo aliyesulubiwa. Wokovu ni ushirika na Kristo aliyesulubiwa katika Roho ya msalaba wake. Wokovu ni muungano na furaha ndani ya Mungu; wokovu ni kushiriki unyenyekevu wa Yesu. Je, ni ajabu kwamba imani yetu ni dhaifu hivi hali kiburi kingali kikitawala, nasi hatujajifunza hata kuutamani au kuuombea unyenyekevu kuwa sehemu ya wokovu iliyo ya lazima na iliyobarikiwa kuliko zote?
Unyenyekevu na imani vimeungamanishwa katika Maandiko kuliko wengi wajuavyo. Uone hilo katika maisha ya Kristo. Kuna visa viwili ambavyo ndani yake alinena juu ya imani kubwa. Je, yule akida, ambaye Yesu aliistaajabia imani yake akisema, “Nawaambieni, sijaona imani kubwa namna hii kwa ye yote katika Israeli,” hakuwa amesema, “Bwana, sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu”? Naye yule mama aliyeambiwa, “Mama, imani yako ni kubwa!” (Mathayo 15:28), je, hakulikubali jina la mbwa, akasema, “Ndiyo, Bwana, lakini hata mbwa hula makombo”? (Mathayo 15:27) Ni unyenyekevu uiletao roho kuwa si kitu mbele za Mungu ndio uondoao kila kizuizi cha imani, na kuifanya iogope jambo moja tu: isije ikamvunjia heshima kwa kutomtumaini kikamilifu.
Ndugu, je, hapa hatuna sababu ya kushindwa kwetu kuufuatia utakatifu? Je, si hili, ingawa hatukulijua, lililofanya kujitoa kwetu na imani yetu kuwa kwa juujuu na kwa muda mfupi? Hatukujua kiburi na nafsi vilivyokuwa bado vikitenda kazi kwa siri ndani yetu, wala jinsi Mungu peke yake, kwa kuingia kwake na uweza wake mkuu, angeweza kuvitoa. Hatukufahamu kwamba ni asili mpya ya Kimungu peke yake, ikichukua kabisa mahali pa nafsi ya kale, iwezayo kutufanya wanyenyekevu kweli.
Hatukujua kwamba unyenyekevu kamili, usiokoma, wa kila mahali ni lazima uwe hulka ya shina ya kila ombi na kila kumkaribia Mungu, na ya kila kushughulika na mwanadamu; na kwamba ni sawa kujaribu kuona bila macho au kuishi bila pumzi, na kuamini au kumsogelea Mungu au kukaa katika upendo wake pasipo unyenyekevu uenezao yote na moyo mnyenyekevu.
Ndugu, je, hatujakuwa tukikosea kwa kujitaabisha sana hivi ili tuamini, hali wakati wote ule ile nafsi ya kale ilikuwapo katika kiburi chake ikitafuta kujitwalia baraka na utajiri wa Mungu? Si ajabu kwamba hatukuweza kuamini. Na tuibadili njia yetu. Na tutafute kwanza kabisa kujinyenyekesha chini ya mkono wa Mungu ulio hodari: naye atatukweza. Msalaba, na mauti, na kaburi, ambamo Yesu alijinyenyekeza, ndivyo vilivyokuwa njia yake ya kuufikia utukufu wa Mungu.
Shauku yetu moja na ombi letu la bidii na liwe kunyenyekezwa pamoja naye na kuwa kama yeye; na tukubali kwa furaha lo lote liwezalo kutunyenyekeza mbele za Mungu au za wanadamu; hii peke yake ndiyo njia ya utukufu wa Mungu. Labda wahisi kutaka kuuliza swali. Nimenena juu ya wengine walio na uzoefu uliobarikiwa, au wanaowaletea wengine baraka, na hata hivyo wanapungukiwa na unyenyekevu. Wauliza kama hao hawathibitishi kwamba wana imani ya kweli, hata yenye nguvu, ingawa waonyesha wazi mno kwamba bado wanatafuta sana heshima itokayo kwa wanadamu. Kuna majibu zaidi ya moja.
Lakini jibu kuu katika habari hii ni hili: kwa kweli wana kipimo cha imani, na kwa kadiri yake, pamoja na vipawa vya pekee walivyopewa, ndivyo ilivyo baraka wanayowaletea wengine.
Lakini katika baraka hiyo hasa, kazi ya imani yao huzuiwa na upungufu wa unyenyekevu. Baraka hiyo mara nyingi ni ya juujuu au ya kupita, kwa kuwa hawaifungui njia Mungu awe yote. Unyenyekevu wenye kina zaidi bila shaka ungeleta baraka yenye kina na ujazo zaidi. Roho Mtakatifu, asiyetenda kazi ndani yao kama Roho wa nguvu tu, bali akaaye ndani yao katika ujazo wa neema yake, na hasa ile ya unyenyekevu, angejitoa kupitia wao kwa waongofu hawa kwa maisha ya nguvu na utakatifu na uthabiti yanayoonekana kwa kidogo mno sasa.
“Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi?” (Yohana 5:44). Ndugu! Hakuna kiwezacho kukuponya na tamaa ya kupokea utukufu utokao kwa wanadamu, wala na wepesi wa kuumia na uchungu na hasira vijavyo usipopewa, ila kujitoa kutafuta utukufu utokao kwa Mungu peke yake.
Utukufu wa Mungu aliye mtukufu kuliko wote na uwe kila kitu kwako. Utawekwa huru na utukufu wa wanadamu na wa nafsi, nawe utaridhika na kufurahi kuwa si kitu. Kutoka katika kutokuwa kitu huku, utakua hodari katika imani, ukimtukuza Mungu, nawe utaona kwamba kadiri uzamavyo katika unyenyekevu mbele zake, ndivyo alivyo karibu zaidi kuitimiza kila shauku ya imani yako.